Na Kelly Ogome
Umoja wa Afrika AU umeipongeza China kwa mchango wake mkubwa katika kuleta maendeleo barani Afrika.
Amani Abou-Zeid, kamishina wa miundombinu na nishati wa Umoja wa Afrika amesema, China ni mshirika mkubwa katika kufanikisha maendeleo barani Afrika kupitia ujenzi wa miradi ya maendeleo kama vile barabara, mabwawa, reli na miradi mingine ambayo imebadilisha sura ya Afrika na kuchochea maendeleo ya bara zima.
Unapozuru nchi zote za Afrika, utajionea miradi kadhaa mikubwa iliyojengwa au hata kufadhiliwa na China. Miradi hii iko kwenye sekta zote muhimu kama vile afya, kilimo na elimu. Taasisi kadhaa za elimu zina maktaba au maabara za kisasa za utafiti zilizojengwa na China. Nchi nyingine zina hospitali za haiba kubwa ambazo ujenzi wake ulifadhiliwa na mashirika au serikali ya China; yote haya yanadhihirisha juhudi za China katika kuibadilisha Afrika kwa manufaa ya Waafrika wote na wageni.
Kwenye mkutano wa mawaziri wa nchi za Afrika ulioandaliwa na Umoja wa Afrika wiki iliyopita jijini Addis Ababa Ethiopia, jitihada za China za kufanikisha maendeleo ya Afrika zilitambuliwa na kupongezwa. Mkutano huo wa mawaziri ambao uliandaliwa kwa mara ya kwanza baada ya janga la Covid-19 kutikisa ulimwengu uliegemea sana mazungumzo ya namna Afrika inavyoweza kujenga mfumo thabiti pamoja na kuharakakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia miradi tofauti- na ikabainika kuwa China ni mojawapo ya nchi zinazoweza kuisaidia Afrika kufikia yote haya.
‘’Tunashirikiana na nchi nyingi kufanikisha maendeleo katika sekta mbali mbali. China ni mojawapo ya washirika wetu wakubwa katika kufanikisha ujenzi wa miundombinu. Nafahamu kuwa ni kupitia maendeleo ya aina hii pamoja na kupatikana kwa nishati ndipo Afrika itajiendeleza’’ alisema kamishna Amani Abou-Zeid.
Kando na kushirikiana na watu binafsi katika miradi ya kuwainua raia, taasisi za China pamoja na serikali kuu zinafanya kazi kwa karibu na Umoja wa Afrika kufanikisha ruwaza ya AU ya miaka 50 ifikapo mwaka wa 2063. Ruwaza hii inalenga kujenga Afrika yenye amani na mafanikio iliyojengwa na Waafrika.
‘’Sisi kama makamishina wa Umoja wa Afrika, tunashukuru na kupongeza mfumo ambao China imechukuwa kushirikiana nasi katika miradi inayofungamana na ruwaza yetu ya mwaka 2063’’ aliongeza bwana Amani Abou-Zeid.
Afrika pia inaendeleza mipango ya ushirikiano na China katika kupanua matumizi ya teknolojia, kuboresha elimu na utafiti ili kwa pamoja kujenga nchi zinazojitegemea. Hili linaweza kudhihirishwa kwa kukamilika kwa baadhi ya vituo vya utafiti kama vile maabara za Luban zilizoendeshwa na taasisi za Afrika kwa ushirikiano na taasisi ya Tianjin ya China.
‘’Tunafanya mambo mengi katika sekta za elimu, utafiti, uvumbuzi na teknolojia kwa kushirikiana na China. Tumeweza kuileta China na Afrika pamoja na kupitia Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, tumetekeleza na tunaendelea kutekeleza miradi mikubwa zaidi hapa Afrika.’’ alisema Hambani Masheleni kaimu wa kitengo cha Elimu, Sayansi, Teknolojia na uvumbuzi katika Umoja wa Afrika.
Takwimu kutoka taasisi ya utafiti ya China-Africa zinaeleza kuwa Angola, Ethiopia, Zambia, Kenya na Nigeria zote ni nchi za Afrika zinazoshirikiana kwa karibu sana na China katika uwekezaji kwenye sekta ya ujenzi wa miundombinu huku mwaka wa 2016 ukiwa mwaka ambao Afrika ilitia saini mikataba mingi ya makubaliano kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu iliyofadhiliwa na China.