Vita hii ni zaidi ya ufisadi --KILANGO

mwanaizaya

Senior Member
Apr 26, 2008
133
1
Vita hii ni zaidi ya ufisadi

Mwandishi Wetu

SIYO siri kwamba wapo wabunge ambao sasa wakisimama bungeni, kuuliza swali au kuchangia hoja yoyote, wabunge karibu wote hutulia na waandishi wa habari wanaoripoti habari za bungeni huwa makini na kalamu zao sehemu waliyopangiwa kukaa.
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela

Kwa wiki tatu nilizohudhuria kama mwandishi wa habari mkutano wa 12 wa Bunge unaoendelea Dodoma niliona hali hiyo. Wabunge wanaoketi jirani huacha ‘kubadilishana mawazo’ na wanaoonyesha vikaratasi juu kwa ajili ya wahudhumu kuja kuvichukua kwa ajili ya kuwapa wenzao huwa nadra kuonekana.

Hiyo ni kwa sababu siku hizi hoja nzito za kuibana Serikali haziko kwa wabunge fulani fulani wa wapinzani tu kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe au Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa.

Wabunge wa CCM nao wamecharuka kutaka ‘kieleweke’ na orodha ya wabunge hao wa chama tawala wanaocharuka kukemea ufisadi na hali yoyote yenye kuumiza jamii, huongezeka kadri mkutano huo wa 12 unavyosonga mbele.

Hakuna shaka kwamba Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, ni miongoni mwa wabunge hao wa chama tawala ambao wamekataa kukaa kimya, kwani wamekuwa wakizinyooshea vidole kasoro wanazoziona hapa na pale ambazo zinaudidimiza umma katika umasikini zaidi kila uchao.

Lakini katikati ya harakati hizo za Kilango, kuna hisia na hasa wapo wanaosema kwamba kuchachamaa kwa mama huyo sasa, kwa kiasi kikubwa kunatokana na ‘hasira’ za kuwa mume wake, Waziri Mkuu wa zamani, John Samwel Malecela, alienguliwa katika kinyang’anyiro cha kuwania Urais mwaka 2005. Je, mama huyo anasemaje kuhusu hilo?

Katika mahojiano maalumu na Raia Mwema wiki iliyopita, Mama Kilango alisema anashukuru kuulizwa juu ya suala hilo ili alitoleee ufafanuzi kwani anashangaa ni kwa vipi kuchachamaa kwake bungeni kukemea uovu kunahusishwa na Urais aliokuwa anagombea mume wake.

Alisema ya kuwa yeye si mtu wa visasi. Kwamba baada ya mume wake kushindwa kuchaguliwa katika mchakato wa kumpata mgombea wa Urais kupitia CCM, alirudi kwao Same Mashariki kugombea ubunge na huko akakumbana na mtu aliyekuwa na nguvu nyingi kisiasa na aliyekuwa waziri muhimu katika serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa.

Mama Kilango ambaye alikuwa akimzungumzia Daniel Yona aliyepata kuwa Waziri wa Fedha na badaaye Waziri wa Nishati na Madini, anasema alifanikiwa kumshinda mtu huyo maarufu katika kura za maoni na kushindana na wagombea wa vyama vingine sita vya upinzani kunyakua kiti cha Ubunge cha Same Mashariki.

Alisema anachokifanya yeye sasa hakina uhusiano wowote na suala la mumewe kugombea Urais na anachofurahi ni kwamba yuko na wenzake wengi wa CCM ambao wameamua kuvalia njuga kasoro katika uendeshaji nchi.

Wapo wanaolaumu kwamba yeye na wenzakake kama Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro, aliyemtuhumu Mkapa kufanya biashara Ikulu wanafanya makosa kusemea bungeni badala ya kwenye vikao vya chama.

Mama Kilango anapingana na watu hao kwa kusema kwamba wanayoyasema bungeni ni yale yaliyofanywa na watu hao kama watumishi wa Serikali na si kama wanachama wa CCM.

Anasema kwamba wao kama wana CCM bungeni wana wajibu mkubwa wa kuwakosoa wenzao walioko serikalini na kwamba si busara kuicha kazi hiyo ikafanywa na wabunge wa Upinzani peke yao.

Anasema katu hawezi kukatishwa tamaa na watu wanaowabeza kwa kuwaita ‘chawa’ waliopo ndani ya CCM. Wanachojali ni kwamba wanasimamia ukweli na haki katika kulilia mabadiliko ya mfumo.

Anasema walioko katika mapambano hayo wako wengi kama inavyojionyesha kutokana na kujitokeza wapya mara kwa mara bungeni wakitoa mchango wao kuonyesha dhahiri kwamba wanakerwa na uozo uliopo serikalini.

Na mbunge wa mwisho kujitokeza alikuwa mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, ambaye wiki iliyopita, aliishikia kidedea Kampuni ya Bayport ambayo mke wa rais wa awamu ya tatu, Anne Mkapa ana hisa. Alidai kampuni hiyo inawaumiza walimu kwa kuwatoza riba kubwa mno. Alisema mwalimu akikopa Sh milioni moja hulazimika kurudisha Sh milioni tatu.

Lakini, Anne Kilango na wabunge wenzake wa CCM wanachokitafuta katika kuichokonoa Serikali ya chama chao ni kitu gani hasa? Ni kukerwa tu na ufisadi au wana watu wao ambao wanawapiga vita kwa sababu wanazozijua wenyewe?

Kwa mujibu wa mama huyo, wabunge wa CCM wa aina yake hawakujitokeza kupiga vita ufisadi tu kama wanavyochukuliwa, bali kila aina ya uozo wakiwa na lengo la kubadilisha mfumo uliopo sasa wa keki ya taifa kuliwa na ‘wajanja’ wachache tu.

Alisisitiza ya kuwa hawapambani na ufisadi tu, bali wanataka kubadilisha mfumo wa hovyo wa sasa ambao kikundi kidogo cha watu kimejitengenezea mazingira ambayo yanafanya nchi iendelee kuwa masikini huku wachache wakivuna manufaa makubwa.

“Sisi tulianza kuhisihisi siku za nyuma kwamba mambo hayaendi sawa. Haiwezekani Tanzania ikiwa ni nchi yenye rasilimali nyingi inaendelea kuwa na wananchi masikini kiasi hiki,” anasema.

Alisema kwa muda mrefu wakiwa na hisia kwamba mambo yanakwenda kombo, waliona kwamba kulalamika kwao kusingekuwa na nguvu hivyo wakawa wanatafuta pa kuanzia na kwa bahati njema suala la nchi kuwa na mikataba mibovu likajitokeza.

“Suala la mikataba mibovu lilipojitokeza, tukapata mahali pa kuanzia. Tukabaini ya kuwa kuna tatizo zito ndani ya Serikali ya CCM. Tunachokitafuta sasa ni kuleta mabadiliko ya mfumo ambayo ni lazima yawepo,” alisema.

Alisema ya kuwa wamegundua na kuthibitisha kwamba kulikuwa na kamfumo ambako kamewafanya baadhi ya viongozi wa Serikali kukasimu madaraka kwa kikundi kidogo kumiliki mapato ya nchi.

Alisema kwamba kikundi hicho kidogo baada ya kupatiwa fursa ya kupata fedha za taifa, bila woga kiliacha kundi kubwa la Watanzania likiteseka na umasikini.

“Tunachopigania ni kukipiga vita kikundi hicho kilichotokana na mfumo usiofaa si ufisadi tu huu,” alisema.

Alisisitiza: “Tunachotafuta ni mabadiliko ya jinsi ya kumiliki rasilimani ya nchi yetu. Lakini tunajua ya kuwa kazi ya kutafuta mabadiliko ya utawala au ya kiuchumi au ya mfumo wa umiliki ya rasimilimali ya taifa ni kazi kubwa sana.”

Alisema ni kazi inayohitaji kujitolea kweli kweli na kutoa mfano wa Afrika Kusini kwamba walipambana na milima na mabonde kufanikiwa walichokuwa wamekivalia njuga.

“Afrika Kusini ni nchi ya Waafrika lakini kwa muda mrefu ilikuwa inatawaliwa na Makaburu. Waafrika walipoamua kuutafuta mfumo wa nchi yao, wengi walikufa, lakini waliobaki hawakurudi nyuma wala kukata tamaa mpaka wakafanikiwa kuondoa utawala dhalimu,” alisema.

Alisema azma ya kubadilisha mfumo ili rasilimali za nchi ziwe za Watanzania na si za kikundi kidogo, inaungwa mkono na wabunge wengi bila kujali itikadi za vyama vyao, na hiyo ni kutokana na kwamba nchi inapita katika kipindi kigumu.

“Tunachotaka ni kufika mahali au kuhakikisha kwamba wanaomiliki mali, mapato ni Watanznaia wote,’ alisisitiza.

Hata hivyo, alisema aonavyo yeye, wabunge wa CCM ndio wenye dhamana kubwa zaidi ya kufanikiwa azma hiyo.

“Sisi wabunge wa CCM lazima tuwe msitari wa mbele na tusimame imara kubadilisha mfumo. Kazi hii tukiacha ifanywe na wabunge wa Upinzani tutatoa picha kwamba sisi tunalinda maovu yanayofanywa na viongozi wenzetu. Na ikifika hatua hiyo wananchi hawatakuwa na imani nasi,” anasema.

Anaongeza: “Lakini ieleweke kwamba wabunge peke yao hawawezi kuleta mabadiliko wala Serikali Kuu haiwezi kuleta mabadiliko. Hata wananchi ambao ndiyo wanaumia zaidi peke yao hawawezi kuleta mabadiliko, hivyo kinachotakiwa ni ushirikiano. Pamoja sote tutaweza”.

Alisema kwa upande wao wabunge wamedhamiria kuleta mabadiliko bila kuogopa misukosuko inayotokana na kutafuta mabadiliko hayo. Serikali Kuu ya awamu ya nne, anasema, imeonyesha utayari wake kwa vitendo vya wazi na ilionyesha mabadiliko tangu siku ya kwanza ilipoingia madarakani.

“Sasa tunahitaji wananchi wote, katika hili ambalo nakiri kwamba ni gumu, tushirikiane. Wakristo wote wamwombe Mwenyezi Mungu kupitia kitabu cha Maombolezo 5:1 kisemacho: “E bwana kumbuka yaliyotupata, utazame na kuona aibu yetu, urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni,” anasema na kuongeza: “Waislamu nao waingie msikitini wamwombe Mwenyezi Mungu tutashinda.”

Pamoja na madai yake kwamba wanaowania mabadiliko ya mfumo ni wengi, Mama Kilango anakiri ya kuwa wabunge wa CCM wamewaganyika kwa hilo.

“Nafahamu wabunge wamegawanyika. Hili ni jambo la kawaida kabisa ndani ya jamii yoyote. Binadamu hawaangalii jambo katika sura ya kufanana. Kila binadamu ndani ya jamii ana mtazamano wake katika jambo linalojitokeza,” anasema.

“Kuna wabunge ambao sasa hivi wanahangaikia mabadiliko hayo lakini wapo wanayoyapinga. Ni wachache sana lakini wana sababu zao za msingi, labda mabadiliko haya yanagusa maslahi yao, kwa hiyo ni lazima wapinge,” alisema.

Alisema wabunge hao wataachwa kama walivyo hata kama watawabeza kwa sababu wao hawatakataa tamaa.

“Siku moja watatuunga mkono kwani sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Ni vyema kabisa kila mtu akaelewa kwamba wale wote ambao wameamua kusimamia mabadiliko ambayo ni ya lazima wajitayarishe kukutana na misukosuko ya aina nyingi sana.

“Kutakuwa na kubeza, kutukanwa, kuchafuliana majina na magazeti ambayo yatatumiwa vibaya, kutakuwa na kuzushiwa mambo ambayo hayapo, lakini yote hiyo ni misukusuko ambayo ni lazima tuifikie ili tufikie katika mabadiliko tunayoyatafuta kwa sababu hakuna mabadiliko ambayo yanapatikana kwa urahisi,” anasema.

Mama Kilango anasema ya kuwa anajua ya kuwa moto waliouanzisha huenda wasione mwisho wake.

“Naomba nikiri ya kuwa tumeanza sisi ambao sasa tunachachamaa. Si lazima kazi hii ya kutafuta mabadiliko haya tuimalize sisi. Wataendeleza wengine tutakapokuwa sisi hatupo mpaka ushindi utakapopatikana,” anasema.

Anasema kazi waliyoianzisha si ya mwaka mmoja au miwili. “Hata walioanzisha kupinga biashara ya utumwa si wao walioitokomeza. Wengi wao walikuwa wamekwisha kuondoka duniani lakini biashara ya utumwa ilikomeshwa. Tutashinda kwa sababu ukweli siku zote unajisimamia wenyewe na si busara kuukana ukweli,” anasema.

Mama Kilango pia alizungumzia umuhimu wa Serikali Kuu kuwa makini na halmashuri za wilaya baada ya kupeleka fedha nyingi huko. Hata hivyo alisema jukumu kubwa liko kwa madiwani pamoja na wabunge kuchochea maendeleo ya huko.

“Madiwani wakilala tayari tumekufa. Kasi iliyoko ndani ya Bunge ya kutafuta mabadiliko iteremke hadi halmashauri ambako ndiko pesa nyingi zimepelekwa. Na wenyewe wakikubali misukosuko na wabunge tuteremke kwenye Halmashuri kwa sababu na sisi ni madiwani. Lazima tushirikiane kwa sababu mabadiliko ni lazima,” alisema.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom