Vigogo kufikishwa mahakamani: Tuna sababu kufurahia? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vigogo kufikishwa mahakamani: Tuna sababu kufurahia?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Dec 4, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Dec 4, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,691
  Likes Received: 82,602
  Trophy Points: 280
  Tuna sababu kufurahia?

  Lula wa Ndali-Mwananzela Disemba 3, 2008
  Raia Mwema~Muungwana na Vitendo

  NINA uhakika wengi wanafurahia kuona "vigogo" wakifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashitaka mbalimbali. Nina uhakika baadhi yetu tumeanza "kuwa na imani" na Serikali na wengine tunamuona Rais Jakaya Kikwete sasa anacheza kama Pele, na wengine tunakenua meno tukiamini kuwa sasa vita dhidi ya ufisadi imepamba moto.

  Si lengo langu kuharibu furaha yenu! Wale wanaofurahia waendelee kufurahia kwani Serikali iliahidi kuwa itafanya kitu "kitakachowafurahisha wananchi". Mimi sina furaha.

  Sina furaha kwa sababu hatukutakiwa kabisa tufike hapa tulipofika leo. Haya tunayoyashuhudia leo lingekuwa jambo moja au mtu mmoja hivi kweli tungekuwa na sababu ya kufurahia lakini tunapokuwa na makumi ya watu tena wazito serikalini na wenye vyeo vyajuu wanapohusishwa na vitendo hivi vya kifisadi ni lazima tujisikie huzuni!

  Si huzuni tu bali pia hasira kwamba tumevumilia kwa miongo kadhaa ubovu, kuulinda na kuutetea na sasa hatuna jinsi isipokuwa kuchukua hatua! Tumefika hapa na kinaudhi kwamba tumefika hapa.

  Sina furaha kwa sababu wizi na mambo tunayoyazungumzia si wizi wa kuku au mbuzi. Ni wizi wa mabilioni ya shilingi za wananchi wa Tanzania. Fedha za walipa kodi ambao wanahenyeka kila kukicha kuzalisha mali kwa njia na mifumo ya kizamani ambayo inashindana na teknolojia mpya. Watu ambao wanahangaika kila asubuhi kwenda kazini, kujitafutia mlo wa kila siku na maisha ya wao na familia zao. Fedha zao zinapokombwa kama vile kutoka kwenye chungu la nyama na inachukua miaka kwa watu kuanza kufikishwa mahakamani wakati wizi ulijulikana muda mrefu hatuna sababu ya kufurahia!

  Sina furaha kwa sababu fedha zilizoibwa kwa kiasi kikubwa hazikuibwa kutoka katika uvungu wa kitanda cha "Bw. Joni" au kuibuliwa toka kwenye mtungi wa Mama Ntilie. Fedha hizi kwa mabilioni yake zimechotwa toka Benki Kuu; kutoka taasisi ambayo ndiyo moyo wa uchumi wa nchi yetu. Huo uwezekano tu kuwa kuna watu wanatuhumiwa kufanya Benki Kuu kuwa benki yao ya binafsi ambako wameweza kuchota fedha kama za wajomba zao unatisha!

  Tunafurahia kwamba watu wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma hizi tu!? Hawa watu wangejazwa mashtaka zaidi ya 100 kila mmoja lakini haya ya "kula njama, kughushi, wizi na kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu" ni kama kumsingizia mtoto kuwa kalamba sukari toka kabatini! Ndiyo hayo mnafurahia?

  Sina furaha kwa sababu kuna baadhi ya hatua zilipendekezwa miaka miwili na ushahidi wote ambao leo wameuangalia ulikuwapo toka wakati huo. Kule Benki Kuu ilionyeshwa mapema kabisa nani awajibishwe na nini kifanyike, lakini hakikufanyika hicho chote kwa muda wote huu na leo miaka miwili baadaye ndipo tunaamua kuchukua hatua, tunatakiwa tushangilie?

  Leo tunatakiwa kufurahia "hatua" hizi. Kuna watu wanatuimbia nyimbo ati "JK afanya kweli" na ya kuwa "Hakuna wa kusalimika". Tunatakiwa tuanze kuruka ruka kwa furaha kuona kina Jeetu na Lukaza wamesimama kizimbani. Watawala wetu wanatarajia tuchekelee kwa furaha kuwa hatimaye "mafisadi wamefikishwa mahakamani". Bahati mbaya sana kuna watu waliokubali mawazo hayo na sasa wanachekelea kuona watuhumiwa ufisadi wanafikishwa mahakamani. Binafsi bado sijaanza kufurahi.

