Vigogo kupigwa panga mikopo ya elimu ya juu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
266
WAZIRI wa Elimu na Mfunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kubadilisha mfumo wa utoaji mikopo kwa sababu mfumo uliopo unawanufaisha watoto wa vigogo na matajiri.
Waziri Kawambwa alitoa agizo hilo jana wakati tayari Rais Jakaya Kikwete ameeleza nia yake ya kuunda tume maalumu kwa ajili ya kuchungunza mfumo mzima wa utoaji mikopo hiyo.

Rais Kikwete alisema serikali yake imeamua kufanya hivyo ili kuhakikisha kuwa tatizo la mikopo linalowakabili wanafunzi wa vyuo vikuu nchini linakwisha.

Alisema kamati hiyo itakuwa imeundwa ifikapo mwezi Januari mwakani.

Kwa muda mrefu yamekuwepo malalamiko kutoka kwa wanafunzi walalahoi kwamba hawatendiwi haki na bodi ya mikopo, kwa vile watoto wa vigogo wanapewa mikopo ya asilimia 100 wakati wao wanapunjwa licha ya wazazi na walezi wao kutokuwa na uwezo.

Akizungumza na watendaji na wajumbe wa bodi hiyo jijini Dar es Salaam jana, Waziri Kawambwa alisema wanafunzi wengi wanaopata mikopo ya asilimia 100, ni watoto wa vigogo na wasomi, wakiwamo maprofesa na madaktari.

“Ili uweze kupata mkopo kwa asilimia 100, lazima uwe na sifa ya kupata alama ya ‘Division One au Two’ (daraja la kwanza au la pili). Ukweli ni kuwa wenye mazingira ya kupata alama hizo ni watoto wetu (mawaziri, maprofesa, madakatari)na si wa mfugaji, mkulima na hata mlalahoi ,’’ alisema Dk Kawambwa.

Kufuatia hali hiyo, Kawambwa pia aliitaka bodi hiyo kukiangalia upya kigezo hicho na kuagiza kuwa sifa hiyo isiwe kigezo pekee katika kutoa mikopo kwa asilimia 100.

Kawambwa alikwenda mbali na kutaka sheria namba 11 ya mwaka 2004 iliyounda bodi hiyo pamoja na muundo wa utendaji wake ubadilishwe ili uweze kukidhi mahitaji.

Awali Mkurugenzi mtendaji wa bodi hiyo George Nyatega aliitaka serikali kukubali ombi lao la fedha za mikopo zinazotolewa zirejeshwe pamoja na riba.

“Kulingana na hali halisi ya mazingira ya elimu yalivyo hususani karo za shule kubadilika, mabadiliko ya thamani ya fedha, sasa tunataka urejesheshwaji wa fedha za mikopo uwe na riba,’’ alisema Nyatega.

Akijibu ombi hilo, Waziri Kawambwa alisema Serikali italifanyia kazi.

Akizungumza na wafanyakazi wa wizara yake katika siku yake ya kuanza rasmi kazi, Dk Kawambwa aliahidi kuboresha maslahi ya walimu na wastaafu wa vyuo vya elimu ya juu vya umma na kwamba atafanya kazi kimyakimya kama 'mchwa' na kuwataka wananchi kupima utendaji wake kwa matokeo ya kazi kwa sababu anaamini kuwa kazi inaweza kufanyika vizuri na mafanikio makubwa bila kutumia maneno makali.

Alitaja vipaumbele vinne atakavyofanyia kazi miaka mitano ijayo ambavyo baada ya uongozi wake katika wizara hiyo anataka wananchi na vizazi vijavyo wamkumbuke, ikikwamo kumaliza matatizo ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige jana alieleza kukerwa na ufisadi uliofanyika katika Wizara ya Maliasili na Utalii na kusababishia Serikali hasara ya Sh606 bilioni na kusema kuwa ataendesha uchunguzi maalumu kubaini wahusika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Maige alisema hasara hiyo imepatikana kupitia Idara ya Misitu ambako watendaji wameshindwa kukusanya kodi ya mkaa.
Kwa mujibu wa Maige, Idara ya Misitu ilitakiwa kukusanya kodi ya mkaa inayofikia Sh672bilioni baada ya kutoza ushuru wa Sh2000 kwa gunia moja la mkaa.
“Inashangaza, licha ya kiwango hicho cha ushuru, idara hiyo imekusanya Sh66bilioni tu mwaka mzima," alisema.

