Vigogo wakwamisha vita ya 'unga' nchini

Balile

Member
Oct 10, 2011
74
140
Vigogo wakwamisha vita ya ‘unga’ nchini

• Rais Kikwete asutwa kwa kutochukua hatua
• Kamishna ataka kujiuzia gari la Tume, anena
• Esther Bulaya avamiwa, asema wanalenga watoto

Vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inazidi kuwa ngumu kutokana na viongozi wa juu wa nchi kukumbatia uozo, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Uadilifu na uzalendo vimepotea na mfumo umesukwa kuwawezesha watendaji kufaidi biashara ya dawa za kulevya tofauti na hali ilivyokuwa wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, vyanzo vimethibitisha.


Wenye kufanya biashara hii wanadaiwa kujenga mfumo hadi ofisi za juu serikalini kwa kiwango kinachoifanya Serikali kushindwa kuchukua hatua, hivyo wadau wamependeka mabadiliko makubwa katika mfumo.

Watendaji waliopewa kazi ya kusimamia vita hii baadhi yao ndani ya Tume ya Uratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya, wanawaza matumbo yao kwanza.
Mushengezi Nyambele, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kwanza wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ameliambia JAMHURI kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji “moyo kabla ya silaha”.

“System (mfumo) ikiishakuwa mbovu nani atamkamata nani? Tunapaswa kurejesha nidhamu, kurejesha uzalendo, na uzalendo huu unapaswa kuanzia juu [kwa Rais] kuja chini… bila haya, hata sheria iwe nzuri kiasi gani, ujangili utaendelea, kodi haitakusanywa. Msingi hapa ni kurejesha maadili katika kila sekta,” amesema Nyambele.

Katika Awamu ya Kwanza, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, Nyambele anasema Serikali haikuvumilia wauzaji, washirika na yeyote aliyejihusisha kwa njia yoyote na biashara ya dawa za kulevya.

“Mwaka 1984 tulikamata kilo tatu za heroin pale Kilimanjaro. Watuhumiwa walifanya mbinu wakashinda kesi, lakini Mwalimu Nyerere alitoa agizo kuwa wote waliokuwa zamu kuanzia maafisa wa TRA, polisi, watumishi wa uwanja wa ndege na wote waliokuwa zamu siku hiyo, walifukuzwa kazi na utumishi wa umma,” anasema Nyambele.

Kwa mshangao, chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete pamoja na kuahidi kuwa anayo orodha ya wauza dawa za kulevya kitambo, watendaji wengi wanaoshukiwa kupitisha dawa katika maeneo mbalimbali wanaendelea kuwa kazini bila wasiwasi wowote, hali waliyosema wachambuzi kuwa ni hatari na Rais Kikwete anapaswa kukazi uzi.

“Leo dawa zinakamatwa kila kukicha, hatuoni watu wakiwajibika,” anasema Nyambele. Anaonya kuwa urafiki uliopo kati ya wanasiasa, watendaji na wasimamizi wa sheria na wauza dawa za kulevya umesitawisha biashara hiyo.

Mwaka 1992, Nyambele yalimkuta. Akiwa mtumishi katika Idara ya Ushuru wa Forodha, walikamata kontena la dawa za kulevya wakalihifadhi katika ghala la Tumbaku Kurasini Dar es Salaam, likawa linalindwa na polisi saa 24.

“La kushangaza, siku tulipotakiwa kupeleka ushahidi mahakamani, tulipofungua kontena tukakuta halina kitu. Pamoja na kulindwa na polisi kwa saa 24, tulikuta mzigo wote uliokuwamo – cannibas chocolates – umeondolewa wote, ila yamesalia mabaki tu. Mabaki hayo yalisaidia kuendesha kesi na kuwatia hatiani wahusika,” anasema.

Baada ya kukamata kontena hilo Dar es Salaam, Idara ya Ushuru wa Forodha wakati huo, iliagiza uchunguzi wa kina ufanywe Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar, baada ya kupata taarifa kuwa yalikuwapo makontena mengine yenye dawa za kulevya katika miji hiyo.

“Nilipokwenda Zanzibar [mwaka 1992], nilipita kwenye hoteli za kitalii, nikapita kwenye fukwe, hali niliyoikuta ilikuwa inatisha. Nikiwa hotelini, nilipokea simu kutoka kwa waziri - simtaji jina - akaniambia mamlaka ya juu imeelekeza nitoke visiwani Zanzibar katika muda usiozidi saa moja. Nilikwenda uwanja wa Ndege Zanzibar, nikakuta ndege ya Coastal Air, nikapanda na kurejea Dar es Salaam”.

