Vijana wasomi toka familia maskini hupata sana kesi za ubadhirifu na kuishia pabaya. Wazazi, serikali na jamii ni ya kulaumiwa

MamaSamia2025

JF-Expert Member
Mar 29, 2012
10,202
22,240
VIJANA WASOMI TOKA FAMILIA MASKINI HUPATA SANA KESI ZA UBADHIRIFU NA KUISHIA PABAYA... WAZAZI, SERIKALI NA JAMII NI YA KULAUMIWA.

Nawasalimu nyote kwa jina la Chama Cha Mapinduzi.... leo nimeamua kuandika huu uzi nikiwa na masikitiko makubwa mno nafsini mwangu. Ni suala linalotuhusu vijana wa nchi hii hasa tuliotokea familia maskini. Baada ya kusoma tutachangia maoni ili kunusuru wengine waliopo makazini.

Kwa miaka ya hivi karibuni hasa utawala uliopita tumeshuhudia kukiwa na kesi nyingi sana za uhujumu uchumi na ubadhirifu kwenye ofisi za serikali. Hata taasisi binafsi kama mabenki kumekuwepo na kesi za wizi na mambo mengine yanayofanania. Wengi tumekuwa ACTIVE siku ile kesi zinavyotangazwa na baada ya hapo tumekuwa hatufuatilii. Mimi kwasababu ya kujaliwa akili nyingi nikaona nifuatilie hapo kidogo kujua wahusika ni watu wa aina gani. Nilichogundua ndo kimenisikitisha.

Nimegundua vijana wengi hasa waliokulia kwenye familia maskini ni wahanga wakubwa wa haya matukio. Utakuta kijana kasoma kwa taabu mno shule za serikali na kufanikiwa kutoboa hadi UDSM kisha kupata degree yake yenye GPA kali na kwa bahati kaajiriwa pazuri serikalini. Baada ya muda mfupi maisha yanabadilika na kuachana na umaskini. Wakati wananchi tukianza kufurahia mafanikio ya kijana wetu ghafla tunaona vyombo vya habari vikitangaza kijana wetu atafikishwa mahakamani kwa tuhuma kadhaa za ubadhirifu/uhujumu. Na matokeo yake kijana anafukuzwa kazi na kesi kuisha kwa yeye kukombwa kila kitu kufidia hasara. Mwisho kabisa kijana kurudi kwenye umaskini. Mimi kwangu ni kama msiba tu.

Je sababu ni nini? Hapa sababu ni kijana mwenyewe, familia yake, mabosi ofisini, serikali, na jamii nzima. Kijana anaepata haya majanga lazima awe wa kwanza kujilaumu. Wengi wa hawa vijana wana tamaa na kutaka utajiri wa ghafla. Husahau walikotoka na kushindwa kupiga hesabu za hatari ya kufanya ujanja ujanja kazini. Vijana waelewe "YOU RUSH YOU CRASH".. Wajitafutie vyanzo vingine vya mapato kihalali. Huu upumbavu wa kuona mafanikio ni kuvaa vikaptula, kupanga nyumba sinza, kuendesha harrier, na mambo mengine yasiyo na tija hutawaacha salama vijana. Kuiga maisha ya magharibi ni anguko kubwa la vijana. Marekani na nchi nyingine za mabeberu wana mchango mkubwa kwenye kuharibu tabia za vijana.

Familia pia ni chanzo kikubwa cha vijana kuwa wezi. Karibu familia zote Tanzania hasa za kimaskini huwa tunawalisha vijana upumbavu toka utotoni kwamba wasome kwa bidii waje waajiriwe taasisi zenye marupurupu kama TRA, TPA, BOT nk. Haya marupurupu kwa tafsiri nyingine ndo hizi hela za upigaji zinazowapeleka vijana jela. Mzazi kama unasoma hapa nakusihi acha upumbavu wa kumpa maadili ya mtoto kuja kuwa mwizi huko ukubwani. Mfundishe toka utotoni njia za kuja kupata pesa kihalali kupitia vipaji vyake na jitihada binafsi. Kumfundisha mambo ya marupurupu ni kuchochea wizi. Mwambie ukweli kwamba wizi mwisho wake ni pabaya. Mfundishe kuipenda nchi yake na aone upigaji ni kitu kibaya. Pia wale wazazi mnaopenda kufananisha maisha ya vijana wengine dhidi ya kijana wako muache huo ushenzi. Utasikia mzazi anamlaumu mtoto wake "Huna akili kabisa, huoni kijana wa Mushi kashajenga nyumba tayari wewe upo upo tu?".... Hii huleta uchungu kwa kijana na kujikuta anaamua liwalo na liwe.

Mabosi ofisini wana mchango mkubwa kwenye haya matukio lakini kwa sababu ya uzoefu wao huwa CLEAN ishu inapotokea. Wengi wao ndo huwaingiza vijana kwenye hizi dili haramu lakini bila wao kuacha alama zozote za uhusika. Vyombo vya dola vinapoanza uchunguzi basi zigo lote humuangukia kijana. Tafadhali ninyi baadhi ya mabosi kuweni na utu na muwafundishe vijana kuwa waaminifu badala ya kuwaingiza kwenye matatizo huku mkiwageuka siku ya matatizo. Hii ni dhambi kubwa sana.

Serikali nayo haiwezi kuepuka lawama. Mimi naisihi sana serikali ya Chama Pendwa CCM ijitahidi kuwa na sera nzuri za kiuchumi ili kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi wake. Haipendezi kuona serikali ikinunua V8 huku kukiwa na wanafunzi hawana madawati. Au inaleta picha gani kuona waziri ambaye anaingiza pesa kuanzia bungeni hadi kwenye uwaziri akipigia debe makato ya pesa nyingi kwenye miamala kwa wananchi wasio na uhakika wa mlo mmoja kwa siku? Serikali iweke vipaumbele vingi vya kumtoa mwananchi kwenye hali ngumu ili kupunguza uhalifu. Hatuko salama kuanzia mitaani hadi kwenye ofisi za serikali endapo bado watu wana njaa kali kila upande.

Jamii pia iache ujinga wa kuhamasisha vijana kwenye upigaji kwa kisingizio cha marupurupu. Kila mmoja awe mshauri wa mwenzake kuwa mzalendo na kuepuka upigaji.

Mwisho niwasihi vijana wenzangu wote ambao tumetokea familia maskini kujiepusha na upigaji maofisini ili tusiingie matatizoni. Nyuma yetu tuna watu wengi wanaotutegemea na wana ndoto zao pia. Ni huzuni kubwa kusoma kwa taabu na kuja kuishia jela. Haipendezi kuona watoto wa viongozi na wao wakija kututawala tena. Tupunguze hii gap iliyopo. Ukimtoa Nikki Wa Pili na wengine wachache utaona viongozi wengi vijana wametoka familia safi.
 
Back
Top Bottom