Vyandarua bila kuharibu mazalia ya mbu ni bure | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vyandarua bila kuharibu mazalia ya mbu ni bure

Discussion in 'JF Doctor' started by MziziMkavu, Aug 12, 2009.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Aug 12, 2009
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,617
  Trophy Points: 280
  8th July 2009

  Vyandarua.

  Hakuna ubishi kwamba pamoja na ukimwi kuwa ni ugonjwa hatari kuliko magonjwa yote kwa sasa kutokana na kutokuwa na chanjo wala tiba, bado ugonjwa wa malaria unaongoza kwa kuua watu wengi zaidi nchini na kwa nchi zote za ukanda wa kitropiki.

  Kwa maana hiyo, juhudi za kutokomeza malaria si tu zinatakiwa ziongezwe zaidi ili kuokoa maisha ya watu wetu hasa watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka mitano, bali pia sera za kukabiliana na ugonjwa huu inabidi zitazamwe kwa umakini zaidi ili kuleta matokeo bora zaidi kwenye jamii.

  Juzi, Mganga Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Deo Mutasiwa, alitangaza programu kabambe ya serikali kwa kushirikiana na wafadhili wa Benki ya Dunia, Serikali ya Marekani na Global Fund, ya kugawa vyandarua viwili vilivyowekwa dawa ya kuua mbu kwa familia milioni 14 nchini kote.

  Mpango huo unaotarajia kuanza mwakani, unalenga kupunguza maambukizi ya malaria na hivyo kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo ambao bado ni tishio kwa uhai wa wananchi wengi.

  Inakadiriwa kwamba mkakati huu wa kugawa vyandarua vya mbu utagharimu Dola za Marekani milioni 100 sawa na Sh. bilioni 120.

  Tungependa kuchukua fursa hii kupongeza juhudi hizi za kugawa vyandarua kwa wananchi, hasa kwa sababu vitatolewa bure, hapana shaka uamuzi huu umezingatia uwezo wetu kwa maana hiyo kila familia kati ya hizo milioni 14 zitapata vyandarua viwili hivyo kusaidia kuwakinga wanafamilia na mbu waenezao malaria.

  Pamoja na kuunga mkono juhudi hizi, tumejiuliza maswali mengi pia juu ya uamuzi huo. Tunafahamu kwa hakika kabisa kwamba ili kuondokana kabisa na malaria njia sahihi zaidi ni kuangamiza mbu wote.

  Kama nguvu kubwa zaidi ikielekezwa kuangamiza mbu, kwa kuharibu mazalia yake; kama kufukia madimbwi, kuweka makazi katika mazingira ya usafi na kunyunyuzia dawa katika mabwawa ya maji machafu, uwezekano wa kupunguza mbu ni mkubwa zaidi na hivyo kupunguza madhara yake kwa binadamu.

  Ndiyo maana tunapotafakari kwa kina mpango mzima wa kugawa vyandarua vyenye dawa tunapata jibu moja kwamba maambukizi ya malaria hutokea kitandani tu wakati watu wamelala.

  Ni dhahiri, wapo watu wanaoumwa na mbu sehemu za kazi, wakiwa kwenye mazungumzo ukumbini nyumbani, wakiwa kwenye malindo usiku au hata wakiwa baa wakijiburidisha.

  Kwa kuwa si rahisi kutembea na chandarua chenye dawa kila mahali ambako kuna uwezekano wa kuumwa na mbu, basi ni dhahiri matokeo ya kuvitumia ili kupunguza maambukizi ya maradhi hayo hayawezi kuwa ya kiwango cha juu sana.

  Ni kwa kutambua ukweli huu tunadhani njia ya kweli na ya uhakika ya kukabiliana na malaria ni kuangamiza mbu kwa kuharibu mazalia yake.

  Kutumia vyandarua vyenye dawa kunaweza tu kupunguza kwa asilimia kidogo maambukizi ya ugonjwa huo, lakini kwa uhakika hakuwezi kutokomeza malaria kabisa.

  Kwa msingi huu basi pamoja na juhudi za kugawa vyandarua viwili bure kwa familia milioni 14, ambavyo hata hivyo havitoshi kwa wanafamilia wote kutokana na wengine kuwa na idadi kubwa ya watu; nguvu pia zielekezwe kwenye kuharibu mazalia ya mbu.

  Hatutaki kuamini kwamba serikali haijui kwamba kugawa vyandarua vya bure pekee hakutatokomeza malaria nchini, inajua jambo muhimu na la msingi ni kuharibu mazalia ya mbu hivyo kuteketeza wadudu hao moja kwa moja.

  Tunajua, mpango huu ni msaada na kwa maana hiyo mwenye kupewa hana chaguo, hupokea kile alichopewa, lakini tukumbuke kuwa ni vema kuwa na mipango yetu inayojitegemea katika kukabiliana na malaria tukilenga kuangamiza mbu kwanza.

  Tujiepushe na mipango ambayo mwisho wa yote itatugeuza kuwa soko za bidhaa za kukabiliana na malaria kama dawa, vyandarua na vitu vingine vinavyofanana na hivyo. Tuamke sasa na kujipanga vizuri.  CHANZO: NIPASHE
   
 2. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #2
  Aug 12, 2009
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,617
  Trophy Points: 280
  10th June 2009

  Mbu.

  Katika miaka ya hivi karibuni, suala la dawa inayofaa kutibu malaria limekuwa na mijadala mirefu ndani ya wataalamu wa tiba, lakini pia miongoni mwa wananchi kwa ujumla wao.

  Kwa mfano, wakati serikali iliposema inaondoa dawa ya klorokwini kwenye tiba ya kwanza kwa malaria, kulikuwa na malalamiko makubwa miongoni mwa jamii, huku wengine wakidai kwamba ni dawa pekee iliyokuwa inawafaa licha ya kutangazwa kwamba utafiti wa kitaalam umebainisha kwamba dawa hiyo imepoteza uwezo wake wa kuua vijidudu vya malaria kwa asilimia 52.

  Kwa maneno mengine usugu wa malaria nchini ulikuwa umeongezeka sana kiasi kwamba klorokwini ikaonekana kwamba haiwezi tena kutibu ugonjwa huo, licha ya kuwepo kwa zaidi ya miongo mitano kama tiba sahihi ya malaria na upatikanaji wake ukiwa ni wa hakika na kwa bei nafuu sana.

  Tangu wakati huo, yaani miaka ya tisini dawa mstari wa mbele ya kutibu malaria zimekwisha kubadilishwa zaidi ya mara tatu, na kila iliyotangazwa kwamba ndiyo inafaa zaidi kuliko ya awali, haikuchukua muda kabla ya kuonekana nayo imezidiwa nguvu na hivyo kutangazwa mpya.

  Bila kutaja madhara kwa wagonjwa kutokana na dawa hizi mpya za kila mara, kama vile watu kubabuka kutokana na madhara ya salfa (sulphur); dawa hizi mpya zilizoidhinishwa ilionekana wazi kwamba hazikutumiwa kwa muda mrefu kama ilivyokuwa klorokwini zamani.

  Kuna wakati hoja zilivuma kwamba isije kuwa biashara ya kutafuta faida ya haraka haraka imevamia sekta ya tiba kwa binadamu kwa maana ya utengenezaji wa madawa, hoja hii iliongezewa nguvu na jinsi makampuni makubwa ya madawa duniani yanavyobadili dawa haraka haraka, huku mamlaka zetu, yaani Wizara ya Afya, ikiridhia mabadiliko hayo bila kujali sana uwezo wa taifa na hali za watu wake.

  Juzi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, alisema kwamba dawa ya mseto ya alu, ni tatizo nchini kwa sababu ya bei yake. Waziri huyu ambaye alihusika katika kuipitisha dawa hii anakiri kwamba bei yake ni ya juu sana kwa Watanzania wa kawaida kuimudu. Dozi moja ni Sh. 13,000 hadi 14,000.

  Kutokana na bei hii kuwa kubwa, ni hakika wananchi wengi hawawezi kuimudu. Wananchi walio wengi wanaishi kwa kipato cha kutatanisha mno, uwezekano wa kupata mlo wa uhakika kila siku ni majaliwa ya muumba, watu wenye dhiki kama hiyo kuwatarajia wamudu gharama ya dawa ya Sh. 14,000 kwa dozi ni muhali mkubwa.

  Hali hii ikitazamwa na ukweli kwamba alu ndiyo dawa iliyo kwenye mstari wa mbele kabisa kutibu malaria nchini, maana yake ni kwamba wananchi wengi hawatapata tiba hiyo kwa sababu moja tu, hawawezi kuimudu.

  Tunajua kwamba malaria ni ugonjwa unaoongoza kwa kuua kuliko magonjwa mengine yote katika nchi za kitropiki, hata Ukimwi ambao ni hatari ukiwa hauna chanjo wala tiba, haufui dafu kwa malaria katika kuteketeza maisha ya watu, kwa hali hii, tulitarajia sera na maamuzi vinapochukuliwa juu ya dawa ya malaria, hadhari ingezingatiwa ili isije kuwa tunabadili dawa lakini hazitakuwa na manufaa kwa watu wetu.

  Hata hivyo, tunafarijika kwamba serikali ikishirikiana na mataifa mengine wanatafuta njia za kupunguza gharama za dawa ya alu, ili walau ipatikane kwa bei kama ilivyokuwa klorokwini hapo zamani.

  Wakati juhudi hizi zikiendelea kwa kushirikiana na mataifa mengine, ni vema serikali ikachukua hatua haraka kukabiliana na hatari iliyoko mbele ya taifa ya watu wake kushindwa kumudu dawa za kutibu malaria.

  Tunafikiri hatua hizi zinaweza kuwa ni pamoja na kuondoa kodi kwenye uagizaji wa dawa hizi, lakini pia hata kutoa ruzuku kwa dawa hizi kwa sababu bila kufanya hivyo malaria itaendelea kuteketeza maisha ya watu wetu. Ni wajibu wa serikali kuhakikisha kwamba dawa sahihi za kutibu malaria zinapatikana nchini na kwa bei ambayo wengi watamudu.
  CHANZO: NIPASHE
   
 3. C

  Caroline Danzi JF-Expert Member

  #3
  Aug 12, 2009
  Joined: Dec 19, 2008
  Messages: 3,629
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145
  Hii ni kweli kama hatuharibu mazalia ya mbu watu wataendelea kuleta vyandarua wakiingiza kipato kwa manufaa yao. Misaada ni business tu watu hatujui.
   
Loading...