Vigogo waongo, Waziri aagiza wabanwe

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,069
265
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe ameishukia Sekretarieti ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, akidai imeshindwa kutumia mamlaka iliyonayo kuwabana vigogo wa serikali wanaojihusisha na rushwa, ufisadi na wanaodanganya juu ya mali walizonazo.

Chikawe alitoa madai hayo mazito alipozungumza na wafanyakazi wa sekretarieti hiyo, Dar es Salaam jana, ikiwa ni ziara yake ya kwanza kuifanya katika taasisi zilizo chini ya ofisi yake hiyo inayoshughulikia utawala bora.

Waziri Chikawe alisema, viongozi wengi wanaojaza fomu za maadili ya viongozi wa umma wanadanganya kuhusu mali zao kwa lengo la kuficha ukweli kitendo alichosema kinapaswa kuchukulia hatua za kisheria mara moja.

Alisema pamoja na kudanganya, lakini pia wapo viongozi wa umma wanajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi, lakini hakuna hatua zozote wanazochukuliwa, hatua inayopotosha dhana nzima ya utawala bora.

Aliitaka sekretarieti hiyo kubadilika mara moja kiutendaji na kufanya uchunguzi wa kina juu ya maadili ya viongozi hao ili kuwafichua na kuwachukulia hatua za kisheria wale watakaobainika kudanganya juu ya mali walizonazo, kuhusika na rushwa au ufisadi.

Chikawe alisema uwezo wa kiutendaji iliyoonesha sekretarieti hiyo ni sawa na asilimia nne ya kazi nzima wanayotakiwa kuifanya, hatua ambayo haikidhi kuudhihirishia umma kwamba ipo makini katika kusimamia maadili ya viongozi.

Kwa mujibu wa Chikawe, umefika wakati kwa sekretarieti hiyo kutambua umuhimu wake kwa umma, na hivyo kuwajibika kwa kuzingatia malengo yaliyosababisha kuwepo kwake.

Alisema, sekretarieti hiyo inawajibika pia kuzifundisha, kuzielekeza na kuziagiza taasisi nyingine, kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kushughulikia masuala yanayohusu rushwa na ufisadi badala ya kuziacha taasisi hizo kufanya kazi zipendavyo.

Alisema ingawa sheria iliyoanzisha sekretarieti hiyo haina meno ya kutosha katika kuwaadhibu viongozi wanaokiuka maadili ya umma, lakini hiyo haiwezi kuchukuliwa kama sababu ya kuwaacha kuendelea kukiuka maadili ya umma bila kuchukuliwa hatua kwani sekretarieti hiyo inaweza kuziagiza taasisi zake ikiwemo Takukuru kuwafikisha viongozi hao mahakamani kwa kutumia sheria zao.

“Natambua umuhimu wa sekretarieti hii na jambo hili nitalipa umuhimu mkubwa ili kuhakikisha tunaandaa utaratibu wa kuifikisha sheria hii bungeni kwa ajili ya kuongezwa makali ili itoe mamlaka ya kuwawajibisha viongozi wasio waadilifu kwa lengo la kukuza na kulinda utawala bora nchini.

“Ifikie mahali muiite Takukuru na kuiagiza ichunguze viongozi fulani mtakaokuwa na mashaka na maelezo yao wanayoyatoa katika fomu za maadili ya viongozi, taasisi hiyo itazifanyia kazi zaidi na kuwafikisha mahakamani watakaobainika kusema uongo pale inapobidi, vinginevyo, ufisadi na rushwa havitakoma,” alisema.

Alisema, wapo viongozi wanaodanganya wakati wana chembechembe za wazi za rushwa na ufisadi, na kwamba ndio maana asilimia moja ya tatu ya bajeti za serikali za kila mwaka zinaishia kwenye rushwa na ufisadi wa viongozi wa umma.

“Hili ni tatizo na kikwazo kwa utawala bora, nitatoa ushirikiano wa kutosha ili tulikomeshe, nipeni na mimi ushirikiano tulifanikishe kulimaliza,” alisema Chikawe.

Jumla ya viongozi wa umma wanaojaza fomu hizo za maadili ya viongozi, kwa mujibu wa Waziri Chikawe ni 7,888 ambapo viongozi wa kisiasa wakiwemo mawaziri ni 4,018 na watendaji wengine wakiwemo Makatibu Wakuu ni 3,870.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom