Viongozi wa Afrika wahimizwa kupambana na al Qaeda

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125


Mtandao wa al Qaeda umechukua mkondo wa kutia wasiwasi Afrika

Rais wa Senegal Abdoulaye Wade ameutoa mwito huo kwa viongozi wa Umoja wa Afrika wakati walipokuwa wakijadiliana kutafuta njia za kukabiliana na majanga na mizozo inayolikabili baraza zima la Afrika. " Lazima tuandae mkutano maalum pamoja na nchi jirani ili tulitatue tatizo hili la kundi la al Qaeda katika eneo la kiislamu la Maghreb," amesema rais Wade kwenye mahojiano yake na shirika la habari la AFP na redio ya kimataifa ya Ufaransa, pembezoni mwa mkutano wa 14 wa viongozi wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.

Rais Abdoulaye Wade amesema nchi kama Senegal au Mali haziwezi kufanya kitu chochote dhidi ya al Qaeda na kuyataka mataifa ya magharibi yaingilie kati kusaidia kwa kuwa tatizo la al Qaeda ni la kimataifa. Kiongozi huyo wa Senegal pia ameonya juu ya biashara haramu ya silaha inayoendelea katika eneo la Sahel na kuzitaka pia nchi za magharibi zijihusishe kupambana na biashara hiyo, bila kutoa ufafanuzi wa kina.

Wanagambo wa kitengo cha al Qaeda Kaskazini mwa Afrika wametishia kumuua mateka wa rehani raia wa Ufaransa waliyemteka nyara nchini Mali mnamo mwezi Novemba mwaka jana. Wanamgambo hao pia wanawazuilia mateka wengine watano raia wa Ulaya katika eneo hilo.
Rais Abdoulaye Wade amesema ana matumaini utawala wa kijeshi nchini Guinea utaheshimu na kutimiza ahadi yake ya kutoshiriki kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu nchini humo. Amesisitiza kwamba makubaliano ya Ougadougou yaliyosimamiwa na Burkina Faso ni mwanzo tu na sharti viongozi wa Afrika wawe macho kuangalia kitakachotokea nchini Guinea.
Rais Wade ameyasema hayo wakati viongozi wa Afrika walipokuwa wakishauriana kuhusu mikakati ya kukabiliana na hali ya wasiwasi inayojitokeza huko Sudan Kusini na maeneo mengine ya mizozo barani Afrika. Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi ameonya kwenye mkutano huo kwamba Sudan inaweza kugeuka na kuwa kama Somalia.



Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon aliyekuwepo siku ya kwanza ya mkutano wa mjini Addis Ababa amezungumzia mustakabal wa Sudan.

"Tutatafuta njia za kufikia makubaliano miongoni mwa nchi wanachama. Tutaendelea kuimarisha kuwepo kwa maafisa wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan. Tutaendeleza mdahalo kuhusu maswala ya baada ya kura ya maoni. Tutajenga na kuimarisha taasisi za Sudan Kusini. Na pia lazima tuendelee kushirikiana kuimarisha uhusiano mwema kati ya Chad na Sudan."

Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka nchini Sudan huku kura ya maoni ikitarajiwa kufanyika ifikapo mwaka 2011 ambapo Sudan Kusini inatarajiwa kuchagua kuwa huru kutoka kwa utawala wa mjini Khartoum, miaka sita tu tangu mkataba wa amani kusainiwa. Wachambuzi wanahofu kujitenga kwa Sudan Kusini huenda kukavuruga amani katika eneo ambalo linakabiliwa na hali mbaya kiusalama barani Afrika.

Wakati huo huo viongozi wa Afrika hii leo wamewataka viongozi wanaohasimiana nchini Madagascar waheshimu makubaliano yaliyofikiwa kwa lengo la kuutanzua mzozo wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo.

http://www.dwelle.de/dw/article/0,,5202203,00.html
 
Back
Top Bottom