Vipepeo Weusi: Mkakati Namba 0034 (Simulizi)

Habibu B. Anga

JF-Expert Member
May 7, 2013
6,557
25,671
SOMA EPISODE 2, POST # 282

SOMA EPISODE 3, POST # 655

SOMA EPISODE 4, POST # 852

SOMA EPISODE 5, POST # 1115


SOMA EPISODE 6, POST # 1656

SOMA EPISODE 7, POST # 1773

SOMA EPISODE 8, POST [HASHTAG]#2517[/HASHTAG]

SOMA EPISODE 9, POST # 3116

SOMA EPISODE 10, POST # 3176

SOMA EPISODE 11, POST # 3212

SOMA EPISODE 12, POST # 3262

SOMA EPISODE 13, POST # 3310

SOMA EPISODE 14, POST # 3311


=========

Muhimu: Simulizi hii inaakisi namna ambavyo kila mmoja wetu anaguswa na mambo ya siri yanayofanywa na watu wenye nguvu na ushawishi. Pia simulizi hii inajitahidi kugusia ulimwengu wa hatari wa "conspiracies" na Ujasusi. Pia msimuliaji anaonyesha namna ambavyo nguvu ya mapenzi inaweza kuokoa nafsi ya mtu na kumfanya kuwa bora kwa wanomzunguka na nchi yake.

Kumbuka simulizi hii ni ya kutunga. Wahusika, matukio na visa vyote vinavyosimuliwa ni vya kufikirika, hivyo mfanano wowote na mtu katika maisha halisi ni bahati mbaya.

Tafadhali si ruhusa kutumia andishi hili mahali popote pasipo ruhusa ya muandishi.

VIPEPEO WEUSI: MKAKATI NAMBA 0034
"Nipe mahali pa kusimama na ndoano mkononi mwangu, naweza nikainua dunia." - The Bold


EPISODE 1

MIAKA 3 ILIYOPITA, Dar es Salaam.
Nimezaliwa miaka 29, miezi minne, wiki mbili, siku tano, masaa 18, na dakika 40 zilizopita. Jina langu naitwa Rweyemamu Charles Kajuna, lakini marafiki na wanafamilia hupendelea kuniita kwa kifupi, Ray.

Nakumbuka miaka mitatu iliyopita. Siku ya kwanza waliponifuata. Siku ya kwanza nilipo fahamu kuwa wanataka niwe mmoja wao au angalau yafaa kusema niwe kibaraka wao.

Ilikuwa siku alhamisi, jioni yapata majira ya saa kumi na mbili kasoro, walifika wakiwa ndani ya gari nyeusi aina ya Land Ceuiser V8. Nilikuwa nimelala kitandani lakini niliamka baada ya kumsikia Shangazi akiongea nao nje.

Nyumba yetu ilikuwa pembezoni mwa barabara ya mtaa katika maeneo ya Mwembe Chai, na nyumba yetu haikuwa na uzio. Hivyo nilivyo amka kutoka kitandani na kuchungulia dirishani niliweza kuwaona wageni waliokuwa wanaongea na Shangazi.

Walikuwa wamepaki gari yao nyeusi ng'ambo ya barabara. Watu wawili walishuka kutoka kwenye gari na kuja mpaka mlangoni mwa nyumba yetu. Wakagonga mlango na shangazi akatoka kuwasikiliza.

Haya yote nilikuwa nayaona kupitia dirishani. Kitu cha kwanza kilichoisumbua roho yangu baada ya kuwaona watu hawa ilikuwa ni gari waliyokuja nayo. Kichwani mwangu nilishawishika kabisa gari hii naifahamu na nimewahi kuiona lakini kumbukumbu ilikuwa haiji ni wapi niliiona au naifahamu vipi.

Nikahisi labda kuna mahusiano na bahasha niliyoipokea wiki mbili zilizopita, nikiwa ofisini Morogoro ililetwa na mtoto anayeuza machungwa akidai kuwa amepewa na mtu nje ya jengo letu la ofisi na akaambiwa aje amkabidhi mtu anayeitwa Ray.

Ndani ya bahasha hii nilikuta simu na kikaratasi kimeandikwa "speed dial 1", ikimaanisha nibonyeze kwa muda kitufe namba moja cha simu ili simu ipige. Suala hili nilikuwa sijalifanya mpaka leo hii na sikuwa na mpango wa kulifanya kwani ni uchizi kutii maagizo ambayo hata haufahamu yaliko toka.

Hisia zangu zikaendelea kufikiri labda watu hawa wana uhusiano na bahasha ile. Lakini pia roho yangu ilizidi kusumbuka kila nilipoiangalia ile gari waliyokuja nayo. Kadiri nilovyoiangalia ndivyo nilivyozidi kushawishika kuwa naifahamu, lakini bahati mbaya sikuweza kukumbuka niliiona wapi.

Nikiwa bado niko dirishani nachungulia kuangalia kinachoendelea mara shangazi akaniita kutokea nje, "Ray.!!"
"Naaaam.!" Nikamuitikia huku nikisogea kwenye dirisha sikuataka wajue kuwa nilikuwa nawachungulia mda wote huu.
"Kuna wageni wako nje hapa"
"Nakuja" nikajibu huku navaa pensi mda wote huu nilikuwa nimevaa bukta ya kulalia na singlendi.

Kabla sijatoka chumbani kwangu, nikachukua begi la mgongoni ambalo lilikuwa pembeni ya kitanda na kufungua zipu kisha nikatoa bahasha pamoja na simu nilivyovipokea wiki mbili zilizopita. Nikaiweka simu ndani ya bahasha na kuikunja ili niweze kuishika mkononi.

Baada ya kufungua mlango na kutoka nikiwa sebuleni shangazi naye alikuwa ndio anaingia kutoka nje. Nikamuuliza "kwanini hujawakaribisha ndani wageni".

