SoC02 Waandaaji wa Filamu, mnakwama wapi Filamu za Uhuishaji (Animations)?

Stories of Change - 2022 Competition

sue bae

Member
Aug 16, 2022
21
13
Habari za wakati huu wana JamiiForums.

Leo napenda kuongea na waandaaji wa filamu Tanzania.

Kwanza niwapongeze kwa kazi kubwa mfanyayo ya kuielimisha na kuiburudisha jamii. Pia, niwapongeze kwa mapinduzi makubwa mnayoyafanya kwenye tasnia ya filamu nchini.

Teknolojia inawasaidia sana kuandaa na kusambaza kazi zenu kwa kasi, hivyo kupelekea kazi zenu kujulikana nchi za nje, lakini teknolojia hii hii bado hamuitumii vizuri.

58812FE2-1481-4C53-9F98-098B4EACD484.jpeg

Picha na #Lucamovie

Binafsi ni mpenzi sana wa filamu za uhuishaji, wengi huziita katuni.

Ninafurahia mno kuona katuni akipewa uwezo wa kibinadamu na kuwasilisha yote yaliyo mpasa mwanadamu kuwasilisha.

Filamu nyingi zimebeba hisia zangu mpaka kujikuta nikilia na kucheka, nikinuna na kufurahi. Filamu kama Soul, Coco, Luca, Charming, Moana na nyingine nyingi.

Mwanzoni filamu hizi zilichukuliwa ni filamu za watoto tu, nadhani sababu hii ndio hutufanya kuwa nyuma kwenye uandaaji wa filamu hizi, lakini ukweli ni kwamba filamu hizi zinatazamwa na watu wa rika zote. Cha kushangaza huku kwetu bado kuna pengo kubwa kwenye uandaaji wa filamu hizi.

Filamu nyingi zinazo oneshwa hapa kwetu, nyingi zinaonekana kufanana maudhui, wahusika, mandhari mpaka wengi kusema ya kwamba eti, tumekosa ubunifu. Je, ni kweli?

Tunafurahia teknolojia kurahisisha maisha yetu, je, mbona bado kuna pengo upande huu? Changamoto ni nini hasa?

303A29CF-D359-4A08-930D-3EC08BD6B736.jpeg

Picha na #soulmovie

Je, ni ukosefu wa ujuzi?

Ni ukweli usiopingika kuwa filamu za uhuishaji zinahitaji ujuzi wa hali ya juu kwenye uandaaji wake.

Kuanzia kuandaa wahusika mpaka mandhari, huhitaji mbinu za sanaa za kitamaduni na mbinu za hali ya juu za matumizi ya picha za kompyuta.

Nchi nyingi za Afrika, waandaaji wengi bado hawajafanikiwa kuwa na ujuzi huu.

Je, mpaka lini hali itakuwa hivi? Ni lini mtajifunza kuandaa filamu hizi?.

Kama changamoto ni kipato cha kujifunzia ujuzi huu, zipo fursa nyingi za masomo kujifunza kuandaa filamu hizi, tuzichangamkie.

Je, ni ukosefu wa fedha?
Filamu ya Coco ili gharimu dola milioni 175 kwenye uandaaji wake lakini filamu hiyo hiyo mauzo yake ni zaidi dola milioni 800.

Ni ukweli usiopingika kuwa filamu hizi zinatumia fedha nyingi kwenye uandaaji wake mpaka usambazaji wake, lakini hiyo si sababu ya msingi sana kwani wapo wawekezaji ambao wapo tayari kusapoti filamu nzuri.

Kama hii ndio changamoto, hizo fedha zitapatiakana lini? Tuwasubiri mpaka lini ndio mtakauwa na fedha za kuandaa filamu hizi?

Zipo fursa nyingi za kudhamini waandaaji wa filamu za uhuishaji. Tuzichangamkie.

Je, mnahofia kukosa Watazamaji?

