Vyama vya upinzani: Polisi inawatisha wapiga kura Igunga

kibakwe

Senior Member
May 10, 2011
171
22
VYAMA vya siasa vinavyowania kiti cha ubunge katika Jimbo la Igunga, vimelishukia Jeshi la Polisi na kulitaka lieleze sababu za kupitisha jimboni humo gari la washawasha juzi huku likipiga king’ora.

Vyama hivyo vimesema kitendo cha polisi kupitisha gari hilo wakati huu wa kampeni ni dalili kwamba lina nia ya kuwatisha wananchi na kuvuruga uchaguzi kwa kuwakimbiza wapiga kura.

Vyama hivyo vimetoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana mbele ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa ratiba ya kampeni zinazotarajiwa kuanza kesho.

Vyama hivyo vilieleza kuwa ujio wa gari hilo utasababisha wananchi wengi wasipige kura na kukimbilia maporini wakihofia vurugu.

Mwenyekiti wa UMD, Lazaro Ndegaya ambaye pia ni mgombea ubunge wa jimbo hilo, alisema kitendo kilichofanywa na polisi kuleta gari hilo, ni kuwashtua wananchi na kuwatia hofu na kinaweza kuwafanya wasishiriki uchaguzi huo kikamilifu.

“Polisi ni mali ya Watanzania, gari lilikuwa likipita jana (juzi) nilifikiri ni ambulance (gari la kubeba wagonjwa) lakini kumbe ni washawasha. Hili linashtua wananchi na hasa ukizingatia Igunga hakuna fujo,” alisema Ndegaya.
“Traditionally (kiutamaduni), Wasukuma ni wapole hivyo wasitishwe na kuwafanya wakimbie kupiga kura.”

Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Chadema, Mwita Mwikwabe Waitara aliishutumu polisi kwa kupitisha gari hilo huku likipiga king’ora kwa nguvu kana kwamba kuna hatari Igunga.

Alisema gari hilo limewatisha wananchi kwa kuwa hawajazoea kulisikia hivyo akalitaka jeshi hilo kutolitumia kuwatisha wananchi katika uchaguzi huu mdogo.

Katibu wa DP Taifa, Kwarrey Amoury alimtaka mkurugenzi wa uchaguzi kuzungumzia kuzungushwa kwa gari hilo mitaani huku likipiga king’ora wakati hakuna hali yoyote ya hatari.

“King’ora cha gari la polisi kimewashtua wananchi hivyo mkurugenzi wa uchaguzi azungumzie hilo. Gari hilo limewashtua na kuwatia hofu wananchi,” alisema Amoury. Katibu wa SAU Wilaya ya Igunga, Shabani Kirita alisema tangu amekaa Igunga hajawahi kuliona gari hilo hivyo limeletwa kuwatisha wananchi na vyama vya upinzani.

“Gari lililokuja linatutisha kwa kuwa hapa Igunga halijawahi kupita, limeletwa kwa ajili ya kutisha wananchi na upinzani,” alisema Kirita.

Alisema kuwa kitendo cha polisi kuleta gari hilo Igunga ni mwanzo wa kuvuruga kampeni kwa kuwa wakazi wa hapo hawatakuwa tayari kuona amani ikivurugwa.

“Polisi watuahidi kusimamia usalama na siyo kutuvurugia amani,” alisema.

Mratibu wa kampeni za CUF, Kirungi Kirungi ameitaka polisi kusimamia usalama kipindi chote cha kampeni badala ya kuanza kuvuruga amani kwa kuwatisha wananchi.

Katika vyama vilivyohudhuria mkutano huo CCM hakikuzungumza chochote kuhusu gari hilo.

Utetezi wa Polisi

Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Igunga (OCD), Issa Muguha alisema kuwa gari hilo halina tatizo lolote huku akivitaka vyama hivyo kutoa ushirikiano ili kufanikisha uchaguzi huo... “Gari lipo na kila mkutano utakuwa na polisi hata kama mkikataa, ”alisema.

Alivitaka vyama vyote kuheshimu muda akisema asingependa kuona kiongozi yeyote akiteremshwa jukwaani kutokana na kupitiliza muda.Katika hatua nyingine vyama hivyo vimeishukia Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kwa kuitaka iseme kama imeshindwa kazi ili watu waendelee kutoa na kupokea rushwa bila hofu.

Ndegaya alisema Takukuru imeshindwa kufanya kazi kwa kile alichosema kwamba ikielezwa kwamba kuna sehemu rushwa inatolewa haichukui hatua.

“Rushwa inaendelea tu hapa hata ukimtuma mtoto mdogo akakuletee ataenda,” alisema Ndegaya.
Kwa upande wake, Karita wa SAU alisema taasisi hiyo imeshindwa kazi Igunga kwa kuwa fedha zinamwagwa lakini haijaonyesha cheche zake... “Waseme kama kazi wameshindwa.”

Kirungi Kirungi wa CUF aliitaka Takukuru kutangaza kuwa imeshindwa kazi ya kupambana na rushwa ili ijulikane.

Takukuru nao wajibu
Kamanda wa Takukuru Wilaya ya Igunga, John Ngunangwa alisema siyo kwamba wameshindwa kazi bali kitendo cha rushwa ni cha siri kubwa hivyo ushirikiano ndiyo utakaoweza kufanikisha vita hiyo.“Takukuru haijashindwa kazi kwa kuwa suala la rushwa ni letu sote, viongozi wasikate tamaa watupe taarifa tutazifanyia kazi,” alisema Ngunangwa.

Akifunga kikao hicho msimamizi wa uchaguzi, Magayane Protas alivitaka vyama vyote kufuata maadili ya uchaguzi na kuhakikisha hayavunjwi.

UPDP, Chausta ndani
Wanachama wawili wa vyama vya UPDP na Chausta jana walijitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge wa jimbo hilo.

Wagombea wa vyama hivyo walifika jana katika ofisi za msimamizi wa uchaguzi 6:30. Mgombea wa UPDP alifika akiwa katika msafara wa Bajaji tatu zilizokuwa zikipeperusha bendera ya chama hicho. Mgombea wake, Hemed Dedu alichukua fomu saa 6:55 na alifuatiwa na mgombea wa Chausta, Hassan Lutegama aliyechukua saa 7:30.

Katika hatua nyingine; Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Kanda ya Kati, imewataka wagombea wote kujaza fomu za kiasi cha fedha watakazotumia pamoja na vyama vyao katika uchaguzi huo.

Mkuu wa kanda hiyo, Muhidin Mapeyo alisema fomu hizo zinatakiwa zijazwe na kurudishwa ndani ya siku saba baada ya uteuzi wa wagombea kufanyika.

“Jimbo hili gharama zake ni 80 milioni hivyo fomu zijazwe na zirudishwe kwa muda unaotakiwa,” alisema.

Vyama vinane vinavyowania Ubunge wa Jimbo la Igunga vinatarajiwa kurudisha fomu zao leo hadi ifikapo saa 10:00 jioni.Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na msimamizi wa uchaguzi leo ndiyo siku ya mwisho ya kurudisha fomu hizo kwa ajili ye uteuzi wa wagombea.

Vyama vinavyawania jimbo hilo ni CCM, UPDP, Chadema, Chausta, DP, SAU, CUF na UMD.
 
Back
Top Bottom