Viongozi wetu wajifunze kuongoza badala ya kutawala

Mheikungu

JF-Expert Member
Oct 15, 2018
214
448
Habari za kazi wanajumui. Niwapongeze kwa sherehe za Christmas na niwatakie heri ya mwaka mpya 2019

Tunaelekea kuhitimisha safari ya kihistoria ya kumaliza mwaka 2018/ na kuukaribisha 2019, naona ni mwaka ambao utagubikwa na matukio na changamoto kali hasa kwa wana siasa tunapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.


Naomba niwakumbushe kisa cha mauaji ya Dr. KLERUU aliyekuwa R.C wa IRINGA

*MNYALUKOLO SAID MWAMWINDI ALIMUUA RC DR. KLERUU SIKU YA KRISMASI HUKO IRINGA!!!*

Leo tarehe 25/12/2018, siku ya Krismasi, ni miaka 47 imepita toka Mnyalukolo, SAID ABDALLAH SIULANGA MWAMWINDI, ammimimie risasi na kumuua aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Iringa, marehemu Dr. WILBERT KLERUU. Mauaji hayo yaliyokea tarehe 25/12/1971 kijijini Mkungugu, Isimani, Iringa.

Dr. WILBERT KLERUU alikuwa ni mzaliwa wa Mwika, Kilimanjaro ambaye alikuwa ni mmoja wa Watanzania wachache wakati huo waliokuwa na shahada ya uzamivu(PHD) ya uchumi wa kijamaa.

Dr. KLERUU alikuwa ni kipenzi cha Baba wa Taifa, Mwalimu JK NYERERE, kutokana na weledi na utendaji wake usio na mfano. Mwanazuoni mwa mwaka 1971, DR.
.KLERUU alikuwaamehamishiwa mkoani Iringa kutokea Mtwara.

Dr. KLERUU alikuwa ni kiongozi machachari sana na ilikuwa kawaida kwake na alikuwa hana hiana kuwafokea hadharani watumishi wa umma wazembe. Kwa hakika, Dr. KLERUU alikuwa mbabe sana. Akiwa Iringa, kuna wakati gari yake ilipigwa "overtake" na gari hilo lililompiga"-overtake" likamziba kwa mbele. Kufumba na kufumbua, Dr. KLERUU alishuka kama komandoo na kwenda kumuwasha vibao dreva wa gari hilo! Dr. KLERUU, mara kwa mara, alipenda kuwafokea watu kwa kuwaambia *"Hamnijui Mimi? Kawaulizeni watu wa Mtwara"* na yeye hakuwa mtu wa kukaa ofisini kama viongozi wengi wa wakati huo, bali alijumuika na wananchi na kufanya nao shughuli za maendeleo bega kwa bega ambapo ilikuwa ni kawaida kwake kushika jembe kwa masaa kadhaa bila kula!.

Kipindi hicho kulikuwa na kampeni kubwa ya kuwafanya wananchi walime mashamba ya pamoja na hivyo wakulima waliokuwa na mashamba makubwa walinyang'anywa, kitendo ambacho hakikuwapendeza Wanyalukolo waliokuwa matajiri wenye mashamba makubwa ya mahindi.

Dr. KLERUU alihamishiwa Iringa ili akatekeleze mpango huo wa serikali na alipofika tu akatangaza kwamba mashamba yote binafsi yanapaswa kuwa ya ujamaa kufikia Novemba 1971.

Bw. MWAMWINDI alihamia eneo la Mkungugu, Isimani mwaka 1954 akitokea Iringa mjini alikokuwa dreva. Alianza kilimo kidogo kidogo hatimaye akawa na mashamba makubwa ya mahindi ya hekari takriban 160. Akawa analima mashamba yake kwa trekta katika eneo hilo ambalo awali lilikuwa ni pori. Kipindi hicho, hakukuwa na sehemu Tanzania iliyokuwa ikizalisha mahindi mengi kama Isimani.

Jumamosi ya tarehe 24/12/1971, Dr. KLERUU alitembelea mashamba mbalimbali maeneo ya Tarafani, Igulu na Ndolela kuhamasisha kilimo cha pamoja. Kesho yake, Jumapili ya tarehe 25/12/1971, Dr. KLERUU( ambaye hakuwa na Jumapili wala skukuu) aliendelea na shughuli hizo za kutembelea mashamba ya wakulima.

Muda wa saa 11 jioni, Dr. KLERUU alifika kwenye shamba la MWAMWINDI na kumkuta akilima kwa trekta lake. Pamoja nae kulikuwa na mtoto wake(Mohamed) na watu wawili aliowaajiri( Yadi Chaula na Charles Mwamalata), Bw. Joseph Kusava ambaye ni mkwe wake pamoja na wake zake waliokuwa wakishirikiana nae kulima siku hiyo. Dr. KLERUU alifika shambani hapo akiendesha gari lake binafsi aina ya Peugeot 404 rangi ya bluu na ubavuni ikiwa imeandikwa RC-Iringa. Baada ya kushuka alimfuata moja kwa moja MWAMWINDI na kuanza kumuhoji maswali mengi kwanini hataki mashamba yake yawe ya ujamaa. Akamwambia *"Unafanya nini hapo?"Shuka shenzi we"*. MWAMWINDI akamuuliza *"kwanini unanitukana?"* Dr. KLERUU akamjibu *"Funga mdomo wako, n'ge n'ge n'ge nini? Kwanini nawaambia hamsikii? Blood fool"*. Katika eneo hilo walikuwa wao wawili tu kwani watu wengine walikuwa mbali kidogo. Dr. KLERUU aliyekuwa na kawaida ya kutembea na kifimbo kidogo akakitumia kumchomachoma nacho MWAMWINDI.

MWAMWINDI akafura sana hivyo akaanza kwenda ndani kupitia eneo la makaburi ya baba yake na ndugu wengine huku Dr. KLERUU akimfuata na alipoyaona makaburi akasema *"Tazama unaendelea kujenga nyumba za kudumu"*. MWAMWINDI akamjibu *"Hizi sio nyumba, ni mahali ninapozika ndugu zangu"*. Dr. KLERUU akajibu *"Ni mahali unapozikia mirija wenzio, mbwa we!"*.

Mnyalukolo MWAMWINDI akawaamehamaki sana. Akasema *"Swela"*, akaingia ndani akachukua gobore akatoka nalo nje na kumfyatulia risasi Dr. KLERUU ambaye alianguka na kufariki hapohapo!!! MWAMWINDI aliuchukua mwili wake akauweka kwenye buti ya gari ya Mkuu huyo wa Mkoa, akachukua na kofia ya Pama ya Mkuu wa Mkoa akaivaa yeye na kuanza safari ya kilometa 40 kwenda Iringa mjini.

Mjini Iringa, watu walishangaa kuona gari ya Mkuu wa mkoa inapita upande wa kulia kwa vile mtaa wa Jamatini ulikuwa ni "One way" lakini wakahisi huenda Mkuu wa mkoa ana dharura. Saa 1 jioni, MWAMWINDI akafika kituo kikuu cha polisi akaenda moja kwa moja kaunta akamkuta PC MBETA KASONDA na kukwambia *"Ebu nenda kwenye buti ukaitoe mbwa yenu nimeishaiua"* na kumkabidhi bunduki pamoja na funguo za gari. PC KASONDA hakuamini macho yake alipouona mwili wa Dr. KLERUU ukiwa umetapakaa damu. Dr. KLERUU alikuwa amevaa ovaroli nyeusi na miwani. Hivyo, mara moja PC KASONDA akamuweka MWAMWINDI chini ya ulinzi. Mtu mwingine aliyekuwepo kituoni hapo ni mzee DAVID BUTITINI(ambaye alikuwa askari polisi na baadaye kada wa CCM Iringa). Tarumbeta likapulizwa na askari wakakusanyika na kupewa rasmi taarifa ya kifo hicho cha Mkuu wao wa mkoa na gari lake likahifadhiwa nyuma ya kituo cha polisi. Askari wanne wakaenda kuleta kitanda cha magurudumu toka hospitali na hatimaye mwili wa Dr. KLERUU ukapelekwa "mortuary". Kesho yake, siku ya jumatatu, mji mzima wa Iringa uligubikwa na simanzi kubwa.

Kuna kundi la watu ambao walikuwa wakimchukia sana Dr. KLERUU kutokana na aina ya uongozi wake hivyo lilipopata tu taarifa za kifo chake wakanunua makreti ya bia usiku huohuo na kuanza kunywa kwa kushangilia hadharani! Msako ulipoanza usiku huohuo, jamaa hao walikuwa wa kwanza kukamatwa!.

Mzee BUTININI ambaye pia alikuwa Mtwara wakati DR. KLERUU alipokuwa Mkuu wa Mkoa, anakiri kuwa ni kweli DR. KLERUU alikuwa mtu wa shoka- *"Ni kweli hata kule Mtwara alionekana mtemi sana mwenye kuhimiza mambo kwa nguvu. Lakini lazma muelewe maeneo ya Mtwara yalikuwa ya vita na tulikuwa tukiwasaidia ndugu zetu wa Frelimo hivyo kule kulihitaji mtu kama DR. KLERUU. Mtwara DR. KLERUU hakukumbana na upinzani ila Iringa hali ilikuwa tofauti. Kwa mawazo yangu, Dr. KLERUU alipaswa kwanza kujifunza juu ya mila na desturi za watu wa Iringa. Maana watu wa Iringa ni watu wa Iringa tu."*

