Vigogo wa CCM hamkani wakijipanga kutosana

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
0
Makala
rajab.jpg


Barazani kwa Ahmed Rajab

Vigogo wa CCM hamkani wakijipanga kutosana…


Ahmed Rajab

Toleo la 239
16 May 2012
VIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanajikaza kisabuni lakini ukiyachambua matamshi yao ya karibuni utaona wazi kwamba wamekwishakuanza kuingiwa na hofu za aina kwa aina.
Hofu yao moja ni ya kudhoofika kwa chama chao. Nyingine na pengine iliyo kubwa ni ya maadui — wa kweli na wa kujidhania.Kile ambacho labda hawakijui ni kwamba maadui wakubwa wa CCM wamo ndani ya CCM yenyewe.
Chama hicho, kilicho kikubwa kuliko vyote vinavyotawala katika eneo zima la Afrika ya Mashariki, hii leo kinakabiliwa na kitisho kikubwa cha kung’olewa kwenye madaraka.
Kila siku zinavyoukaribia uchaguzi mkuu ujao ndipo kitisho hicho kinavyozidi kufukuta ndani ya chama chenyewe.
Hofu nyingine inayowakumba viongozi wa CCM inatokana na ufisadi wa baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho au serikali yake. Inaeleweka kwa nini viongozi hao wazidi kuwa na hofu hiyo. Sababu ni kwamba wanatambua ya kuwa katika enzi hizi za leo za uwazi hawawezi tena kuwafumba macho wananchi au kuwalaghai.
Juu ya kuwa mfumo wa kidemokrasia haujashamiri vilivyo katika jamii, viongozi hao wanajua kuwa hawana nguvu za kisheria za kuzizima kelele na hasira za wananchi. Na sheria pia inaifunga mikono yao wasiweze kutumia mabavu dhidi ya wananchi na kuwakandamiza.
Sababu kubwa inayoifanya serikali ya CCM ikabiliwe na hizo ghadhabu za wananchi ni kushindwa kwake kuwachukulia hatua za haraka na zinazostahiki viongozi kadhaa wa zamani na wa sasa wanaoshtumiwa kwa maasi kadha wa kadha ya ama ufisadi, utumizi mbovu wa madaraka, ubadhirifu wa fedha za umma au uzembe kazini.
Kuna visa mbalimbali vya ufisadi vilivyoibuka rasmi hivi karibuni ingawa vimekuwa midomoni mwa watu kwa muda. Hivyo, visa hivyo si vigeni kwa wananchi na kashfa za ufisadi zimekuwa zikiwaandama viongozi kwa muda mrefu.
Ushahidi umejaa tele wenye kuonyesha kwamba viongozi wamezoea kuyatumia madaraka yao kwa kujinufaisha binafsi kinyume cha sheria. Walio waadilifu miongoni mwao ni wachache. Wengine kwa lugha ya mkato ni wezi, majambazi na malaghai.
Wanatenda maovu wanayoyatenda huku wakijitapa kwamba wao ni wazalendo na ndio walinzi wa maslahi ya taifa. Ukweli wa mambo unaonyesha kwamba kweli wao ni walinzi lakini ni walinzi wenye kulindana wenyewe kwa wenyewe.
Hapo ndipo unapodhihirika udhaifu wa CCM na serikali yake ambayo inaonekana kwamba haina ubavu wa kuweza kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wake wakuu wanaokiuka maadili ya utawala bora.
Kuna jingine lenye kuainisha udhaifu wa CCM ya leo. Nalo ni kukosekana umoja au mshikamano miongoni mwa wakuu wa ngazi za juu wa chama hicho. Si tu kwamba hawana tena umoja lakini pia wamo mbioni wakijaribu kutosana. Hakuna muamala wala muamana baina yao.
Historia inatufunza kwamba kwa kawaida utawala aina hiyo wa mafisadi wasio na umoja huwa haudumu. Tumeyashuhudia hayo, kwa mfano, katika siku za mwisho mwisho za utawala wa chama cha KANU nchini Kenya chini ya uongozi wa Daniel arap Moi.
Moi hakutimuliwa madarakani kwa sababu ya kashfa za ufisadi — ambazo alikuwa nazo nyingi na zikijulikana. Aliangushwa na wale waliohisi wanahatarishwa na uchu wake wa madaraka na ukatili wa serikali yake.
Kama nilivyokwishakugusia uchaguzi ujao utapokuwa unakaribia nchini Tanzania tutaona jinsi mchuano wa kuunyaka uongozi wa CCM utapozidi kupamba moto. Hivi sasa mchuano huo umekwishaanza kuwafanya viongozi wakuu wa chama hicho wazidi kutoaminiana.
Ni dhahiri kwamba mvutano uliopo katika ngazi za juu za uongozi wa CCM ni moja ya sababu zinazomfanya mwenyekiti wa chama hicho ashindwe kuwafukuza kwenye uongozi au hata kuwavua uwanachama wale wanaoitwa ‘wanamtandao.’
Mvutano huohuo pia ni moja ya sababu zinazomfanya asiutumie wadhifa wake wa urais na kuamrisha wapandishwe mahakamani mawaziri na watumishi wakuu wa serikali walioroa ufisadi au wenye utovu wa nidhamu ya utawala bora.
Kusitasita huko kwa Bwana Mkubwa Kabisa kunazidi kukifanya chama chake kijiharibie jina na kudhoofika zaidi.
Hapa tulipo tunaona jinsi watawala wa Tanzania ambao ni vigogo vya CCM wanavyotahayari kwa ufisadi wa baadhi yao na walivyoanza kuonyesha dalili za kuwaogopa wananchi. Sidhani kama siku hizi vigogo hao wa CCM wanapata usingizi sawasawa tangu pale Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alipotoa ripoti yake iliyowahusisha mawaziri kadhaa katika vitendo vya ufisadi na utovu wa nidhamu.
Bila ya shaka hatua iliyochukuliwa ya kuwawajibisha mawaziri na watendaji serikalini pamoja na viongozi wa mashirika ya umma waliobainika kuhusika na ubadhirifu ni hatua ya kupongezwa. Lakini haitoshi. Na imechelewa kuchukuliwa, taakhira ambayo inaeleza mengi kuhusu uadilifu wa chama chenyewe.
Kama kweli serikali ya CCM imekamia kuusafisha mfumo uliopo na kuuzika ufisadi, basi inatakiwa ichukuwe hatua kali zaidi zitakazowafanya wengine wasiweze hata kufikiria kujiingiza katika ufisadi.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, ananukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba CCM hakikutikiswa na kashfa zilizowakumba mawaziri waliohusika. Hayo ni matamshi ya ajabu kabisa na ni wazi kwamba ni ya kujitoa kimasomaso tu. CCM kilipata pigo na kilitikisika. Ndiyo maana kikawatosa waliohusika na kashfa. Kiliwatosa kwa sababu kilitambua kwamba kashfa zilizofichuliwa na CAG pamoja na kamati za Bunge na wabunge ziliwapandisha mori wananchi bila ya kiasi.
Kufichuliwa kwa kashfa hizo kuliwapa fursa Watanzania ya kufuatilia kwa makini na kwa kina malalamiko yaliyotolewa na wabunge wa vyama vyote juu ya ubadhirifu wa mali za umma. Uwazi huo umewawezesha wananchi wawe na hoja za kutosha za kutokwa na imani na serikali ya CCM na kuifanya iwaogope.
Jambo la kustaajabisha — na kuhuzunisha — ni kuuona utawala ambao kwa muda mrefu umekuwa ukitamba na kujigamba kwamba uko pamoja na wananchi uwe leo unawaogopa wananchi haohao.
La kutisha ni kwamba hatujui patazuka nini utaporipuka mzozo mkubwa wa kisiasa ndani ya chama kinachotawala.
Tanzania imebahatika kwamba haikuwahi kukumbwa na mchafuko wa kisiasa kama ile michafuko iliyotokea nchi mbalimbali barani Afrika — kwa mfano, Kenya, Madagascar, Côte d’Ivoire, Guinea-Bissau au Mali.
Juu ya yote hayo CCM sasa i hamkani kwa sababu pamoja na mivutano ya ndani chama hicho pia kinakabiliwa na upinzani ambao hauna tena woga wa kukandamizwa. Huu pia ni upinzani ambao kila uchao unazidi kupata nguvu hasa katika sehemu za mijini na kuwavutia wafuasi wa CCM.
Jambo kubwa linalowafanya wananchi wavutiwe na upinzani na wakipe mgongo CCM ni sera za kiuchumi za serikali yake. Hadi sasa sera hizo hazikuweza kuupunguza umasikini licha ya kuwa tangu mwaka 2000 uchumi wa taifa umekua kwa wastani wa asilimia 6 kwa mwaka. Kwa hakika, umasikini umezidi kuenea hasa katika sehemu za vijijini wanakoishi takriban asilimia 90 ya Watanzania.
Ingawa kilimo ndicho kinachowapatia Watanzania wengi ajira yao, wale wenye kulima, kufuga mifugo na kuvua ndio walio masikini zaidi.
Yote hayo ni matokeo ya sera za kiuchumi za ulibirali mamboleo zinazotegemea soko huru na utandawazi. Ni sera zenye kufuata maamrisho ya ubepari kwani tunapokuwa tunazungumzia uchumi wa soko tunachokizungumza kwa hakika ni mfumo wa uchumi wa kibepari, mfumo ambao kwa sasa unaonyesha bayana udhaifu wake hasa katika baadhi ya nchi za Ulaya.
Nchi kama Tanzania zinashurutishwa na wakubwa wa dunia hii zizifuate sera hizo ili nchi hizo ziweze kubanwa zaidi na makucha ya utandawazi. Ndiyo maana nchi zetu zinakuwa haziwezi kufurukuta zikikabiliwa na matakwa ya nchi kubwa.
Athari mbaya za sera hizo zimewafanya watu wa nchi mbalimbali waandamane kuzipinga serikali zao na kuzisababisha ziondoke madarakani. Hatukuyashuhudia hayo nchini Tunisia na Misri tu bali hata huko Ugiriki na Uhispania.
CCM kishukuru kwamba hadi sasa ghadhabu za wananchi juu ya ukali wa maisha na ufisadi bado hazijawafanya wamiminike mitaani na kuchukuwa hatua mithili ya zile tulizozishuhudia mwaka jana Misri na Tunisia.
Historia inatufunza kwamba uvumilivu wa wananchi daima huwa na kikomo. Hufika wakati wakasema ‘basi yanatosha’. Hapo ndipo ngoma inapoanza.
[h=2]Soma zaidi kuhusu:[/h]CCM

[h=2]Tufuatilie mtandaoni:[/h]
check-big.png
check-big.png
check-big.png
check-big.png
check-big.png
check-big.png

Wasiliana na mwandishiAhmed Rajabahmed@ahmedrajab.com
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom