Viongozi acheni kuwatetea wanaokiuka maadili

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Posted Date::6/7/2008
Viongozi acheni kuwatetea wanaokiuka maadili
Mwananchi

SAKATA la kifo cha kutatanisha cha mjamzito, Teddy Kimoso, kilichotokea katika Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita limeonyesha jinsi viongozi wetu wanavyopenda kuwatetea maafisa wao wa chini yao kwa kutegemea taarifa za upande mmoja.

Jumanne iliyopita, gazeti hili liliripoti habari ya mwanamke aliyefariki katika hospitali hiyo kutokana na kukosa huduma, kwa vile hakukuwa na vifaa vya kujifungulia wala fedha za kununulia mahitaji hayo.

Inadaiwa kuwa alipofika hospitalini hapo, wauguzi wa zamu hawakumhudumia mpaka walipoona anaanza kujifungua, ndipo wakamchukua kumpeleka wodini akiwa katika hali mbaya, tena baada ya watu waliokuwepo kwenye eneo la mapokezi kupiga kelele, walipoona mama huyo yuko katika hali hiyo.

Gazeti hili lilipochapisha habari za madai hayo, kesho yake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Noel Mahyenga aliamua kuwaita baadhi ya waandishi wa habari na kukanusha madai hayo kuwa haikuwa kweli na kwamba habari hizo zilikuwa za uongo, bali mama huyo alikufa kutokana na matatizo mengine ya kiafya yaliyokuwa yakimsumbua.

Lakini chakushangaza, siku hiyo hiyo Manispaa ya Kinondoni ilitoa mafuta ya dizeli, kujaza kwenye gari lililobeba mwili wa marehemu kwenda nyumbani kwao Morogoro kwa mazishi. Ajabu! Hatua hiyo ilizaa maswali mengi, yakiwamo ya imekuwaje wahusika (manispaa) watoe mafuta kwa msiba huo?

Kama walishindwa kutoa msaada wa vifaa vya kumwezesha kujifungua vyenye gharama ndogo, wamewezaje kutoa mafuta ya malaki ya shilingi? Ina maana walingoja afe ndipo wasaidie kusafirisha maiti? Au ni kawaida yao kugharamia kila msiba wa mgonjwa anayefia katika hospitali hiyo? Au labda misiba ambayo haikugharamiwa kuna mchezo ulichezwa?

Tafsiri ya haraka juu ya msaada huo, ilionyesha kuwa walitoa msaada huo ili kuwapoza ndugu wa marehemu na walikuja kujisafisha ili kuzima madai ya wanandugu.

Mbali na Mkurugenzi wa Manispaa, Alhamisi iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro pia aliingilia kati suala hilo, baada ya gazeti hili kuchapisha muendelezo wa habari hiyo, ulioonyesha kuwa ndugu wa marehemu hawakubaliani na taarifa ya kukanusha iliyotolewa na Mahyenga kwa maelezo kwamba kilichosemwa ni cha uongo na wanakusudia kwenda mahakamani kuishtaki hospitali hiyo kwa kusababisha kifo cha ndugu yao.

Mbali na wana ndugu hao, baadhi ya madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo waliomba iundwe tume huru ya kuchunguza kifo hicho na mambo mengine, kwa madai kuwa wamechoshwa kufedheheshwa na vitendo vya baadhi ya wauguzi, ambavyo vinawashushia hadhi watumishi wote wa hospitali hiyo na kuahidi kuwa watasema yote wakiitwa, likiwemo tatizo la kutowatendea haki wagonjwa.

Kandoro ambaye anaonekana kwamba, alijitoma kwenye sakata hilo ili kuokoa jahazi baada ya wakuu wa hospitali na Manispaa ya Kinondoni kushindwa, alikanusha kwamba haukufanyika uzembe katika sakata hilo, ikimaanisha kuwa habari zilizotolewa ni za uongo na waliozichapisha ni waongo au hawakufanya utafiti wowote wa kina?

Wasi wasi wangu ni kwamba, viongozi wetu hawapedi kutumia nguvu kazi walizonazo kwenye maeneo yao ili kupata taarifa sahihi katika kufanikisha mambo yote yanayogusa jamii na maisha yao, badala yake wamekuwa wakiwalinda wahusika au watuhumiwa.

Kibaya zaidi, zinapotokea taarifa za kashfa wanashtuka na kukanusha kwa kutumia maelezo yaliyoandaliwa na watuhumiwa (watendaji wakuu wa ofisi au taasisi ya umma), kama ilivyotokea kwenye sakata hilo, badala ya kutumia njia nyingine kupata taarifa za ziada ili kujua ukweli wa suala hilo.

