Vigogo waipeleka TANESCO kitanzini

G.MWAKASEGE

Senior Member
Jun 29, 2007
153
15
HUKU Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) likiwa linakabiliwa na hali mbaya ya kifedha, imebainika kuwa kuna mpango mahususi wa kuliangamiza shirika hilo unaofanywa na baadhi ya watendaji serikalini kutokana na maslahi binafsi.

Habari kutoka serikalini zinaeleza kwamba tayari mpango kamambe unaandaliwa kuhakikisha shirika hilo linaingia katika mikataba mingine itakayolikamua zaidi kifedha ambayo ni mbali na muswada wa kuruhusu watu binafsi kufanya biashara ya umeme.

Imeelezwa kwamba uamuzi wa serikali kuwasilisha bungeni muswada wa kuziruhusu kampuni nyingine kuuza umeme bila kuiandaa TANESCO kibiashara na kwa upande mwingine kuendelea kuikamua kimapato ni hatua ya kutaka kuiua kabisa TANESCO.

Ofisa mmoja wa juu serikalini ameliambia RAIA MWEMA kwamba, kiongozi mmoja wa juu serikalini ameelezewa kuilazimisha TANESCO kulipa mamilioni ya fedha kwa kampuni ya Independent Power Limited (IPTL) jambo ambalo limekua likipingwa hata na baadhi ya viongozi wenzake serikalini.

Kwa mujibu wa habari hizo baadhi ya viongozi na watendaji pia wanasukuma kubadilishwa wa kampuni ya Songas inayozalisha umeme kwa maelezo kwamba kampuni hiyo inalipwa fedha kidogo kulinganisha na makampuni mengine yanayoiuzia TANESCO umeme, mpango ambao umeelezwa kuwashangaza wengi.

TANESCO inauziwa umeme unaozalishwa na Songas kwa senti za Marekani 5.5, wakati makampuni mengine kama IPTL senti 11, Richmond senti 4.5 na Aggreko senti 4.99 na hivyo viongozi hao wameionea ‘huruma’ Songas kwamba na wao wanahitaji bei zaidi.

Hata hivyo, vyanzo vya habari ndani ya sekta ya nishati vinaeleza kwamba kwa kawaida baada ya uzalishaji kuanza, bei ya umeme ilitakiwa kushuka na si kupanda na kwamba kulikua na mpango wa kubadili viwango hivyo na kuwa vya chini na si kuvipandisha.

“Ninavyofahamu ni kwamba kitaalamu kwa sasa bei ya umeme unaouzwa kwa TANESCO inapaswa kupungua kimahesabu kwa kuwa kuna mahesabu ya kitaalamu yanayowezesha hali hiyo, sasa kama umesikia wanataka kupandisha hiyo kwangu itakua habari ya ajabu kabisa, ama haiwezekani. Lakini kwa nchi yetu mambo ya ajabu kabisa huwa yanawezekana, hivyo fuatilia tuone,” alisema mtaalamu mmoja aloiyebobea katika uchumi wa nishati.

Kuhusu suala la IPTL, habari zinaeleza kwamba katika kikao kimoja cha ndani, kiongozi mmoja wa juu serikalini aliwaambia TANESCO ni lazima wawalipe IPTL fedha wanazotaka ili ‘kuepuka aibu’ kwa Serikali, uamuzi ambao ulipingwa vikali na wanasheria binafsi wanaoitetea Serikali na TANESCO.

“Unajua nimeelezwa kwamba ilikua ni aibu, kwani badala ya viongozi wetu kuwa upande wa TANESCO wanakua upande wa IPTL, jambo ambalo lilimkera hata mwanasheria ambaye alikua akiitetea Serikali. Sijui alikua akiwakilisha maslahi ya nani,” alisema ofisa mwingine mwandamizi wa Serikali.

Serikali ya Tanzania ilisitisha malipo kwa IPTL kwa maelezo kwamba kampuni hiyo imeshindwa kuwekeza kama inavyopaswa katika uzalishaji wa umeme na pia imedanganya gharama halisi za mradi jambo ambalo TANESCO inaamini kwamba kimahesabu kampuni hiyo ndio inayopaswa kuwalipa wao.

IPTL kuona hivyo iliamua kufungua kesi katika mahakama moja nchini Marekani ikidai kulipwa zaidi ya Shilingi bilioni 30/-, kesi ambayo imeelezwa bado inaendelea na hivyo TANESCO bado inaona si busara kulipa fedha hizo wakati majadiliano yanaendelea.

Hata hivyo, mmoja wa watu wenye hisa ndogo katika IPTL, mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Markerting Limited, James Rugemalira, amepinga uamuzi huo wa wanahisa wenzake.

Rugemalira ambaye alinukuliwa na gazeti la serikali la Daily News mwishoni mwa mwaka jana, alisema pamoja na udhaifu mwingine wa kisheria, kesi hiyo imefunguliwa bila idhini ya bodi ya IPTL.

Wanahisa wengine wa IPTL ni pamoja na Mechmar Corporation (Malaysia) Berhad, ya Malaysian ambayo ndio wenye hisa kubwa za asilimia 70 wakati VIP wanashikilia asilimia 30 pekee, na sasa wana kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusiana na mgogoro baina yao, kesi ambayo Rugemalira anasema ni lazima imalizike kabla ya wanahisa kufungua kesi nyingine.

Novemba 15, 2007, IPTL ilifungua kesi katika mahakama moja ya New York, Marekani wakidai kulipwa Dola za Marekani 27,169,882.67 (Karibu Sh bilioni 30/-) kwa madai kwamba TANESCO imekiuka mkataba baina yao uliosainiwa 1995.

Tayari Serikali inajiandaa kuwasilisha muswada wa kuruhusu watu binafsi kushindana kibiashara na TANESCO, katika hatua nyingine ninayotajwa kulibebesha mzigo shirika hilo linaloelemewa na mzigo wa madeni na gharama zinazotokana na malipo ya ununuzi wa umeme katika makampuni ambayo Serikali iliingia nayo mikataba yenye utata.

Kwa sassa TANESCO ina mzigo wa kulipa gharama ya kukodi mitambo ya Richmond kwa Sh 4.7 bilioni kwa mwezi huku tayari ikiwa inalipa IPTL ya Sh 3.3 bilioni kwa mwezi na Songas Sh. 5.8 bilioni kila mwezi, mikataba yote ikiwa imetokana na majadiliano ama msukumo kutoka serikalini.

Aidha, Serikali imeelezwa kuitoza TANESCO riba kubwa zaidi ya mikopo ambayo Serikali imekopeshwa na mashirika ya kimataifa kwa riba ndogo zaidi.

Mzigo mwingine ni wa Shirika la Umeme la Zanzibar ambalo inaelezwa kwamba linasita kulipa gharama mpya za umeme ambazo tayari watumiaji wa Tanzania Bara wanalipa.

Ofisa mwingine wa Serikali, naye akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, ameliambia RAIA MWEMA kwamba, kwa sasa tayari Serikali imekwisha kukabidhi miundombinu ya TANESCO katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kampuni moja binafsi kabla hata ya muswada wa kuruhusu watu binafsi kuendesha biashara ya umeme.

“Unajua huo muswada unalenga kuzibeba kampuni zilizoingia nchini kuuza umeme kama vile Dowans, Songas, Aggreko na nyinginezo. Pamoja na kuwa watasaidia kupunguza makali ya umeme, kuna athari kubwa pia kwa uchumi na usalama wa nchi kwani hii si biashara ya kufanywa na kila mtu kiholela,” alisema ofisa huyo.

Ukiritimba wa TANESCO unatarajiwa kukoma iwapo Bunge la Jamhuri ya Muungano litapitisha muswada huo wa sheria mpya ya huduma za nishati ya umeme na kisha Rais kutia saini.

Muswada wa sheria hiyo ambao umekwisha kusomwa bungeni kwa mara ya kwanza, unatarajiwa kuondoa ukiritimba kwa TANESCO kama ilivyokuwa kwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Katika muswada huo, moja ya jambo la msingi ni kwamba wazalishaji wa umeme wataweza kuzalisha na kusambaza bila kupitia TANESCO kama ilivyo sasa.

Hata hivyo, tegemeo kubwa kwa wananchi na TANESCO litakuwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ambayo imeelezwa kuwa na wataalamu mahiri katika kusimamia huduma hiyo.

Imeelezwa kwamba pamoja na Serikali kuwa na Mpango wa Kulijengea Shirika hilo uwezo wa kifedha, mpango huo unaweza kuwa kiini macho ikiwa Serikali haitawekeza fedha za kutosha kwa shirika hilo kama ruzuku na kubeba mizigo ya madeni na gharama za mikataba mibovu.

Tayari Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashidi, ametoa taarifa kwa umma kwamba shirika hilo lina hali mbaya kifedha na kwamba linalazimika kupandisha bei kwa asilimia 40 lakini EWURA iliikubalia asilimia 21.7.

Source:Raia Mwema(Jan 09)
 
...nishachoka na hilo shirika linaloitwa Tanesco bora life tuu maana halisaidii chochote na waruhusiwe watu binafsi kuzalisha na kuuza umeme,same story tuu kama TTCL,ATC,RTC,TBL kabla ya kaburu etc hivi kuna ugumu gani wa kuruhusu watu kuuza umeme? mnawapa monopoly hao ambao hata kukusanya bills hawawezi,hope hizo sheria za kikoloni zitakwisha soon
 
...nishachoka na hilo shirika linaloitwa Tanesco bora life tuu maana halisaidii chochote na waruhusiwe watu binafsi kuzalisha na kuuza umeme,same story tuu kama TTCL,ATC,RTC,TBL kabla ya kaburu etc hivi kuna ugumu gani wa kuruhusu watu kuuza umeme? mnawapa monopoly hao ambao hata kukusanya bills hawawezi,hope hizo sheria za kikoloni zitakwisha soon

Sina hakika na unayoyasema; Hivi aliyelifikisha hapa lilipo ni nani? Ni serikali,, sasa unasema bora iwe kama TTCL umesahau na NBC, ilianza kusemwa kwamba haipati faida na ndio wakapewa watu bureeeeeeeeeee. TTCL wimbo ule ule. Sasa Tanesco pamoja na matatizo waliyonayo ni shirika nyeti kwa usalama wetu na ndio maana munaweza hata kupiga kelele za kudai huduma bora. Angalia sasa NBC na TTCL.. Angalia ATC ilivyochezewa na makaburu.

Hakuna ubaya kwa kuruhusu ushindani lakini kuna mambo muhimu ya kuzingatia, lakini pia isiwe sababu ya watu kuchukua bure kama NBC na Kiwira.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom