Uchaguzi 2020 Vyama mbalimbali vya siasa vyatoa wito kwa Polisi kutenda haki na kutopendelea Chama chochote

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Vyama vya siasa nchini vimeliomba Jeshi la Polisi kutenda haki na kutoonyesha kupendelea upande wowote kuelekea kwenye uchaguzi, ili kutunza amani na utulivu.

Kwa upande wake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, kwa kazi nzuri ya kulinda raia na mali zao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao walisema iwapo jeshi hilo litasimamia sheria, kanuni na taratibu bila ubaguzi au kubeba chama chochote cha siasa, hakutakuwa na uvunjifu wa amani utakaotokea.

Viongozi hao walikuwa wakizungumzia kauli ya IGP Simon Sirro, aliyoitoa mwanzoni mwa wiki akihojiwa na Kituo cha luninga cha ITV, ambaye aliwaonya wanasiasa wanaoanzisha shari kupitia matamshi yao.

Msemaji wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tumaini Makene, alisema CHADEMA inashangazwa namna ambavyo Polisi hawajachukua hatua kwa watu waliotoa kauli za vitisho dhidi ya mgombea urais wao, Tundu Lissu, ambazo zinaashiria shari na kutaka kuvuruga amani.

“Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alishamwandikia barua IGP ili achukuliwe hatua dhidi ya waliotaka kumuua Lissu mwaka 2017 na wanaotoa lugha za kutishia uhai wake, hadi sasa hakuna majibu na badala yake kinachozungumzwa ni kitu kingine,” alisema.

Alisema chama hicho kitafanya siasa kwa mujibu wa kanuni na sheria za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), na kwamba kampeni zao zote zitazingatia hayo na si maelekezo ya polisi.

“Kama polisi wanataka uchaguzi uwe wa amani na utulivu watende haki, waachie wananchi wafanye uamuzi kwenye sanduku la kura, kusiwe na maelekezo ya mara kwa mara kwa vyama,” alisema.

Makene alitolea mfano wa matukio ya hivi karibuni ya mgombea wa ubunge Jimbo la Ruangwa kusakwa na polisi, huku wanachama wao waliokuwa wanamsindikiza mgombea ubunge huko Mpwapwa kurejesha fomu kukamatwa.

“Jeshi la Polisi litende haki kwa vyama vyote, tunafahamu maadili na sheria na si kwa maelekezo ya jeshi la polisi,” alibainisha.

CCM YAMPONGEZA IGP

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa kimatiafa, Kanali mstaafu, Ngemela Lubinga, alisema CCM kupitia Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli, ndiyo walianza kuzungumza na kusisitiza amani na utulivu wakati wa uchaguzi.

“Sisi ndiyo tulianza Mwenyekiti wetu alishasema kampeni ziwe za amani na utulivu, vyombo vya ulinzi na usalama vilishaagizwa kuhakikisha amani na utulivu vinakuwapo wakati wote,” alisema.

“Tunamshukuru na kumpongeza IGP Sirro kwa kutimiza wajibu wake,” alisema.

ACT-WAZALENDO

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, alisema vyama vinafanyakazi kwa mujibu wa Katiba na sheria, na kwamba polisi hawafanyi kazi kwa matakwa ya mtu au chama chochote.

“Hatuna shari, tunafuata sheria, uchaguzi ukifuata taratibu, mshindi akapewa ushindi wake tutamaliza kwa amani,” alisema.

“Tukiona ushindi wetu unaporwa hapo ndiyo hatutakubali, tunachotaka haki itendeke na hiyo shari haitaonekana,” alisema Shaibu.

Kwa mujibu wa Shaibu, Jeshi ni chombo kilichopo kisheria kulinda usalama wa raia na mali zao, na kwamba kazi yao si kupendelea chama chochote cha siasa.

“Wakifanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni hakuna vurugu itakayotokea, ila kuna ushahidi kuwa litakuwa chanzo,” alisema.

KAULI YA CUF

Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Taifa wa CUF, Juma Kilaghai, alisema ni vyema polisi wakatenda haki, huku akirejea moja ya video iliyosambaa ikimwonyesha mmoja wa makamanda wa polisi akiwa kwenye mkutano wa CCM akizungumza, lakini IGP Sirro hakutoa kauli yoyote.

CUF inaangalia na ikiona kiashiria chochote italijulisha Jeshi la Polisi, mfano sasa baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi hawajui kinachoendelea wakati baadhi ya wagombea wananyimwa kanuni na nyaraka muhimu.

“Haya yote amani inaweza kuvurugika, tukikutana na hali hiyo tunaiandikia Tume, tunataka haki itendeke kwa vyama vyote kusiwe na kubeba chama chochote,” alisema.

NCCR-MAGEUZI

Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma, Edward Simbeye, alisema chama hicho hakitafanya siasa za kulichokoza Jeshi la Polisi bali zenye tija kwa wananchi zitakazostawisha amani, weledi na utulivu kwa maslahi ya nchi.

“Hatutakuwa sehemu ya kulichokoza Jeshi la Polisi na wao wasiwe chanzo cha kuvichokoza vyama vya siasa, litende haki,” alisema.

Chanzo: IPP MEDIA
 
Ccm wanampongeza igp kwa kufuata Sheria,😂😂😂 uhalisia Ni kua....wanampongeza kwa kufuata maagizo yao na kuonea vyama vingine
 
Back
Top Bottom