Vigogo njia panda

Mbonea

JF-Expert Member
Jul 14, 2009
640
20





SIKU chache tu kabla ya kuanza kwa mwaka wa mchakato wa kuelekea kilele cha Uchaguzi Mkuu, baadhi ya wabunge waliopoteza matumaini ya kurejea bungeni wameanza kusitisha harakati hizo huku baadhi wakishindwa kuwatembelea wapiga kura kwa miezi kadhaa sasa, na wengine wakijaribu mbinu mpya kurekebisha mchafuko wa hali ya hewa kwa upande wao, Raia Mwema, imebaini.
Wabunge hao takriban 100 kwa muda sasa baadhi wameanza kupunguza kasi ya mawasiliano kati yao na wapiga kura na wengine wachache kati yao, wamekata kabisa mawasiliano hayo kutokana na kujiridhisha kwao kwamba hawana tena fursa ya kushindana na hatimaye kurejea bungeni.
Taarifa mbadala zinaeleza pia kwamba baadhi ya wabunge wa sasa, ingawa ni wachache, wanaokusudia kuhama kuwania majimbo, baadhi wakielekea vijijini na wengine wa maeneo ya vijijini kujielekeza maeneo ya mijini.
Hayo yote yakiendelea, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umekwisha kuanza kazi ya kusimika wagombea wake wa ubunge karibu katika kila jimbo la uchaguzi, kigezo kikubwa kikiwa ni kete ya ujana na baadhi ya maeneo kigezo kikiwa ni elimu.
Katika hali inayoshitua zaidi, vijana hao wamekuwa wakipandikiza wagombea ubunge vijana hata katika majimbo ambayo wabunge wake wa sasa ni vijana na wengine wakiwa na ukaribu zaidi na kambi za vijana hao.
Taarifa za uhakika zilizothibitishwa na wahusika wa mkakati huo zinaeleza kuwa viongozi wa UVCCM ambao wengi wao wamesoma katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) wameanza kuwapachika wasomi wenzao na baadhi wakiwa rafiki zao waliosoma pamoja chuoni hapo.
Tayari fungu la fedha limechangwa na mtandao huo wa vijana kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kufanikisha mkakati huo na kwamba, sehemu ya timu ya vijana hao imekuwa ikipita katika mikoa kadhaa nchini lakini baada ya kutanguliza timu nyingine inayoshirikisha wenyeji wa majimbo husika ambao wanasaidia kufanya kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni ‘ukachero’ kupima upepo.
Ingawa kundi hilo la vijana linajizatiti kuingia bungeni kama kundi baada ya kushinda ubunge majimboni, inatarajiwa kuwa hatua yao hiyo itakabaliwa na upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya wakongwe wa sasa, ikiwamo ndani ya CCM wakati wa kupitisha majina ya wana-kundi hilo, ambalo linaelezwa kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela ni kati ya wanaokwenda kuwania ubunge jimbo mojawapo mkoani Shinyanga, ama Kishapu au Shinyanga Mjini.
Tayari kumekuwapo na malalamiko kuwa UVCCM imeanza kutumiwa na vijana kama kijiwe cha kuandaa mikakati yao kama kundi lenye ajenda zake ambazo zinahofiwa wakati ukifika zitaleta mpasuko CCM.
Inaelezwa kuwa upo uwezekano mkubwa wa wabunge takriban 60 wenye hali mbaya nafasi zao kunyakuliwa na wana-mtandao huo wa vijana, japokuwa kati ya majimbo hayo wengine ni vijana na baadhi ni mawaziri na naibu mawaziri wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Majimbo ya wabunge hao wanaokaribia 100 yapo katika takriban mikoa yote na dalili za wazi zinathibitisha kuwa katika kila mkoa, si wabunge wote watarejea bungeni baada ya Uchaguzi Mkuu. Mikoa inayotajwa kupoteza wabunge kwenye timu ya sasa ni pamoja na Dar es Salaam ambako habari zinasema walau wataingia wabunge wapya wasiopungua watatu kuchukua nafasi za waliopo ambao kisiasa wako mahututi wakiwakilisha majimbo ya Kawe aliko Rita Mlaki, Ubungo aliko Charles Keenja, Kigamboni (kwa Mwinchumu Msomi) na Temeke kwa Abbas Mtemvu.
Mkoa wa Morogoro pia unatarajiwa kuingiza wabunge wapya wasiopungua wanne, huku hali halisi ikibainisha kuwa hata ambao watafanikiwa kurejea bungeni, watakuwa wamepitia kwenye mchuano mkali kwelikweli, na hao ni pamoja na wabunge vigogo kama Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo (Kilosa) na waziri wa zamani, Dk. Juma Ngasongwa (Ulanga Magharibi).
Majimbo mengine mkoani humo yanayoonyesha kuibuka kwa wagombea wapya ni Mvomero aliko Suleiman Saddiq anayezongwazongwa na Amos Makalla, mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mweka Hazina wa chama hicho; Morogoro Kusini Mashariki aliko Sameer Lotto; Morogoro Mjini kwa Omar Mzeru; Morogoro Kusini kwa Hamza Mwenegoha na Mikumi ambako tangu mwaka 2005 liko mikononi mwa Clemence Lyamba na Kilombero kwa Castor Ligallama.
Taarifa zinasema hali ni tete mkoani Iringa ambako wabunge wanne wamo hatarini kutorejea bungeni ingawa pia ni wazi kuwa wabunge kama Joseph Mungai walikwisha kuonyesha kwamba hawatagombea.
Majina yanayotajwa kupingwa mkoani Iringa ni ya Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Mahamudu Msolla (Kilolo); mbunge wa siku nyingi Jackson Makwetta (Njombe Kaskazini) ambaye jimbo lake linatajwa kuwa litagawanywa ili kutoa mbunge mmoja mpya na Monica Mbega, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Mbunge wa Iringa Mjini.
Mkoani Ruvuma wabunge wasiopungua wanne wana wakati mgumu kutokana na sababu mbalimbali lakini zinazotajwa sana zikiwa ni kutokuwa karibu na wapiga kura na kushindwa kutimiza ahadi za mwaka 2005. Lakini pia zinatajwa sababu za kwamba wanaowinda nafasi hizo wana sifa zaidi ya waliopo sasa.
Wanaosukwa sukwa ni pamoja na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi (Songea Mjini), John Komba (Mbinga Magharibi), Vita Kawawa (Namtumbo) na Gaudence Kayombo (Mbinga Mashariki).
Mkoani Mbeya hali ni tete zaidi kutokana na wabunge wa sasa kujiimarisha zaidi kwa wapiga kura wao.
“Kinachowafanya wabunge wengi wa Mbeya kuonekana kuweza kurudi bungeni ni vuguvugu kubwa la kisiasa mkoani humo linalowafanya muda wote wabunge kulazimika kuwa na mawasiliano na wapiga kura wao,” anasema kiongozi mwandamizi wa CCM mkoani Mbeya aliyezungumza na Raia Mwema kwa sharti la kutoandikwa gazetini.
Lakini pamoja na hali ya mambo kuwa hivyo, inaelezwa kuwa wabunge wawili bado hali zao si nzuri, hao ni Mchungaji Luckson Mwanjale (Mbeya Vijijini) na Victor Mwambalaswa wa Lupa.
Lakini wabunge ambao hatima yao itategemea hali ya kisiasa ndani ya CCM ni pamoja na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye taarifa zinaonyesha kwamba akiteleza kidogo, hataibuka kutokana na sababu kwamba kuna mikakati mizito ya kuhakikisha kwamba harejei bungeni 2010.
Mkoani Rukwa kama ilivyo maeneo mengine, wabunge watatu wanaweza wasirejee. Hawa ni waliopata kuwa na majina makubwa bungeni, baadhi wakiwa wamewahi kushika nafasi za dola kama viongozi wa kitaifa. Hao ni Chrisant Mzindakaya (Kwela), Ponsiano Nyami (Nkasi) na Paul Kimiti wa Sumbawanga Mjini.
Kutoka mkoani Pwani taarifa za kiuchunguzi zinabainisha kuwa wabunge wengi hawako salama, na hususan wabunge wanne. Naibu Waziri wa Nishati na Madini Adam Malima (Mkuranga), Athumani Janguo (Kisarawe), Abdul Marombwa (Kibiti) na Profesa Idris Ali Mtulia wa Rufiji hali zao si nzuri kama zilivyo mbaya za Mohamed Abdulaziz (Lindi Mjini), Mudhihir Mohamed Mudhihir (Mchinga) na Dk. Samson Mpanda wa Kilwa mkoani Lindi.
Taarifa zinaonyesha kwamba huenda Lindi ikaongoza kwa kubadili wabunge kutokana na sababu kwamba wanatajwa watu watano wapya kuibuka mkoani humo ambako Jimbo la Ruangwa li wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge, Sigifrid Ng’itu.
Mkoani Mtwara majimbo ya Masasi (Reynard Mrope), Lulindi (Anna Abdallah) na Mtwara Vijijini aliko Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi) Hawa Ghasia nako kunafukuta na taarifa zinasema huenda wakapatikana wabunge wapya watatu.
Mkoani Tanga hali si nzuri sana kwa waziri wa zamani, Bakari Mwapachu (Tanga Mjini), Balozi Abdi Mshangama (Lushoto) na Mohamed Rished wa Pangani na katika Mkoa wa Kilimanjaro, wenye uhakika wa kutorudi wameanza kujitambua na habari za uhakika kutoka kwa wazoefu wa siasa za mkoa huo zinaeleza kuwa angalau wabunge wapya watatu watachomoza katika Bunge lijalo.
Walioko hatarini ni pamoja na Aloyce Kimaro (Vunjo) ambako inaelezwa kwamba hali yake mbaya inachangiwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja na siasa za kuendekeza ukoo na sasa unajitokeza tena ukoo wa Mrema (Augustine, Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party na John Mrema wa CHADEMA) ambao umeanza kung’aa zaidi kisiasa pamoja na Kimaro mwenyewe kupigwa vita kutokana na kuibuka kwa makundi ya kisiasa ndani ya CCM.
Mbunge Fuya Kimbita wa Hai naye anaelemewa na nguvu za kisiasa za Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ambaye dhahiri sasa anataka kurudi bungeni baada ya kugundua kwamba kuwania urais ni maji marefu.

Mkoani Arusha ambako kumeanza kuwa na uhasama wa kisiasa kama ilivyo mkoani Mbeya, chanzo kikiwa ni siasa za makundi, inaelezwa kuwa kuna kazi nzito kupenya sura mpya za wabunge mwakani, na kwamba hali hiyo inaweza kujitokeza tu ikiwa baadhi ya majimbo yatamegwa.
Hata hivyo, taarifa huru zinaeleza kuwa vitendo vya hujuma kati ya makundi hasimu vinaweza kuisaidia Kambi ya Upinzani kuingiza sura mpya bungeni mwakani, huku kukiwa na hali ya sintofahamu kuhusu idadi ya wabunge wa sasa wanaoweza kuanguka mwakani.
Wabunge wapya wanaweza kuibukia mkoani Manyara na kuingia katika Bunge lijalo. Changamoto zinazohusiana na masuala ya ufugaji ni kete inayotajwa kuweza kuwaangusha baadhi ya wabunge wa sasa. Wabunge walioanza kuonyesha dalili za kung’oka ni pamoja na Waziri wa Biashara na Viwanda, Dk. Mary Nagu (Hanang), Mbunge wa Babati Mjini, Omar Kwaangw’ na Mbunge wa Kiteto, Benedict Ole-Nangoro, ambao hali ya kisiasa katika maeneo yao imebadilika kwa kasi kutokana na matukio mbalimbali ikiwamo migogoro ya ardhi.
Kutoka Singida, mkoa unaotajwa kuwa ngome ya CCM ukitajwa kuongoza kwa idadi ya kura kitaifa ambazo alipigiwa Rais Jakaya Kikwete, baadhi ya wabunge wamepata upinzani mkali wakiwamo Juma Kilimbah (Iramba Magharibi), Mohamed Missanga (Singida Kusini) na John Lwanji wa Manyoni Magharibi.
Mkoani Mwanza baadhi ya viongozi wa kitaifa wapo kwenye ukanda wa hatari ikitarajiwa sura mpya nne kuchomoza mwakani katika Bunge. Wanaotajwa kuwa katika hali mbaya ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani Lawrence Masha (Nyamagana) na Samuel Chitalilo wa Buchosa.

Mkoani Shinyanga, sura mpya zisizopungua nne zinatarajiwa kuchomoza lakini pia wabunge wengine waliosalia wako katika wakati mgumu kujitetea na kurudi bungeni na hali halisi inaonyesha kuwa pia wanaweza kupoteza. Mbunge wa Kishapu aliyejitokeza katika kundi la wapambanaji ufisadi, Fred Mpendazoe, amekaliwa kooni na wagombea wapya huku Mbunge wa Shinyanga Mjini, Dk. Charles Mlingwa akionekana kupwaya na kutoa nafasi kwa mgombea mpya kupita.

Mkoa wa Tabora ambao pia unatajwa kuwa na harakati za siasa za makundi, kundi moja likijumuisha Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya na Mbunge wa Igunga Rostam Aziz, unatarajiwa kuibua wabunge wapya watatu, ingawa baadhi wanaweza kuwa wa Viti Maalumu waliodhamiria kwenda majimboni. Mbunge wa Tabora Mjini Siraju Kaboyonga amekaliwa kooni na wagombea wapya wakati Mbunge wa Bukene, Teddy Kasela Bantu anapambana kurejea tena bungeni kutokana na kupata upinzani mkali kutoka kwa wagombea wapya huku Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, akiwa bado hajathibitisha kutogombea kama ilivyotajwa awali. Kugombea au kutogombea kwa Rostam kutaibua changamoto katika siasa za mkoa wa Tabora.

Kigoma ambako kunatajwa kuwa na vuguvugu la mageuzi kama ilivyo kwa mikoa ya Kilimanjaro na Mara, wabunge wote wa mkoa huo wanatajwa kuwa kurudi kwao bungeni hakutabiriki kutokana na sababu mbalimbali, kuanzia utendaji wao na hata kushuka hadhi yao ya kisiasa mbele ya wapiga kura. Hatima ya wabunge Peter Serukamba (Kigoma Mjini), Manju Msambya (Kigoma Kusini) na Daniel Nsanzugwanko (Kasulu Mashariki) iko mikononi mwa wana CCM wa maeneo hayo lakini wote wanaonyesha kukabiliwa na upinzani mkali ndani na nje ya chama hicho.
Hatima ya Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), inategemea zaidi mambo kadhaa ikiwa ni pamoja uamuzi wake wa kugombea ama kutogombea huku hali ya sintofahamu kati yake na wenzake ndani ya CHADEMA ikiwa changamoto kubwa kwa mbunge huyo kurejea.
Mkoani Mara, wabunge wapya wanne wanatarajiwa kuibuka, lakini waliomo katika hatihati ya kutokuvuka ni Charles Kajege wa Mwibara na Charles Mwera wa Tarime ambaye taarifa zinasema anaweza kuangushwa na mgombea mwingine kutoka chama chake cha CHADEMA.

Mkoa wa Kagera hali ya mabadiliko inatajwa kutegemea aina ya wagombea wapya na makundi yanayowaunga mkono, hata hivyo inaelezwa sura mpya mbili zinaweza kuibuka katika Bunge lijalo japo si kwa uhakika wa asilimia 100. Mkoani Dodoma, wabunge wapya watatu wanatarajiwa kuibuka baada ya kuwabwaga wabunge wa sasa, ikiwa ni pamoja na Mbunge wa Dodoma Mjini Ephraim Madeje ambaye amekaririwa akisema hatagombea. Wengine wanaotajwa kuwa katika hali ngumu ni William Kusila (Bahi), Job Ndugai (Kongwa) na George Simbachawene (Kibakwe).

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baadhi ya sura hizo mpya zitahusisha vyama vya siasa vya upinzani, ikiwa ni pamoja na kung’oana wenyewe kwa wenyewe kwenye kura za maoni au ikibidi kati ya chama kimoja na kingine.
Hata hivyo, nguvu ya CCM bado inaelezwa kuwa kubwa na chama hicho tawala kinatarajiwa kuingiza sura mpya nyingi zaidi kutoka upande wake ikilinganishwa na vyama vya siasa vya upinzani ikiwa hali ya kisiasa haitabadilika.
hs3.gif



Source: http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=1923
 
Dua zetu wakati wote ni kwamba: Tuongeze wapinzani bungeni kama kweli tunaipenda nchi yetu, na ikumbukwe pia kwamba wapinzani ni watanzania pia wapewe nafasi (fursa sawa kwa wote). Kwa kumbukumbu mambo ya vyama vingi kenya yalianza baada ya sisi kuanza lakini wame advance katika siasa kuliko sisi what's wrong with us?

Tuache upambe kwenye mambo ya kitaifa hawa jamaa wameshaonyesha hawana jipya, tuwape nafasi kubwa wapinzani na nchi itaongozwa vizuri zaidi kama CCM watakuwa wapinzani kwani wanaujua uchafu wote hivyo watakuwa watchdogs wazuri kuliko hata ilivyo kwa wapinzani hivi sasa.

Nawasilisha kwa wapiga kura!!
 
Back
Top Bottom