Vyura 1000 wa Kihansi kurudishwa nchini

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
SERIKALI inatarajia kuwarudisha vyura 1,000 wa Kihansi kati ya 5,248 waliopo nchini Marekani hivi sasa katika miezi minne ijayo.

Vyura 499 walipelekwa na serikali nchini humo mwaka 2000 baada ya kubainika kufa kwa wingi kwa ugonjwa wa kuvu.

Idadi hiyo ni awamu ya kwanza ya majaribio endapo wataweza kuishi katika mazingira ya nchini, na kwa kuwa mradi wa vyura hao unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) kumalizika Desemba mwaka huu, serikali itaendeleza mradi huo.

Gharama zilizokuwa zikitumika katika mradi huo kupitia WB kwa mwaka ni Sh milioni 353.6 sawa na dola za Marekani 260,000.

Wanasayansi na wataalamu wa viumbe kutoka ndani na nje ya nchi, waliridhia hatua hiyo ya urejeshwaji wa vyura hao wanaozaa badala ya kutaga, Juni na Julai mwaka huu katika mkutano wao wa siku tatu, uliomalizika juzi jioni, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo uliandaliwa na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano huo, wanasayansi hao walisema muda huo wa miezi minne ni mahususi kutoa nafasi kwa serikali kukamilisha uandaaji wa bajeti ya mradi na pia kukamilisha utafiti wa kinga ya magonjwa hasa kuvu ambao umeelezwa kuwepo katika korongo la Kihansi, eneo la makazi ya asili ya vyura hao.

Akizungumza na gazeti hili baada ya makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Zuolijia na Hifadhi ya Viumbe Pori ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Cuthbert Nahonyo alisema “tumekubaliana vyura warudi nchini Juni au Julai na hii imefikiwa baada ya kukamilisha makubaliano yaliyofanyika Bagamoyo mwaka 2007, hayo ni pamoja na kukamilisha nyumba za kuwatunzia kabla ya kuwarejesha porini.”

Dk. Nahonyo alisema vyura hao watakaporejea watatunzwa katika nyumba maalumu iliyoko UDSM ili kuendelea kuwafanyia utafiti na kuwaacha wazaliane kwa miaka miwili kabla ya kuwapeleka nyumba kama hiyo iliyoko katika korongo la Kihansi na kisha kuwarejesha porini.

Alisema hivi sasa muda uliobaki ni wa kuendelea kufanya utafiti wa magonjwa hasa kuvu ambao hivi sasa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kinatarajia kuanza kutengeneza kinga ya kibaiolojia ya kuwanusuru vyura hao kufa kwa ugonjwa huo.

Kuhusu gharama, Mratibu wa Mradi wa Kihansi nchini, Dk. Fadhila Khatibu alisema mchakato wa kujua kiwango hasa kitakachotumiwa na serikali katika mradi huo kitajulikana baada ya mwezi mmoja kwa kuwa majadiliano na taarifa kadhaa zinatarajiwa kuanza kukusanywa kutoka kwa taasisi za serikali, za kijamii na za kimataifa.

Katika hatua nyingine, Mratibu wa Shirika la WCS, Dk. Jennifer Pramuk, aliiomba serikali kupitia mkutano huo kutoa kibali mapema cha kuwapeleka vyura hao katika taasisi na vituo vya utafiti nchini humo ili kuwapunguzia gharama za kuwatunza au vingine iridhie baadhi wauawe.

Mwakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambao ndio wahusika wa suala hilo aliyekuwepo katika mkutano huo kwa niaba ya Wizara, Herman Keraryo alisema ombi hilo atalifikisha kwa Katibu Mkuu ili akae na wataalamu wake na jibu watafikishiwa mapema iwezekanavyo.
 
Back
Top Bottom