Viongozi wa dini wapinga ubabe wa serikali dhidi ya vyombo vya habari....

only83

JF-Expert Member
Oct 15, 2010
5,343
2,525
MAASKOFU wamelaani hatua ya serikali ya kulifungia gazeti la MwanaHalisi na kusema kuwa kitendo hicho kinaashiria kuua uhuru wa vyombo vya habari nchini.


Julai 30 mwaka huu, serikali ililifungia gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na mwenendo wake wa kuandika habari na makala za uchozezi.


Wakizungumza na Tanzania Daima jana, kwa nyakati tofauti, maaskofu hao walisema kuwa, hatua ya kufungia vyombo vya habari haioneshi taswira njema na haikubaliki kwa jamii iliyojengwa katika misingi ya demokrasia.


Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, alisema kuwa hatua ya kukifungia chombo cha habari inaashiria wazi kuwa serikali haipo tayari kupokea taarifa zinazotolewa na jamii.


“Hali hiyo imetupa shaka hata sisi maaskofu, kwani ni wazi kuwa wanaweza kutunyamazisha hata viongozi wa dini iwapo tutakuwa tukiwakosoa,” alisema.


Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa, alisikitishwa na kitendo hicho na kusema kuwa jambo hilo limeathiri jamii nzima.


Alisema kuwa taarifa zilizokuwa zikitolewa na gazeti hilo ziliwasaidia katika kukaa na kulikomboa taifa na hata wakati mwingine kuweza kuishauri serikali.


Dk. Mokiwa, alisema, kuzuiwa kwa chombo hicho kumewanyima fursa ya kujua sehemu ya kusimamia na hata jinsi ya kuisadia serikali ili iweze kuenda katika mstari unaotakiwa.


“Tumesikitika sana maana gazeti hilo lilikuwa ni msaada mkubwa kwetu sisi viongozi wa dini, ni muhimu kukubali kukosolewa na jamii kwani kukubali kusifiwa pekee ni kubaya, maana hiyo ni sawa na methali ya unapakwa mafuta kwa mgongo wa chupa,” alisema.


Naye, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Antony Makunde, alisema kuwa, serikali haikupaswa kuchukua uamuzi huo bali ingekaa na gazeti hilo na kushauriana.


Hata hivyo, alivitaka vyombo vya habari kuhakikisha vinazingatia misingi ya uandishi ili kuepuka kutokea kwa migogoro inayoweza kuhatarisha amani nchini.


Kwa mujibu wa serikali, sababu nyingine iliyosababisha kufungiwa gazeti hilo ni pamoja na kujenga uhasama na uzushi, likiwa na nia ya kusababisha wananchi wakose imani na vyombo vya dola, hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa nchi.
 
Back
Top Bottom