Viongozi wajifunze kupima uzito wa hoja, si mtoa hoja | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Viongozi wajifunze kupima uzito wa hoja, si mtoa hoja

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Mbonea, Oct 9, 2009.

 1. Mbonea

  Mbonea JF-Expert Member

  #1
  Oct 9, 2009
  Joined: Jul 14, 2009
  Messages: 640
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  [​IMG]
  [​IMG]
  KWA bahati nzuri, uhuru wa kutoa maoni hapa nchini hautokani na ridhaa ya chama chochote cha siasa iwe kupitia vikao vyake rasmi au vinginevyo, na hasa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Na zaidi, uhuru huo wa kutoa maoni pia hautokani na uamuzi binafsi wa viongozi kuanzia wa serikali, taasisi nyingine binafsi na hata za kimataifa, wakiwamo wafadhili.
  Uhuru wa maoni nchini ni fursa inayotolewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo basi, uhuru wa kutoa maoni hautokani na uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania binafsi, Makamu wake, Waziri Mkuu au viongozi wengine waandamizi wa CCM.
  Kinyume chake, uhuru huo wa kutoa maoni haupaswi kuhujumiwa na wakuu hao kwa njia zozote. Katiba inawashurutisha kulinda uhuru wa kila mtu katika kutoa maoni yake, kwa masharti kuwa mhusika havunji sheria. Ndiyo, Katiba inawashurutisha kuwa wameapa kuilinda na kuitetea.
  Lakini wakati Katiba ikitambua au kutoa fursa ya kuwapo kwa uhuru wa maoni nchini, fursa hiyo imeanza kutumiwa vibaya kwa njia mbalimbali na leo nitazungumzia upande wa baadhi ya viongozi. Njia mojawapo ni baadhi ya viongozi walioko madarakani kutumia fursa yao ya uhuru wa maoni kupinga kwa njia inayoweza kutafsiriwa kuwa ni kuhujumu fursa ya uhuru wa maoni, kwa watu wengine.
  Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sehemu ya kwanza inaeleza; ‘‘Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.’’
  Kwa viongozi, wakiwamo wa CCM kumeanza kujitokeza baadhi yao wanaoona kuwa kitendo cha viongozi wenzao wakiwamo wastaafu, kutoa maoni au ukosoaji hadharani ni dhambi kubwa. Wamekuwa na mtazamo huo hasi kwa kuzingatia vigezo hafifu, na zaidi wameamua kufanya jaribio haramu la kutisha au kuzima ushauri au ukosoaji husika.
  Viongozi hao wanaokerwa na wenzao kutoa maoni wamekuwa wakiwataka kutumia vikao vya chama chao kufanya hivyo. Binafsi sikubaliani nao katika baadhi ya maeneo, na hasa kwa ushauri unaolenga kuwataka viongozi wa umma (si wa chama) kujirekebisha mwenendo wao, kwa manufaa ya taifa au kwa lugha nzuri kwa manufaa ya kila Mtanzania.
  Nimeanza kuamini kuwa huenda wanaokasirishwa na ushauri wa hadharani wana ajenda ya siri, ambayo haibebi maslahi ya taifa. Kwa mfano, ni kwa nini viongozi waliopo madarakani wahofie wananchi kusikia ushauri unaowata kujirekebisha katika kupunguza pengo lililopo kati ya masikini na matajiri?
  Au ni kwa nini viongozi waliopo madarakani wakasirike wanaposikia mwenzao mmoja na hasa mstaafu, ameshauri au kukosoa hadharani kuhusu serikali kujiweka karibu mno na matajiri pamoja na wawekezaji wa kigeni, na wakati huo huo wakiwasahau wananchi?
  Ni kwa nini viongozi waliopo madarakani iwe serikalini au katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) wahofie kusikia ushauri kutoka kwa viongozi waliowahi kushika nyadhifa za kidola, wakitoa maoni yao kuhusu uzoefu wao wa kiutendaji enzi zao na hali wanayoiona sasa? Nini msingi wa hofu hiyo? Je, ni kupoteza madaraka au kuingilia ulaji wa waliopo madarakani?
  Nimetumia maneno uzoefu wao katika kushika nyadhifa za dola na si za CCM kwa sababu moja kubwa. Sababu hiyo ni kwamba, unapokuwa kiongozi wa serikali maana yake unakuwa mtumishi wa wananchi wote, tofauti na unapokuwa kiongozi wa chama cha siasa ambapo unakuwa kiongozi wa kundi fulani miongoni mwa mamilioni ya Watanzania.
  Hivyo basi, ushauri au ukosoaji unaotoka kwa mtu aliyewahi kuwa kiongozi wa serikali (dola) ni mzito zaidi ikilinganishwa na mtu aliyewahi kuwa kiongozi wa chama, hata hivyo, ushauri wa ukosoaji husika uzito wake ni vema ukapimwa zaidi kwa kutazama namna utakavyolisaidia taifa, na wananchi kwa ujumla.
  Hata kwa wanaoaguswa na ushauri wa ukosoaji husika, matakwa ya busara hayawaelekezi kuwa na jazba au kushambulia wanaowashauri. Matakwa ya busara yanawataka kuwa watulivu kifikra na kutafakari namna ya kujikwamua na ukosoaji huo au namna ya kutekeleza ushauri wenye manufaa kwao na kwa taifa.
  Natambua kuwa wakati mwingine yapo masuala ambayo hayapaswi kuzungumzwa hadharani na badala yake yanastahili kuzungumzwa katika vikao rasmi vya wahusika. Hata hivyo, pamoja na kutambua hivyo ni vema kuwapo na mipaka juu ya mambo gani yanastahili kuzungumzwa ndani ya vikao na yapi yanastahili kuzungumzwa hadharani.
