Vigogo wavizia kutwaa mgodi - Sheria mpya ya madini yawapa ‘ruksa’ bila kujali mgogoro kimadaraka | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vigogo wavizia kutwaa mgodi - Sheria mpya ya madini yawapa ‘ruksa’ bila kujali mgogoro kimadaraka

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Jan 5, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Jan 5, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 65
  Trophy Points: 145
  Mwandishi Wetu - Raia Mwema
  [​IMG]


  Mgodi wa TanzaniteOne
  *Wasuka mpango kuwazidi ujanja wachimbaji wadogo wa tanzanite
  *Sheria mpya ya madini yawapa ‘ruksa' bila kujali mgogoro kimadaraka


  KUKOSEKANA kwa sheria inayozuia viongozi wa umma kujihusisha na biashara wakati wakitumikia ofisi za umma, kumezidi kutoa mwanya kwa baadhi yao kujinufaisha na rasilimali za nchi kwa kadiri wanavyotaka, bila kujali makundi mengine ya wananchi, Raia Mwema, limezidi kubaini.

  Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kuwa kundi la baadhi ya viongozi wa kisiasa limeungana na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa tanzanite, kutwaa kwa namna yoyote mgodi unaoendeshwa na Kampuni ya Afrika Kusini, TanzaniteOne Ltd, ambayo leseni yake inakwisha Machi, mwaka huu.

  Ingawa leseni ya kampuni hiyo inakwisha, kwa mujibu wa sheria na sera mpya ya madini, kampuni za kigeni haziruhusiwi kuhodhi migodi ya vito kwa asilimia 100, isipokuwa si zaidi ya asilimia 50 tu.


  Upenyo huo wa kisheria na kisera ndiyo unaotoa mwanya wa wanasiasa hao kutwaa sehemu ya hisa hizo ambazo pia, wachimbaji wadogo wanataraji wanufaike kama walivyopata kuahidiwa.


  Raia Mwema
  limethibitishiwa kuwa TanzaniteOne Ltd, bado ina mpango wa kuendelea kuchimba tanzanite na hivyo imeomba kuongezewa muda wa leseni. Uthibitisho huo umetolewa na Kaimu Kamishna wa Madini Tanzania, Ally Samaje.


  Juhudi za kuhakikisha kundi hilo la wanasiasa kwa upande mmoja kuhujumu wachimbaji wadogo kwa upande mwingine, ili kutwaa mgodi huo au baadhi ya hisa, msingi wake ni ahadi ya Rais Jakaya Kikwete, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.


  Kikwete aliwaahidi wachimbaji wadogo kuwamegea eneo la mgodi huo baada ya TanzaniteOne Ltd kumaliza mkataba wake.


  Kumbukumbu zinabainisha kuwa, ahadi hiyo aliitoa akiwa Kijiji cha Lengast,
  wilayani Simanjiro, mkoani Manyara wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2010.


  Uamuzi wa TanzaniteOne

  Kwa kutambua kuwa leseni yao inakwisha, TanzaniteOne Ltd wamewasilisha maombi mapya ya leseni Wizara ya Nishati na Madini tangu Juni, mwaka jana (2011), ili waendelee kuchimba tanzanite katika Mererani, Simanjiro, maombi ambayo hata hivyo, bado hayajajibiwa.

  Lakini licha ya maombi hayo kutojibiwa na kwa hiyo, kampuni kutokuwapo kwa uhakika kama watapewa leseni mpya, TanzaniteOne wameendelea na shughuli nyingine zinazoashiria wana uhakika wa kubaki.


  Uchunguzi wetu umebaini kuwa kampuni hiyo inayochimba madini hayo kwa zaidi ya miaka 15 sasa, imeendelea kujenga nyumba mpya za wafanyakazi, maghala pamoja na mipango ya kuajiri wafanyakazi wapya katika idara mbalimbali kuanzia Januari 10, mwaka huu, hali inayoashiria wana uhakika wa leseni mpya.


  Habari zaidi zinaeleza kuwa kampuni hiyo inachosubiri kwa sasa ni kutangazwa kukubaliwa kwa maombi yake ya leseni mpya. Inaelezwa kuwa tangazo hilo linatarajiwa kutolewa na Waziri wa Nishati na Madini, mwishoni mwa mwezi huu.


  Mwenendo wa TanzaniteOne

  Rekodi zinabainisha kuwa kampuni hiyo imewahi kubadilisha jina lake kwa zaidi ya mara tatu, kuanzia mwaka 1996 iliwahi kufahamika kwa majina ya; Mererani Mining Company Ltd (MML), Sammax, AFGEM na baadaye TanzaniteOne, iliingia mkataba wa kuchimba madini hayo mwaka 2005.

  Hata hivyo, kampuni hiyo imekuwa ikiendesha shughuli zake za uchimbaji katika mazingira yenye mivutano kati ya mgodi kwa upande mmoja na wachimbaji wadogo kwa upande mwingine. Wachimbaji wadogo wamekuwa wakilalamika kunyanyaswa na kampuni hiyo.


  Wachimbaji hao wadogo wamekuwa wakiendesha shughuli zao katika maeneo ya vitalu A, B, D na eneo la Karro ambalo hata hivyo, si maarufu kwa uzalishaji wa madini hayo.


  Kigugumizi wizarani

  Uchunguzi zaidi umebaini kuwapo kwa taarifa zinazohusu Wizara ya Nishati na Madini, kupata wakati mgumu juu ya namna ya kutimiza ahadi zake za kuwagawia maeneo wachimbaji wadogo, ambalo waliahidiwa kupewa eneo la kitalu C, leseni ya TanzaniteOne ya sasa itakapokwisha.

  "Serikali iliwaahidi wachimbaji wadogo tangu mwaka 1995 kwa nyakati tofauti kuwa watapewa eneo la kitalu C, hasa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2000, 2005 na 2010, kwa hiyo, kutokana na mazingira hayo bado wizarani wanapata wakati mgumu kuamua kuhusu maombi ya TanzaniteOne," kilieleza chanzo chetu cha habari.


  Gazeti hili lilimtafuta bila mafanikio Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kutoa ufafanuzi wa suala hili lakini hakupatikana hata kupitia simu yake ya mkononi.


  Aliyepatikana kwa niaba Ngeleja ni Naibu Waziri wa wizara hiyo, Adam Malima, mwishoni mwa wiki.


  Malima alimjibu mwandishi wetu kuwa hayuko tayari kuzungumzia suala hilo kwa sababu amepigiwa simu akiwa kwenye mapumziko.


  "Mimi nilifikiri umenipigia simu labda umeme umekatika mtaani kwenu lakini kama ni jambo hilo naombe unistahi leo ni siku ya mapumziko siwezi kulizungumzia…. nipe heshima kidogo, heshimu faragha yangu tafadhali," alijibu Malima.


  Mgongano kuhusu sheria

  Uchunguzi wetu unabainisha kuwa wachimbaji wadogo wamekariri sheria kwamba haiwaruhusu wawekezaji wageni kuchimba vito nchini na kwa hiyo, TanzaniteOne ni lazima waondoke.

  Lakini wakati wachimbaji hao wadogo wakiamini hivyo, Serikali kupitia kwa Kaimu Kamishna wa Madini, Ally Samaje, wanaeleza kuwa sheria inawawekea mipaka wachimbaji wa kigeni tu na si kuwazuia kabisa kuchimba madini ya vito
  Nchini.


  Samaje anasema; "Sheria haizuii wageni kuchimba madini ya vito kama tanzaniteisipokuwa imeweka masharti wasimiliki migodi kwa asilimia inayozidi 50 na nyingine zinazobaki ni lazima zimilikiwe na wazawa.


  "Kwa hiyo, TanzaniteOne kwanza ndiyo wenye leseni hadi sasa na kwa sheria iliyopo, hawakatazwi kuendelea na shughuli zao isipokuwa ni kuomba upya leseni na kitakachofanyika kama watakubaliwa basi watamiliki mgodi kwa asilimia zisizozidi 50,"


  "Wanaweza kuamua kumiliki asilimia 30 au hizo hizo 50 na nyingine zinazobaki katika asilimia 100 ni kwa ajili ya wazawa, suala hapo ni je, hao wazawa wanapatikana katika mpangilio gani?" anaeleza Samaje.


  Msimamo wa wadau wengine

  Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wauzaji Madini ya Vito Tanzania (TAMIDA), Sammy Mollel, aliiambia Raia Mwema kuwa, wanachosubirini ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali kugawa eneo husika kwa wachimbaji wadogo.

  "Tumesubiri kwa muda mrefu sana, sasa muda umefika wa Serikali kutimiza ahadi yake ili eneo hilo ligawanywe kwa wachimbaji wadogo nao wajikomboe kiuchumi baada ya kukandamizwa kwa muda mrefu na mfumo wa uchimbaji usio na uwiano sawa,"anasema Mollel.


  Mollel ambaye pia anamiliki baadhi ya migodi ya tanzanite aliweka bayana kuwa watashangaa iwapo waziri mhusika atapuuza ahadi ya Rais kutotoa tena leseni kwa TanzaniteOne.


  "Kauli ya Rais ni zaidi ya sheria kwa ufahamu wangu, kwa hiyo, sitarajii waziri atakwenda kinyume cha ahadi ya Rais mbele ya hadhara na pia muda umefika sasa wa Serikali kuwawezesha wazawa badala kuwakumbatia wageni ambao wamekuwa wanamaliza rasilimali zetu," alisema Mollel.


  Njama za vigogo

  Habari zaidi mkoani Arusha zinaeleza kuwapo kwa shinikizo kutoka kwa baadhi ya wamiliki wa migodi walioungana na baadhi ya wanasiasa ili ‘kunyakua' migodi ya TanzaniteOne, inayomaliza muda wake wa leseni.

  Wachimbaji na wanasiasa hao ambao wanaelezwa kuwa wenye ushawishi na nguvu za kisiasa nchini majina yao yanahifadhiwa kwa sasa, wamekuwa katika harakati za muda mrefu kushawishi maofisa Wizara ya Nishati na Madini ili wapewe mgodi huo.


  "Tayari wako katika mipango ya kuanzisha kampuni itakayoomba leseni ya kuchimba eneo la kitalu C, baada ya wawekezaji kutoka Afrika ya Kusini kuondoka. Kigezo chao ni kwamba, kampuni hiyo ni ya wazawa hivyo wanahaki ya kupewa leseni kwa mujibu wa sheria za sasa," anaeleza mmoja wa wachimbaji anayemiliki mgodi eneo la Mererani.


  Kwa mujibu wa mchimbaji huyo, ishara za kuwapo kwa mgogoro mkubwa endapo wachimbaji wadogo watakosa eneo husika.


  Madini ya tanzanite ambayo yaligunduliwa kati ya mwaka 1968 na 1972 katika miinuko ya Milima ya Mererani, Simanjiro, mkoani Manyara, yamekuwa chanzo cha utajiri kwa baadhi ya wachimbaji, kutokana na thamani yake katika soko la ndani na hata soko la dunia.


  Ingawa hakuna takwimu rasmi, inakadiriwa kuwa migodi hiyo imetoa ajira kwa watu zaidi ya 50,000 wa vijiji vya jirani pamoja na miji ya jirani kama Arusha, Hai na Simanjiro.


  Msimamo wa Januari Makamba

  Gazeti hili lilizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Januari Makamba, kwa simu akiwa Dubai, ili kujua kama kamati yake imepata taarifa za njama za viongozi kutwaa mgodi husika.

  Makamba alijibu; "Hatuna hizo taarifa na wala sikuwa nikijua kama leseni ya TanzaniteOne inakwisha Machi, wewe ndio unaniambia.


  "Lakini suala la msingi ni sheria na sera ya madini inayoruhusu madini ya vito yachimbwe kwa kuhusisha wazawa, isimamiwe vizuri ili kuwalenga wachimbaji wadogo kama kipaumbele cha sheria.


  "Haina maana unamwondoa mwekezaji mkubwa wa kigeni halafu unawapa kikundi cha watu fulani matajiri na kwa hiyo, mazingira ya mgodi kunufaisha kikundi kidogo yataendelea. Nadhani ni vizuri kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapewa fursa ya kufaidika na rasilimali za nchi yao."

   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Jan 5, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 65
  Trophy Points: 145
  VIongozi wetu wengi wa sasa ni wazito yuko wapi Magufuli?
   
Loading...