Vurugu zilizotokea Zanzibar hazikubaliki | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vurugu zilizotokea Zanzibar hazikubaliki

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, May 30, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 30, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Maoni ya Katuni


  Vurugu kubwa zilitokea Zanzibar juzi na jana na kusababisha shughuli za kiuchumi kusimama baada ya kile polisi wanachosema ni matokeo ya jaribio la wafuasi wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu (Uamsho) la kutaka kuvamia Kituo cha Polisi cha Mkoa Mjini Magharibi ili kumkomboa kiongozi wao anayeshikiliwa na Jeshi hilo.

  Kiongozi huyo anadaiwa kukamatwa Jumamosi iliyopita baada ya wafuasi wake kujikusanya na kufanya maandamano yasiyo na kibali cha polisi.

  Habari zilizoripotiwa kwa uzito wa juu kabisa na vyombo vya habari jana, zilisema kuwa, vurugu hizo zilianza Jumamosi majira ya jioni na kuendelea hadi juzi (Jumapili) mchana, huku wafuasi wa Uamsho wakichoma moto matairi ya magari, kurusha mawe, kuweka vizuizi katika baadhi ya barabara kuu za kuingia na kutoka katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar.

  Habari hizo zilisema kuwa wafuasi hao ambao walikuwa wameficha nyuso zao kwa vitambaa vyeupe, walisikika wakiimba nyimbo za kuukataa Muungano na aya za kumsifu Mwenyezi Mungu kwa kusema “Takbiir” na kujibiwa “Allah Akbar”, huku wakirusha mawe na kusababisha uharibifu wa mali.

  Miongoni mwa uharibifu huo ni magari kadhaa kuchomwa moto likiwemo la Askofu wa Kanisa la Assemblies of God liliopo eneo la Kariakoo, huku ukuta wa kanisa hilo nao ukiharibiwa.

  Taarifa za kipolisi pia zilisema kuwa, Kanisa Katoliki la Mtakatifu Theresa liliopo Bububu lilichomwa moto baada ya kuvamiwa saa sita usiku kufuatia vurugu hizo zilizotanguliwa na maandamano yaliyofanyika mchana bila ya kufuata taratibu za kisheria kuanzia viwanja vya Lumumba na kupitia maeneo ya Mlandege, Michenzani, Kisonge na kurejea katika viwanja vya Lumumba.

  Madhara ya vurugu hizo yameelezwa kuwa ni makubwa mno, biashara katika eneo la soko kuu la Darajani ziliathirika kutokana na kutofunguliwa kwa maduka baada ya wafuasi hao kuweka vizuizi katika barabara kuu ya Darajani na kusababisha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na kufanikiwa kulidhibiti eneo hilo kwa kuifunga barabara hiyo muhimu kwa shughuli za kiuchumi mjini Zanzibar.

  Mbali na madhara hayo, wakazi wa Zanzibar walijikuta katika wakati mgumu zaidi kwa kushindwa kutumia vyombo vyao vya usafiri, kama magari; baadhi ya watu walilazimika kuyaacha magari yao na kuyaegesha katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na kuondoka kwa miguu kutokana na njia nyingi kufungwa na kuhofia usalama wao baada ya barabara za Mlandege, Darajani na Michenzani kufungwa.

  Katika uharibifu huo baa tatu zilivamiwa na kuchomwa moto katika maeneo tofauti ya Manispaa ya mji wa Zanzibar na kuporwa fedha na masanduku ya pombe kuhujumiwa kwa kuvunjwa chupa, baa zilizotajwa kuhujumiwa ni Amani Fresh, Daraja Bovu na Amani, ambako watu wasiopungua 200 wakiwa na silaha za kienyeji walizivamia kuanzia juzi saa sita mchana.

  Tukio hili hakika ni baya, hakuna maneno mengine yanayoweza kutumika kulielezea mbali tu ya kusema ni baya na ambalo kwa hakika wanaochochea vurugu hizo hawaitakii nchi hii amani; tunasikitika kwamba wapo watu wanaosukumwa na ushabiki wa namna hii wa kueneza uhalifu ndani ya nchi kwa kisingizio cha kudai haki. Tunalaani na kuwataka wapenda amani wote wa nchi hii waungane nasi kukemea na kulaani vurugu hizi.

  Tunajua Jeshi la Polisi limesema kuwa halitakubali kuona watu wachache wanatumia haki ya msingi ya kikatiba ya watu kukutana na wengine au kujieleza kutumbukiza nchi katika janga, ndiyo maana limesema linawasaka viongozi wote waliopanga vurugu hizo ili sheria ichukue mkondo wake.

  Kumekuwa na dalili ambazo siyo nzuri jinsi vurugu hizi zilivyoendeshwa, ni kana kwamba wanalengwa watu wa aina fulani na taasisi za dini fulani, tunahisi kuwa mwenendo huu una harufu ya ubaguzi na kwa kweli ubaguzi ni mbegu mbaya sana kama ikiachwa imee na kuota mizizi katika taifa lolote lile.

  Tunajua kuwa Zanzibar ni kitovu cha utalii, ni sehemu ambao watu wengi duniani kote hutamani sana kutembea kwa sababu nyingi, lakini mojawapo historia yake; hatuamini kwamba hawa wanaoendesha vurugu hizi wanataka kuuvuruga utalii huu ambao ndiyo mkondo mkuu wa kuingiza fedha za kigeni zinazohitajika sana kwa kuendesha maisha ya wakazi wake.

  Tunasema bila kumung’unya maneno kwamba hakuna mwenye haki ya kuendesha vurugu katika nchi hii kwa sababu yoyote ile, kila mwenye shida zake, tashwishwi au kero anapashwa kufuata njia zilizoanishwa kisheria kudai haki yake; kuvamia watu wengine, kuwaumiza na kuharibu mfumo wa miundombinu na taasisi za makundi mengine katika jamii ni mambo ambayo hayakubaliki.

  CHANZO: NIPASHE

   
 2. HAZOLE

  HAZOLE JF-Expert Member

  #2
  May 30, 2012
  Joined: Feb 25, 2011
  Messages: 1,331
  Likes Received: 64
  Trophy Points: 145
  hawajitambui.
  tatizo hata uongozi wa muungano bado haujui unachofanya..... hawajasoma alama za nyakati. kama ni majadiliano kuhusu muungano yamefanyika sana but hakuna jipya coz watu hawaoni benefits za muungano si bara wala visiwani.
   
Loading...