Mwaka 2021, Filamu ya Luca ilikuwa na watazamaji zaidi ya Bilioni 10.5.

Labda changamoto mnayohofia ni kukosa Watazamaji wa filamu hizi. Bado mnadhani katuni ama filamu za uhuishaji hutazamwa na watoto tu? Hapana.

Watazamaji Bilioni 10 ni wengi mno na wengi wao waliitazama kwenye majukwaa ya mtandaoni, Je walionunua filamu hiyo ni watoto? Hapana.

Inamaana filamu hizi zinawatazamaji wengi sana. Kwanini nasi tusitumie fursa hii kuingiza kipato?

Je, tatizo ni ubunifu?
Kuwa na ujuzi ni suala lingine na kuwa mbunifu ni suala lingine.

Ubunifu huja mara baada ya mtu kuwa na ujuzi wa jambo fulani.
Labda wapo waandaaji wa filamu wawezao kuandaa filamu hizi lakini changamoto ikawa ni ubunifu hafifu.

Kama waafrika tunazo historia nyingi sana za kutuhusu, ubunifu waweza kuanzia hapa. Uwepo wa kazi zinazofanana huashiria kuwa tumekosa ubunifu, hadithi inaweza kuwa ni ile ile ila ubunifu ukaifanya ionekane ni ya tofauti sana.

Filamu za uhuishaji ni ubunifu pia.

Je, hutumia muda mrefu kwenye uandaaji wake?
Filamu ya Moana imetumia miaka mitano (5) kwenye uandaaji wake.

Kitu kizuri chochote huhitaji muda kwenye maandalizi yake. Ni ukweli usiopingika kuwa filamu za uhuishaji huhitaji muda mwingi wakati wa uandaaji wake kwani hutumia ubunifu na ujuzi wa hali ya juu.

Waandaaji wengi wa filamu hizi huwa tayari kuwekeza muda mwingi katika hili wakijua faida yake hapo baadae.

Je, na sisi waandaaji wa filamu Tanzania, ni kwamba hatuhitaji kutumia muda mwingi katika uandaaji wa filamu hizi? Tunaharakia nini hasa?

Je, changamoto ni mahali pa kuuzia filamu hizi?

Wengi tumeitazama Filamu ya Soul kupitia Majukwaa mbalimbali mtandaoni.

Asante teknolojia kwani kila kukicha majukwaa mengi huanzishwa kwaajili ya kuuza na kuonesha filamu mtandani. Majukwaa kama Netflix, Netnaija, Amazon, Swahili flix, na kadhalika.

Kama hiyo ni changamoto basi si changamoto tena kwani majukwaa haya yapo tayari kupokea kazi nyingi ili mradi ziwe na ubora na kufikia viwango watakavyo.

Nawapongeza sana waandaaji wa filamu ya BINTI kwa hatua kubwa waliyoipiga kwa kuona fursa iliyoletwa na teknolojia na kuitumia vyema mpaka sasa kuoneshwa Netflix.


Hitimisho
Yapo mengi ya kutuonesha kwamba tunafaidika na teknolojia kwenye kila nyanja za maisha kama afya, elimu, na kadhalika. Mbali na hayo sekta ya sanaa inaonekana kuwa hatua moja nyuma kwenye kunufaika na teknolojia hii hasa tasnia ya filamu nchini. Sasa ni wakati wa waandaaji wa filamu kuinuka na kuikamatia fursa hii. Filamu za uhuishaji hupendwa sana na pengo lake lahitaji mzibaji. Tunaifurahia teknolojia katika kurahisisha maisha yetu basi tuitumie kujifunza na vitu kama hivi. Waandaaji wa filamu tuichukue hii kama changamoto, na kama mpo mbioni kutoa kazi kama hizi basi msichelee, tusiwe wa mwisho kwenye matumizi ya teknolojia.

Asante.
 
Back
Top Bottom