“Nilijiuliza mamlaka hayo ni nani yenye kumwagiza Waziri? Walijuaje nipo na nafuatilia suala la dawa za kulevya? Hata hivyo, nilivyorejea niliandika ripoti nikamkabidhi Kamishna wangu nikasema nilichokiona Zanzibar baada ya miaka 10 Zanzibar itakuwa janga katika dawa za kulevya, na kweli imetokea,” anasema Nyambele.

Afisa huyo mstaafu, anasema ingawa Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, anafanya kazi nzuri na ya kupigiwa mfano, anaamini kuwa baadhi ya polisi wasio waaminifu wanamwangusha.

Idara ya Mahakama pia, anasema inaacha maswali mengi katika uamuzi inaoufanya, hali inayofanya kazi ya vita dhidi ya dawa za kulevya kuwa ngumu. Anashauri utaratibu aliouacha Mwalimu Nyerere urejeshwe ambapo TRA kupitia Idara ya Forodha ndio ifanye kazi ya kukamata dawa za kulevya na kuhifadhi vidhibiti, kisha polisi wafanye kazi ya kuchunguza matukio.

Anaamini chini ya utaratibu wa sasa ambao polisi wanachunguza, wanakamata na kuendesha mashitaka, kwa kiwango cha mmomonyoko wa maadili uliopo, vita hii haiwezi kusonga mbele. “Ni lazima kazi hii ifanywe na chombo zaidi ya kimoja kuepusha uamuzi tata,” anasema.
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya (ADU), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Godfrey Nzowa, amesema suala la maadili ni muhimu kwa nchi kupigana vita hii kwa ufanisi na akasema hata sheria ya sasa si mbovu, bali inahitaji kujitoa katika kuisimamia.

Kamishna na gari la Tume
Wakati Nyambele akijenga hoja ya uadilifu kupungua, miezi miwili baada ya kuingia kazini kama Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, Kenneth James Kasseke, ameanza kuwatia shaka wapambanaji wa dawa za kulevya nchini iwapo ana nia ya dhati kupambana na dawa za kulevya.

Katika hali inayotia wasiwasi iwapo ataweza kuifanya kazi ya kupambana na wauza ‘unga’ kwa uadilifu na ufasaha, Kasseke ameanzisha mchakato wa kujiuzia mali za Tume hatua ambayo inaweza kudhoofisha utendaji wa Tume.

Tume inamiliki magari matatu, mawili yakiwa aina ya ‘pick up’ na yana hali mbaya, Kamishna Kasseke anataka kujiuzia gari pekee jipya lililopo kwenye Tume hiyo, linalotumiwa kupambana na dawa za kulevya nchini kwa sasa.

“Tumepata mshtuko mkubwa mno. Gari hili ni jipya kabisa halina hata miaka miwili tangu linunuliwe. Maafisa ndio wanalolitumia kufukuza wauza unga na kupanda milima kwenda kuteketeza bangi huko Morogoro, Arusha na Lushoto - Tanga, lakini ajabu huyu baba ambaye ana miezi miwili tu ofisini anataka auziwe gari hilo.

“Hii ina maana akiuziwa hili gari, Tume itakuwa haina gari lolote linaloweza kusafiri safari ndefu na kupanda milima kama ya Morogoro kwa nia ya kuteketeza mashamba ya bangi. Ameandika barua rasmi kuomba kuuziwa gari hilo, na sisi hapa utumishi tukashangaa kweli kupokea ombi hili,” kimesema chanzo chetu kutoka Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Nakala ya barua hiyo, ambayo JAMHURI limeipata na kumpelekea Kasseke kwa njia ya Whatsapp, inakwenda kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, S. L. P. 2384, Dar es Salaam, ya Oktoba 17, 2014 ikiomba kuuziwa gari namba STK 5337 (Hard Top) Chasis Na. jTERB71j00---47106 Engine Na. 1HZ-0590111, analoliita chakavu.

Baada ya JAMHURI kupata taarifa hizo, iliwasiliana na Kasseke aliyekiri kuwa na nia ya kununua gari hilo, kwa kusema: “Ndiyo, nataka kulinunua,” alipoulizwa kwa nini anataka kununua gari ambalo si chakavu na ndilo tegemezi kwa Tume akaongeza: “Gari hili si tegemezi na ni chakavu, lakini kuna magari mengi tunayoyatumia kwenye Tume.”

Majibu hayo yasiyo na uhalisia, yalilifanya JAMHURI kuwasiliana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, William Lukuvi, alipoulizwa juu ya nia ya Kasseke kununua gari la Tume alisema:
“Miezi miwili tu kazini ameishataka kununua gari, hii ni hatari. Ndo napata taarifa hizi, lakini nakuhakikishia nitazifanyia kazi kwa kina. Nitafute wiki ijayo nitakuwa na jibu sahihi. Hii haikubaliki,” alisema Lukuvi.

JAMHURI lilipomtafuta Lukuvi wiki moja baadae, alisema: “Nimekwishaagiza uuzaji huo usitishwe mara moja. Hili limenishtua, na napata tabu kama wahusika wana nia ya dhati ya kupambana na dawa za kulevya. Tutawabana na kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria.”
Kwa Upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi, alishukuru kwa kupewa taarifa na kuahidi kulifuatilia kwa kina suala hili.

Mbali na kuteuliwa Mei 19, 2014 kumrithi Kamishna Shekiondo aliyestaafu, Kasseke (58) ameingia rasmi ofisini Agosti 1, 2014 na hivyo kwa kutoa ombi la kunua gari Oktoba, baadhi ya watumishi wa umma wamesema kasi yake ya ubadhirifu inatisha.
Tume hii inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa na hili ndilo gari pekee linalotegemewa hivyo likiuzwa itakuwa imeishiwa uwezo kabisa wa kufanya kazi kwa mujibu wa watumishi waliopo ndani ya Tume hii.

Bulaya alia na Ofisi ya DPP
Ester Bulaya, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), ameliambia JAMHURI kuwa kwa kiasi kikubwa ofisi ya DPP imejaa watu wenye uhusiano wa karibu na wauza ‘unga’ hivyo ilihitaji nguvu ya Mungu kumpata DPP asiyeendekeza rushwa.

“Katika hoja yangu bungeni nilisema Ofisi ya DPP ina watu wanaoshirikiana na wauza unga. Hii ni hatari, na Serikali hadi leo imekaa kimya haijajibu. Ni kutokana na hili nasema ilihitaji umakini wa hali ya juu kumpata DPP msafi,” alisema Bulaya.

Habari kutoka ndani ya ofisi ya DPP zinasema yupo Mwanasheria Mwandamizi aliyekuwa anapigiwa debe hadi na mawaziri ateuliwe kuwa DPP ila historia yake ya kushirikiana na wauza unga imemponza.

“Amefanya kampeni kubwa huyu bwana. Amewasiliana na watu wengi, amezungukia wakubwa wengi akiomba wamsaidie kuwa DPP lakini [Biswalo] Mganga historia yake ikambeba kuteuliwa kuwa DPP. Ana historia ya kutukuka huyu bwana na matumaini yetu ni makubwa kuwa atainyoosha ofisi hii,” alisema mtoa habari wetu.

Rais Jakaya Kikwete alimteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka, Biswalo Mganga, kuwa DPP Oktoba 3, mwaka huu. Biswalo hakutarajiwa na wengi kuwa angepewa wadhifa huo kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya maovu mbalimbali katika jamii.
Novemba mwaka 2011, Biswalo Mganga akiwa Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka alisimamia kesi kubwa ya kilo 95 za dawa za kulevya aina ya heroin zilizokamatwa Machi 15, 2010 kwenye eneo la Kabuku mkoani Tanga.

Kesi hiyo iliyomhusisha Assad Aziz Abdulrasul ambaye ni mdogo wa mwanasiasa maarufu nchini, Rostam Aziz, aliyekuwa akituhumiwa kusafirisha kilo 95 za dawa za kulevya aina ya heroin aliisimamia bila kuyumba katika Mahakama Kuu Kanda ya Tanga hadi watuhumiwa wakatiwa hatiani.
Mganga aliongoza mashitaka kupinga watuhumiwa kupewa dhamana, ambapo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Kipenka Mussa (wakati huo) alikubaliana na hoja za Mganga katika kesi hiyo Na.1/2011 na kuwanyima dhamana watuhumiwa pamoja na mashinikizo makubwa kutoka pande mbalimbali yaliyokuwa yakimkabili.

Mbali na Assad watuhumiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni Kileo Bakari Kileo, Yahya Makame, Mwamadali Podadi ambaye ni raia wa Iran, Salum Mparakesi, Saidi Ibrahim Hamis na Bakari Kileo ‘Mambo’ ambao walikuwa wakitetewa na mawakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza na Edward Chuwa. Watuhumiwa walitiwa hatiani, wakafungwa miaka 25 jela na faini ya Sh bilioni 1.1 kila mmoja

DPP Biswalo alonga
Biswalo ameliambia JAMHURI kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya ni ya jamii yote. “Vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji ushirikiano wa jamii nzima. Tunahitaji ushirikiano wa polisi, Serikali na Mahakama. Hili si la kuachwa kwa Serikali pekee, ni la Watanzania wote. Kila mtu apigane hii vita, Mahakama isijione iko salama kwa kuachia watuhumiwa. Watanzania wote tuwajibike wahusika tuwafikishe kwenye vyombo vya sheria,” anasema Biswalo.
Ameitaka jamii kufikiria nguvu kazi inayopotea kwa vijana wengi nchini kuathirika na dawa za kulevya na kuongeza kuwa kila mwananchi anapaswa kuhakikisha watuhumiwa wanafikishwa kenye vyombo vya sheria.

Biswalo anasema mbali na vijana kushindwa kuzalisha kwa kupoteza nguvu kazi, dawa za kulevya ni tishio kwa usalama wa taifa kwani ni rahisi vijana walioharibiwa akili na dawa za kulevya kusaliti nchi au kujiingiza katika vitendo vya wizi na ujambazi kwa nia ya kupata fedha za kununulia dawa.
Kwa upande mwingine, Kamishna wa Ofisi ya Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya ameteuliwa mwaka huu. Kwa muda wa mwaka mzima kati ya Agosti, mwaka 2013 na Agosti, 2014 ofisi hiyo ilikuwa inakaimiwa na Aida Tesha. Aliyeteuliwa ni Naibu Kamishna wa Polisi, Kenneth Kaseke.
Kwa mujibu wa kifungu cha 27(1)(b), Kamishna wa Tume hiyo ndio pekee anayeruhusiwa kutoa cheti chenye kuonyesha thamani ya dawa za kulevya alizokamatwa nazo mhusika, na hakuna afisa mwingine anayekaimu au kushika wadhifa mwingine anayeweza kusaini cheti hicho kikakubalika mahakamani. Kaseke alipoteuliwa amesaini hati 50 za kesi kubwa.

Taarifa za kiuchunguzi zilionyesha kuwa wauza ‘unga’ wamekuwa wakitumia mwanya wa kutokuwapo Kamishna wa Tume kuendesha biashara zao bila wasiwasi kwani walijua fika kuwa Kaimu Kamishna hakuwa na nguvu za kisheria kusaini cheti cha thamani ya dawa za kulevya ambacho ni kigezo muhimu katika kuamua iwapo kesi ni ndogo au kubwa.

Kifungu hicho cha sheria kinasema kesi yoyote ambayo thamani ya dawa kwenye cheti kilichosainiwa na Kamishna wa Tume inazidi Sh milioni 10, basi mtuhumiwa hapewi dhamana na kama ni chini ya kiasi hicho anaweza kupewa dhamana.

Katibu (mstaafu) wa TRA Nyambele, ameliambia JAMHURI kuwa kuchelewesha kuteuliwa kwa Kamishna wa chombo hicho nyeti ni hatari kwani kwa umuhimu wa nafasi hiyo haipaswi kupita hata siku mbili kabla uteuzi haujafanyika. Anasema sheria ya utumishi wa umma inataka anayestaafu kutoa taarifa miezi sita kabla ya kustaafu, hivyo muda huo unapaswa kutumiwa kuchunguza mtumishi mwingine wa kuteuliwa.
“Hii kukaimu ni uozo katika serikali yetu. Kwa chombo nyeti kama hiki, huwezi kuruhusu watu kukaimu na kesi kukwamishwa,” anasema Nyambele na kuongeza kuwa unahitajika uhakika iwapo hilo lilitokea kwa bahati mbaya au makusudi.

Bulaya avamiwa nyumbani kwake
Katika hatua nyingine, Bulaya ameliambia JAMHURI kuwa baada ya kuwasilisha Maelezo Binafsi Bungeni, Machi mwaka huu, watu wasiofahamika walivamia nyumbani kwake Dodoma wakavunja dirisha na kuingia ndani wakapekua kila mahali lakini hawakuchukua chochote.

“Walifika watu wakamuuliza mdada wa kazi iwapo nipo akawaambia sipo. Na kweli nilikuwa nimesafiri, lakini baadae nikaja kukuta walifika wakapekua kila sehemu kwenye masanduku na kabati yangu, lakini hawakuchukua chochote isipokuwa waliacha vitu vimetapakaa chini,” amesema Bulaya.
Bulaya amesema viongozi waliopewa jukumu la kudhibiti dawa za kulevya nchini hasa kwa njia ya kukamata na kuendesha mashitaka wanapaswa kuifanya kazi hii kwa moyo mkuu kutokana na mpango mbaya walionao wauza dawa za kulevya kwa jamii hii, aliouita mpango wa kishetani.
“Mbaya zaidi wafanyabiashara wa dawa hizi haramu sasa wameanza kuwatumia watoto wa shule za msingi chini ya falsafa isemayo “wapate wakiwa wadogo… wafanye watumwa wa dawa za kulevya… na kupata uhakika wa soko la baaadae pale ambapo watakuwa wameajiriwa au wamejiajiri,” anasema Bulaya.

Rehema Salum Abdallah, 53, mkazi wa Temeke Mikoroshini Dar es Salaam, amesema Tanzania ikiliacha taifa likawa kichaka cha kuuza dawa za kulevya, uchumi utanguka na heshima ya jamii itatoweka.

“Bila kudhibiti hii hali tutageuka kuwa wanyama. Leo teja (kijana aliyeathirika na dawa za kulevya) akikuta sufuria hapa nje analichukuwa. Kwa gari lako kama hili ukitoka kidogo tu, anachomoa ‘side mirror’ na anakwenda kuiuza si zaidi ya Sh 2,000. Hapa Temeke jamii imeharibika kweli. Naiomba Serikali na wananchi tushirikiane kupambana na janga hili ambalo ni hatari kuliko Ukimwi, maana ukimwi unakwenda kuutafuta mwenyewe, lakini ‘mateja’ wanakuja nyumbani kwako bila kujua,” anasema Rehema.


Taswira ya Tanzania kimataifa
Dafrosa Deogratias aliyehitimu Stashahada ya Uzamili katika Chuo cha Diplomasia Kurasini Dar es Salaam mwaka huu na kufanya utafiti juu ya uuzaji wa dawa za kulevya unavyoathiri heshima ya Watanzania nje ya nchi, anasema kwa aliyobaini hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa.
“Leo Watanzania wanaposafiri nje ya nchi wanapekuliwa kuliko inavyostahili. Hati za kusafiria za Tanzania zamani ziliheshimika, lakini kwa sasa mtu akikuona nayo wazo la kwanza linakuwa ni kwamba labda unakwenda kuuza unga. Hii ni hatari na haikubaliki. Lazima viongozi wachukuwe hatua kudhibiti janga hili,” anasema Dafrosa.

Kwa siku za karibuni vita dhidi ya dawa za kulevya iliyumba kutokana na Ofisi ya Kamishna wa Tume kuwa na Kaimu kwa maana kwamba hakuna ambaye angeweza kusaini hati ya thamani ya dawa alizokamatwa nazo mtuhumiwa na hivyo kufanya mapambano yadorole. Ukiacha upungufu wa baadhi ya watendaji, ni imani ya jamii sasa kuwa vita hii itaanza kwa kasi mpya sasa.

Uchunguzi huu umefanywa kwa udhamini wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa kushirikiana na Ofisi ya Kuzuia Uhalifu na Dawa za Kulevya ya Umoja wa Mataifa (UNDOC), na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini (DCC).

Chanzo:jamhurimedia

 
Tatizo letu Watanzania ni unafki, hakuna asiyejua kuwa kuna vigogo wanaojihusisha na biashara hii na ndio maana vita yake haifanikiwi.

Tunachotaka kujua ni vigogo gani hao.

Nafikiri mwandishi ndio angekuja na jibu kwakuwa ameshafanya uchunguzi. Sasa kila siku vigogo vigogo majina hamuwataji mnategemea watu wa kawaida wafanyaje?
 
Ukweli ni Mchungu kuusikia,lakini kuna Prof mmojaaliongea bungeni kinagaubaga akisema kwa kujiamini kabisa hawawezi kuwakamata wauzaji wa madawa ya kulevya sababu watoto wao ndiyo wafanyabiashara wenyewe.

Poleni watanzania wenzangu,kama Mbunge ameweza kuyasema hayo inamaana kuna hata WABUNGE hii ndiyo biashara yao inayowaweka mjini.
 
Hii vita ni kubwa duniani. Marekani imepambana kwa muda mrefu kuiangamiza biashara hii haramu hasa Colombia na Mexico, kwa kupeleka vikosi maalumu lakini bado. Hii ni kwa sababu Vigogo wengi serikalini wanahusika.

Vita hii ya madawa ya kulevya inanikumbusha movie inaitwa "THE HARD WAY." Enzi hizo nikiwa mdogo sana.
 
Back
Top Bottom