Vipi Ripoti ya Ukaguzi BoT ikabidhiwe kwa Rais kinyemela?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,029
Ama kweli siri kali!

Posted Date::1/8/2008
Vipi Ripoti ya Ukaguzi BoT ikabidhiwe kwa Rais kinyemela?
Mwananchi

JUZI Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG), Ludovick Utouh, alimkabidhi Rais Jakaya Kikwete Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kimya kimya bila kuwaita waandishi wa habari.

Siku ya kukabidhi ripoti hiyo kwa Rais Kikwete ilikuwa ikaisubiriwa kwa hamu na Watanzania wengi kwa kuzingatia umuhimu wake unaotokana na ukaguzi huo kufanyika kufuatia madai yaliyotolewa na kambi ya upinzani kwamba kuna ubadhilifu na ufisadi wa hali ya juu katika akaunti hiyo.

Vyama vya siasa vya upinzani vimekuwa vikihoji kwa nyakati mbalimbali sababu za ripoti hiyo kuchelewesha kutolewa baada ya wakaguzi kumaliza kazi yao, hivyo kuwa na hofu na kutamka bayana kwamba serikali inataka kuibadilisha ili kuficha ukweli.

Serikali kwa upande wake kupitia kwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji imekuwa ikijitetea na kuwahakikishia Watanzania kwamba ripoti hiyo itatolewa wazi na hakutakuwa na mazingira yoyote ya usiri ili kuwaondoa hofu Watanzania juu ya fedha zao na kwamba watakaohusika watachukuliwa hatua.

Lakini leo hii kauli hiyo ya Waziri Meghji haionyeshi ukweli kwa kuwa badala ya kutumia njia ya uwazi katika kumkabidhi Rais ripoti hiyo mbele ya watanzania kupitia vyombo vya habari kama wanavyofanya kwenye matukio na ripoti nyingine, wamefanya kinyemela ikionyesha kwamba kuna usiri wa aina fulani.

Kilichoshangaza ni kwamba CAG alipeleka ripoti hiyo kwa rais kimya kimya na baadaye kuita vyombo vya habari vya serikali na kuvitaarifu juu ya ripori hiyo kukabidhiwa kwa rais na baadaye kudaiwa kuwa alikuwa ameita mkutano wa waandishi wa habari!

Tungependa kujua ni kwa nini ripoti hiyo ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu na Watanzania wote ipelekwe kwa Rais kimya kimya badala ya utaratibu uliozoeleka? Mbona ripoti nyingine nyeti zimekuwa zikikabidhiwa kwa viongozi wetu mbele ya waandishi ili kuweka ushahidi kwamba kazi hiyo ilifanyika na imekamilika?

Mazingira yaliyotumika kukabidhi ripoti hiyo kwa rais yanatia shaka kwamba hakuna uwazi kama Waziri Meghji alivyoahidi kwamba kila hatua itakuwa wazi.

Ikumbukwe kwamba wananchi na vyombo vya habari vilipofuatilia ripoti hiyo mwishoni mwa mwaka jana, Utouh alisema kazi imekamilika inasubiri kukabidhiwa kwa Rais wakati wowote atakaporudi kutoka likizo mapema Januari.

Hata baada ya Rais kurudi kutoka likizo wananchi walikuwa wanasubiri kufahamishwa kupitia vyombo vya habari kwamba ni lini atakabidhiwa ripoti hiyo na lini itaanikwa hadharani.

Lakini cha ajabu ni kwamba tendo hilo limefanyika kwa siri, ikimaanisha kwamba kuna uwezekano wa kucheleweshwa kutangazwa hata kama rais ataipitia, ili kupooza makali ya uhitaji wa wananchi wa taarifa hiyo kutolewa.

Tunaiomba serikali iache kufanya kwa siri mambo yanayogusa jamii na ambayo yanapigiwa kelele na wananchi, ili kuwa kwenye nafasi nzuri na kuamini, kwa kueleza wazi kila hatua kwani hakukuwa na sababu ya kuificha.

Sisi hatuoni sababu ya kufanya tendo hilo kimya kimya na tunajiuliza kwamba serikali iliogopa nini?
 
Back
Top Bottom