  Kweli sisi tuna akili timamu kufurahia kuona kina Mramba wamefikishwa mahakamani? Hivi Rais Kikwete, Mramba, Yona si wote walikuwa mawaziri katika baraza moja la mawaziri wakati wa Mkapa? Baada ya Yona kuendelea na biashara zake na Rais Mkapa baada ya kumaliza muda wake, Rais Kikwete si aliingia madarakani? Si yeye ndiye aliyemteua Basil Mramba na kumpa Uwaziri? Ina maana wakati anampa uwaziri alikuwa hajui masuala hayo ya kodi?

  Si Rais Kikwete huyu huyu aliyemrudisha Andrew Chenge kwenye Baraza lake licha ya wapiga kelele kama mimi kupaza sauti zao kuwa Chenge anatuhumiwa ufisadi? Rais Kikwete huyu huyu si ndiye amewaacha wengine wastaafu kwa kwa heshima zote na mafao yao yote licha ya wao kuhusika na makampuni ya kifisadi ambayo yanajulikana kwa karibu miaka minne sasa? Hivi tufurahie kuwa "wamestaafu" na kumpongeza Rais kwa kufanya "mabadiliko ya makatibu wakuu"?

  Wapo kina Idi Simba na Juma Ngasongwa walipata kukumbwa na kimbembe cha aina ya leo na hata kusababisha wajiuzulu. Ngasongwa alitajwa kwenye ripoti ya Warioba (akiwa waziri wa utalii na maliasili) na akajiuzulu. Pamoja na hayo hawa wawili hawakufikishwa mahakamani na baadaye Ngasongwa akarudishwa kwenye Baraza la Mawaziri na Mkapa na baadaye Rais Kikwete mwenyewe? Kweli tufurahie tu kwa vile watu wametajwa kuwa ni mafisadi?

  Kama mtu kuchukua maamuzi yenye kulisababishia Taifa hasara ndicho kigezo cha kuwafikisha watu mahakamani hatuna budi kuhoji vipi lile la Buzwagi? Vipi kuhusu uuzwaji wa nyumba za serikali? Vipi mikataba yote mibovu iliyoingiwa? Kuna vitu vya kufurahia ndugu zangu, na vitu hivyo bado havijatokea.

  Tutafurahia pale wamiliki hasa wa kampuni za Meremeta na Kagoda watakapotajwa hadharani. Kati ya makampuni hayo mawili fedha za Watanzania karibu bilioni 200 na ushee zimenywewa hivi hivi utadhani kwa kata na hadi sasa watu bado wanarembuliana macho kuona nani atamfunga paka kengele. Tutatabasamu kidogo endapo tutasikia uchunguzi umeanzishwa mara moja dhidi ya wote waliohusika na kampuni hizo, hata kama nafasi zao zilikuwa nyeti. Wachunguzwe pia kwa uhusika wao katika kampuni kama Tangold na Deep Green Finance. Tena basi uchunguzi wa hawa kutokana na nafasi zao itakuwa vizuri uendeshwe na taasisi ya nje na hapa tunaweza kuwaomba watu wenye utaalamu wa kesi za namna hii na ambazo zinagusa maeneo nyeti kweli (na watu wanaweza kujifunza). Natoa wito tuwaombe aidha Scotland Yard au Shirika la Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Kilaghai (Serious Fraud Office) la Uingereza. Siri ya wizi wa Benki Kuu ifumuliwe na wahusika wote wajulikane na wapandishwe kizimbani.

  Lakini hilo halitoshi. Ili wananchi wafurahi kweli tunatarajia katika kesi zilizopo sasa mashitaka hayo yaangaliwe tena ili mashtaka ya ziada ambayo hayajaongezwa yaongezwe. Lengo ni kuhakikisha kuwa watuhumiwa wetu hawapati mwanya mwepesi wa kutokea. Hapa nazungumzia mashtaka ya kuhujumu uchumi, usafirishaji wa fedha haramu, kuiibia serikali, n.k Watu wanapochezea benki kuu, na kusababisha mabilioni ya fedha kuchotwa, hawashtakiwi kwa wizi tu bali kwa kuuhujumu uchumi wetu!

  Lakini kubwa ambalo wananchi tunatakiwa kufurahia na tujiandae kufurahia si watu kufikishwa mahakamani. Haitoshi kujua wamiliki wa Kagoda na Meremeta ni nani? Haitoshi kujua nani alifanya nini, lini na wapi. Kinachohitajika ni ushahidi wa vitendo vya kihalifu ambao unaweza kusimama mahakamani na kusababisha wakutwe na hatia. Katika hili ni lazima tuhakikishe kuwa ushahidi uliopo unapatikana na kutunzwa vizuri.

  Leo hii tunaambia baadhi ya nyaraka muhimu za Kagoda na Meremeta zimetoweka, lakini watumishi wa mamlaka husika wameendelea kuwa wale wale na wengine kuitwa kuwa mashahidi. Hawa waliozembea kiasi cha nyaraka halisi (original copies) kutoweka iweje leo wao waendelee kuzikalia ofisi hizo.

  Tunachotakiwa kufurahia si mchakato tu! Tusifurahie kuona watu wameingizwa kwenye karandinga na kukalia mabenchi ya mahakama. Tutakuwa watoto wa kiakili na watu tusiokomaa kifikra kama tutashangilia na kufurahia kuona watuhumiwa wengine wanatajwa kufikishwa mahakamani (kama inavyotarajiwa.) wakati wowote.

  Je, inawezekana kinachofanyika sasa ni jaribio la mchana kweupe la kuwasafisha watu hawa wote kwa kutumia mahakama? Hebu fikiria kwa sekunde chache; kesi hizi zote zinaenda mahakamani, ushahidi unatolewa, mashahidi wanaitwa, na mawakili wa serikali ambao kwa kila kipimo wana kazi ngumu kulinganisha na mawakili wa binafsi, wanaelemewa na majopo ya utetezi ambayo yanajua kesi hizi hazina msingi. Mwisho mahakama zote zinawakuta wahusika wote hawana makosa makubwa isipokuwa mawili matatu ambayo wanatakiwa kulipa faini na wale wengine kuachiliwa kabisa. Utasemaje?

  Ninachosema ni kuwa hadi hivi sasa kesi hizi hazikuandaliwa vizuri, ushahidi umesimamiwa vibaya, na siasa nyingi imeingizwa ndani yake. Matokeo kesi ni dhaifu mno na sitoshangaa (yakariri maneno yangu) watu ambao watajikuta wanabebeshwa mzigo mkubwa wa haya yote ni watumishi wa Benki Kuu. Kwa mbinu za kiufundi n.k kesi hizi msijekushangaa zikapanguliwa na watuhumiwa wote kuachiliwa huru na wakaamua kushtaki serikali na kulipwa fidia ya mabilioni!

  Siku ya kufurahi kweli ni pale ambapo baada ya haya yote na kesi hizi zote kufanyika Mahakama ya Rufaa ikathibitisha hukumu dhidi yao, hukumu ya kuwaona wana hatia au hata nyongeza ya adhabu. Pasipo watuhumiwa kukutwa na hatia, pasipo kuwa na kesi nzuri dhidi yao, pasipo ushahidi wa uhakika na mchakato utakaohakikisha haki zao kama raia zinalindwa na hatimaye kuhakikisha kuwa mahakama inaonyesha kuwa wanahusika na tuhuma dhidi yao, basi hatuna sababu ya kufurahia.

  Kama wananchi tunaweza kutabasamu kidogo kuona mchakato huu unaanza. Lakini shangwe, vigelegele, na furaha yetu tuizuie hadi siku ile tukisikia watuhumiwa wa wizi wa mali zetu na hazina za Taifa letu WOTE wametiwa mbaroni, kushtakiwa, kukutwa na hatia na kutupwa jela miaka mingi na kazi ngumu na ufunguo kutupwa bahari ya Hindi.

  Nje ya hapo, hatuna sababu ya kushangilia kwani kama ni maandalizi ya kilimo kilichofanyika ni kukata visiki tu na kuondoa magogo. Kazi iliyopo kuona kama hiyo ardhi kweli italimika na kama mazao yatakua. Tukianza kupanga bei na kufurahia mauzo ya mazao ambayo hatuna, tutakuwa ni sawasawa na watu wanaoshangilia ndoto na wakiamka hakuna kitu, isipokuwa hisia ya raha tu! Mnaofurahia kufikishwa watuhumiwa mahakamani endeleeni, mimi nasubiri hukumu zao ndipo nitaanza kurukaruka kama ndama!

  Niandikie: lulawanzela@yahoo.co.uk
   
 2. Waberoya

  Waberoya Platinum Member

  #2
  Dec 4, 2008
  Joined: Aug 3, 2008
  Messages: 11,596
  Likes Received: 3,888
  Trophy Points: 280
  Supported!! good nakala and analysis.

  Mtu anakuja kuomba kura, anataka tumwajiri, akifika ofisini nampa his responsibilities wakati akianza kufanya naanza kumsifu, sili , silali ni kumsifu tu ,kitu ambacho ndicho alichotakiwa kufanya mika 3 iliyopita!
   
Loading...