Vunja Mbavu: Barua ya Wazi ya shabiki wa Arsenal, Yanga kwa Sa Godi

Mkazamoyo

JF-Expert Member
Sep 3, 2013
1,256
2,061
C&P From mwanaspoti
REJEA kichwa cha habari juu baba. Mimi mja wako naomba unipatie ujasiri mkubwa. Wa kuachana na ushabiki wa hizi timu baba. Wewe mwenyewe unazijua vyema baba.

Moja ipo hapo Kariakoo nyingine huko kwa Mabeberu. Zinanipa majaribu makubwa baba.
Nashindwa kuelewa ni ibilisi gani mpuuzi aliyenipa mahaba kwa hizi timu. Miaka na miaka zinanipa presha, lakini nimo tu kama zuzu.

Yaani nashindwa kula zinapofanya vibaya. Basi nimekuwa mshinda njaa kwani miaka yote, miezi yote na wiki zote zinafanya vibaya.

Timu ina zaidi ya umri wa Bibi yangu. Lakini mpaka leo haina uwanja wake. Haina duka lake la vifaa. Haina ‘jimu’ wala bwawa la kuogelea. Yaani inaendeshwa kama vikoba kwa michango na huruma ya watu. Nilinde na hili pepo la mapenzi ya kisulisuli baba.

Timu inasajili laini za chuo wao wanatuambia kuwa ni wachezaji. Mchezaji gani msimu unaisha hajacheza hata dakika tano uwanjani? Halafu wanamuita wa kimataifa. Baba niondoe kwenye hili huba la miujiza ya kiibilisi kwa kupenda vitu vya ajabu ajabu.

Alikuja Mdosi wetu akataka kuweka mzigo tutakataa. Akataka kukodisha tukagoma. Leo hii tunaishi kwa michango na sadaka kama kanisa la maombezi.

Wenzetu wamemkamata Gabachori wao wakampa timu kaweka mpunga. Wakati tulitakiwa kuwa wa kwanza.

Wakati wenzetu walimtimua Mzee mmoja aliyetaka kuleta ligi na tajiri. Sisi baba tulikuwa madubu ya akili ya kufuata akili ya vizee ambavyo siyo tu shule hamna bali hata mpira wenyewe haviujui. Leo hii timu ipo kama tambara la deki lililokauka hatuwaoni. Lakinu tajiri akija tu vinaiubuka kama senene za msimu.

Kule kwa mabeberu huko ndo kwenye shida kubwa baba. Afadhali ya hawa wenye makazi pale madimbwini. Hao mabeberu ndo nyambafu kabisa.

Mtoto wangu kazaliwa kasoma na sasa anatafuta degree ya kwanza timu haina ubingwa. Kila siku ni matatizo kama barabara ya Makongo Juu baba.

Tulidhani ubahiri wa kale kazee kavaa suti za Paris. Kenye pua iliyichongoka kama msumali wa nchi sita. Kalikosumbuliwa na zipu za makoti yake kuliko mafua. Tukakazomea tukakatimua.

Hakakautaka nongwa na sisi kakatuachia shipa letu hili sasa baba.

Tumeletewa ‘Amita Bachani’ sijui ‘Mituni Kalagabochi’ sijui. Sasa ndo tumejua kuwa ACBD inatamkwa kama Aaa Bee Chee Dee. Maana hili ndo kopo la wanzuki kabisa.

Anapanga timu kama nguo za watoto kabatini. Tumeishia kuchezea kipigo kika siku kamam vibaka wa Tandika.

Naye kapigiwa kelele wee kasepeshwa na kiingereza chake cha kibwege. Tukaona tumpe mkongwe mmoja wa timu naye ndo yaleyale. Yaani tumeipua makande kisha tukabandika magimbi. Mungu nini kosa langu hata ukafanya niwe shabiki wa hizi korosho pori?

Timu inajiri waalimu wa chekechekea kila siku sijui au matajiri ndo wana akili ya chekechea. Maana wanasajili vitoto utadhani timu imekuwa kituo cha kliniki. Tunapigwa nje tunapigwa ndani. Tunaishi kama wageni ndani ya dunia yako baba. Niokoe na jinamizi hili hata niwe shabiki wa mbio za farasi.

Tunasajili makenchi ya vituo vya mwendokasi tunaita mabeki. Tumenunua viungo vya pilau tunaita ‘midifildi visheti’. Ndo maana ikifika Xmass tu huwa tunatandikwa sana maana tuna viungo vya pilau pale kati.

Tunatafunwa tu na wenzetu. Baba sikia kilio changu hiki na utende miujiza.

Ni mimi wako katika dhambi za kujitakia kijinga. Ninayeishi Maneromango, lakini nateswa na wakazi wa London Kaskazini.

Ninayejiumiza moyo na timu ambayo inamtajirisha pimbi mmoja wa Kimarekani. Asante baba wa kupokea barua yangu. Amen.

Nimenukuu gazeti mwanaspoti toleo la Dec8, 2019 hata leo yanga na aseno bado ni walewale povu ruksa!!!!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom