Vijana walapo na vigogo mafisadi huisaliti jamii | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vijana walapo na vigogo mafisadi huisaliti jamii

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Pdidy, Aug 8, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Aug 8, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,448
  Likes Received: 5,700
  Trophy Points: 280
  Na Joseph Mihangwa

  WAKATI jamii ikiendelea kusukwa sukwa na mawimbi ya bahari iliyochafuka kutokana na ukinzani wa kitabaka, uonevu na ukandamizaji, vijana wa Tanzania nao sasa wanaona kumekucha kudai nafasi za uongozi wakisema wamepuuzwa na kunyanyaswa vya kutosha kwa kuitwa "Taifa la Kesho".

  Lakini, pamoja na kujitambua hivyo, hawasemi wataitulizaje bahari iliyochafuka na ni vipi wataiongoza salama meli ya matumaini iliyo mikononi mwa manahodha wakongwe, bila kuzua mtafaruku.

  Wakati nchi ikienda kombo kwa kukosa dira, uzalendo kuporomoka, maadili ya taifa kuyoyoma, ufisadi na rushwa kukithiri kwa kukingiwa kifua na vigogo wa Chama na Serikali; vijana wa leo ambao "sasa na kesho" yao inaangamizwa, wamekosa ubavu wa kutahadharisha; badala yake wameungana na wakongwe hao kama washika vipeperushi na mikoba ya vigogo wakati wa chaguzi za kuweka viongozi madarakani. Kama wamejiunga na uozo huu wa tabaka la machweo, nini maana sasa ya wao kudai madaraka?

  Wakati nchi ikiangamia kwa kukosa sera makini, uwekezaji usiojali na uporaji wa rasilimali za taifa unaofanywa na wageni kwa kushirikiana na baadhi ya "vigogo" madarakani, na udini na ubaguzi wa kitabaka kutishia amani na utulivu nchini, vijana wamejenga tabia ya mbuni kwa kujivika taji la ukada wa vyama vya siasa, wakijiliwaza kwamba yote yanayotokea ni asali tamu. Je, vijana wa leo wamepeleka wapi ujasiri wa miaka ya 1960 na 1970, wasiweze kulaani maovu katika jamii?

  Tusidanganyike, vijana wa leo wametupa zana zao za vita ya kujenga na kulinda taifa, na badala yake wamejiunga na uozo unaoangamiza jamii kwa matarajio ya kuokota ganda la muwa la jana; wakidhani kuwa hiyo ndiyo pepo inayowangojea, kana kwamba wanajiandaa kuishi ughaibuni, na kwamba hapa sio kwao.

  Kama kuna mfano bora wa kuigwa na vijana, kuonyesha nguvu na nafasi yao katika kuleta mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini dhidi ya uozo wa wakongwe wenye kuangamiza nchi; basi, mfano huo ni ule mgomo wa vijana wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Oktoba 1966.

  Kwa manufaa ya vijana wa leo nitauelezea mgomo huo, chimbuko lake, ulivyofanyika na jinsi ulivyobadilisha uwanja wa siasa na maisha ya Watanzania pamoja na fundisho tunalopata. Mmoja wa viongozi wa mgomo huo ni Spika wa sasa wa Bunge la Tanzania, Mheshimiwa Samwel Sitta, ambaye umakini wake katika kuliongoza Bunge ni kielelezo tosha jinsi vijana wa zamani walivyopikika wakaiva, ikilinganishwa na vijana wa leo.

  Februari 1966 Serikali ilichapisha Muswada kwa madhumuni ya kuanzisha Programu ya Jeshi la Kujenga Taifa [JKT] kwa lazima kwa vijana wote waliomaliza elimu ya Kidato cha Sita na Vyuo vya Elimu ya Juu kikiwamo Chuo Kikuu pekee cha Dar es Salaam.

  Mpango huo, ulioendeshwa na kusimamiwa na wakufunzi wa kijeshi kutoka Israeli, uliwataka vijana kutumikia JKT kwa miaka miwili ambapo miezi sita ilikuwa kwa mafunzo ya kijeshi kambini na miezi 18 ya kutumikia Jeshi nje ya kambi kama watumishi wa umma, na kukatwa asilimia 60 ya mshahara kama mchango kwa taifa.

  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilitoa wasomi wake wa kwanza mwaka 1964 ambao walionekana tishio kwa nafasi za vigogo madarakani kwa sababu ya elimu yao. Ni vigogo hao walioasisi wazo la programu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Vijana.

