Vita ya ukabila na tishio jipya kwa usalama Tarime, Rorya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vita ya ukabila na tishio jipya kwa usalama Tarime, Rorya

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Jun 2, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jun 2, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Na Dinna Maningo,Tarime

  MOJAWAPO ya matatizo kadhaa ambayo yamekuwa yakiusumbua mno Mkoa wa Mara ni uhasama na vita baina ya koo na makabila.

  Hata hivyo, juhudi mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na Serikali, taasisi na asasi mbalimbali katika kukabiliana nayo au kujaribu kuyapunguza.

  Kwa kiasi kikubwa, Jeshi la Polisi limetumika katika kukabiliana na hali hiyo, kiasi kwamba jeshi hilo limejikuta likilazimika kuanzisha Mkoa wa Kipolisi wa Tarime na Rorya ili kuweka karibu huduma za ulinzi na usalama kwa wananchi.

  Lakini, kabla ya kuanzishwa kwa mkoa wa huo mwaka 2009, wilaya za Tarime na Rorya zilikabiliwa na mapigano ya mara kwa mara ya koo.

  Chanzo cha mapigano hayo kinaeleza kuwa ni wizi wa mifugo na migogoro ardhi na mipaka.

  Mapigano hayo yamesababisha athari kwa jamii kwani wapo waliouawa , wengine kupata ulemavu wa kudumu, pia wengine nyumba na mashamba yao kuchomwa moto na mazao kuharibiwa.
  Hali hiyo ilirudisha nyuma maendeleo ya wananchi katika maeneo hayo.

  Mapigano hayo ya koo yaliyowahi kutokea mwaka 2008 ni ya koo za kabila la Wakurya, baina ya Wanchari na Warenchoka (2008),Wanchari na Wakira(2008),Wanyabasi na Wairege(2009),Wamera na Wahunyaga(2009),Wahunyaga na Wasweta(2009) pamoja na Wamera na Waluo.

  Baada ya kuanzishwa kwa mkoa wa kipolisi waTarime Rorya ukiongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Constantine Massawe, ambaye amehamishiwa Tanga hali ya mapigano ilipungua hadi Mei 4 mwaka huu yalipoibuka tena mapiganyo hayo baina ya Waluo na Wakurya wa jamii ya Warenchoka.

  Uchunguzi unayonyesha kuwa mapigano ya sasa yametokana na tatizo la migogoro ya ardhi pamoja na tatizo la ukabila..

  Tatizo la kuwepo kwa ukabila baina ya Waluo na Wakurya ndani ya mkoa huu wa kipolisi wa Tarime/Rorya umekuwa ukiendelea kudumishwa na baadhi ya watu wa makabila hayo, jambo ambalo limekuwa likisababisha kuzuka upya kwa mapigano baina yao.

  Tukio la Mei 4 mwaka huu la mapigano baina ya Waluo, wakazi wa Ikoma, Kata ya Ikoma wilaya ya Rorya na Wakurya, waishio Nyamuhonda, Kata ya Mwema Wilayani Tarime yameibua upya hisia za chuki ambazo zilikuwa zimetoweka.

  Kuwepo kwa ukabila kwa watu hao umesababishwa na kuwepo kwa tatizo la umilikaji wa radhi ambapo kabila hili ili linasema wao ndio wamiki halali wa ardhi huku lingine ilikisema wao ndiyo wanapaswa kuwa wailiki halali wa ardhi.

  Hali hiyo imesababisha kutokea kwa mapigano yaliyoharibu mali za wananchi, mazao kuchomwa moto na wengine kujeruhiwa.
  Baada ya kutokea kwa mapigano hayo ya siku moja, uchunguzi wa Mwananchi katika vijiji vya Ikoma na Nyamuhonda katika wilaya hizo mbili umeonyesha kuwa sababu ya kuzuka upya kwa mapigano hayo ni mgogoro wa ardhi.

  Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Girago Lucas (28), mkazi wa kitongoji cha Nyantacho, kijijini Ikoma, Wilayani Rorya anaelezea jinsi tukio hilo lilivyokuwa.

  “ Tukio limetokea Mei 4 usiku wakati tukio limetokea mimi nilikuwa kwa baba yangu katika kijiji cha Ikoma, wakati narudi nikakuta nyumbani kwangu kunawaka moto, nikajibanza katika giza nene na kuona watu kadhaa wamesimama na wengine wako mbele wanaondoka.

  Baadhi yao wakiwa wamebeba mali na vitu mbalimbali kutoka kwangu, sikuweza kuwazuia, wangenidhuru, anaeleza Lucas ambaye asili yake ni Mluo wa ukoo ya Suba.

  Anaongeza: ” Bahati nzuri mke wangu na mtoto walifanikiwa kukimbia baada ya hapo nilipiga kelele, lakini sikupata msaada kwa wakati huo kwani majirani wenzangu nao walikuwa wamevamiwa wakachukuwa plau (jembe la kulima kwa kukokota na ng’ombe),wakachukua pia baiskeli,redio,gunia la mahindi, nguo, kuku 30, godoro na vyombo mbalimbali.

  " Niliwatambua watu watatu kati yao ambao ni wakazi wa Nyamuhonda, ambao ni Wakurya kwa sababu ya mwanga wa nyumba iliyokuwa inawaka moto."

  Lucas anaongeza kuwa baada ya muda walikutana ana wenzao walipiga yowe wakaanza kufukuzana kwa mikuki ambapo baadhi yao walijeruhiwa na kujipatia tiba kwa siri kwa kutumia miti shamba hawakutaka kwenda hospitali kwa kuhofia kukamatwa na polisi ambapo baada ya muda wakapiga simu polisi ambao waliwasili mahali hapo saa 5 usiku kutoka kituo cha Sirari.

  “Wakati tunampigia simu OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya), watu hao walikuwa kwa jirani yangu aitwaye Nyapura Nyamhanga, ambako nako walipora vitu vyote, wakaiba pia na kuku na kukatakata mabati yaliyoezekezea paa la nyumba yake.

  "Kwa kweli kulitokea mapigano na watu kadhaa wakajeruhiwa, lakini huku huwa hawaendi hospitali wanajiganga kwa sabau ili upate tiba hospitalini ni lazima uwe na PF3 kutoka polisi, wao hawaendi polisi wanahofia kukamatwa,”anasema.

  Wakati wa mapigano hayo, wakazi hao wanadai kuwa baadhi ya wanawake walibakwa walipovamiwa ndani ya nyumba zao ambapo wahalifu hao waliondoka na mwanamke mmoja ambaye baada ya kumbaka walimwachia saa 8 mchana kesho yake aliporejea kwake akiwa na maumivu makali.

  Naye Peter Bugeme, mkazi mwingine wa maeneo hayo anasema wahalifu wale walimbaka mke wa jirani yake aitwaye Julius Mikael wakati akiwa ndani peke yake, wakamkata mapanga , wakaiba vitu vyote na kumwacha akiwa amepoteza fahamu.

  Bugeme anaeleza kuwa mwanamke alipelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando iliyoko Mwanza kwa matibabu.

  Mkazi huyo anamtaja mke wa mkazi mwenzake aitwaye Remi ambaye pia anadai alibakwa , kisha kuondoka naye kwenda mahali kusikojulikana, lakini akaachiwa kesho yake mchana.

  Pamoja na uharifu huo, mkazi huyo anadai watu hao walivamia mashamba ya watu yenye mazao kama mahindi,mtama na kuanza kuyaharibu na kuyafyeka pamoja na kukata miti mbalimbali ikiiwamo ya matunda.

  Askari polisi kwa upande wao, wanadaiwa kuendesha kamata kamata wakiwamo wasiohusika na tukio hilo la uhalifu wala mapigano, anaoeleza Nyapura Nyamhanga.

  “Baada ya tukio polisi walifika na kuanza kukamata watu ovyo wengine wakikutwa hotelini, wengine majumbani mwao, kitu cha kusikitisha wakamkamata hadi mlemavu wa mguu aliyekuwa anashona cherehani kibandani kwake,wakapiga wengine kwa mabomu na kujeruhi watu wapatao 30.

  Sagi Mugore(58) anasema kuwa tatizo la mapigano si la leo, bali lilianza tangu mwaka 1993 kati ya Waluo na Wakurya.

  ”Mwaka huo tulivamiwa na Wakurya wakachukua mashamba yetu, wakatufukuza kutoka katika kitongoji cha Nyamuhonda tulikokuwa tunaishi tukahamia Ikoma.

  "Tazama, sasa watu wameanza kurudi kwenye maeneo yao hao watu wamerudi tena na kufanya uvamizi ili mapigano yakome kijengwe kituo cha polisi Ikoma," anaeleza.

  Pia, wananchi hao wanaeleza kuwa tatizo lingine linalosababisha mapigano ni viongozi wa vijiji kuuza na kukodisha mashamba kwa raia wa kigeni wanaotoka vijiji vya Nyamsense, Mtimrabu na Byamiti na mashamba hayo hutumiwa kwa kilimo cha Bangi na Tumbaku huku na kuwaacha wazawa wakikosa ardhi ya kuishi na kulima.

  Pia, wanaodaiwa kuwa tatizo ni wenyeviti wa mitaa na vijiji wanaodaiwa kuuza ardhi kwa wageni kinyume cha sheria na bila hata wananchi kujua.

  Viongozi hao wanadaiwa kuwakaribisha wageni kutoka nchi jirani na kuwapa ardhi ambayo wanaishi na matokeo yake hao wageni ambao pia ni jamii ya Wakurya wanaungana na wenzao wa Tanzania na kufanya mashambulizi na kuwanyang’anya ardhi Waluo, matukio na tayari mengi yanayotokea na wahusika wanatoka nchi jirani na wengine wanaoishi Nyamuhonda.

  Pamoja na malalamiko hayo ya kabila la Waluo, Wakurya nao walijitetea kwa kudai kuwa baada ya kutengwa na kuhesabiwa kuwa Rorya, Waluo wamekuwa na ukabila kwa kuwanyang’anya mashamba na kutoshirikiana nao katika maswala mbalimbali ya kijamii

  “Wakati Rorya inaanzishwa kama wilaya, Serikali iliweka mpaka wa Tarime na Rorya na baadhi ya Wakurya waishio Nyamuhonda wakahesabiwa kuwa wanakijiji wa Ikoma -Rorya, tulipokaa mkutano mwaka jana tuliazimia Wakurya waliotengwa kwenda Rorya wakae huko wamilikishwe ardhi wafanye maendeleo huko huko, tukaambiwa tusajiliwe kule Ikoma.
  "Tukaenda kwa mwenyekiti wa kijiji Ikoma ili atusajili, matokeo yake akatuambia ili tusajiliwe kila mtu anatakiwa kulipa Sh 200,000, tukashindwa na tukarudi Nyamohunda kwa Wakurya wenzetu, nako pia mtendaji wa kijiji akatukataa kuwa sisi si wananchi wake, Serikali ilishatugawa kwenda Ikoma.

  Sasa wanataka tukakae wapi kwani kule Ikoma tunabaguliwa, Nyamuhonda nako tunatimuliwa, inalazimu watu wachukue ardhi kwa nguvu, walime walishe familia zao na mahitaji mengine matokeo yake kunakuwepo na migongano ya ardhi na hivyo kusababisha watu kupigana,”anasema Chacha Wambura.

  Kutokana na na mapigano, Mei 7-8 Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa na viongozi mbalimbali wakiwamo wa kamati mbalimbali za ulinzi na usalama walifika Ikoma kuzungumza na wananchi ili kusikiliza nini chanzo cha mapigano na kutafuta suluhu.

  Ndipo ikabainika kuwa sababu za mapigano hayo ni migogoro ya ardhi inayosababishwa na viongozi wa vijiji hivyo vya Ikoma na Nyamuhonda

  RC Tupa akawataka wananchi hao kuondoa ukabila ambapo pia aliwahimiza wazee wa mila kuungana kwa pamoja kuondoa tofauti zao kwa kutumia busara zao kufichua wale wote wanaovunja amani na kufanya uharibifu wa mali za wananchi wenzao.

  Vile vile, RC Tupa akawataka maofisa uhamiaji wa Rorya na Tarime kuanza zoezi mara moja la kuhakiki uraia wa wananchi wa Ikoma na wananchi113 wanaotakiwa kusajiliwa Ikoma pamoja na wale wa Nyamuhonda,Tarime kama njia ya kuwabaini raia wa kigeni wanaoishi na kumilikishwa ardhi kinyume cha sheria.

  Akawaagiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya hizo kushughulikia tatizo la kukodishwa ardhi kwa wageni na kwamba endapo wasipotekeleza agizo hilo na kukatokea tena mapigano ataanza kwa kuwawajibisha wao kuanzia vijiji, kata na wilaya kutokana na kuwa mishahara wanayolipwa ni kodi za wananchi, hivyo wanapaswa kuwajibika na kutatua migogoro pindi inapotokea na siyo kungoja RC afike mahali hapo.


  Kepsheni:

  Picha - 1;Nyumba ya Girago Lucas, mkazi wa Kitongoji cha Nyantacho akiwa amesimama kwenye nyumba yake iliyochomwa moto wakati wa uvamizi na mapigano ya kabila la wajaruo na wakurya yaliyotokea hivi karibuni.

  Picha- 2:Nyumba ya mkazi wa Kijiji cha Ikoma iliyobomolewa wakati wa mapigano ya Waluo na Wakurya.

  Picha -3 nyumba mkazi wa Ikoma, Peter Bugeme iliyobomolewa wakati wa mapigano

  Picha- 4 Nyumba iliyokatwa mlango kwa mapanga wakati wa uvamizi na mapigano ya Waluo na Wakurya,

  Picha- 5 Mazao yaliyofekwa wakati wa mapigano ya Waluo na Wakurya. Picha zote na Dinnah Maningo

  Vita ya ukabila na tishio jipya kwa usalama Tarime, Rorya
   
Loading...