Vijana amkeni.....Tz Yenu inaangamia,By Fred mpendazoe

RUV ACTVIST.

JF-Expert Member
Jan 14, 2012
472
110
Wito kwa vijana: Nchi yenu inaangamia, amkeni muiokoe
Fred Mpendazoe Toleo la 382 3 Dec 2014
Vijana
Fred Mpendazoe
fmpendazoe@hotmail.com
More information about text formats
Text format
Kijana jiulize, utaifanyia nini Nchi yako, na wala usiulize nchi yako itakufanyia nini.
Vijana ni Taifa la leo, si Taifa la kesho.
UPEPO wa mabadiliko unaovuma sehemu nyingi duniani, likiwemo Bara la Afrika,
kwa jumla, na hasa Tanzania, ni kielelezo kuwa jamii zinataka mabadiliko –
mabadiliko ya mifumo ya utawala, sera, sheria na mengineyo ambayo
yataihakikishia nchi maendeleo ya kweli, uhuru wa kweli na ustawi wa kweli.
Kwa nini mabadiliko yataletwa na vijana? Hiki ni kizazi cha Joshua. Imani yangu
inatokana na historia yetu. Katika vitabu vya kale (Kurani na Biblia), habari ya
wana wa Israeli inasimuliwa kwamba Musa aliwaongoza kutoka nchini Misri kwa
takribani miaka 40.
Katika miaka hiyo 40, wana wa Israeli walipitia misukosuko mingi, lakini kutokana
na uongozi imara wa Musa, waliikabili misukosuko hiyo na hatimaye kufanikiwa
kushinda. Wakiwa wamekaribia kabisa kuingia Nchi ya Ahadi; yaani Kanani.
Mungu alimchukua Musa hadi juu ya mlima mrefu, akamwonyesha Nchi ya Ahadi
ilivyokuwa nzuri. Baada ya kumwonyesha, Mungu alimwambia Musa kwamba
Joshua na Kalebu ndiyo watakaoongoza wana wa Israeli kuingia Kanani, na si yeye
Musa. Joshua na Kalebu walikuwa vijana.
Natumia mfano huu kuwapa vijana wa Tanzania ujumbe kwamba wao ndiyo
watakaoiingiza Tanzania kwenye mabadiliko makubwa ya kijamii, kiuchumi na
kisiasa yenye kunufaisha makundi yote katika nchi - vijijini na mijini.
Vijana ni kizazi kipya kama Joshua na Kalebu. Wana maono mapya kuhusu nchi
yetu. Wazee waliopigania uhuru wamefanya kazi kubwa kumtoa mkoloni.
Wametimiza wajibu wao. Maono yao yameishia hapo.
Kumwondoa mkoloni mkongwe ilikuwa kazi ngumu, lilikuwa jambo jema na la
heshima kwa nchi. Lakini tunahitaji kwenda mbele zaidi ya hapo ili kudhibiti
ukoloni mamboleo unaowafanya wananchi wengi kuishi katika hali ya ufukara wa
kupindukia wakati nchi yao ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizobarikiwa
kwa utajiri wa maliasili. Ili kwenda zaidi ya hapo, yanahitajika maono mapya
yatakayoleta mabadiliko yatakayowanufaisha Watanzania wote.
Ni nini kilisababisha Musa asiingie Nchi ya Ahadi wakati alikuwa amekaribia
kabisa? Mungu hakosei. Alimzuia Musa asiingie – ilikuwepo sababu ya msingi.
Tafakari!
Upepo mkubwa wa mabadiliko unavuma pande zote za dunia. Tawala dhalimu na
kandamizi zinazojali zaidi maslahi ya watawala na kuacha wananchi wengi
wakitaabika, zinang’olewa.
Hivi karibuni kule Burkina Faso, Campaore amepinduliwa kwa ufagio wa umma
alipotaka kubadili Katiba ili aendelee kutawala. Vijana wengi walijitokeza
wakasema liwalo na liwe, wakaenda kulizingira Bunge na kuzuia kubadili Katiba na
hatimaye aliyekuwa rais akaikimbia nchi. Popote penye wimbi la mabadiliko, vijana
ndio wanaoongoza harakati hizo kwa sababu ni wakati wa mabadiliko.
Vijana wana maono. Kutokana na maono haya, wana hamasa na nguvu za kuleta
mabadiliko hayo. Hakika ni mabadiliko mema yenye kuwakumbusha watawala
kuwa wenye mamlaka ya mwisho kuhusu namna wanavyotaka nchi iendeshwe ni
wananchi wenyewe. Hivyo ni muhimu kwetu sote tuwaunge vijana mkono.
Maono hupatikana palipo na fikra safi zenye kujitegemea. Vyama vingi vya siasa
vilivyopigania uhuru katika nchi nyingi za Afrika, kwa sasa vimetoweka, au
vimeondolewa madarakani, au viko kambi ya upinzani.
Vyama ambavyo bado viko madarakani, vimechoka au kuchakaa kisiasa. Vingine
viko mbioni kufa au kujikuta kambi ya upinzani. Vyama hivi vilifanya kazi nzuri
zamani, lakini kila haki ina wakati wake.
Wengi wa wazee wetu na viongozi waliopigania uhuru wanashindwa kwenda na
mabadiliko. Matokeo ya kushindwa kwao ni kuwa katika nchi zao kuna vurugu na
migogoro isiyoisha.
Natumia nafasi hii kuwapongeza kwa dhati vijana wote ambao wamejitokeza kwa
wingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa kama wagombea na kama wapiga kura.
Kujitokeza kwa wingi kwa vijana katika kujiandikisha, kupiga kura na kusimamia
ushindi katika maeneo mengi ni ushahidi tosha kwamba mabadiliko Tanzania
yataletwa na vijana.
Vijana ni taifa la leo, si taifa la kesho peke yake. Piganieni mabadiliko
yatakayowanufaisha leo, watoto wenu kesho na wajukuu na vitukuu vyenu miaka
mingi ijayo.
Vijana kubalini na vumilieni kutaabika leo, lakini faida ya taabu yenu ni kubwa, kwa
kuwa taifa ambalo halitakubali kutaabika kwa faida yake lenyewe, bila shaka
litataabishwa na watu wengine. Vijana mnaweza kuthubutu.
Kuweni na ujasiri wa kupigania haki; maana bila uthubutu wa kuleta mabadiliko,
watu wachache wanaonufaika na mfumo wa kifisadi wataendelea kuifilisi nchi.
Ni vema kila kijana atambue kuwa vijana ndio chachu na nguvu ya mabadiliko.
Wazee hutumia muda mwingi kutafakari mapito yao badala ya kusonga mbele.
Wazee hutumia muda mwingi kufarijiana na kutukuzana kwa yale waliyoyapitia na
waliyoyafanya.
Maono yao yanaelekea kufifia. Wanataka kupumzika na kuvikwa taji. Hivyo, kama
tunataka maisha ya Watanzania wengi yabadilike, kunahitajika ushujaa na ujasiri
mkubwa zaidi wa vijana, mfano wa Joshua na Kalebu waliowaongoza wana wa
Israeli kuingia Nchi ya Ahadi.
Vijana wa Tanzania ni muhimu mjipange kuhakikisha kuwa katika chaguzi
zitakazofuata wanapatikana viongozi makini wa kuiondoa nchi yetu hapa
ilipokwama.
Vijana wa kike na wa kiume waliobahatika kupata elimu, iwe ya sekondari au chuo
kikuu, wenye maono ya kuiondoa nchi yetu hapa ilipokwama kiuongozi, wajiandae
kikamilifu kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Nchi itapata mabadiliko makubwa, kiuchumi na kijamii, iwapo itapata viongozi
vijana wachapakazi, wenye upeo mzuri, uadilifu na nia ya dhati, hasa katika ngazi
za vijiji, mitaa na wilaya. Hawa watakuwa chachu muhimu ya kubadilisha fikra za
watu ili kuipeleka nchi kwenye mabadiliko yatakayowanufaisha wananchi wote.
Hivi sasa vitongoji, vijiji na mitaa mingi inaongozwa na watu waliochoka, wasio na
maono wala nia ya dhati ya kuhamasisha mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na
kisiasa.
Kutokana na hali hiyo, makundi ya kijamii, wakiwemo vijana, wanawake, wenye
ulemavu na wazee wasiojiweza wanataabika kwa kukosa haki zao za msingi na
wamekata tamaa kuhusu hatma yao na nchi yao. Uongozi madhubutu katika ngazi
za vitongoji, vijiji na mitaa ni chimbuko la uongozi imara wenye maono na dhamira
njema katika ngazi ya udiwani, ubunge na urais.
Ili kufanikisha jamii ya Watanznaia kufika kwenye nchi ya ahadi, ni muhimu vijana
wajiunge kwenye vyama vya siasa. Bila kujiunga na chama cha siasa, kwa hali
ilivyo katika nchi yetu sasa, ni vigumu kuchaguliwa kuwa kiongozi.
Vijana pia waweke maadili na uzalendo mbele; kwa maana watu watakufa na
vyama vitakufa, lakini taifa lenye watu wenye maadili safi litabaki kuwa taifa imara.
Taifa likibaki salama na imara, sote tutabaki salama. Huo ndio ushindi wetu sote,
vijana na wazee, wanawake na wanaume. Kila kijana Mtanzania aweke mbele
utaifa. Awe macho.
Vijana msijiunge kwenye chama cha siasa kwa kushawishiwa kwa fedha au hongo
ya aina yoyote. Tusimpigie mtu au chama cha siasa kura kwa kuogopa vitisho vya
aina yoyote.
Kijana unapaswa kuwa jasiri na kutambua kwamba unayo nafasi ya pekee leo
kuamua hatma ya nchi yako Tanzania. Ukipokea rushwa katika mchakato wa
uchaguzi utakuwa umeshiriki kuikabidhi nchi yetu mikononi mwa kikundi cha watu
wachache wenye nia mbaya ya kujinufaisha binafsi kwa gharama yoyote; yaani
mafisadi.
Kijana using’ang’ane kutetea chama cha siasa kwa lengo la kulinda au kutafuta
maslahi yako binafsi kama vile kupata cheo au kitu chochote kile. Ukiwa
mwanachama wa chama cha siasa kwa sababu ya maslahi binafsi, utakosa ujasiri
wa kupigania maslahi ya taifa.
Utabaki ukibeba chama hata kama chama hicho hakina maono au kimekuwa cha
kulinda maslahi ya watu wachache wasiopenda mabadiliko. Kumbuka; kijana
kuweka mbele maslahi binafsi kuliko maslahi ya nchi ni usaliti kwa taifa lako.
Swali la msingi ambalo kila kijana anapaswa kujiuliza kila wakati huu ni hili:
Nafanya nini kuleta mabadiliko chanya ili kusitokee chama au kikundi cha watu
wachache kuhodhi raslimali au uongozi miaka nenda miaka rudi, watu wanaohodhi
sauti ya kufanya watakavyo juu ya maisha ya wananchi walio wengi na wanaofuja
raslimali za nchi yetu?
Naomba niwakumbushe vijana juu ya wito alioutoa aliyekuwa Rais wa Marekani,
John F. Kennedy, Januari 20, 1960. Wakati ule, Kennedy alikuwa amemaliza tu
kula kiapo cha urais baada ya kushinda uchaguzi.
Wakati ule, Marekani ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi ndani na nje.
Kennedy aliwataka Wamarekani wawe kitu kimoja, waondoe tofauti zao za kiitikadi
na waonyeshe uzalendo halisi kwa nchi yao.
Vilevile mataifa yaliyokuwa yanaitegemea Marekani kubadili mtazamo wa
kitegemezi na kutafuta mkakati mpya wa kushirikiana. Ndipo aliposema: “Ndugu
zangu wananchi wa Marekani, usiulize nchi yako itakufanyia nini, bali jiulize wewe
utaifanyia nini nchi yako!”
Na kwa nchi zilizokuwa zinaitegemea Marekani alisema: “Ndugu zangu wananchi
wa nchi nyingine, msiulize nchi ya Marekani itawafanyia nini, bali tujiulize kwa
pamoja tufanye nini kuleta uhuru kwa wananchi wetu”.
Hivyo kulingana na ujumbe alioutoa Kennedy, natoa wito kwa kila kijana wa
Tanzania, bila kujali itikadi ya chama chako, ujiulize utaifanyia nini nchi yako na
siyo nchi yako itakufanyia nini.
Huu ndiyo uzalendo mnaotakiwa kuuonyesha, enyi vijana kwa sasa. Na kwa
Watanzania wengine wote, tujiulize: Tuchukue hatua gani kwa pamoja bila kujali
itikadi za vyama vyetu vya siasa ili kuleta mabadiliko yenye tija kwa Taifa letu
badala ya kudai kuwa serikali itachukua hatua gani kuleta mabadiliko chanya.
Mdau wa kwanza wa mabadiliko ni mwanachi mwenyewe, wala si serikali.
Mwisho, vijana nawaomba nitafakari maneno ya mwanafalsafa wa kale aliyeitwa
Plato kwamba: “Binadamu kama hujagundua jambo lolote ambalo uko tayari kufa
kwa jambo hilo, basi hufai kuishi”. Kijana
 
Yeye alifanya nini??!!
Asubiri wakati wa hesabu naye atahesabiwa tu!!!

Pengine katambua kuwa hakuutumia wakati vyema...

Hivyo hataki na wengine wafuate njia ileile ya makosa ambayo kwayo kaipitia...

Kosa si kosa bali kosa ni kuendelea kuimarisha kosa...
 
Pengine katambua kuwa hakuutumia wakati vyema...

Hivyo hataki na wengine wafuate njia ileile ya makosa ambayo kwayo kaipitia...

Kosa si kosa bali kosa ni kuendelea kuimarisha kosa...

Ndio maana nataka aseme makosa yake ili wengine wasifuate njia hiyo maana yeye kama alikosea sehemu basi aseme wazi na aelekeze wengine kuwa ukiona this and that ujue hiyo sio njia sahihi na njia sahihi ni 1, 2, 3. . . . . . . we should learn from the lived experience of elders sio wao wawe watoa nasaha tu bila ya pragmatic explanations!!!
 
Back
Top Bottom