Simaanishi kwamba wasipokee taarifa kutoka kwa watuhumiwa, la hasha, wazipokea ili ziwasaidie kujua ukweli wa watendaji wao na wakati huo huo, watumie njia nyingine kupata taarifa za ndani zaidi kwa lengo la kupata ukweli wa jambo hilo.

Naamini kwamba, Mkuu wa Mkoa ni mtu mkubwa sana katika eneo lake na ana mamlakla ya kutumia njia na watu wote waliomo kwenye mkoa wake kufanikisha jambo lolote na hasa kumsaidia kupata habari zinazoweza kumpa picha hali ya matukio yote.

Inakuwaje anategemea watendaji wakuu wa hospitali tu kumpa taarifa kwa kashfa inayowahusu, halafu anaridhika nayo na kuitumia jinsi ilivyo, badala ya kutumia njia nyingine kupata taarifa zaidi zitakazomuweka kwenye nafasi nzuri na ya kuzitendea haki pande zote?

Kwa mfano katika suala la Mwananyamala, ametumia ripoti ya madaktari ambao wanalinda nyadhifa zao, badala ya kupata taarifa za ziada kutoka kwa watu wa chini kabisa, kama manesi na wahudumu wengine, ambao kwa ujumla ndiyo wanaojua mambo mengi ya kweli kuliko wakubwa wao, ambao hushughulikia masuala ya kiutawala na kulinda maslahi ya hospitali kwa njia zozote, hata kama ni za uwongo.

Nimelazimika kusema hayo kwa sababu udhaifu huu wa viongozi wetu, kutotumia ipasavyo rasilimali walizonazo kusimamia, kulinda na kutetea wananchi kumesababisha haki isitendeke katika jamii.

Kuna matukio kadhaa ambayo viongozi wetu wamekuwa wakitumia siasa kuzima ukweli, lakini kutokana na nguvu ya vyombo vya habari hujikuta wanakula matapishi yao, kama vile suala la waliobomolewa eneo la Tabata Dampo jijini Dar es Salaam, ambalo lilishupaliwa na viongozi wa Manispaa ya Ilala lakini baadaye walisalimu amri.

Lingine ni upasuaji tata wa watu wawili uliotokea katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), ambalo pia lilikanushwa kwa nguvu zote, lakini baada ya kushupaliwa na vyombo vya habari, ikaundwa tume na kubaini kuwa ulifanyika uzembe wa hali ya juu katika kuwahudumia wagonjwa hao.

Hivi ni kwa nini viongozi wetu huwakingia kifua watendaji wao wanapotuhumiwa kabla ya kufanya uchunguzi wa kina? Je, ni kuwalinda na kama ni kuwalinda, kwa maslahi ya nani?

Inaonyesha kwamba, viongozi wetu huenda wanashindwa kutofautisha kati ya masuala ya kisiasa na ya kijamii kiasi kwamba, wanapoyashughulikia huyaweka kwenye utendaji wa kisiasa ambao wakati mwingine unawaumiza wananchi kwa kuingiza propaganda.

Hilo liliwahi kutokea katika Wilaya ya Ulanga wakati wa kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tatu, wananchi wa huko walipokuwa wanakabiliwa na njaa hadi kufikia kula majani na mizizi na wengine kufa, lakini Mkuu wa Wilaya hiyo akawa anakanusha kwamba hakuna kitu kama hicho, mpaka gazeti moja la kila siku lilipotuma mwandishi wake, ambaye aliandika makala zilizofumua uozo huo, ambao hatimaye ulimfukuzisha kazi.

Mwananyamala kuna matatizo ya kuwanyanyapaa wagonjwa kwa muda mrefu, na ninaamini kwamba ofisi ya Manispaa ya Kinondoni na mkoa zina kumbukumbu ya taarifa hizo, kwani aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba aliwahi kuwatimua kazi baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo kwa uzembe wa aina hiyo.

Daniel Mwaijega ni Msanifu Mkuu wa Habari, Gazeti la Mwananchi. Anapatikana kwa simu 0713704898 au barua pepe mwaijega@yahoo.com
 
Wasipowatetea mafisadi wa chini nani atawalinda pale wanapoiba fungu la kununulia madawa na moboresho ya hospitali zetu???

Tukitaka kuung'oa mti ni kuanza na mizizi kwani matawi (ya juu) yatanyauka yakikosa lishe kutoka chini (mafisadi wadogo)
 
Back
Top Bottom