John Mnyika
JF-Expert Member
- Jun 16, 2006
- 713
- 1,241
Hotuba hii ilitolewa na Mzee Mtei Machi 29 mwaka 2008(jumamosi iliyopita)
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
MISINGI YA DHANA: VIJANA NI TAIFA LA LEO
Mhe. Mwenyekiti wa Vijana wa CHADEMA,
Wahe. Wabunge,
Wahe. Wageni Waalikwa, na
Wahe. Vijana wote Walioitikia mwaliko wa Tafrija Hii,
Awali ya yote, nataka kuwashukuru kwa moyo wa dhati walioandaa tafrija hii kwa kunialika kama Mgeni Rasmi. Mimi nilikuwa katika kundi la vijana miaka ya mwanzo ya 1960 wakati Waasisi wa Taifa letu wakikamilisha harakati za ukombozi na tukajipatia uhuru wa bendera. Mnavyofahamu, Chama cha TANU kilikuwa pia na Umoja wa Vijana ambao umeendelea na kuwa sasa ni Umoja wa Vijana wa CCM. Licha ya kwamba viongozi wengi wa zama hizo walikuwa si wazee, na walikuwa ndio wakisimamia wizara serikalini na shughuli nyingi za chama, Mbiu ya vijana (motto) ilikuwa Vijana Taifa la Kesho!
Waasisi wa Chama cha Demokrisia na Maendeleo kwa miezi zaidi ya sita, kati ya Oktoba 1991 na Juni 1992 tulijadili kwa kina sababu zilizokuwa zinaathiri maendeleo ya taifa letu katika hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Tulibaini kwamba sababu ni kutoshirikisha umma wote kwa uwazi na kwa uhuru, katika maamuzi yanayogusa maisha na maendeleo yao. Umma wote hapa tulimaanisha ni makundi yote ya wananchi: wazee, watu wazima wanawake kwa wanaume, vijana, vikundi vya dini, vyama vya ushirika, vyama vya wafanyakazi na taasisi zote za elimu na za dini. Tulibaini kwamba Tanzania tulikuwa na tabia ya kukubali bila kusita, lolote lililoamuliwa au kufikiriwa na viongozi wetu. Hizo zilikuwa zama za Ndiyo Bwana, Hewalla mzee, Zidumu Fikra za Mwenyekiti, Mwenyekiti Hachelewi au Hakosei.
Matokeo ya mtindo na utamaduni huu yalikuwa ni kwamba hata utawala wa kiimla ulikubalika kama jambo la kawaida. Hakuna mtu aliyehoji. Matokeo yakawa ni kwamba wakubwa hasa waliokuwa katika Chama cha Mapinduzi walihodhi madaraka na maamuzi yote muhimu juu ya maisha ya wananchi. Kwa hiyo fursa ya kuwa na vyama vingi vya siasa ilituwezesha sisi Chadema kutafakari hata kauli mbiu ya Vijana ni Taifa la Kesho kama CCM kilivyokuwa kinatamka.
Baada ya kutambua kwamba vijana ndio waliokuwa nguvu kazi ya taifa, katika mashamba, viwanda, serikalini, wanajeshi na kadhalika tuliamua kauli mbiu yetu iwe ni Vijana ni Taifa la Leo. Tulipozindua CHADEMA rasmi pale Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Augosti Tarehe 4, 1992 tukasema hivyo na tukaendelea kusema kwamba Wazee ni Dhamana, Wanawake ni Walezi na Watoto:Taifa la Kesho.
Katika mtiririko huo wa mawazo na fikra mpya, Chadema tulibuni alama yetu ya VEMA au ushindi; na jinsi tulivyokua, tumeendelea kububujika mawazo mapya na tukisisitiza kwamba chama chochote cha demokrasia ya kweli na uhuru wa kweli ni lazima kiwe ni chimbuko la Nguvu ya Umma yaani Peoples Power. Uongozi wa Chadema umeendelea kusisitiza kwamba maendeleo ya kweli yatatokana na wananchi kujituma na kutumia uwezo wao wote katika kuendeleza rasilmali ya nchi yao kiuzalendo, kwa juhudi na maarifa na kwamba chama ni lazima kijitolee kushawishi na kuelimisha umma mpaka kieleweke. Hakuna kulala!
Mhe. Mwenyekiti, Wahe. Wabunge, Mabibi na Mabwana, Mimi kama Mgeni Rasmi niliombwa na waandalizi wa Hafla hii nizungumze kwa muda mfupi sana. Ninataka kuzingatia ombi hilo ili muendelee kufurahia vinywaji na vitafunio vyenu na hasa pia vijana muweze kusikilizana na kujadili hatma ya taifa letu na dhima ya vijana katika kuifikia. Kwa hiyo, baada ya kuwaelezeni kwa nini Vijana ni Taifa la leo, ningetaka kwa kifupi nigusie udhamini wangu kwani Wazee ni Dhamana.
Taifa letu katika kipindi cha karibu nusu mwaka limeshuhudia msisimko wa siasa ambao umetokana na ujasiri na uzalendo wa wanasiasa wa Upinzani wakiungwa mkono na baadhi ya wanachama wa chama tawala ambao wameshtushwa na kiasi cha ufisadi na rushwa vinavyoathiri maslahi ya wananchi. Nchi hii inanuka rushwa. Wakubwa wanatafuna nchi. Wakati wakubwa wakila kuku kwa mrija umaskini unazidi kuota mizizi nchini, wengi wakishindwa kupata mlo wa siku, wakifa kwa kukosa matibabu na wengi wakishindwa kuwapatia watoto wao elimu inayoridhisha.
Ujasiri wetu umefichua madudu mengi. Hata hivyo vijana ni lazima mjihadhari na mbinu zitakazotumiwa na hawa walanchi kujinusuru. Fedha zao chafu zinatumika na zitatumika kuwababaisha na hasa kuwapaka matope viongozi wenu kwa njia mbali mbali. Mtazushiwa kina aina ya uovu. Mafisadi watapenyeza fedha zao katika vyama vya upinzani, wakati mwingine bila sisi wenyewe kutambua. Pia ni lazima tutambue kwamba kuna vyama vya upinzani ambavyo vimeanzishwa maksudi na hawa mafisadi ili utawala wao udumu madarakani milele. Vyama hivi vinatugawa bila aibu. Vingine hata havitambui kwamba vinatugawa kwa vile havijui kuchambua mambo kwa kina. Tuvijue hivyo vyama, na tubuni mbinu za kuvipuuza. Mafisadi wameshaanza kununua na kudhibiti memejimenti za baadhi ya magazeti yaliyokuwa yanatoa kipaumbele katika kueneza sera na mikakati ya wapinzani. Wananunua waandishi wa habari katika yale magezeti waliyoshindwa kuyadhibiti. Tutambue hayo na tukisoma magazeti tujue yana malengo gani.
Wakati sisi tunakaa hapa kujadili hatma ya nchi yetu na jinsi ya kujinasua kutoka katika makucha ya ufisadi, Chama kilichosababisha haya yote kina kikao huko Butiama kujipanga upya jinsi ya kuendeleza utawala wake. Sisi katika Chadema tumeshasema kwamba Watanzania ni lazima wapewe fursa ya kubadili watawala kwa vile miaka 47 imetosheleza kuijaribu CCM. Hawataweza kuwa na jipya, kwa vile wamedumaa kimawazo na sasa wametekwa na mafisadi.
Katika kujipanga upya tunahitaji kwanza kuwa na viongozi jasiri. Tunahitaji viongozi wanaoweza kuchambua kwa kina kiini cha matatizo yetu; viongozi wabunifu, wanaoona mbali. Tunahitaji viongozi wanaojali wananchi na kuwaonea huruma kwa adha na shida wanazozipata kutokana na ufukara unaoongezeka kila kukicha. Umaskini unatumaliza.
Tunahitaji vijana wataalamu wanaojiamini. Viongozi wetu watambue kwamba nchi yetu ina utajiri wa maliasili ambayo itaweza kutufanya tuwe taifa tajiri, katika muda wa maisha yetu, bora tu tuwe na sera safi na hasa tuepuke mikataba mibovu inayotufanya tuwe fukara kutokana na viongozi walarushwa kuikubali.
Nchi yetu imekuwa tegemezi kiasi kwamba tunajivunia pale Rais wetu anapoahidiwa kwamba tunapewa vidola na watawala wa nchi ambazo zinalaaniwa na ulimwengu kwa ukatili na uonevu. Utu wetu kitaifa umetoweka. Mimi binafsi naamini kwamba kama mikataba ya migodi ya madini ingerekebeshwa ili Tanzania imiliki migodi hiyo kwa asilimia 51, na miradi hiyo ikasimamiwa na kuendeshwa kwa ufanisi na kulipa kodi stahili, serikali yetu haingehitaji hii misaada toka kwa wahisani kiasi cha 40% katika bajeti yake. Kama taifa tutaweza kujitegemea tukizingatia hilo.
Namalizia hapo, nikiwaasa vijana mzingatie hayo katika juhudi zenu za kuleta Mabadiliko ya Kweli na Uhuru wa Kweli.
AHSANTENI.