  Kabla ya programu hiyo, JKT, iliyoanzishwa mwaka 1964, ilikuwa kwa vijana wa kujitolea tu. Hata hivyo hadi Oktoba 1966, ni vijana 25 tu wa kujitolea waliokuwa wamejiunga.

  Na mpango huo ulipochukua mkondo wa kuwaingiza wasomi kwa lazima, Muswada wake haukupokelewa vyema na jamii ya wasomi nchini na baadhi ya wabunge.

  Wabunge wasomi kama kina Nicholaus Kuhanga na wengine, wakati wakijadili muswada huo, walisema wazi kuwa "Kudai kwamba kuwakata vijana asilimia 60 ya mishahara yao ni Ujamaa ni uongo; wabunge na viongozi wa Serikali wanasahau kwamba, ni wao hao hao wanaomiliki majumba yenye thamani kubwa na magari ya kifahari ambacho ni kinyume cha Ujamaa. Kwa hiyo wanapashwa kuonyesha kwanza kwamba wao ni Wajamaa kabla ya kuwataka vijana hawa masikini kuwa Wajamaa" [Hansard, Septemba 22 – Oktoba 11, 1966 ukurasa 249].

  Muswada huu ulizua ukinzani mpana katika jamii hadi maofisini ambapo kuliripotiwa kisa kimoja wakati wa mjadala bungeni, juu ya mabishano makali ya maofisa wawili; mmoja msomi na mwingine asiye msomi, wakiapizana; yule asiyesoma akisema, "Kusoma si hoja, ukiwa na digrii mtatufanya nini wakati tuna majumba, magari vipusa [warembo] na madaraka tunayo?" [Hansard, kama hapo juu].

  Mara tu muswada huo ulipopita, wanafunzi waliwasilisha serikalini madai yao ya kutaka muda wa JKT upunguzwe kutoka miaka miwili hadi miezi sita, na makato ya asilimia 60 ya mishahara yaondolewe. Na pale madai hayo yalipokataliwa, waliona kwamba Serikali haikuwa na nia njema kwao; saa ya machafuko ilikuwa inajongea taratibu.

  Ziara za mara kwa mara za viongozi wa Serikali chuoni hapo kuzungumza na wanafunzi, hazikubadili hisia za wanafunzi hao. Mambo yalitibuka zaidi pale Naibu Waziri wa Ulinzi na JKT wa wakati ule, Richard Wambura, alipowahutubia wanafunzi, Oktoba 18, 1966; katika hotuba ambayo ilitafsiriwa kuwa mpango huo wa JKT ulikuwa wa hila, kwa lengo la kuwaonea na kuwanyanyasa vijana kwa kuwa tu wao ni wasomi.

  Baada ya hotuba hiyo, wanafunzi waliitisha mkutano wa dharura ambapo ziliundwa kamati mbili: moja ya kwenda kuonana na Rais kuelezea malalamiko yao; na ya pili, kwenda Polisi kuomba kibali cha kufanya maandamano.

  Kamati iliyokwenda kuonana na Rais ilitoa taarifa kuwa Mwalimu hakuwa na uhakika juu ya kile kilichokuwa kikiendelea; akayatupilia mbali malalamiko yao. Na ile iliyokwenda Polisi, ilitaarifu juu ya kukataliwa kibali. Oktoba 21, 1961, wanafunzi waliitisha kikao kingine cha dharura; wakaazimia kuandamana bila kibali cha polisi, kwenda Ikulu kukutana na Mwalimu Nyerere.

  Waliandaa mabango yenye ujumbe mbalimbali. Kwa kutaja baadhi tu, yalisomeka "Tumechoka kutumikia Wabenzi [mafisadi]", "Afadhali wakati wa Ukoloni", "Kumbuka ya Indonesia", "Atokomezwe Kawawa na mpango wake", na mengine mengi.

  Hili la "Kumbuka ya Indonesia" liliikumbusha Serikali jinsi Serikali ya Rais Suharto wa nchi hiyo ilivyopinduliwa kwa maandamano ya wanafunzi. Lakini hili la "Afadhali wakati wa Ukoloni", kuna taarifa zisizothibitishwa kwamba halikuwa na ridhaa ya wanafunzi, na kwamba lilipandikizwa tu na watu wa Usalama wa Taifa ili kuchokoza hasira ya Mwalimu Nyerere aweze "kuwaadabisha" waandamanaji.

  Bila ya wanafunzi hao kujua, huko Ikulu, Oktoba 22, 1966, Mwalimu aliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri kuamua jinsi ya kukabiliana na waandamanaji watarajiwa. Iliazimiwa kuwa, maandamano yaongozwe na Polisi kuingia Ikulu hapo Oktoba 22, 1966.

  Ilivyotokea ni kwamba, maandamano hayo hayakuwahusisha vijana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pekee, bali walijiunga wengine wengi kutoka Chuo cha Uganga cha Muhimbili, Chuo cha Ualimu, Chang'ombe, Chuo cha Biashara [CBE] na Shule ya Sekondari Aghakhan.

  Pale Ikulu, waandamanaji hao walilakiwa na Mwalimu, Makamu wa Pili wa Rais Rashid Kawawa na Mawaziri. Kisha, Mwalimu alimkaribisha msemaji wa waandamanaji kutoa malalamiko yao; naye, kwa lugha ya Kiingereza fasaha, akatamka masharti yao kwa ukali akisema: "Serikali inajaribu kuutupa mzigo wa kugharamia mpango huu [JKT] mabegani mwa wanafunzi masikini …… Ama tulipwe haki zetu zote za mishahara, ama wale wote wanaopata mishahara ya juu nao watumbukizwe katika utaratibu huu ili uonekane kweli kuwa ni wa kujitolea na si wa kunyonywa".

  Ndipo akagonga nyundo iliyomsitua Mwalimu kwa kusema: "Kwa hiyo Mheshimiwa, kama utaratibu huu pamoja na mawazo ya viongozi wa juu hayakubadilika, hatuukubali mpango wa JKT kwa moyo. Miili yetu inaweza kwenda, lakini mioyo yetu itabaki nje ya mpango huu"; akashangiliwa sana na waandamanaji wenzake.

  Kisha akamaliza kwa kishindo kwa kusema: "Na vita baina ya wanasiasa na watu wenye elimu vitaendelea daima. Aksante". Hapo akawa amemchokoza Mwalimu.

  Mwalimu alianza kujibu risala, kwanza kwa pole pole na kwa sauti tulivu: "Nilielewa hili; nimeyaelewa malalamiko yenu. Sisi Serikali tumepata ujumbe wenu; natafuta njia ya kueleza kidogo; maneno yenu tuliyowaambia viongozi wenu yamewafikia", akasema Mwalimu, akiangaza macho huku na kule.

  Sauti ikaanza kupanda kidogo; "Sasa mimi nimeyakubali masharti yenu; naweza kuwahakikishia kwamba sitamlazimisha mtu yoyote. Mnayosema ni sawa: hata miili yenu ikienda [JKT], mioyo yenu haitakuwa huko ………. Sitampeleka hata mmoja katika JKT ambaye moyo haupendi [makofi], maana huko si gerezani ………..Lakini hata hivyo mpango wa JKT utaendelea kuwa wa lazima kwa kila mwanafunzi ambaye hatimaye atafanya kazi serikalini. Kwa hiyo ni juu yenu kuamua……".

  Akaendelea: "Mnayosema juu ya mishahara ni ya kweli, ni mikubwa mno [shangwe], mimi na ninyi tumo katika kundi la wanyonyaji. Je, hayo ndiyo mambo nchi hii iliyopigania? Je, juhudi yote tuliyofanya ni kwa sababu ya kuneemesha kikundi cha wanyonyaji huku juu?", akahoji kwa sauti kali.

  Kisha akawaeleza juu ya mapinduzi yanayotakiwa, "Siku nitakayoweza kumlipa mfanyakazi wa Tanzania mshahara wa Shilingi mia tano kwa mwezi, tutakuwa tumefanya mapinduzi makubwa sana; hapo tutaweza kusimama juu ya Mlima Kilimanjaro na kutangaza Mapinduzi ya Tanzania".

  Ili kuthibitisha kwamba alikuwa hatanii juu ya mishahara mikubwa, Mwalimu alisema: "Mshahara wangu mnajua ni kiasi gani? Shilingi elfu tano kwa mwezi; ni mkubwa mno". Hapo akapandisha sauti, akasema: "Mshahara wangu naupunguza kwa asilimia ishirini kuanzia sasa hivi ………nchi hii ya hovyo; mishahara minene mno"; akafoka.

  Akarejea kwenye hoja ya siku hiyo, akasema: "Mimi nimeyakubali maneno mnayosema……….. Na ninyi, mimi nawaomba mwende nyumbani kwenu. Rashid [Kawawa], ni jukumu lako kuhakikisha kwamba wanakwenda kwao". Kwa kauli hiyo, alikuwa amewafukuza wanafunzi wote 415! Mara wakazingirwa na Polisi, wakaanza kushughulikiwa kwa kipigo na kudhibitiwa.

  Oktoba 28, 1968 Chama cha Wanafunzi [USUD], kupitia barua iliyotiwa sahihi na Kaimu Rais wa chama hicho, kilimwomba Mwalimu atumie hekima yake kuwasamehe wanafunzi waliofukuzwa. Barua nyingine ya Oktoba 30, 1966, iliweka bayana kuwa malalamiko ya wanafunzi hayakutendewa haki kwa kueleweka vibaya, kwamba wanafunzi hao walitaka kupindua Serikali.

  Hatimaye Rais alikubali kuwarejesha wanafunzi 392, Julai 1966, isipokuwa 23 waliobainika kuwa viongozi wa mgomo, akiwamo Spika wa sasa wa Bunge la Tanzania, Mheshimiwa Samwel Sitta. Hawa walitakiwa kuomba radhi kwa Mwalimu ana kwa ana kuonyesha kwamba kujuta kwao kumethibitika kuwa na manufaa kwa jamii. Walifanya hivyo na kurejeshwa miezi kumi baada ya wengine kurejeshwa.

  Pamoja na kufukuzwa kwa wanafunzi hao, Mwalimu hakuweza kuipangua hoja yao juu ya vigogo wa Serikali kujineemesha kwa jasho la wanyonge wa nchi hii, na hivyo akachukua hatua hima ya kupunguza mishahara ya viongozi wote nchini.

  Kwa kuwafukuza wanafunzi hao, Serikali ilikuwa inajitafutia sifa na umaarufu rahisi kwamba ilikuwa inatekeleza matakwa ya wananchi, wakati ukweli ulikuwa ni kinyume chake; tabia ambayo inaendelea hadi leo.

  Profesa T. O. Ranger katika barua aliyomwandikia Msaidizi wa Rais, Mama Joan Wickens, Kumb: C3/SA.13 ya 2/3/1967, kumwomba amshawishi Mwalimu awarejeshe wanafunzi hao 23, alisema wazi kuwa, haikuwa halali kwa wanafunzi hao kutumika kama chambo kwa Serikali iliyokuwa imepoteza dira na yenye kujaa mafisadi, wasiojali maslahi ya umma.

  Ukweli huu ulijidhihirisha pale Mwalimu Nyerere alipoyatafsiri kwa vitendo madai ya wanafunzi kwa kutangaza Azimio la Arusha, Februari 5, 1967, kama dira ya sera za uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujenzi wa jamii yenye usawa, tofauti na ile iliyokuwa ikijengeka mwaka 1966.

  Azimio la Arusha na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea vilipokelewa kwa nderemo na vifijo na jamii ya wasomi kama mkombozi wa wanyonge. Kuanzia hapo, hatimaye Tanzania ikaamua kufuata siasa za mrengo wa Kisoshalisti. Kuanzia hapo, wanafunzi Vijana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakafunga fungate ya uswahiba na Serikali iliyokuja kukatwa na sera za soko huria kupitia Azimio la Zanzibar mwaka 1992.

  Lakini historia hujirudia. Ya mwaka 1966 yamerejea. Kama Tanzania sasa ni masikini kuliko ilivyokuwa kabla ya uhuru, kuna tofauti gani kati ya sasa na wakati wa ukoloni? Kama matabaka nchini yameruhusiwa kujijenga, kuna tofauti gani kati ya enzi za Wabenzi wa 1966 na mafisadi wa sasa?

  Jamii yetu imewekeza kwa vijana kwa kujinyima ili wapate nguvu ya kuhemea maendeleo ya nchi kwa wote. Lakini ilivyo sasa, wanagawana na vigogo mafisadi walichohemea kabla hakijamfikia mwananchi. Huu ni usaliti kwa jamii walioukataa vijana makini mwaka 1966 kwa ushindi mkubwa. Hawa wa sasa wanalisaliti taifa.
   
Loading...