Viongozi vijana, mnayo changamoto kubwa, msituangushe!

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
UKURASA mpya umeandikwa katika vyombo vya aamuzi kwa ongezeko la vijana wawakilishi, tofauti na chaguzi za awali. Kupata wabunge vijana wa kuchaguliwa takribani 15 (CCM (4), CHADEMA (8), NCCR-Mageuzi (3) tofauti na matokeo ya awali katika chaguzi ya mwaka 2005 ambako kulikuwa na mbunge mmoja tu wa kuchaguliwa, Zitto Kabwe toka Kigoma Kaskazini.

Kijana tunayemzungumzia hapa ni kwa mujibu wa sera ya Taifa ya vijana ambayo inamtafsiri kijana kama mtu mwenye umri wa miaka kati ya 18-35.

Idadi kubwa hiyo ni zao la juhudi kubwa na za muda mrefu za wadau mbali mbali mathalan asasi za kiraia hususan za vijana kupiga chapuo hitaji la ongezeko la uwakilishi wa vijana katika ngazi za maamuzi.

Lakini hatuwezi kupuuza usikivu wa vyama vya kisiasa ambavyo viliweza kuona tunu ya wito wa kuwekeza kwa vijana kwa kuwapa ridhaa vijana kusimama kama wagombea katika majimbo. Hakika imedhihirisha inawezekana!

Ushindi ambao vijana wengi wameweza kuupata ni taswira pana ya mabadiliko ya kimtazamo kuwa vijana si tu wasindikizaji ama wapambe wa wagombea bali wao pia wanaweza kuwa wagombea na kuwa wawakilishi wa wananchi katika ngazi za maamuzi.

Imani ambayo Watanzania wamewekeza kwenu vijana wabunge kupitia kura zao mnapaswa mjitahidi kuishi kwa vitendo, mnapaswa irejeshe imani hiyo kwa utumishi uliotukuka kwa kusimamia maslahi ya wananchi.

Vijana waliofaulu kuchaguliwa kuwa wabunge wasisahau wao ni sampuli ndogo miongoni mwa vijana wengi ambao wanauwezo na utashi wa kuwatumikia wananchi hususan kwa kuwakilisha katika vyombo vya kimaamuzi, hivyo ni jukumu lao kuenenda na kuthibitisha vijana ni tunu na hazina katika mabadiliko.

Licha ya majukumu mazito ya wabunge vijana wa kuchaguliwa wanayo dhidi ya wananchi wao katika majimbo yao, kundi la vijana haliwezi kuacha kuwaangalia wao kama watetezi pekee wa ajenda na vipaumbele vya vijana.

Baadhi ya ajenda ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele kwa zaidi ya miaka mingi sana na vijana toka makundi mbali mbali kama asasi za kiraia za vijana, taasisi za kisiasa, taasisi za kitaaluma nk tena baadhi ya vijana waliokuwa katika harakati hizo miongoni mwao sasa wamefaulu kuwa wabunge, tunatarajia wataendelea sasa kusimamiwa kidete katika ngazi ya juu na uwezo wa ushawishi wa kimaamuzi kwa bunge na serikali nzima.

Mwaka 2010 kama ilivyokuwa mnamo mwaka 2005 asasi za kiraia kadhaa zenye kujihusisha na masuala ya vijana zikiratibiwa na asasi ya TYVA zimeweza kukusanya na kutathmini vipaumbele vya vijana na Taifa zima kwa ujumla. Vipaumbele ambavyo kwa asilimia kubwa ndivyo vilio vya vijana hivyo tunapaswa kuwakumbusha tena na tena wabunge vijana ambao ni wawakilishi wa sampuli ya vijana katika vyombo vya kimaamuzi kuweza kuvitetea.

Ni kundi hili dogo la vijana wabunge ambao vijana wote wa kitanzania wanaweka matumaini yao kuwasikia wakiwa mstari wa mbele kutetea uanzishwaji wa baraza huru la vijana la Taifa na haswa kusimamia na kuhakikisha sera ya vijana ya Taifa inatekelezwa kwa mapana yake licha ya changamoto zake.

Ni vijana hawa wabunge ambao wanaujua uchungu wa ukosefu wa ajira, mazingira magumu yaliyopo katika kilimo hususan kwa wakulima wadogo wadogo, ukosefu wa ujuzi na ukomavu wa fani na ujasiri wa kupambana katika soko la ndani na kimataifa, na ni wabunge hawa vijana ambao wanajua hali na mazingira magumu ya upatikanaji wa mitaji na fursa za kuwekeza kwa vijana nchini. Tunaamini hawatatusaliti!

Ni wabunge hawa vijana ambao kwa asilimia kubwa wamepitia katika mifumo ua kielimu nchini ambayo changamoto zake hakika naamini hawajazisahau kama ilivyo kwa sekta ya afya. Naamini watapaza sauti sasa kusimamia mabadiliko yake.

Nina amini mmeshuhudia ufu wa vipaji vya vijana wenzenu na wachache ambao walisimama kidete kutetea vipaji hivyo jinsi walivyokuwa na ugumu katika kufaidika naamini mtahakikisha sera na usimamizi madhubuti wa ukuzwaji na mazingira bora ya uchocheaji vipaji nchini kama tunu ya mchango wenu kwa kundi kubwa hili.

Mazingira bora ya ukuzwaji wa vipaji mathalani michezo kwa kuhakikisha tabia ya ubinafsi ya kuuza viwanja vya wazi ambavyo baadhi ya hivyo vilikuwa vikitumiwa na vijana kucheza michezo mbalimbali. Naamini hamtakenua haya yakitendeka na hata kwa baadhi ya maeneo mtarudi nyuma na kusawazisha mabonde.

Kwa msukumo wa ujana wa chachu ya fikra mpya, ubunifu, nguvu mpya na uwezo wa uthubutu naamini mtakuwa na uthubutu wa kusukuma uwepo wa mchakato wa kufanyia mabadiliko Katiba ya Tanzania.

Uundwaji wa katiba mpya imekuwa kilio cha muda mrefu cha makundi mbali mbali katika jamii ya Tanzania mathalani vyama vya kiraia, vyama vya siasa (ambavyo ndimo mnakotoka), wasomi na hata wananchi wote kwa ujumla. Hakika tunawapa jukumu la kusimamia uwepo wa mabadiliko! Kuhakikisha uundwaji wa katiba mpya.

Ni katiba mpya inaweza kutoa fursa hata kwa kijana kushika nyadhifa ya juu ya kiuongozi nchini ya urais ambayo kwa sasa kwa mujibu wa katiba kijana hawezi kuwa rais na kuhakikisha mabadiliko ya kigezo cha umri toka miaka 40 hadi japo miaka 35 yanafanyika.

Naamini mnatambua kuna vijana wengi wamekosa fursa kusimama kuwa wagombea kutokana na baadhi ya vyama kutotoa fursa kwa vijana. Ni mabadiliko ya kikatiba mkiyasimamia mathalan kuruhusu mgombea binafsi yanaweza kuwa suluhu kwao.

Mmezunguka na kusikiliza wananchi, hakika wengi wana hali duni kiuchumi. Naamini hamtawasaliti na kuwasahau kuwa wameweka matumaini yao kwenu mtawatoa katika mfumo ambao unapelekea kuwa na hali duni ya kiuchumi na kupunguza umaskini wa mtu mmoja mmoja.

Tumaini la vijana wenye ulemavu lipo mikononi mwenu. Naamini mnatambua hali duni inayowakabili katika upatikanaji wa huduma za kijamii mathalani elimu, mazingira duni katika sekta za kiafya, na hata wenye elimu kukabiliwa na changamoto ya kunyanyapaliwa katika fursa za ajira na vyombo vya kimaamuzi. Kuweni sauti yao!

Tunaamini mtakuwa wabunge wenye chachu na mwamko mpya katika kusimamia kuleta mabadiliko katika nchi yetu. Ni matumaini ya wananchi katika ujana ambao mnao mtakuwa na nguvu na fikra mpya kuweza kuwa nuru kwa Taifa na kurejesha imani kubwa la kusimamia maslahi ya nchi hususan ya wanyonge na makundi yanayosahaulika ama kutengwa.

Kumbukeni daima maneno ya Frantz Fanon kwamba kila kizazi kinapaswa kung’amua utume wake na aidha kiutekeleze ama kiusaliti. Hakika msimamo wenu ndiyo chachu ya maendeleo yetu.
 
Back
Top Bottom