Imeelezwa kuwa takribani vijiji 6000 vitaunganishwa na huduma ya umeme katika mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu unaofadhiliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani jijini Dar es Salaam wakati akitoa maelezo ya utekelezaji wa Bajeti ya REA kwa mwaka wa Fedha 2015/2016 na mpango wa utekelezaji wa Bajeti hiyo kwa mwaka wa Fedha 2016/17 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Dkt. Lutengano Mwakahesya akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya REA kwa mwaka wa Fedha 2015/2016 na mpango wa utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2016/17 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake imeanza vikao na Kamati hiyo kutoka tarehe 12 Aprili 2016.
Alisema utekelezaji wa Mradi huo wa Awamu ya Tatu utaanza mara baada ya kukamilika mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Pili unaotarajiwa kufikia ukomo mwezi Juni mwaka huu.
“Mradi huu wa REA Awamu ya Tatu tumepanga kuutekeleza kwa muda wa miaka mitatu ambapo tunategemea kutumia jumla ya shilingi trilioni 1.5 na tunatarajia utakuwa ni wa Awamu wa Mwisho,” alisema Dkt. Kalemani.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Dkt. Lutengano Mwakahesya, (pili kushoto) akiwa na watendaji wa REA, wakipitia taarifa iliyokuwa ikiwasilishwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Shirika hilo kwa mwaka wa Fedha 2015/2016 na mpango wa utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2016/17 iliyowasilishwa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Wa kwanza kulia ni mjumbe wa Bodi ya REA, Rehema Tukai.
Dkt. Kalemani alisema kuwa Serikali imejikita katika kusambaza umeme mijini na vijijini ili kutimiza lengo lake la kuhakikisha kuwa asilimia 85 ya wananchi wanapata umeme ifikapo mwaka 2025.
Aidha, Dkt. Kalemani alieleza kuwa kwa kampuni zinazosambaza umeme vijijini katika Awamu ya Pili ambazo zina tuhuma mbalimbali ikiwemo za kufunga vifaa vya umeme chini ya kiwango, rushwa, kutolipa vibarua na wakandarasi wadogo, hawatapewa kazi ya kusambaza umeme Awamu ya Tatu.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ( mtari wa mbele) na Watendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA)( mtari wa nyuma) wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani katika kikao kilichokuwa kikijadili utekelezaji wa Bajeti ya REA kwa mwaka wa Fedha 2015/2016 na mpango wa utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2016/17.
Alisema kuwa utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Usambazaji Umeme vijijini kwa sasa imefikia asilimia 89 na kueleza kuwa kwa vijiji ambavyo vilirukwa katika Awamu hiyo vitaingizwa katika mradi wa REA Awamu ya Tatu na hivyo kutoa wito kwa wadau kutoa taarifa kwa ofisi za TANESCO ili vijiji hivyo viingizwe katika mpango wa kupelekewa umeme.
Alisema kuwa sehemu za huduma za kijamii kama vile mashule, vituo vya afya, sehemu za ibada, visima vya maji ndizo hupewa kipaumbele wakati wa uunganishaji umeme ili kuweza kuwafaidisha wananchi wengi zaidi na kurahisisha utoaji wa huduma katika sehemu hizo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Watendaji wa Wizara na Taasisi zilizochini ya Wizara katika kikao kilichokuwa kikijadili utekelezaji wa Bajeti ya REA kwa mwaka wa Fedha 2015/2016 na mpango wa utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2016/17.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa REA, Dkt. Lutengano Mwakahesya alieleza kuwa mradi wa REA Awamu ya Pili ulilenga kupeleka umeme katika Makao Makuu ya wilaya 13 ambazo ni Buhigwe, Busega, Chemba, Itilima, Kakonko, Kalambo, Kyerwa, Mkalama, Mlele, Momba, Nanyumbu, Nyasa na Uvinza ambapo mpaka sasa ni wilaya ya Momba tu ndiyo haijapelekewa umeme.
Alieleza kuwa pamoja na miradi ya REA Awamu ya Pili kukamilika kwa kiasi kikubwa lakini kumekuwa na changamoto ya wananchi wachache kujiunga na huduma hiyo ambapo alisema kuwa juhudi za kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma ya umeme zinaendelea kwa kushirikisha Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Alisema kuwa lengo la Serikali ni kuunganisha umeme katika vijiji vyote nchini ifikapo mwaka 2021 hivyo wamepanga kuunganisha umeme katika vijiji 2,000 kwa mwaka ili takribani vijiji 15,000 vilivyopo nchini viwe vimepata huduma hiyo ambapo mpaka sasa vijiji 5,200 vimeshaunganishiwa umeme.
Aidha, alieleza kuwa moja ya changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo ni miundombinu ya umeme kama vile nguzo kuharibiwa na wananchi kwa kukatwa au kuunguzwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya umeme kupita juu ya vijiji vyao bila kushushwa.
Hata hivyo alifafanua kuwa katika vijiji ambavyo umeme umepita juu, tayari mikoa Sita nchini imeshafanyiwa tathmini ili kutambua vijiji hivyo lengo likiwa ni kushushiwa umeme.
Wakitoa michango yao mara baada ya uwasilishaji wa taarifa hiyo, wajumbe mbalimbali wa Kamati hiyo waliusifu Wakala huo kwa kazi nzuri ya usambazaji umeme vijijini na kusisitiza kuwa ni vyema umeme huo ukafika katika sehemu ambazo shughuli za maendeleo zinafanyika ili kuchochea shughuli za kiuchumi katika vijiji husika.
Pia waliishauri REA kubuni njia nyingine za kuwabana wakandarasi wazembe na wanaofunga vifaa duni vya umeme katika maeneo ya kazi badala tu ya kushikilia sehemu ya malipo yanayotakiwa kulipwa kwa wakandarasi hao.
Pia waliiagiza REA kuendelea kusimamia miradi yake kwa ufanisi ikiwemo kuhakikisha kuwa vibarua wanaofanya kazi kwenye kampuni zinazosambaza umeme vijijini wanalipwa stahili zao kama makubaliano yanavyoelekeza kabla ya mradi husika kukamilika na mkandarasi kukabidhi mradi kwa TANESCO.
Vilevile, waliishauri REA kupeleka umeme katika mikoa ya pembezoni ambayo imepakana na nchi nyingine na kuangalia uwezekano wa kutumia nguzo za zege ambazo zinadumu kwa muda mrefu badala ya zile zinazotumika sasa ambazo hupata athari mbalimbali ikiwemo kuunguzwa na moto.
Imeandaliwa na:Teresia Mhagama na Zuena Msuya,Maafisa Habari,Wizara ya Nishati na Madini,754/33 Mtaa wa Samora,S.L.P 2000 Dar es Salaam,Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606Barua Pepe: info@mem.go.tz Tovuti: mem.go.tz