Mauaji hayo ya Dr. KLERUU yalimsikitisha sana Mwalimu NYERERE, wakuu wa mikoa na wananchi mbalimbambali. Lilikuwa ni tukio lililoongelewa nchi nzima. Majirani na wazee wengi waliokuwa wakilima pamoja na MWAMWINDI walisombwa na vyombo cha usalama na kumwekea ndani kuisaidia polisi ambapo walikuwa wakikamatwa na kusafirishwa usiku kwa ndege za jeshi. Takribani watu 30 walikamatwa wakiwemo wazee maarufu kama IBRAHIM KHALILI, PESAMBIL, MURSALI na wengineo na kupelekwa sehemu mbalimbali za nchi mf Shinyanga, Mwanza na Zanzibar. Cha kusikitisha ni kwamba ndugu zao hawakujua wamepelekwa wapi! Aidha, nyumbani kwa MWAMWINDI huko Mkungugu kukawa kunalindwa na askari wa FFU muda wote.

Kitendo cha kukamatwa majirani na marafiki wa MWAMWINDI kilileta uhasama mkubwa baina ya ndugu wa majirani hao na familia ya MWAMWINDI.

Ikabidi mwanae (AMANI MWAMWINDI)(21) alazimike kutafuta kibali cha DC Iringa kwenda gereza la Dodoma alikokuwa anashikiliwa MWAMWINDI. Alipoganikiwa kukipata alikwenda na akamueleza hali hiyo ambayo ilimsukitisha sana Mzee MWAMWINDI. AMANI akamshauri baba yake aandike barua kwa Rais NYERERE, nae akafanya hivyo siku hiyohiyo. Katika barua hiyo, MWAMWINDI alimueleza Mwalimu kwamba yeye ndiye aliyemuua Dr. KLERUU hivyo wengine hawahusiki hivyo waachiwe. Baada ya kupita siku kadhaa, wazee hao majirani wakaachiwa na kurejea kijijini hapo, Isimani. Hata hivyo, tafrani hiyo iliyokuwaimewakumba ikafanya wengi wahame eneo hilo kwani waliishaona "togwa limeingia nzi"!.

Upelelezi wa mauaji hayo ulienda haraka na MWAMWINDI akafunguliwa kesi ya mauaji ya kukusudia Mahakama kuu. Kesi ilipoanza kusikilizwa, ilivuta hisia za watu wengi na umati wa watu uliokuwa ukitamalaki kila siku mahakamani ulikuwa "si wa nchi hii!.

Tarehe 2/10/1972, baada ya mashahidi wa pande zote kutoa ushahidi wao akiwemo RPC wa Iringa (Abubakar Hassan) aliyetoa ushahidi upande wa MWAMWINDI kwamba hakuwa na taarifa kwamba Mkuu huyo wa Mkoa angetembelea eneo hilo ndio maana hakumpa "Police escort", Jaji GABRIEL CHIKE ONYIUKE toka Nigeria(aliyehudumu Tanzania toka 1970-1973) alimtia MWAMWINDI hatiani na kumuhukumu kunyongwa hadi afe. Hii ilikuwa ni baada ya kuukataa utetezi wake kwamba alitenda kosa hilo baada ya kurukwa na akili na pia alikasirishwa "provoked" na marehemu, Mh. Jaji aliona kwamba ingawa ni kweli MNYALUKOLO wa kawaida huwa si mtu wa mchezo-mchezo anapodhihakiwa hasa mbele za wake zake lakini kitendo cha MWAMWINDI cha kwenda ndani kufuata bunduki kilionesha, pasina shaka, kwamba aliua kwa kudhamiria.

Adhabu hiyo ya kifo ilitekelezwa mara moja kwani Mwalimu NYERERE alisaini hati ya kifo cha MWAMWINDI
. Hayo hiyo, ilikuwa ni moja ya hati tatu za vifo zilizosainiwa na Mwalimu NYERERE kuidhinisha kunyongwa kwa binadamu katika uongozi wake wa miaka 24 katika taifa hili.

Kesi hii ilikuwa ya aina yake na haikuchukua hata mwaka mmoja toka tukio kutokea na adhabu kutolewa tofauti na kesi nyingine za mauaji ambazo, kwa kawaida, huchukua miaka mingi kabla ya hukumu kutolewa. Kesi hii ilichukua miezi kumi tu.

Baada ya msiba, familia ya DR. KLERUU ilirudi Kilimanjaro. Hata hivyo, Mwalimu NYERERE na KARUME na baadae ABDU JUMBE walikuwa karibu sana na mjane wa DR. KLERUU na wakawasomesha wanawe nchini Urusi na Bulgaria. Aidha, viongozi wengine waliwatia moyo na kuwafariji sana mf. Marehemu Mzee RASHID KAWAWA na mama GETRUDE MONGELA. Dr. KLERUU aliacha watoto wanne.


Tujifunze kupitia tukio hili kwasababu naona kina KLERUU na kina MWAMWINDI bado wapo kwenye jamii zetu. Mwosha huoshwa
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom