Vitabu vyangu bora vya nyakati zote. Vipi vyako?

Wildlifer

JF-Expert Member
May 12, 2021
1,826
5,055
Salaam WanaJF!

Binafsi ni msomaji sana wa Vitabu. Kupitia vitabu nimejifunza mengi, nimesafiri kwenda kwingi na nimekutana na wengi. Katika Usomaji wa vitabu, kila mtu anavyo vitabu ambavyo kwake ni bora zaidi na kwa sababu zake. Kupitia uzi huu naomba tushirikishane vitabu bora kabisa kwako, hii ni njia ya kubadilishana vitabu. Hivi hapa chini ndio vitabu bora kabisa kwangu vya nyakati zote.

GUNS, GERMS and STEEL Chake JARED DIAMOND.

Hiki ndio kitabu bora zaidi nilichowahi kisoma. Katika kitabu hiki Mwanahistoria na Mwanajiografia kutoka Chuo kikuu cha California, Jared Diamond amefanya utafiti ili kujibu swali Kwanini jamii ya Wamagharibi wameendelea zaidi ya jamii zingine zote duniani. Katika utafiti wake, Diamond alikuja na majibu kuwa Maendeleo ya jamii mbalimbali duniani yameamuliwa na Mazingira wala sio ubora wa mbali(race) kama inavyoaminiwa.

Katika hoja hii, anasema kuwa hapo awali jamii zote duniani zilikuwa ni za wawindaji na wakuokotaji chakula (hunter-gatherers). Hadi kufikia miaka 11,000 iliyopita jamii kadhaa mfano za Mashariki ya kati (Fertile Crescent) na baadae China ndio zilianza ufugaji na uzalishaji wa chakula(ngano). Walianza kilimo sababu walikuwa na bahati ya kimazingira ya kuwa na mimea pori na wanyama ambao walikuwa wanafaa kufugwa. Hivyo jamii hizi zilipata faida hii ya kimazingira na hatimaye kilimo kiliwawezesha jamii hizi kuwa kubwa, sababu kilimo na ufugaji kulifanya jamii hizi zipate chakula cha kutosha na kuzaliana sana, hatimaye kuwa na watu wengi waliowezesha kuwa na majeshi, watawala na faida nyingine sababu watu wachache waliokuwa wanazalisha, iliwawezesha wengine kujikita kwenye shughuli zingine kama za ubunifu mfano uhunzi na uchongaji. Faida hii, jamii ambazo bado ziliendelea kuwa za uwindaji hazikuweza kuzipata hivyo kuachwa nyuma kimaendeleo.

Diamond anaeleza katika mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababishwa na matumizi makubwa ya ardhi huko mashariki ya kati, yalipelekea kukwama kwa kilimo, na hivyo watu wa mashariki ya kati, sababu ya kuwa kijiografia watu walio kwenye Latitude moja basi wanakuwa na hali sawa ya hewa (hivyo waliweza kuambaa kuelekea mashariki ie ulaya na afrika ya kaskazini), hivyo kueneza kilimo na hatimaye jamii za afrika ya kaskazini kama misri na ulaya nazo zilishamiri kwa kilimo na ufagaji, hatimaye kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Hivyo jamii ambazo ziliweza kuendelea kwa uzalishaji wa kilimo na ufugaji, zilipata muda wa kuwa na kundi la wabunifu waliotengeza dhana za chuma (Steel) na baadae Bunduki (Guns)]ambazo ziliwezesha kilimo kukua na dhana za vita zilizowezesha kufanya uvamizi wa jamii ambazo hazikuwa zimeendelea. Mfano Hispania chini ya Pizzaro walikuwa wameendelea sana in terms of steel tools na farasi, na kuwawezesha kuiteka na kuitalawa Cajamarca (Peru ya leo).

Jambo lingine muhimu ni kuwa, jamii za wafugaji kibaolojia zilikuwa zimetengeneza kinga kubwa ya magonjwa kutokana na kuishi na wanyama karibu. Walipoenda jamii ambazo hawakuwa wafugaji, waliwapelekea vimelea (Germs) ambavyo ilikuwa ni silaha ya kibaolojia (bila ya wao kujua) na iliwaua wenyeji kwa kiwango kikubwa sana. Hii ilitokea wahispania walipovamia Peru, America (Small Pox) na wazungu pia walipofika Kusini mwa afrika.

Hivyo, Diamond anasema kuwa maendeleo duniani yamekuwa hivi yalivyo leo kwa sababu ya Jiografia. Kitabu hiki kilitoka mwaka 1999, na kilishinda Tuzo ya Pulitzer.

2017-06-27-11.30.15-e1498560008434-scaled.jpg


PRINCE cha NICCOLO MACHIAVELLI.

Kitabu hiki kilichapwa mwaka 1532 (karne ya 16) na mwanasiasa na mwanafalsafa wa kiitaliano Niccolo Machiavelli. Katika kitabu hiki Machiavelli anaelezea ni mbinu zipi mwanasiasa au mtawala azitumia katika kuyatafuta na kuyadhibiti Mamlaka ya kisiasa. Machiavelli, alikuwa kiongozi kwenye serikali ya Italy (Florence), lakini baadae familia iliyotawala kwa miaka mingi ya Medici, ilirudi madarakani na Machiavelli kutolewa serikalini na hatimaye kufungwa. Alipokuwa uraiani, ndipo alipoandika hiki kitabu, kama njia ya kujikomba kwa Mtawala wa Florence, Lorenzo de Medici. Machiavelli alisema kuwa, watu wengi huwapa zawadi watalawa za mali kama farasi, ila yeye zawadi bora ya kujipendekeza aliona ni MAARIFA. Ndipo akaandika kitabu hiki.

Kitabu hiki kimepata ukosoaji mkubwa kwa kuwa kinaleza zaidi mbinu ambazo pia ni hasi (kama kueneza utawala wa kimabavu), lakini binafsi nakiona kama ni kitabu kilichoelezea mambo halisia, kwani mbinu hizo za madaraka zinatumika hadi leo na watawala madikteta na wasio madikteta. Humu anaelezea njia za kupata madaraka, jinsi ya kudeal na wapinzani, Umakini katika kuunda mashirikiano, na jinsi gani ya kuwa na jeshi imara. Pia anaeleza sifa na mienendo ambayo mtawala anapaswa kuwa nayo, mfano anasema mtawala kama huwezi kuwa na vyote basi ni vyema uogopwe kuliko kupendwa, kwani heshima na mamlaka yapo kwenye kuogopwa kuliko kupendwa. Pia, Machiavelli anaisistiza kwa mtawala ni elimu kuhusu Majeshi na vita. Jeshi na ulinzi imara ndio usalama wa nchi. Mtawala anapaswa kuwa yeye binafsi physically fit, ajue skills and military discpline, awe mjuzi wa jiographia na aboreshe jeshi lake hasa wakati wa vita. Wananchi wengi huwa na utulivu pale wanapojua wana jeshi imara.

Kwenye kitabu hiki, pia anaeleza namna mbalimbali za utawala na jinsi zinavyokuwa, mfano anaelezea kuhusu Composite Principalities. Hii ni utawala mpya lakini uko attached na wa zamani. Anasema kunatokea natural difficulty. Pale waliopambana kumuweka mtawala madarakani mambo kwenda kinyume na walivyotarajia na pili mtawala mpya kujihisi anadeni kwa aliopigania nao utawala. So hapa Prince (mtawala) anakua na maadui wawili, kundi la kwanza ni wale aliowajeruhi katika kusaka madaraka na pili ni wale aliopambana nao kutafuta madaraka lakini hawezi watimizia watakacho na hawezi pia kuwaendesha sababu amepambana nao pamoja, so he feel in less control to them.

King Louis XXII quickly occupied Milan, and as quickly lost it; this was because those who had opened the gates to him to power, finding themselves deceived in their hopes of future benefit, would not endure the ill-treatment of the new prince, so they battled against him.

Machiavelli anashauri kuwa ili kufanikiwa katika mazingira hayo, Prince ni lazima afanye mambo yanayopendeza raia wake lakini busara zaidi ni kudeal na wale waliomuweka madarakani ili kuimarisha zaidi utawala wake. So, katika eneo hili Machiavelli anahimiza matumizi ya vyombo vya dola , kutumia kila nafasi inayojitokeza kudeal na adui zake (ikiwemo aliopambana nao kuingia madarakani) na kuipanga mamlaka katika namna ambayo kwake ni rahisi kuicontrol na kudhibiti.

Kimsingi, Machiavelli alikuwa na Muono kuwa [nami nakubaliana nao], [all] political battles, are not moral but are more of board game with established rules and that politics has always been played with crime, deception and treachery. He also contend that, [if] intention and results are beneficial, then a ruler who is establishing a kingdom or a republic, and is criticized for his deeds, including violence, should be excused. Unaweza tazama utawala wa Tanzania, kwa maraisi wote, hata dunia kwingine, kuwa minyukano ya kisiasa haina uungwana.

220px-Machiavelli_Principe_Cover_Page.jpg



PRISONERS OF GEOGRAPHY Chake TIM MARSHALL.

Tim Marshall ni Mwandishi wa habari wa kiingereza ambaye amefanya kazi maeneo mbalimbali duniani hasa mashariki ya kati akireport kwenye vyombo kama Sky News. Ameandika vitabu kadhaa lakini binafsi hiki ndio bora zaidi kutoka kwake. Kitabu hiki kimetoka mwaka 2015. Hoja yake kuu kwenye kitabu hiki ni kuwa, siasa na mahusiano ya kimataifa duniani kote yanaamuliwa na jambo moja kwa nguvu zaidi, nalo ni jiografia. Kwenye kitabu hiki, ameelezea maeneo kumi duniani ambayo ameelezea asili yake, mahusiano yake na dunia, Maendeleo yake, vikwazo vyake na hatma yake kwa kiasi gani vimefungwa na jiografia zao. Maeneo haya ni Urusi, China, Marekani, Ulaya magharibi, Afrika, Mashariki ya kati, India na Pakistan, Korea na Japan, Latin America na Arctic. Mfano, kuhusu Urusi. Mfano, kuhusu Urusi, Tim anaeleza kuwa inahasara mbili za kijiografia. Moja ni kutokuwa na bandari ambazo zina maji moto muda wote wa mwaka. Akimaanisha kuwa bandari nyingi za Urusi, zina maji ya barafu ambazo muda mwingi wa mwaka zinakuwa zimeganda. Hasara kubwa ya bandari za namna hii zinazuia shughuli wakati wa miezi ya baridi. Inaongeza gharama zaidi kwa kuwa na Icebreakers. Hivyo Urusi bandari anayoitegemea zaidi ni Savastopol, iliyopo Crimea na faida yake kubwa zaidi ipo upande wake wa kusini ambapo inampa access na Black sea, ambayo ndio nguzo yake kijeshi. Hivyo, baada ya Ukraine kuanza kuwa na uelekeo mkubwa kwa Marekani, Urusi hakua na namna zaidi ya kuivamia Crimea na kuiweka chini ya himaya yake.

Pia humu anaelezea eneo la Mashariki ya kati kwa mtazamo wa kijiografia na inavyochangia migogoro ya eneo hilo. Maeneo haya ya mashariki ya kati yako na waislam walio katika madhehebu ya shia na sunii ambayo yako na migawanyiko mingi zaidi ambapo kimakazi toka zama za kale walikuwa wameundwa na mipaka ya kijiografia kama milima au mito ambayo ndio iliamua utawala uweje. Waingereza walipochora mipaka kwenye Sykes-Picot Agreement, hawakuzingatia uhalisia huu wa kijiografia na kuwaweka pamoja watu ambao hawakuzoea kukaa pamoja na kuongozwa na watu wasio na utashi nao kiimani. Mfano Uturuki, inapambana na wakurdi ambao wanataka wawe na utawala wao wenyewe wa Kisunni na wenzao waliopo Iraqi na Syria. Hatimaye imezaa migogoro ya kidini ambayo imekuzwa na uwepo wa mafuta eneo hilo na kuwafanya mataifa ya magharibi kama Marekani na Uingereza kushamirisha migogoro hiyo. Pia eneo lingine nililolipenda ni kuhusu Marekani na China. Kuhusu Marekani, Tim anahoja kuwa Marekani bado ataendelea kuwa global super power kwa karne ijayo, kwa sababu ya faida za kijiografia alizonazo. Kwanza hadi kufiki 2027 atakuwa amejitegemea kwenye nishati, hivyo hatakuwa na utegemezi kutoka maeneo mengine, pili bado anafaida ya kuwa bahari mbili pembeni yake Atlantic na Pacific ambapo ni warm mwaka mzima. Hii inampa faida ya kuendelea kuwa Naval Power (kigezo muhimu cha kuwa global superpower), kitu ambacho kwa mchina hana. China anahasara ya kuzungukwa Na mataifa yenye kumpa changamoto ya matumizi ya bahari ya kusini mfano Japan. Pia anapakana na India ambaye ni mshindani wake mkubwa, jambo ambalo kwa Marekani ana faida ya kutokuwa na washindani jirani yake. Pia nchi ya China ni moja ya mfano wa kwanini Jiografia inafanya mataifa yasitake kuyapoteza au kuyapa uhuru baadhi ya maeneo(kama ilivyo kwa Zanzibar hapa kwetu), mfano Tibet. Tibet ndio mnara wa maji wa China ulipo. Tibet ndio ilipo plateau, ambayo ndio chanzo cha mito mitatu mikuu inayoendesha uchumi wa China Yellow, Yangtze na Mekong. Kuipoteza Tibet ni sawa na china kujipoteza mwenyewe, hawezi kubali. Na kwa Marekani ataendelea kuitia Chokochoko maeneo kama Tibet ili yaweze kuwa na vuguvugu la kujitenga yote haya yatamkwamisha China kutulia na kumpa faida zaidi Marekani ya kuendelea kuwa global superpower.

Kimsingi, kama unataka kuzielewa Geopolitics, basi hiki ni kitabu cha kusoma. Kina lugha rahisi, hakina blah blah za kupoteza muda, ametumia ramani na kina uzoefu wake binafsi mwandishi katika maeneo hayo.
910UbuyEEHL.jpg


HOW TO RIG AN ELECTION kimeandikwa na NIC CHEESMAN na BRIAN KLAAS.

Kitabu hiki kinaelezea mbinu mbalimbali zinazotumika kuiba uchaguzi duniani. Humu ameeleza kihistoria, kwa mifano mbinu sita ambazo zimekuwa zikitumika kuiba uchaguzi. Mbinu hizi ziko katika kutumia vurugu, sheria, mifumo ya kidigitali na mipaka ya uchaguzi. Mbinu ya kwanza ilioelezwa ni kuiba Uchaguzi bila 'kushtukiwa'. Hii ni mbinu ambayo uchaguzi unaibwa kabla ya upigaji kura. Mfano, ni kuengua wagombea kwa vigezo vya kisheria. Au mbinu kama kuweka wagombea ambao watachanganya wapiga kura. Mfano, mwaka 1998, St Petersburg kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, Governor Vladimir Yakovlev alikuwa akibaliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa Oleg Sergeyev aliyekuwa ni Mwandamizi kwenye masuala ya Taasisi za Pensheni. Njia waliyotumia kupunguza kura za Sergeyev, ni kuweka mgombea mwingine mwenye jina kama hilo, na kuchukuliwa 'muhuni tu' wa mtaani mwenye jina la Oleg Sergeyev. Ilifanikiwa, maana wapiga kura hawakujua yupi ni yupi. Mbinu zingine ni kama Rushwa na kununua wapiga kura na wagombea iliyotumika sana Uganda, matumizi ya vurugu, kuhack mifumo ya uchaguzi, kutoa habari za uzushi na kudanganya matokeo, kubadili matokeo baada ya kuhesabu na mwisho ni chaguzi za kuwalaghai jumuiya ya kimataifa. Kwenye kitabu hiki, jambo moja interesting ni kuwa mbinu za kuiba na kuvuruga uchaguzi zinazotumika leo duniani, nyingi chanzo chake ni Ulaya na Marekani. Marekani ndio kinara wa wizi wa uchaguzi kwa kutumia 'akili'. Mfano Gerrymandering. Mbinu hii ilianza karne ya 18, ambapo Mmarekani Elbridge Gerry alitumia mbinu ya kuvuruga mipaka ya eneo la upigaji kura ili kutafuta ushindi. Mbinu hii imetumika hadi leo nchini mwetu ambapo maeneo ambayo CCM imekuwa ikiona ina dalili za kupoteza jimbo, basi huligawa na kutoa majimbo mawili la mjini na vijijini na hatimaye hubaki na jimbo moja lao.

How-to-Rig-an-Election-cover.jpg


ALCHEMIST cha PAUL COELHO.

Riwaya hii imetoka mwaka 1988, ikielezea kisa cha Kijana mchungaji wa Andalusia(Hispania) kuhusu safari yake ya kwenda kutafuta utajiri huko misri. Dhima kuu ya Riwaya hii ni hamasa ya mtu kutafuta ndoto zake kwa kuzingatia kile moyo wake unatamani huku ujumbe mkuu ni kuwa, Mafanikio katika ndoto yako ndani ya mtu mwenyewe binafsi. Mafunzo makuu niliyoyapata kwenye Riwaya hii ni kuwa, Furaha ya kufanya jambo ni kuhakikisha unalifanya lile ambalo moyo na nafsi yako inataka, pili unachokitaka kufanya, fanya kwani dunia itaungana kukusaidia kufanya. Maana yake ni kuwa unapofanya jambo fulani utakutana na watu, mazingira na matukio ambayo bila hata kutegemea yatakusaidia kutimiza. Tatu ni kuwa mambo yote unayoyataka, basi yamekwisha pangwa (maktub), hili ni suala la imani zaidi. Na nne ni kuwa, mambo yote muhimu katika maisha yatazame kwenye mambo madogo madogo. Ni mambo madogo madogo ndiyo yenye kuleta maana na mabadiliko.
71aFt4+OTOL.jpg


A SHORT HISTORY OF NEARLY EVERYTHING cha BILL BRYSON

Dunia imeshuhudia tafiti na gunduzi nyingi za kisayansi. Kuna vitabu vingi ambavyo vinaelezea historia ya mambo hayo. Ila kitabu hiki kimeelezea kwa ufupi juu ya masuala haya. Kimejitahidi kujibu maswali mengi kuhusu masuala ya sayansi. Mfano, ni kwa nini Mbu licha ya kufyonza damu ya mwanadamu, hawezi kuambukiza Ukimwi. Kitabu hiki kimetoka mwaka 2003, kinastahili muda wako.

9781784161859.jpg


MOHAMED ALI: HIS LIFE AND TIMES cha THOMAS HAUSER.

Wakati Muhamad Ali akipigana ngumi sikuwa nimezaliwa, lakini ni mwanamasumbwi ninayemuhusudu zaidi duniani. Kubwa zaidi ni kuhusu misimamo yake. Maisha yake yanagusa mengi, harakati za Haki za kibinadamu Marekani, vita Vietnam, Uislam ndani ya Marekani, Ubaguzi wa Rangi, Mahusiano ya Uislam, Ukritso na Utumwa nchini Marekani, masuala ya kidiplomasia na dunia ya masumbwi kwa ujumla kama biashara ilivyo, figisu zake mapromota, siasa ndani yake. Yote haya unaweza yapata ndani ya kitabu hiki.

51WVd9djHfL.jpg


ALEX FERGUSON: MY AUTOBIOGRAPHY Cha ALEX FERGUSON.

Ushabibiki na Unazi wa Mpira kwangu ulipotea miaka ya 2010, nikiwa mshabiki mkubwq Arsenal. Lakini, nilikuwa navutiwa sana na mpira wa harakati (Old English football style) ya Manchester United. Kikosi chao kilikuwa kikinivutia sana, kina David Beckham, Ryan Giggs, Paul Scholes(my fav footballer wa Man U), Roy Keane n.k. Lakini Kocha wao Alex Ferguson alikuwa akinivutia sana. Nilipokisoma hiki kitabu, mwaka 2015, nilijifunza mengi kuhusu Historia ya Man U, biashara ya Mpira Uingereza, mikimiki ya mpira wa Uingereza na hasa mikwaruzano kama ya David Beckham na Ferguson, au Jose Mourinho na Fergie. Hiki ndio kitabu bora cha Michezo changu cha wakati wote.
Screenshot_20210723-153433.png


LIFE 3.O BEING HUMAN IN THE AGE OF ARTIFICIAL INTELLIGENCE Cha MAX TEGMARK

Max Tegmark ni Mmarekani aliyebobea kwenye utafiti wa Masuala ya Jinsi mashine zinavyopata utambuzi. Tunajua kuwa wanadamu kihistoria na kibaolojia ndiye kiumbe Smart kuliko viumbe wote. Lakini mashine hivi sasa zimeanza kuwa na uwezo huo wa kibinadamu kufanya utambuzi kwa kuwa na akili bandia, Artificial intelligence. Tafsiri yake ni kuwa mashine inakuwa na uwezo sawa (baadae zaidi ya mwanadamu) je Maisha yatakuwaje? Vita, kazi, imani, uzalishaji, mapenzi vyote vitakuwa na sura gani katika zama hizo. Hivyo katika kitabu hiki Tegmark anaelezea, kwa mashaka, AI itaathiri vipi maisha ya mwanadamu. Hiki ndio kitabu changu bora zaidi kuhusu Artificial intelligence. Kitabu hiki kilichapwa mwaka 2017.

512e828a4140b74088a11c6a26976351.jpg

POPE AND MUSSOLINI: THE SECRET HISTORY OF PIUS XI AND THE RISE OF FASCISM IN EUROPE Kimetolewa mwaka 2014 na DAVID KERTZER.

Kitabu hiki pia kilishinda tuzo za Pulitzer. Kwa kanuni za kawaida za kimaadili, kanisa au msikiti unategemewa kusimama katika misingi ya haki na kukemea dhulma, uonevu, matumizi mabaya ya madaraka na mauji. Historia imeshuhudia watawala dhalmu na katili kama Benito Mussolini wa Italia miaka ya 1930. Kikanuni, haitegemewi taasisi ya dini iwe na mahusiano na mtawala kama huyu. Lakini katika mazingira ambayo kanisa liko na hali mbaya kifedha, limewekewa mazingira magumu ya kisheria kufanya kazi na linakandamizwa na dola na kutamani kurudi kwenye hali ya kawaida ya ustawi, kanisa katoliki chini ya Papa Piusi wa 16, liliweza kuweka misingi kando na kusaidia utawala wa kifashisti wa Benito Musolini kuweza kusimama na kuungwa mkono bila kujali udhalimu wake huku kanisa likipata maslahi ya kifedha, unafuu wa kufanya kazi na kustawi zaidi.

Kitabu hiki, ni ushahidi na somo kuwa taasisi za dini ni nyenzo na mdau mkubwa wa mtawala ambao hutegemeana na hukingana pale wanapotaka kila mmoja kutimiza ayatakayo.

91SFNNJar1L.jpg


KING LEOPOLD GHOST: A STORY OF GREED; TERROR AND HEROISM IN COLONIAL AFRICA cha ADAM HOCHSCHILD, 1998.

Ukoloni ni mada maalumu unapozungumzia Bara la Afrika na historia yake. Lakini historia hii ina pande mbili. Pande inayoelezwa zaidi ni ile yenye mtazamo wa Kimagharibi kuwa, wakoloni walikuja kuistaarabisha Afrika kama kueneza dini, na mila 'nzuri' na kukomesha utumwa. Historia ya pili ni kuhusu uhalisia wa nini hasa kilifanywa. Kitabu hiki cha Adam, ni uhalisia wa nini hasa wakoloni walikifanya Africa. Ukiukwaji wa haki za binadamu, mauji, wizi wa rasilimali, utumwa ambavyo vilipekea mamilioni ya waafrika kupoteza maisha, kupoteza mifumo yao ya maisha na uzalishaji huku vikiitajirisha bara la ulaya kwa kasi na kiwango kikubwa sana cha Maendeleo. Kitabu hiki kinaelezea madhira yaliyofanywa na utawala wa Mfalme Leopold II wa Ubelgiji huko Kongo. Kimeelezea ukoloni wao kutoka 1880s hadi miaka ya 1980 na jinsi hadi sasa makampuni makubwa ya kibelgiji, kifaransa na Kimarekani yanaendelea kuinyonya Kongo na kupandikiza watawala wao kama Mobutu Seseko na kuwapoteza wazalendo kama Patrice Lumumba. Hii ndio historia halisi ya Ukoloni Afrika.
51aRi4OPVnL.jpg


ADILI NA NDUGUZE cha SHABANI ROBERT.

Mara ya kwanza nilisikia simulizi hii Radio Tanzania, bado nikiwa kijana mdogo miaka ya 1990. Nilikisoma tena miaka 2000 katika hatua tofauti tofauti za kimasomi. Mafunzo yake hadi leo ninayahusudu sana. Hii ni Riwaya iliyotoka mwaka 1952, ikielezea kisa cha kijana Mkarimu, na mwenye upendo mkubwa kwa nduguze (Hasidi na Mwivi) ambao walinfanyia visa na vitimbi vingi vya Husda, chuki, tamaa, majaribio ya kumuua kuliko sababishwa tu na tabia zao za kupenda starehe na anasa, tamaa za mali. Mafunzo makuu ya kitabu hiki ni jinsi gani ya kuishi na ndugu kwa tahadhari. Kitabu hiki pia kina mafunzo mengi ya siasa na uongozi katika ngazi mbalimbali kama familia.
54155688._SY475_-1.jpg


A KNIGHT IN AFRICA: JOURNEY FROM BUKENE cha ANDY CHANDE.

Kitabu hiki kimetoka mwaka 2005 kikielezea safari yake ya maisha Andy Chande kutoka kuzaliwa kwake, kukua kwake Bukene, Nzega Tabora, hadi kuja kuwa Kiongozi wa Jumuiya ya Freemason Afrika Mashariki.

Katika safari yake hii ina mafunzo mengi sana ambayo ni ngumu kuyapata darasani. Mfano, amegusia chimbuko la jumuiya ya wahindi hapa nchini na afrika mashariki. Kuna sura kuhusu harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Katika sura hii ameelezea mbinu za kidiplomasia za Nyerere kudai uhuru na mashirikiano ya jamii mbalimbali kama wahindi na pia waafrika katika harakati hizo. Ameelezea pia mapinduzi ya zanzibar na madhila waliyopitia jamii ya wahindi na waarabu waliouawa katika mapinduzi hayo. Kuna sura kuhusu utawala wa Nyerere. Hapa kuna mambo matatu, moja ni Juhudi za Nyerere kujenga taifa moja. Hapa anaelezea Nyerere alivyosimama kidete kupinga sera ya kuwabagua wazungu, wahindi na waarabu (Afrikanaizesheni) iliyokuwa miongoni mwa wana TANU. Unaona kwanini Nyerere alilazimika kuchukua hatua za kidikteta kama kufuta vyama vingi, kuanzisha sheria ya kuweka watu kizuizini bila kushatakiwa, na kufuta vyama vya wafanyakazi kwa kuviweka chini ya usimamizi wa Serikali yake, kufuta utawala wa kichifu na kusimika kiswahili-kwa hili akifanikiwa kujenga umoja wa kitaifa, Pili anaelezea Ujamaa wa Tanzania na kufeli kwa sera ya utaifishaji kukuza uchumi. Chande anaeleza humu kuwa, uchumi chini ya Nyerere ulikwama kwa sababu tatu, moja ni kuwa tulifungamana na nchi zilizokuwa hoi kiuchumi kama China, pili vijiji vya ujamaa viliharibu mifumo ya kiuchumi ambayo tayari ilikuwa inafanya kazi na tatu utaifishaji uliwapa biashara watu wasio na ujuzi wa kuendesha biashara kama yeye alinyanganywa kiwanda na kuwa chini Mkuu wa wilaya mstaafu. Tatu anaelezea mchango wake katika mashirika ya umma wakati wa Nyerere baada ya kupokwa kiwanda, mfano anaelezea alivyopambana bila msaada wa kifedha wa serikali kulirudisha fuvu la mtu wa kale lilochukuliwa na Dr Leakey na kupelekwa Ulaya. Anaelezea Utawala wa Mwinyi ulivyofungua milango ya uchumi wa soko, na jinsi gani Utawala wa Mkapa ulivyojenga taasisi za kiuchumi. Pia kuna sura mahususi anaelezea kuhusu ufrimason. Sura hii amejibu dhahania nyingi kuhusu ufrimason, ameelezea kwanini unafanywa siri, jinsi ya kujiunga na kupinga dhana kuwa ufrimason unatoa kafara na utajiri. Ni kitabu kizuri kuhusu historia ya Tanzania.

1340359722.0.x.jpg


HARAKATI ZA JORAM KIANGO vitabu vya BEN MTOBWA

Hivi ni vitabu kuhusu mpelelezi Joram Kiango katika kupambana na uhalifu mbalimbali nchini Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla. Ni vitabu ambavyo vingu viko kipindi cha vuguvugu la uhuru wa afrika miaka ya 1960 hadi 1990. Ni riwaya zinazohamasisha Uzalendo wa kiafrika.

54155688._SY475_-1.jpg


VITABU VYA WILLY GAMBA Vyake ELVIS MUSIBA.

Ni kama vya Joram Kiango, lakini hivi ni kuhusu jasusi Willy Gamba na harakati za kupambana na madhira ya mkoloni hasa kaburu barani Afrika. Riwaya hizi zinaelezea Misheni mbalimbali alizitekeleza jasusi huyu katika Afrika. Mfano, ni ile ya kupambana na Vikundi vya kigaidi vya Kaburu wa Afrika kusini huko Kongo, vilivyokuwa vikiuua viongozi wa wapigania uhuru wa afrika katika kisa alichokiita Kikosi cha Kisasi.

DSC_1885.png


HISTORY OF GOD: A 4,000 QUEST OF JUDAISM, CHRISTIANITY AND ISLAM cha KAREN ARMSTRONG.

Nadhani kuna kosa moja juu ya jina ka hiki kitabu, Kitabu hiki hakielezei Historia ya Mungu, bali kinaelezea Historia ya dhana ya Mungu. Hivyo nadhani kilipaswa kuitwa HISTORY OF GOD AS A CONCEPT. Mengine yapo kama yalivyo, muandishi ameelezea kwa kina mitazamo mbalimbali kuhusu ni nini Mungu na ilivyokuwa ikibadilika kwa nyakati na mazingira tofauti hadi sasa. Ameelezwa Chimbuko la dini kuu tatu za Ukristo, Uislam na Uyahudi na mazingira ambayo dini hizi zilianzia. Pia ameelezea hatima ya mitazamo ya watu kuhusu Mungu.
712WZC2izHL.jpg


1374427_20160502_174612.jpg


WHEN THERE IS NO DOCTOR cha DAVID WERNER.

Mama yangu alikuwa nesi, hiki kitabu alikuwa nacho nyumbani. Ni kitabu ambacho kinatoa muongozo wa magonjwa mbalimbali yale ya 'muhimu', dalili zake na matibabu yake. Kilitolewa miaka ya 1990 mwanzoni kabisa na David Werner, ambaye ni mtaalamu wa Afya ya jamii, ambaye kwa miaka mingi amefanya kazi ya kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya akiwa zaidi vijijini katika nchi zaidi ya 50 'maskini'. Nchi hizi, kwa ambao tumekaa vijijini, tunajua zina sifa moja, kumpata Daktari ni sawa na kutafuta sindano porini. Nadhani kwa uzoefu huu, ndipo Werner aliona umuhimu wa kuandika kitabu ambacho mtu anaweza kujitazama dalili zake na kujua nini hasa anachoumwa na afanye nini ili walau kupata ahueni ya haraka huku zikifanyika jitihada za kusafiri kwenda kumtafuta Daktari, ambayo kwa kawaida ni nje ya kijiji. Pia amependekeza dawa ambazo mtu anaweza zitumia. Lakini pia amependekeza dawa ambazo ni za kawaida katika mazingira ya nyumbani. Mfano, kutumia mchanganyiko wa maji ya vuguvugu na chumvi, kusukutua ili kutibu fizi iliyovimba. Nimekua na hardcopy, ila teknolojia ishukuliwe, sasa kuna softcopy.

View attachment 1875004

View attachment 1875005
 
View attachment 1864683
Usawa katika pato la taifa, umegawanywa kimatabaka. Hiki kitu si rahisi kukuta wakizungumzia lakini ni topic nyeti sana ambayo bila kuangaliwa kwa jicho la tatu, inaweza pelekea umaskini wa kizazi hadi kizazi.
Sijawahi kifahamu. Tony ametoa strong proposals, i've put it in my TBR List. Thanks!
Screenshot_20210723-163155.jpg
Screenshot_20210723-163136.jpg
 

Attachments

  • Screenshot_20210723-163209.jpg
    Screenshot_20210723-163209.jpg
    75.6 KB · Views: 56
Things fall apart
The river between
Mine boy
No longer at ease
Song of Lawino and Song of Ocol
Is it possible
The African child
Passed Like a shadow
Mabala The farmer
Hawa the bus driver

Nakumbuka nilikuwa napenda sana Literature. Siku moja nikamfuata mwalimu kumuuliza 'What career should I pursue?' akanijibu nakuona kuwa mkalimani au mkutubi. Dah!
 
Things fall apart
The river between
Mine boy
No longer at ease
Song of Lawino and Song of Ocol
Is it possible
The African child
Passed Like a shadow
Mabala The farmer
Hawa the bus driver

Nakumbuka nilikuwa napenda sana Literature. Siku moja nikamfuata mwalimu kumuuliza 'What career should I pursue?' akanijibu nakuona kuwa mkalimani au mkutubi. Dah!
Ulifuata maono hayo kaka?
 
Things fall apart
The river between
Mine boy
No longer at ease
Song of Lawino and Song of Ocol
Is it possible
The African child
Passed Like a shadow
Mabala The farmer
Hawa the bus driver

Nakumbuka nilikuwa napenda sana Literature. Siku moja nikamfuata mwalimu kumuuliza 'What career should I pursue?' akanijibu nakuona kuwa mkalimani au mkutubi. Dah!
Things fall apart, Okonkwo. Moja ya Riwaya nzuri sana. Na ina filamu yake pia.
 
38 Reactions
Reply
Back
Top Bottom