  Lakini pamoja na kutambua huko kwamba yapo yanayostahili kuzungumzwa hadharani na mengine faragha katika vikao rasmi, bado naamini kuwa mzani umeleemea upande wa mambo yanayopaswa kuzungumzwa au kushauriwa kupitia umma na hususan kupitia vyombo vya habari. Wakati mwingine ni busara zaidi kuacha vikao vichukue nafasi ya kupanga na kutafakari namna ya kutekeleza ushauri au kufanyia kazi ukosoaji.
  Naamini hivyo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ile ya kutimiza bila shaka yoyote dhana ya uwazi na ukweli. Katika nchi inayojizatiti kujiendesha kidemokrasia, tena si demokrasia bandia bali ni demokrasia pevu, inayoheshimu na kufurahia uhuru wa maoni ushauri unaotolewa kwa viongozi kupitia umma ni bora zaidi na unabeba nguvu za uhalali.
  Ushauri wa namna hiyo ni bora na unabeba nguvu kubwa za uhalali kwa kuwa mhusika atakuwa amejipanga vizuri, atahakikisha ushauri wake hauundwi kwa vigezo vya unafiki, fitina au malengo haramu ya binafsi. Atajipanga kutoa ushauri bora na madhubuti kwa kuwa umma utasikia na kumpima. Maana yake ni kwamba; mbele ya umma, mkosoaji au mtoa ushauri ataweza kujitafutia hukumu yake.
  Umma kwa upande mmoja na viongozi waliolengwa kwa upande mwingine, tena kwa wakati unaofanana watakuwa na jukumu la kuchekecha ushauri au ukosoaji husika. Watalinganisha matokeo ya ushauri au ukosoaji huo kama utalenga kuboresha mustakabali wa taifa lao au la.
  Tunayo mifano mingi ya ushauri uliowahi kutolewa kwa siri kwenye vikao na baadaye ushauri huo, na hasa baada ya kutekelezwa ukaonekana wa kipuuzi mbele ya wananchi. Ukaonekana ushauri wa kinafiki, unaolenga kutimiza malengo ya kikundi cha wachache kujiimarishia himaya yao ya uovu.
  Kwa mfano, tumeelezwa kuwa katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM mjini Dodoma kuna ushauri ulitolewa ndani ya kikao hicho kwamba Spika wa Bunge avuliwe uanachama kwa kuwa anaendesha mijadala ya ufisadi kwa uwazi na hivyo anakiumiza chama na serikali (badala ya kuumiza wahusika), lakini ikashindika. Mfano huu ni aina ya ushauri ambao umejaa unafiki na malengo binafsi, na ni ushauri ambao mbele ya umma ungemdhalilisha mzungumzaji, lakini ndani ya kikao ulipata waungaji mkono ambao kwa mtazamo wa kawaida watakuwa na malengo yanayofanana na mtoa ushauri.
  Hii maana yake ni kwamba, ndani ya vikao ingawa ni vizuri kupitisha baadhi ya ushauri au ukosoaji humo lakini ukweli bado unabaki kuwa kuna nafasi kubwa ya unafiki sambamba na juhudi za kufanikisha malengo binafsi.
  Hivyo basi, kwa masuala yanayohusu mustakabali wa wananchi moja kwa moja na katika mazingira yasiyo ya ulazima wa vikao, ni vizuri ushauri kutolewa kupitia umma. Viongozi wa kitaifa wafikishiwe ushauri au ukosoaji kuhusu masuala ya nchi kupitia umma ili fursa ya mchujo wa ushauri huo au ukosoaji huo iwe pana na shirikishi.
  Viongozi wetu wamekuwa wakihimiza dhana ya utendaji na uamuzi shirikishi, tujiulize, je, ni kwa nini baadhi yao hawako tayari kupokea au kusikia ushauri au ukosoaji wa wazi dhidi yao? Kwa nini kila jambo hata ushauri au ukosoaji dhidi yao uwe siri? Je, tumewachagua kwa siri ili waendeleze usiri na waipeleke nchi huko wanakotaka kwa siri?
  Ninachofahamu, viongozi wetu wameomba kura hadharani, wakapigiwa hadharani. Wamekula kiapo hadharani, wanapaswa kuendesha nchi kwa mfumo wa kuimarisha uwazi kiutendaji na hivyo kuruhusu ukosoaji wa haki na wa wazi, dhidi yao na pia kutoa kipaumbele kupata ushauri wa wazi, unaopitia au kusikika kwa umma.
  Kukasirishwa na ushauri unaofikishwa kwao kwa njia ya kushirikisha umma ni makosa makubwa na si jambo la kujivunia kwa kiongozi makini wa kisiasa, na ambaye mwenye ndoto ya kuweka rekodi bora ya kiuongozi nchini. Kiongozi bora wa kisiasa ni yule aliyeko tayari kufungua milango ya ushauri na ukosoaji kupitia njia zote, lakini wakati huo huo, awe mgumu kukubali njia zinazoruhusu ushauri wa kinafiki, ambao katika hali ya kawaida, hutolewa ndani ya vikao.
  Kama nilivyoeleza awali, kuna tofauti kubwa na manufaa makubwa kwa nchi, kati ya ushauri unaotolewa kwa njia ya siri (vikaoni) na ushauri unaotolewa kwa kushirikisha umma (mfano mikutano ya hadhara au vyombo vya habari). Hasara za ushauri wa siri ni kubwa zikiwamo kujipenyesha kwa kiasi kikubwa cha unafiki, kuliko uhalisia.
  Nitoe ushauri wangu kwa viongozi wote kwamba, wasifadhaike wanaposhauriwa au kukosolewa mbele ya umma watambue kuwa hizo ndizo gharama za kupigiwa kura au kuteuliwa kuwa viongozi. Badala ya kujibu mashambulizi au kutaka kutumia mbinu nyingine haramu za kumdhalilisha mtoa ushauri au mkosoaji, wanapaswa kutafakari uzito wa ushauri au ukosoaji husika bila kutanguliza jina la mhusika, itikadi yake au vinginevyo.
  Viongozi wawe tayari kupokea ushauri kwa kupima uzito au mantiki ndani ya ushauri huo na si kwa kutazma aliyetoa ushauri huo yupo kwenye kundi la siasa pinzani au la.
  Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
   
 2. Waberoya

  Waberoya Platinum Member

  #2
  Oct 9, 2009
  Joined: Aug 3, 2008
  Messages: 11,582
  Likes Received: 3,883
  Trophy Points: 280
  Mkuu umesema vyema, lakini hili ni janga la kitaifa, Huwa hatuwatengenezi hawa viongozi, wanafikia ngazi za kitaifa ndiyo tunataka wafanye vitu ambavyo hawakulelewa navyo, hawajui.

  Tumerithi ile 'zidumu fikra za mwenyekiti;

  viongozi hawashauriki, kwani ni miungu watu
  hawajui kuwa wanatakiwa kuwa watumwa na sio maboss, hili nalo tumerithi(angalia wanavyojinunulia magari) you can tell

  tabia za kiongozi zinatakiwa zifundishwe tangu primary, pamoja na masomo ya mazingira na ufundi.

  maana uongozi unaanzia nyumbani.
   
 3. Ndahani

  Ndahani JF-Expert Member

  #3
  Oct 9, 2009
  Joined: Jun 3, 2008
  Messages: 14,324
  Likes Received: 1,791
  Trophy Points: 280
  Ndio maana tunazungumzia haja ya kubadilika. Bila kukubali mabadiliko ambayo huja kama watu wana nia ya kusoma mazingira basi tutaishia kwenye shida kubwa.Ukweli ni kuwa watu wengi hawawatambui viongozi kama miungu watu hata kama wao wanajichukulia hivyo. Kwa mantiki hiyo ipo siku wanaweza kukataa kuburuzwa.Hilo nalo sio jambo linalohitaji mtabiri kuliona maana liko wazi.
  Ugumu wa kukubali mabadiliko unatokana na sababu za kimaslahi zaidi kuliko utaifa. Ndio maana kila linalosemwa na watu wanaoshauri linaonekana kama jaribio la maadui zidi ya watawala
   
 4. Mbonea

  Mbonea JF-Expert Member

  #4
  Oct 9, 2009
  Joined: Jul 14, 2009
  Messages: 640
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  uko ryt Mkuu Ndahani
   
 5. Dr. Chapa Kiuno

  Dr. Chapa Kiuno JF-Expert Member

  #5
  Oct 9, 2009
  Joined: Sep 11, 2009
  Messages: 445
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  Serikali yetu hii........
   
Loading...