Maige alisema kila mwaka misitu imekuwa ikizalisha magunia 39 milioni ambayo nusu yake, inatumika katika mikoa wa Dar es Salaam na Pwani.

“Inaonyesha wazi kuwa kuna vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na watu wachache, kutokana na maofisa wa idara hiyo kushindwa kukusanya kodi. Nimepanga kuwashughulikia watendaji wote ambao wameshindwa kuwajibika katika maeneo yao ya kazi,” alisema Maige.

Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo ataendelea na uchunguzi ili kuhakikisha kuwa watendaji hao wanabainika na kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kwafikisha katika malaka husika ili waweze kuwajibishwa.
Alisema kutokana na vitendo vya ufisadi, watendaji hao wameshindwa kuwasilisha kiasi hicho cha fedha na kusababisha hasara kuongezeka.
Alibainisha kuwa kutokana na hali hiyo wizara hiyo imeshindwa kufanya kazi ya ukusanyaji wa kodi katika idara hiyo na kusababisha hasara ya zaidi ya asilimia 90.

Alisema, watendaji hao wamekuwa wakifanya safari za mara kwa mara nchi za nje ambazo kwa namna moja au nyingine hazina mafanikio yoyote lakini wanashindwa kwenda porini kufanya ukaguzi na kuzungumza na watendaji.
Pamoja na hayo Maige alisema wizara yake inatarajia kununua helikopta kwa ajili ya kufanya ukaguzi katika hifadhi za taifa ili waweze kuwakamata majangili ambao kwa muda mrefu wamekua wakihujumu Serikali kwa kiasi.
Alisema hivi sasa wako kwenye mchakato wa mwisho wa ununuzi wa helikopta hiyo ambayo wanaamini kuwa ikiwa itaanza kazi itawasaidia kubaini majangili hao na kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria.

Nyae Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ameitaka kampuni ya uzalishaji umeme ya Songas kukamilisha ukarabati wa mtambo wa megawati 35 ulioharibika, ifikapo Ijumaa wiki hii ili kupunguza tatizo la mgao wa umeme nchini.

Ngeleja ambaye jana alifanya ziara katika mitambo hiyo ikiwa ni pamoja na Tanesco na IPTL, aliitaka kampuni ya Songas kufanya hivyo kwa kuwa mtambo huo sasa umeshafanya kazi kwa saa 50,000 na hivyo kuhitaji marekebisho.

"Inawezekana mkakamilisha hilo ifikapo Ijumaa, fanyeni kazi usiku na mchana kama mlivyosema ili kuhakikisha hilo linafanikiwa,"alisema Ngeleja.

Mbali na hilo Waziri Ngeleja aliwajia juu watendaji wa Tanesco kuhusu matatizo ya Luku ambayo hayaishi na kumwagiza Mkuu wa Kitengo cha Luku kulimaliza tatizo hilo ndani ya mwezi mmoja.

"Nataka tatizo la Luku liishe ndani ya mwezi huu na kama mkurugenzi hawezi kusimamia hilo atafutwe mkurugenzi mwingine asimamie," alisema Ngeleja.

Alisema kuwa wakati anaapishwa alitoa ahadi kuwa tatizo la umeme lazima liishe hivyo atasimamia hilo.

"Tutamaliza mgawo wa umeme nchini kama nivyosema wakati naapishwa, hizi si mbwembwe," alisema Ngeleja.

Akizungumzia mustakabali mzima wa umeme nchini, Ngeleja alisema kuwa baadhi ya mitambo iliyoharibika kama wa Kipawa jijini Dar es Salaam inafanyiwa ukarabati ili kuhakikisha mgao unakwisha mapema.

Alisema hali ilivyo hivi sasa kwa IPTL ni nzuri baada ya mafuta kuendelea kupatikana, na hivi sasa utatoa megawati 70 kwa gridi ya taifa.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom