Vyuo vikuu watoa tamko juu ya EPA, Richmond

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,087
Vyuo vikuu watoa tamko juu ya EPA, Richmond
Frank Leonard, Iringa
Daily News; Sunday,February 24, 2008 @00:03

WANAFUNZI wa vyuo vya elimu ya juu mjini Iringa vya Mkwawa, Ruaha na Tumaini, wamefanya maandamano mjini hapa na kutaka bei ya umeme ishuke mara moja. Aidha wanafunzi hao pia wametaka waliochangia kupanda kwa huduma hiyo ya kijamii wafikishwe mahakamani haraka, wafungwe maisha au kunyongwa.

Maandamano hayo yaliyofanyika jana yalianzia katika vyuo vyao na kupita barabara kuu hadi zilipo ofisi za Tanesco za mkoa wa Iringa ambako walisimama kwa muda na kutoa tamko kali dhidi ya ufisadi. Askari Polisi waliyasindikiza maandamano hayo yaliyoishia katika uwanja wa Mwembetogwa mjini hapa.

Baadhi ya viongozi wa vyuo hivyo waliopata fursa ya kuzungumza na wananchi waliofurika kuwaunga mkono, waliwataka Watanzania kutokubali kubebeshwa mzigo wa gharama kubwa za maisha kwa sababu ya mafisadi wachache wanaotafuna uchumi wa nchi.

Makamu Rais wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, Peter Brayani, aliwataka Watanzania waungane kuwasaidia viongozi wanaoonekana kutoridhishwa na jinsi mambo yasivyokwenda serikalini. Aidha, aliwataka wawang'oe madarakani katika uchaguzi wa mwaka 2010 viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wameshindwa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Naye Makamu Mkuu Rais wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, Kitalima Tamasha alisema suala la viongozi kufilisi nchi na hatimaye kujiuzulu halisaidii asilimia 90 ya Watanzania ambao wamekithiri kwa umasikini. Alisema mafisadi wote wanaoguswa na tuhuma za Benki Kuu, Richmond na nyingine nyingi, wajiuzulu bila shinikizo na mamlaka zinazohusika ziwashtaki haraka iwezekanavyo.

Naye Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, Safari Lawrance, alisema Tanzania sio masikini kama watu wengi wanavyoamini. "Ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi mabwanyenye nchini unadhihirisha kwamba Watanzania wengi zaidi wanaweza kupata elimu ya msingi hadi chuo kikuu na huduma za matibabu kwa asilimia 100 bure," alisema.

Alisema ufisadi umesababisha huduma nyingi za kijamii, ikiwamo huduma muhimu ya umeme kupanda mara kwa mara, hali inayomuongezea mzigo wa maisha Mtanzania. "Kule Shinyanga, akina mama wanaoshindwa kutumia huduma ya umeme kwa sababu ya bei kubwa wamekuwa wakitumia kuni na hivyo kufanya macho yao yawe mekundu, hali ambayo imesababisha baadhi yao wauawe kwa madai kwamba ni wachawi,” alisema.

Akitoa tamko hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Tahliso, Edwin Chitage alisema umoja wao utaendelea kupaza sauti hadi wafu akiwemo Baba wa Taifa hili Mwalimu Julius Nyerere afufuke ili ajiunge nao kulia kilio kitakachookoa nchi hii. Katika tamko hilo, Tahliso inataka serikali itangaze mchakato wa namna ya kushusha bei za umeme, isiendelee kuwalilia wananchi kwamba haina uwezo wakati mabilioni yakiliwa na wachache.

Tamko hilo linataka pia Takukuru iwe chini ya Bunge, ifanye kazi kwa maamuzi ya wabunge, serikali isikilize ushauri wa wataalamu, wabunge warudi kwa wananchi washirikiane kuupigania ukweli bila kujali itikadi. Iwapo serikali itaamua kutowachukuliwa hatua mafisadi hao, umoja wao kupitia kwa wanasheria wao utaandaa mashitaka dhidi ya mafisadi wote na kuyafikisha mahakamani, inasema sehemu ya tamko hilo.



 
Back
Top Bottom