"Wamesema hawakai wana haraka" akanijibu kwa ufupi huku akielekea chumbani kwake. Nikafungua mlango nikatoka nje. Wageni wangu walikuwa ni watu wawili, mmoja alikuwa ni muhindi, mtu mzima kiasi mwenye umri kati ta miaka 40 hadi 42 na mwenzake alikuwa ni mswahili na kijana zaidi kwa makadirio ya umri kuanzia miaka 34 hadi 36.

Yule muhindi alikuwa amevalia shati, suruali ya jinzi na viatu vyeusi, na yule mwenzake mswahili alikuwa amevalia suti ya kaunda. Jamaa huyu mswahili alikuwa na mwili uliojengeka kimazoezi kiasi kwamba hata suti ilikuwa imemkaa sawia. Kwa mtazamo wa haraka nikahisi kwamba jamaa huyu mswahili alikuwa ni mlinzi binafsi wa huyu muhindi.

"Hujambo Ray?" Yule muhindi alisalimia huku anatabasamu mara tu nilipofika walipokuwa wamesimama.
Sikutaka kuitikia salamu yao, nikaenda moja kwa moja kwenye hisia zangu "mmefuata mzigo wenu?" Nikawauliza huku nawaonyesha bahasha niliyotoka nayo ndani.

Yule muhindi akatoa tabasamu kubwa na kuniuliza "nini kinachokufanya uhisi huo ni mzigo wetu na ndicho kilichotuleta?".
"Kama sio mzigo wenu niambieni niurudishe ndani alafu nije niwasikilize hicho kilicho waleta?" Nikaongea kwa kujiamini huku nimemkazia macho yule muhindi.

Akaichukua bahasha kutoka mkononi mwangu kisha akampa yule mswahili aishike, kisha akaniuliza kwa kifupi tu "kwa nini haukupiga simu?".
"Mimi sio mpumbavu nifuate maelekezo nipige simu wakati hata sijui hiyo bahasha ilikotoka!" Nikamjibu haraka huku nikijitahidi kuonyesha kujiamini. Yule muhindi akatabasamu tena huku akitingisha kichwa "ndio maana tumeamua tuje ili tuongee kwa mdomo, relax" akaongea yule muhindi.

"Siwezi kurelax wakati siwafahamu hata nyinyi ni kina nani, mnatokea wapi na mnataka nini." Nikajitutumua zaidi. Rohoni nilijisikia raha kwasababu nilijihisi kama nimeshika usukani wa haya maongezi.
"ooohh usijali, mimi naitwa Sultan na mwenzangu anaitwa Kevin"

Nikamkazia macho yule muhindi huku, na yeye akinikodolea macho kana kwamba anajaribu kusoma ninachofikiria.
"Mmejitambulisha wawili tu, kwanini hamjamtambukisha mtu wa tatu mliyekuja naye?" Nikamuuliza huku nimemkazia macho kwa kujiamini.
Yule muhindi Sultan akageuka wakatazamana na yule mswahili Kevin kisha akanitizama mimi, "Ray mtu gani wa tatu unamuongelea"

Sikupepesa macho wala kutazama pembeni, nikaendelea kumkazia macho na nikasogea hatua moja mbele kuelekea aliposimama Sultan. Kisha nikamuangalia moja kwa moja machoni kwa kujiamini na kumueleza, "nimewaona tangu mnakuja, mlipofika hapa na gari lenu wewe ulishuka kwenye gari kwa mlango wa kushoto wa mbele, na huyu mwenzio alishuka kutoka mlango wa nyuma, kwahiyo nina hakika kuna aliyekaa upande wa kulia mbele ambaye ndiye anayeendesha gari na hajashuka!"

Nilipowaambia maneno hayo wote macho yetu kwa pamoja yakaelekea kwenye gari lililokuwa wamepaki ng'ambo ya barabara. Gari ilikuwa na vioo vyeusi visivyoonyesha ndani. Kutokana na pale tulipokuwa tumesimama nikafanikiwa kuona namba za gari, T 228 CNL. Namba hizi zikazidi kuniaminisha hisia zangu kuwa gari hii naifahamu lakini bado kumbukumbu zangu haziji kuelewa gari ile niliwahi kuiona wapi.

Sultan akaangaliana na mwenzake Kevin kisha Kevin akatingisha kichwa kumpa kama ishara ya kukubali. Kisha akaniangalia mimi, "ok Ray, twende tukamsalimu".

Tukavuka barabara mpaka mahali walipopaki gari. Tulipofika Kevin akagonga kwa kidole kioo cha gari. Kioo kikafunguliwa taratibu na kilipofunguka chote mpaka chini, ndipo hapa nikaelewa kwanini kumbukumbu zangu ziliniambia kuwa nalifahamu hili gari.

Ndani ya gari kwenye siti ya dereva alikuwa ameketi Dr. Boniface Shirima.
Dr. Shirima ni mwalimu wangu wa Uchumi, au yafaa kusema alikuwa mwalimu wangu wa uchumi Chuo Kikuu cha Mzumbe kabla sijahairisha masomo miezi minne iliyopita ili niweze kujizatiti katika shughuli zangu za taasisi niliyoianzisha.

Nilimuangalia kwa mshangao kwa dakika kadhaa bila kuongea chochote.
Bumbuwazi langu lilikatishwa na Dr. Shirima ambaye alitabasamu na kunisalimu "hujambo Rweyemamu?"
"Shikamoo dokta, tafadhali nieleze kinachoendelea hapa sielewi" nikamjibu haraka haraka ndani ya nafsi yangu nikihisi kuwa labda walau sasa kuna mtu ninaye mfahamu anaweza kunieleza mini kinaendelea.

"Usijali Ray, kwanini haukupiga simu wiki mbili zote hizi" Dr. Shirima alikwepa swali langu na kuniuliza swali lingine.
"Dokta nimeshawaeleza hawa wenzako nimeletewa bahasha katika mazingira ya kutatanisha na ndani nakuta simu yenye kikaratsi chenye maelezo kwamba nipige simu!

Mimi sio mpuuzi kiasi hicho kufuata maelezo nisiyoyajua yalikotoka" nikamjibu Dr. Shirima, kwa mbali hasira zilinza kunishika kwenye nafsi. Nilianza kuchoshwa na hiki kilichokuwa kinachoendelea.

Kana kwamba Dr. Shirima alisoma akili yangu kwa haraka akendeleza maongezi, "Ray, hauna haja ya kuogopa wala kuwa na wasiwasi. Inawezekana haujafikiria hili lakini nchi hii inahitaji vijana wenye maono kama yako. Sisi ni marafiki, pia tuna pambana usiku na mchana kuhakikisha nchi inasonga mbele"

Kwa muda wa sekunde chache nikajaribu kutafsiri maneno yake kichwani ili niweze kuelewa kile ambacho labda alimaanisha na alikuwa hakitamki. Nikatafakari maneno kadhaa 'nchi inahitaji vijana wenye kama yako', 'tunapambana usiku na mchana kuhakikisha nchi inasonga mbele'!

Kiasi nikahisi kama nimemuelewa anachojaribu kukisema, hivyo nikataka nipate uhakika nikamuuliza, "Dokta kama mko na Idara ya Usalama wa Taifa, sidhani kama huu ndio utaratibu wa kurecruit watu ku…."
"No no no no hatuko na Usalama wa Taifa" Dr. Shirima alinikatsha kabla sijamalza nilichotaka kusema.
"Kama sio Usalama wa Taifa, nyinyi ni akina nani?" Nikamuuliza nikionyesha wazi mshangao wangu.

Dr. Shirima hakunijibu moja kwa moja akaingiza mkono kwenye begi dogo lilikuwa pembeni yake na kutoa simu inayofanana kabisa na ile niliyoletewa wiki mbili zilizopita niliyo wakabidhi Sultan na Kevin. Akanikabidhi simu na kunambia, "ni rahisi sana kukujibu sisi ni akina nani na kwanini tunakuhitaji, unachotakiwa kufanya, leo ikifika saa nne usiku bonyeza 'speed dial' namba 1"

Nikaipokea simu, nikaiangalia na kuigeuza geuza, nikijiuliza kichwani nimrudishie au nifanyeje?
"Na kama sitopiga simu hiyo saa nne?" Nikamuuliza.

Dr. Shirima akainamisha kichwa chini kama anafikiria kitu hivi kisha akaniangalia usoni, "kama hutopiga simu basi tutaachana nawe, lakini kabla haujafanya uamuzi huo kumbula kitu kimoja, nafahamu ni kiasi gani unapata tabu kutafuta funds za kuendesha program yako ya 'Sote Hub'! Tuna uwezo wa kukusaidia kwenye hilo, we can point you to the right direction upate hizo funds" Dr. Shirima alinieleza huku amenikazia macho, alijua wazi kabisa ni kiasi gani maneno haya yatakuwa yamenigusa moyoni.

Moyo wangu ulilipuka niliposikia anataja kuhusu 'kuniwezesha kupata funds kwa ajili ya 'Sote Hub'. Nikamuangalia usoni, Dr. Shirima akatabasamu, nilikuwa na uhakika kuwa amefahamu ni kiasi gani maneno aliyoyasema yamenigusa.

Akatabasamu, "Ray, fikiria kwa makini uamuzi ni wako, leo saa nne usiku fanya uamuzi sahihi." Akanieleza kwa kifupi huku akiwapa ishara wenzake Sultan na Kevin ambao mda wote walikuwa wamesimama kando yangu wakifuatilia mazungumzo yetu mimi ma Dr. Shayo. Wakapanda kwenye gari na mimi nikaanza kuondoka.

"Hey Ray.." Dokta aliniita, nilikuwa nataka kuvuka barabara na wao walikuwa wameshawasha gari. Nikageuka.
"Yes.." Nikamuitikia
"Msalimie cheupe!" Dr. Shirima akaniambia kwa utani huku anatabasamu. Na mimi nikashindwa kuzuia tabasamu usoni, nikamuitikia tu kwa kutingisha kichwa. Kichwani mwangu nikawaza "hawa washenzi wanafahamu vitu vingapi kuhusu mimi?". Nikatabasamu.
Wakawasha gari na kuondoka na mimi nikavuka barabara na kurejea nyumbani.

Nilipoingia ndani nikamkuta shngazi sebuleni na aliponiona tu akaanza kuniangalia kwa macho ya udadisi.
"Uko sawa?" Akaniukiza huku bado ananitazama kwa kijicho cha udadisi.
"Yeah shangazi, niko poa tu" nikamjibu kwa mkato huku nikielekea chumbani, sikutaka kubaki sebuleni hata dakika moja maana namfahamu shangazi yangu, ungeanza mfululizo wa maswali ambayo nilikuwa sitaki kuyajibu mda huu. Lazima angeanza kuniuliza Wale kina nani, wamesemaje, wanataka nini, unafahamiana nao vipi??
No, sikutaka kujibu maswali haya sasa, nikapitiliza mpaka chumbani kwangu na kufunga mlango.

Nilipofika chumbani nikajitupa kitandani kifudifudi, "aaaaaaarrrrggghh". Nikajiungurumia mwenyewe. Kichwa kilikuwa kinauzunguka nikitafakari mambo kadhaa kwa wakati mmoja.

Kitu kikubwa zaidi nilichokuwa nakiwaza na kikijirudia tena na tena akilini mwangu ilikuwa ni kauli ya D. Shirima, "tunaweza kukusaidia kupata funds kwaajili ya 'Sote Hub'". Nilitabasamu kila nilipofikiria kauli hii. Nikajiuliza ni kama ni kweli wana uwezo wa kufanya hivyo au ilikuwa ni mbinu ya kunipata na kuniingiza katika mipango yao waliyo nayo ambayo bado sikuijua mpaka muda huu.

Lakini jambo moja lilikuwa bayana, kwamba ndani ya mwezi mmoja ujao kama sitoweza kupata funds kwa ajili ya program ya Sote Hub sitakuwa na chaguo lingine zaidi ya kutii amri ya serikali ya kufunga ofisi.
Kila nilipofikiria dhana ya kufunga ofisi moyo wangu uliniuma na kulipuka. Nikikumbuka jinsi nilivyo vuja jasho na 'damu' mpaka kuanzisha Sote Hub, hakika kufunga ofisi itakuwa moja ya mapigo yatakayo niuma zaidi kwa maisha yangu yote.

Nikikumbuka jinsi safari ya kuanzisha Sote Hub ilivyo moyo wangu uliuma.
Safari hii ilianza mwaka mkoja uliopita nikiwa kama mwanafunzi wa mwaka wa kwanza chuo kikuu cha Mzumbe nikichukua shahada ya 'Economics and Project Planning'.

Nilipata wazo la kusaidia wanafunzi wenye talanta ya ujasiriamali. Nikaanzisha shindano la michanganuo ya biashara. Shindano hili nililiita 'Anzisha Business Competition'. Nikapata ufadhili kutoka kampuni ya Coca Cola.

Wanafunzi kutoka vyuo mbali mbali Tanzania walituma michanganuo yao ya mawazo ya biashara. Kisha mimi pamoja na panel yangu akiwemo Dr. Shirima ambaye alikuwa ni mwalimu wangu wa uchumi na moja ya watu ninaowahusudu sana kitaaluma kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuona mambo kwa mtazamo mpana zaidi, tulichagua wanafunzi thelathini wenye mawazo bora zaidi kisha tukawashindanisha na kuwachuja na kubaki na wanafunzi kumi pekee ambao waliingia raundi ya mwisho ya fainali.

Fainali za shindano hili la Anzisha Business Competition zilirushwa kwenye televisheni ambapo washiriki walijieleza juu ya idea zao hizo na namna gani zitakavyo tekelezeka na kuleta faida za kiuchumi kwao na kuajiri vijana wengine.
Mshindi wa kwanza alipewa shilingi milioni kumi kutoka kampuni ya Coca Cola na mshindi wa pili alipatiwa milioni tano na watatu milioni mbili.

Miezi mitatu baadae tulipotembelea washindi hawa kufanya tahimini ya shindano tukakuta wote biashara zao walizianzisha lakini zimekufa.

Ndipo hapo katika kikao chetu cha majumuisho, nakumbuka Dr. Shirima akaeleza kuwa kumpatia mtu fedha pekee haisaidii bali anahitaji pia apatiwe mafunzo afahamu ulimwengu wa ujasiriamali ukoje, afundishwe kuhusu kutambua masoko, branding ya bidhaa yake na hata apate 'mentor' wa kumjenga kisaikolojia kuhusu biashara.

Ndipo hapa nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa pili, nikachukua hatua ya kuanzisha kituo cha kukuza biashara za vijana wenye ideas za tofauti na zenye uwezo wa Kukuwa kuwa kampuni kubwa.

Nilidhamiria kituo hiki kichukue vijana wenye mawazo bora kabisa ya kibiashara, kisha wapewe mafunzo kuhusu masoko na 'branding', watafutiwe mentors na mwishoni wapemwe mtaji wa kuanzisha biashara zao (seed capital).
Sisi kama kampuni tunaowasimamia tutachukua asilimia ndogo za hisa katika kampuni zao watakazo zianzisha.

Nikasajili kituo/kampuni hii kama 'Sote Hub' (SOTE - startup operations and trainings in Entrepreneurship).

Nikavuja jasho kuhangaika usiku na mchana kutafuta wafadhili wa kusaidia kuanzisha program hii. Baada ya miezi kadhaa ndipo nikafanikisha kuingia mkataba na Vodacom kudhamini hii programu. Ambapo kwa mwaka wa kwanza watatoa kiasi cha shilingi milioni 120 ambazo zitatolewa kwa awamu tatu, milioni 40 kila baada ya miezi minne.

Kwakuwa nilikuwa bado mwanafunzi chuo kikuu mzumbe, hivyo kituo hiki nikakianzisha Morogoro mjini na ofisi zake zilikuwa katika ghorofa la Hajram Mtaa wa Boma Road.
Ofisi na programu yenyewe zikazinduliwa kwa sherehe kubwa ya kufana mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya Morogoro. Ikarushwa katika taarifa za habari za televisheni mbali mbali na kutokea kwenye magazeti.

Vodacom wakanipa awamu ya kwanza ya funding, shilingi milioni 40. Utekelezaji wa programu ukaanza. Vijana kutoka kila pembe ya nchi wakatuma michanganuo ya biashara. Tukatumia takribani miezi miwili kupitia michanganuo yote na hatimae kupata vijana watano ambao ndio watakuwa chini ya programu hii kwa awamu hii ya kwanza.

Tukafanya press conference kuwatangaza. Vijana wakasafiri kutoka walipo wakaja Morogoro. Lengo lilikuwa ni 'kuwapiga msasa' kuhusu masuala ya kibiashara kwa miezi mitatu kisha mwishoni wanapatiwa seed capital ya milioni 10 kila mmoja.
Kutokana na kuwa bize sana kusimamia shugjuli za programu ikanibidi nihairishe masomo chuoni.

Vijana wakapatiwa mafunzo kwa mwezi wa kwanza. Ilipofikia mwanzoni mwa mwezi wa pili wa Programu, kukatokea mabadiliko makubwa ya kisera na uongozi ndani ya Vodacom. Uongozi mpya ukasitisha mikataba mingi ya udhamini ukiwepo mkataba wao na Sote Hub.

Hapa ndipo mushkeli ulipoanza katika maisha yangu. Nikahangaika usiku na mchana kutafuta sponsor mwingine wa kusaidia kuifikisha mwisho programu tuliyoianza lakini hakukuwa na mafanikio yoyote.

Sasa leo hii napata wageni tata, ambao ni dhahiri wana agenda ya siri na mimi na wanaahidi "tunaweza kukusaidi upate funding kwaajili ya Sote Hub".
Nilibaki na alama ya kuuliza kichwani. Niliwaza na kuwazua kwa masaa kadhaa. Nikaangalia saa kwenye simu ilionyesha ni saa tatu na dakika tano.

Nikachukua simu nimpigie Hasnat. Yes, Hasnat. Roho ya roho yangu. Mtu pekee ambaye nikisikia sauti yake hata niwe nimepaniki kiasi gani kila kitu kinakuwa shwari. Hasnat, mwanamke wa maisha yangu. Mwanamke niliyempenda na tunapendana tokea utotoni, na mwanamke pekee ambaye nataka niendelee kumpenda kwa maisha yangu yote duniani. Hasnat, mwanamke anayenifahamu pengine kuliko hata mimi ninavyojifahamu.

Nikachukua simu na kumpigia.

"Nambie kichwa" Sauti ya Hasnat iliongea kutoka upande wa pili wa simu. Taratibu taharuki yangu ikaanza kuyeyuka.
"Fesh tu, uko poa cheupe"
"Niko poa baba, nimechoka choka tu nilikuwa discussion ndio naingia room sahizi hapa wakati unapiga"
"Ok, skia cheupe! I have some bad news and worse news, what do you want first?"

"Hahahaha no i want the good news"
"OK! Kuna watu wamekuja home leo wanataka kunisaidia nipate funding kwaajili ya Sote Hub, the problem is I don't trust tem.."
"Are you kidding me, that's really a good news, kwanini unasema ni habari mbaya and kwanini huwatrust?"

"Sijui nisemeje but nadhani its better nichukulie hii positively, unakumbuka ile stori nilikwambia kwenye nchi za Asia wanaamini ukitembea barabarani kipepeo akikugusa hiyo inaashiria baraka, labda ndio vipepeo wenyewe hawa hahaha."

"Yeah but sio kila kipepeo ana rangi za kupendeza, vipepeo wengine ni vipepeo weusi majanga tupu hahahaha kidding honey, I think you should take the deal"
"Yeah kesho nitaenda kuonana nao"
"That's ma boi, good luck honey mi wacha nilale nimechoka kinyama yani"
"Poa! Usiku mwema cheupe, nakupenda"
"love you more kichwa"

Hasnat alikuwa na miujiza ya aina yake au labda ni kutokana na kumpenda kupindukia, kwani kusikia sauti yake tu kulifanya taharuki yote iliyokuwepo ndani yangu kuyeyuka. Lakini kuna maneno aliyoyatamka yaliendelea kujirudia kichwani mwangu na kufanya kuanza kurudiwa na hofu. "Sio kila kipepeo ana rangi ya kupendeza, kuna Vipepeo weusi pia". Maneno haya yalijirudia tena na tena kichwani.

Nikaangalia tena saa kwenye simu, ilikuwa ni saa nne na dakika mbili. Nikajipa moyo, "fu*k it! Wawe na rangi ya kupendeza au nyeusi, kipepeo ni kipepeo tu"
Nikachukua simu niliyopewa na Dr. Shirima na kubonyeza speed dial namba moja na kuweka sikioni.

"Halo!" Nikasubiri kusikia sauti kutoka upande wa pili.
"Una peni na karatasi hapo" sauti nzito upande wa pili wa simu iliongea bila hata kuitikia salamu yangu wala yeye kunisalimia. Haraka haraka nikafungua zipu kwenye begi la mgongoni lililokuwa pembeni mwa kitanda na kutoa kalamu.

"Ndio ninavyo" nikamjibu haraka haraka.
"Kesho saa kumi na nusu, PPF House, ghorofa ya saba, Unimax Marketing, jina lako ni Ally Hassan" ikaongea sauti upande wa pili wa simu bila nukta, haraka haraka.
"What, jina langu ni Rweyem….." Kabla sijamaliza kuongea simu ilikuwa imekata.

Nikaangalia taarifa nilizokuwa nandika kwenye kikaratasi nilipokuwa natajiwa na ile sauti kwenye simu. 'Saa kumi na nusu. PPF House. Ghorofa ya Saba. Unimax Marketing. Ally Hassan.'
"What the fu*k is this?" Nikajisemea kimoyo moyo..
Nikakikunja kile kikaratasi nikakiweka kwenye begi la mgongoni pembeni ya kitanda, kisha nikajilaza nikitafakari hiki kinachoendelea. Na baada ya kama dakika ishirini usingizi ukanipitia.

* * * * *

Saa kwenye simu ilikuwa inanionyesha ni saa tisa na dakika arobaini. Nilikuwa nje nimesimama nasubiria taxi. Nilikuwa nimempigia simu Musa, dereva taxi maarufu maeneo ya mwembechai ninaye mfahamu toka niko nasoma sekondari.
Kama dakika tano baadae Musa aliwasili na bila kuchelewa kama ilivyo ada yetu waswahili nikafungua mlango wa mbele na kukaa pembeni ya dereva badala ya kukaa siti ya nyuma ambapo ndipo haswa anapotakiwa kukaa abiria.

"Niaje kichwa?" Musa akinisalimu kwa uchangamfu na tabasamu kama ilivyo kawaida yake.
"Poa tu, mishe vipi" nikamjibu na kumuuliza.
"Mishe mwanana tu mwanangu! Adimu sana kichwa vipi mtoto mzuri gani kakuficha mwanangu hahaha!" Kama kawaida Musa akaanza masikhara na kucheka kama kawaida yake.

Musa alikuwa na desturi ya kupenda masihara na mara zote yeye mwenyewe ndiye anakuwa wa kwanza kucheka kwa sauti kubwa hahahaha.
"Nifichwe wapi mwanangu! Kutafuta ugali tu." Nikamjibu.
"Nakuaminia sana baharia wangu! Alafu unajua j'mo tunawakalisha kama watoto"

Daah ndio akanikumbusha kuwa jumamosi kuna mechi kali ya Barcelena na Madrid. Mawazo niliyokuwa nayo yalinisahalisha kabisa kuwa kuna mambo mengine yanayoendelea duniani.
Musa alikuwa mnazi wa Barcelona na mimi nilikuwa mnazi wa Madrid.

"Mumkalishe nani wachumba nyinyi, subiri uone tunavyowapakata" nikamjibu nikijitahidi kuwa natural kuficha mawazo niliyo nayo kichwani.
"Tunaelekea wapi babu?" Hatimaye akaniuliza.
"Stesheni mwanangu, PPF House."
"Mia mia"

Safari ikaendelea pamoja na utani wa hapa na pale, na dakika ishirini baadae tukafika PPF.
Nikatoa noti mbili za elfu kumi nikampatia Musa. "Ya uchakavu hii mwanangu" nikampatia
"Shukrani" Musa akajibu huku anatoa shilingi efu tano anirudishie chenji.
"Zuia hiyo mwanangu usijali" nikamzuia asinipe chenji.
"Dah shukrani kichwa"
"Mia"

Tukaagana na kushuka kwenye gari nikaingia ndani ya jengo la PPF House.
Jengo hili nalifahamu vizuri sana, kuna shemeji yangu alikuwa anafanya kazi hapa miaka ya nyuma, nimewahi kufika hapa mara kadhaa lakini sikuwahi kusikia kampuni ya Unimax Marketing kuwa na ofisi katika jengo hili. Nilikuwa najua PPF wenyewe, Sumatra na kampuni nyingine kutumia jengo hili lakini sio Unimax Marketing. Na si hivyo tu bali pia hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuisikia kampuni ya Unimax Marketing.

Nikaenda mpaka kwenye meza ya kuandika majina ya wageni.
Mlinzi akaniuliza "Mfanyakazi au mgeni?"
"Mgeni" nikamjibu kwa mkato.
Akanisogozea kaunta book lililokuwa limefunguliwa liko juu ya meza.
Nikalivuta karibu na kabla sijaandika nikapitisha macho haraka haraka na niliangalia zaidi kwenye jedwali watu wanapoandika ofisi anayo kwenda. Nikaona majina tu ya PPF, Sumatta, BUMACO yakiwa yanajirudia rudia lakini sikuona Unimax Markering hata sehemu moja.

Nikaandika jina langu, kisha nikapita kwenye Mashine ya ukaguzi na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye lifti. Kwenye lifti nikabonyeza kitufe namba saba na ndani ya dakika moja mlango wa lifti ukafunguka nikiwa ghorofa namba saba.

Nilitoka na kusimama koridoni na mbele yangu kulikuwa na mlango wa kioo ulioandikwa Unimax Marketing. Nikaufungua na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye meza ya mapokezi.

"Habari yako dada" nikamsalimu mdada mrembo aliyekuwa mapokezi.
"Salama tu, nikusaida nini kaka" akaniuliza.
Nikashikwa na kigugumizi kwa sekunde kadhaa. Sikujua nimjibu nini. Anisaidie nini??.

"Aaaah natakiwa niwe hapa jina langu naitwa Ally Hassan" nikakumbuka jina nililotajiwa jana kwenye simu na nilijitahidi kujieleza kwa kumung'unya maneno.
"Subiri hapo kwenye kiti tafadhali"
Yule dada alinijibu haraka baada ya kumtajia jina la Ally hassan akionekana ameelewa ninachozungumza. Nikasogea pembeni na kukaa kwenye kiti cha wageni.

Dada akainua simu ya mezani na kumpigia mtu. "Amefika" alimwambia kwa kifupi huyo aliyekuwa anaongea nae. Baada ya hapo akawa bize anaendelea na shughuli zake. Dakika moja baadae akaja mdada mrefu, mrembo haswa amevalia sketi fupi nyeusi na shati jeupe.
"Habari, yako? Nifuate tafadhali"
Dada alinisalimu na kabla sijamjibu akanipa maelezo nimfuate.

Nikainuka na kumfuata. Kulikuwa na milango kadhaa ya ofisi yote ikiwa ya vioo, tukakata kushoto na kufuata korido iliyoenda moja kwa moja na mwishoni kulikuwa na mlango wa mbao. Yule dada akaufungua tukaingia. Ndani kulikuwa kama chumba cha daktari au theater. Nikaanza kushikwa na hofu kiasi.
Baada ya kuingia tu, akaingia mwanamama mwingine amevalia suti amebeba kibriefcace kidogo.

"Jina langu ni Zuhura na huyu mwenzangu anaitwa Jeniifer, atakufanyia utaratibu wa kawaida ili tuweze kuendelea na ratiba nyingine." Aliongea yule dada mrefu. Siku sema chochote nilibaki tu nawakodolea macho.

Yule mama aliyetambulishwa kama Jennifer akaweka kibriefcase chake juu ya meza na kukifungua. Akatoa gloves na kuzivaa mkononi. Mapigo ya moyo yakaanza kuniaenda mbio. Nikaanza kujutia kwanini hata nimekuja hapa.
Mara akatoa bomba la sindano na pamba. "Naomba mkono wako wa kushoto" yule mama akaongea.

"Hey wait!" Nikafoka huku namuangalia yule dada aliyejitambulisha kama Zuhura. "Unaweza kinambia nini kinaendelea hapa." Nikamuuliza huku natetemeka.
"Sikiliza Ray, tunaweza kuendelea na utaratibu au unaweza kufungua mlango na kuondoka" alinijibu huku amenikazia macho bila kuyapepesa.
Nikajishangaa mpaka mimi mwenyewe, Zuhura aliniruhusu kama sitaki kuendelea na 'utaratibu' wanaoufanya basi naweza kwenda,

lakini jambo la ajabu kuna sehemu kubwa ya nafsi yangu ilikuwa haitaki kuondoka, inataka kufika mwisho wa hili jambo. Ni kama unapotamani usinywe pombe lakini nafsi yako inashindwa kujizuia. Nikajifariji moyoni kuwa nimeshakula ng'ombe mzima wacha nimalizie mkia.

"Fu*k it!" nikajikuta nimetamka kwa nguvu na kumnyooshea mkono yule mama Jennifer. Atumia sindano kunitoa damu kiasi kwenye mkono wa kushoto na kisha sindano ile yenye damu akaihifadhi kwenye kifaa kama kimkebe na kurudisha kwenye briefcase yake. Kisha akatoa kifaa kama simu ya 'tablet' na kuanza kuniscan viganja vya mikono, akaanza na mkono wa kulia na kisha mkono wa kushoto. Nikaelewa alikuwa anachukua alama za vidole.
Akipomaliza akaweka vifaa vyake vyote kwenye briefcase na kuondoka.

"Tumemaliza tunaweza kuendelea sasa, nifuate" aliongea yule dada Zuhura huku akigeuka kuanza kuelekea kwenye mlango. Nikainuka na kumfuata. Tukapita tena koridoni kwenye milango ya vioo ya ofisi na kukata kushoto tukatokea mapokezi. Hapo tulimkuta jamaa ambaye jinsi alivyo vaa na umbo lake anafanana kabisa na Kevin ambaye alikuja Jana nyumbani.

Alikuwa na umbo la miraba minne na alikuwa amevalia Kaunda suti. Alipotuona akasimama. Tulipo mkaribia akafungua mlango na wote kwa pamoja mimi, Zuhura na huyo jamaa tukatoka nje kuelekea kwenye lifti.
Tukashuka chini na jamaa akatuongoza mpaka kwenye parking ya magari.

Tukapanda gari nyeusi inayofanana kabisa kabisa na waliyokuja nayo nyumbani Dr. Shirima na wenzake jana. Land cruiser V8 nyeusi.
Safari ikaanza tukaikamata Morogoro Road moja kwa moja mpaka Ubungo. Ubungo tukapinda kulia Kuifuata Barabara ya Sam Nujoma moja kwa Moja mpaka mwenge.

Kwenye makutano ya barabara tukanyoosha moja kwa moja na mbele kidogo tukakata kushoto kisha kulia. Nikaelewa kuwa tunaelekea Mikocheni B, kitu ambacho sikuwaelewa ni kwanini tumezunguka sana. Hii tayari ilikuwa imefika saa mbili usiku.

Mikocheni B tukapita Kanisa la Mlima wa Moto, tukaenda mbele kidogo mtaa wa nyuma yake. Tukaifikia nyumba moja iliyokuwa imejitenga kiasi na nyingine. Ilikuwa na uzio wa ukuta mrefu na juu una waya za umeme na geti kubwa.

Tulipofika nje ya geti hili bila kupiga honi geti likafunguliwa. Pembeni ya geti kwa ndani kulikuwa na watu wawili ambao walionekana walikuwa ni walinzi lakini walinzi hawa walikuwa na tofauti. Walikuwa wamevalia sawa kabisa na jamaa huyu tuliyeongozana nae kuja hapa na Kevin aliyekuja jana nyumbani. Wote wana miili ya mazoezi na walivalia Kaunda suti.

Nyumba hii ilikuwa na ghorofa moja na moja kwa moja jamaa akaenda kupaki gari ambapo hapa tulikuta karibia gari ishirini za aina tofauti. Range Rovers, V8, BMW, n.k. moja kwa moja nikajua gari hizi si za mtu mmoja bali kuna watu wamekuja nazo kama sisi. Hii ilimaanisha kulikuwa na kikao hapa. Na kwa muonekano wa gari hizi za gharama ni dhahiri kilikuwa ni kikao kizito.

Tukashuka kwenye gari, yule jamaa tuliyekuja naye akaelekea getini kwa 'wenzake' na Zuhura akaniongoza kuingia ndani ya Jumba hilo. Kadiri tulivyokuwa tuna pig a hatua kuingia ndani moyo wangi ulizidi kulipuka kwa hofu. Nilikuwa kwenye taharuki kubwa kiasi kwamba nilianza kutokwa jasho.
Baada ya kuingia ndani tukapandisha ngazi zilizokuwa zinaelekea juu ghorofani.

Tulivyofika juu, tukakutana na korido ndefu ambaye tuliifuata mpaka kufika katikati ilikuwa inaungana na korido nyingine ndogo mkono wa kushoto. Tukipokata kushoto kulikuwa na mlango mkubwa. Zuhura akaufungua na kunikaribisha ndani.

Kilikuwa ni chumba cha mikutano lakini hakikuwa na mtu. Kulikuwa na meza ndefu ya mikutano ya kiofisi na viti vinne kila upande.
Zuhura akaniashiria niketi.
"Subiri hapa" akanieleza kwa mkato tu kisha akatoka nje.
Ndani nikabaki peke yangu. Upande mmoja wa chumba hiki ulikuwa ni kioo tupu, hii iliniwezesha nione kwa urahisi kinachoendelea nje.

Baada ya kama dakika kumi hivi, nikaona nje geti linafunguliwa na gari tatu aina ya Range Rover ziliingia zikiwa zimeongozana. Baada ya kuingia hazikwenda kupark bali zilienda mpaka mlango wa mbele wa kuingia ndani ya nyumba. Magari mawili kati ya yale matatu, milango ilifunguliwa na watu wakashuka lakini gari la katikati milango haikufunguliwa kwa muda wa takribani dakika moja.

Wale walioshuka ambao wote wamevalia suti, waliangaza macho kila upande. Kisha wakafungua mlango wa nyuma wa gari ile ya kati kati na kuna mtu akashuka na wakaanza kuingia ndani ya jengo. Walitembea katika mtindo ambao yule mtu alikuwa katikati mbele yake kulikuwa na watu wawili, nyuma watu wawili na kulia na kushoto watu wawili wawili. Wakaingia ndani ya jengo. Nilijitahidi kadiri niwezavyo nione sura yake lakini sikufanikiwa kutokana na Giza na jinsi alivyozungukwa na walinzi.

Nikabaki nikitafakari sehemu hii nilipo. Nini kinaendelea, na kwenye hiki kitu nilichojiingiza. Nikajiuliza tena na tena, hawa watu ni akina nani, malengo yao ni nini na wanataka nini kutoka kwangu.
Niliwaza na kuwazua, nikasimama na kuanza kutembea kutoka upande mmoja wa chumba mpaka upande mwingine, tena na tena.

Baada ya kama dakika 45 msafara wa yule mtu mwenye walinzi ulitoka na moja kwa moja wakapanda kwenye gari zao na kuondoka. Kama dakika kumi baadae nikaona watu wengine karibia kumi na tano wanatoka na kwenda kupanda kwenye zile gari tulizozikuta wakati tunafika. Wote walikuwa wamevalia suti nadhifu na zote zilikuwa rangi nyeusi.
Nikajaribu kuwatazama kwa umakini niweze kung'amua walau watu wachache.

Nilipata mshtuko nilipoweza kuwang'amua watu wawili.
Wa kwanza alikuwa ni mfanyabiashara maarufu nchini na mmliki wa vyombo vya habari. Mzee Bernard Shayo
Wa pili alikuwa ni mbunge kijana na mwanasiasa mashuhuri nchini, Zephania Zuberi.

Presha ilinipanda na mshtuko nilioupata nikaanza kutokwa jasho mpaka shati nililolivaa kikaanza kulowa.
Nikakaa chini kwenye kiti. Nikitafakari, na kuwaza lakini akili ilikuwa haifanyi kazi kabisa kutokana na mshangao niliokuwa nao.

Mara mlango ukafunguliwa. Nilipigwa na butwa nilipomuona aliyeingia. Alikuwa ni Dr. Shirima akiwa amevalia suti nadhifu ya rangi nyeusi kama wale wengine niliowaona. Pia katika ukosi wa koti la suti usawa wa mfuko alikuwa ameweka pini kama ile inayovaliwa na viongozi wa kiserikali ikiwa na bendera ya nchi. Lakini pini hii ilikuwa tofauti, ilikuwa na rangi nzuri ya zambarau na kwa ndani ilikuwa na mchoro kama wa kichwa cha simba ambao ulikuwa na rangi ya dhahabu.

"Hujambo Ray?" Alinisalimia Dr. Shirima kwa tabasamu, mkononi alikuwa ameshika bahasha.
"Hapana dokta siko ok, nimeenda kwenye ofisi ambayo sijawahi kuisikia, nimetolewa damu, nimechukuliwa alama za vidole alafu naletwa hapa jumba lenye mazingira ya kutatanisha, so yes am not ok dr. Labda unieleze kinachoendelea."

Kama kawaida yake, Dr. Shirima akatabasamu "Relax Ray." Akaongea huku ananipa bahasha aliyokuwa ameishika mkononi.
Nikaipokea na kuiweka juu ya meza.

"Naomba upitie hizo document zilizomo ndani, kuna mambo namalizia kidogo nitarudi baada ya nusu saa! Zisome na uzielewe." Dr. Shirima aliongea huku ananitazama usoni kwa udadisi. "Unaonekana kama una swali Ray, uliza."
"Who are you people?" Nikamuuliza huku nimemkazia macho, nikiwa namaanisha kweli kweli.

"The Board! Karibu sana Ray." Dr. Alinijibu kwa ufupi na kutoka nje.

Nilikuwa nimebaki tena peke yangu ndani ya chumba hiki ma nikiwa na nusu saa tu kupitia hizi document kabla Dr. Shirima hajarudi tujadiki hicho anachotaka tujadili. Nikaifungua ile bahasha. Ndani kulikuwa na karatsi zipatazo kumi na karatasi ya juu ilikuwa na kichwa cha habari T.B.F.Q Strategy # 0034.

Nikaketi kwa utulivu, nikavuta pumzi ndani na kuzishusha kwa taratibu. Akili ikakaa sawa. Nikaanza kuzisoma.

The Board ni watu gani? Malengo yao ni yapi? Wanataka nini kutoka kwa Ray? Mkakati # 0034 unahusu nini?

The Bold.
 
Eeeeeh bwana eeeh? What a story?
Ni kama nilikuwa naangalia movie vile.
Mtiririko wa story ulio na maelezo ya kina kwa kila hatua umenivutia sana.
Siwezi kusubiri jumamosi...damn sipendi pressure za story kama hizi basi tu sina jinsi safari hii nimepatikana.

Story nzuri,kama kawaida hukosei honey
 
Mkuu The Bold naomba unitag ukiendelea ili nisikose. Naona ni mbali mno. Assume umeitoa last Saturday kwa hiyo iendelee leo. Hahaha.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom