Vigogo Escrow waipa mtihani mkubwa mahakama ya mafisadi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,006
Vigogo waliotuhumiwa kwa kashfa kubwa zilizotikisa nchi miaka ya nyuma likiwamo sakata la uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, hawatashtakiwa katika mahakama hiyo, imefahamika.

Divisheni hiyo maarufu kwa jina la Mahakama ya Mafisadi, ilianza kazi rasmi Julai 8, mwaka jana ikiwa ni moja ya ahadi zilizonadiwa na Rais John Magufuli katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Wakati kukiwa na matarajio kwamba Mahakama ya Mafisadi itashughulika na vigogo wanaodaiwa kushiriki katika kuihujumu nchi kupitia kashfa mbalimbali za kifisadi ikiwamo hiyo ya akaunti ya Tegeta Escrow, Nipashe imebaini divisheni hiyo nyeti ya Mahakama Kuu haitakuwa na meno dhidi yao.

Chanzo chetu kilieleza kuwa hata vigogo wanaodaiwa kutafuna mabilioni ya shilingi kupitia sakata linalochunguzwa la mkataba wa Kampuni ya Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi nao hawatafikishwa mbele ya mahakama hiyo ikiwa watabainika kuhusika katika kashfa hiyo.

UTAWALA WA SHERIA
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, katika mahojiano maalum na Nipashe wiki iliyopita, alisema kisheria isingekuwa sahihi kuyachukua makosa yaliyotendwa zamani kuyapeleka mbele ya Mahakama ya Mafisadi.

“Sisi ni taifa linaloheshimu utawala wa sheria ambao unazuia utoaji wa adhabu kwa makosa ya zamani kwa kutumia sheria mpya au vifungu vya sheria vipya. Kwa Kiingereza tunaiita sheria (au vifungu vyake) yenye "retrospective effect". Hata Katiba ya nchi inazuia hili kutokea chini ya ibara ya 13(6)(c),”alisema.

Ibara ya 13(6)(c) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kinasema: " Ni marufuku kwa mtu kuadhibiwa kwa sababu ya kitendo chohote ambacho alipokitenda hakikuwa ni kosa chini ya sheria, na pia kwamba ni marufuku kwa adhabu kutolewa ambayo ni kubwa kuliko adhabu iliyokuwapo wakati kosa linalohusika lilipotendwa."

Dk. Mwakyembe aliendelea kubainisha kuwa sheria ya uhujumu uchumi imefanyiwa marekebisho siyo tu kwa kupanua wigo wa makosa ya kusikilizwa na Mahakama ya Mafisadi kama vile utakatishaji fedha haramu, ugaidi, makosa ya ukiukaji sheria za uhifadhi wa maliasili - wanyama, misitu na hata kuyaongezea adhabu baadhi ya makosa.

Alipoulizwa kwanini kumekuwa na upungufu wa kesi katika Mahakama ya Mafisadi, Dk. Mwakyembe alisema: "Ulipoandaliwa utaratibu wa kurekebisha Sheria ya Uhujumu Uchumi ili kuanzisha divisheni hiyo ya Mahakama Kuu, matukio mengi ya rushwa, wizi, ujangili, ubadhirifu nchini yalikuwa ya mabilioni ya fedha."

Aliongeza: "Ili Mahakama ya Mafisadi isihemewe na makosa madogo madogo bali makubwa machache yanayoathiri uwezo wa nchi kuhudumia wananchi wake ipasavyo, iliamuliwa kuweka kigezo cha makosa kuanzia Sh. bilioni moja na kuendelea kushughulikiwa na mahakama hiyo maalum."

Alisema kuadimika kwa kesi kubwa toka makahama hiyo ianzishwe rasmi Julai mwaka jana, kunatoa tafsiri ya mafanikio makubwa ya mabadiliko ya sheria yaliyofanyika ambayo yamewaogopesha wezi.

“Aidha, tumepitisha bungeni sheria ya kuwalinda watoa taarifa za uhalifu na kuwalinda mashahidi kwa lengo la kuimarisha upelelezi na uendesha mashtaka wa kesi za rushwa na uhujumu uchumi,” alisema.

Dk. Mwakyembe alisema kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi ni moja ya mafanikio makubwa kwa Wizara ya Katiba na Sheria mwaka 2016. Mafanikio mengine ya wizara hiyo aliyoyabainisha, yataelezwa katika machapisho yajayo ya gazeti hili.

"Ukiangalia Ilani ya Uchaguzi ya chama tawala ya mwaka 2015 na hotuba elekezi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa bungeni Novemba 20, 2015, unaliona suala la vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu likibeba kipaumbele nambari moja kwa upande wa sekta ya sheria," alisema.

"Hivyo, moja ya majukumu yetu makuu ya kwanza kama wizara ilikuwa ni uanzishwaji wa Divisheni Maalum ya Mahakama Kuu kushughulikia makosa hayo tu kwa haraka na kwa ufanisi wa hali ya juu."

KIBALI CHA DPP
Aidha, katika mahojiano mahsusi na Nipashe Oktoba 23, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju, alisema kisheria, sheria haiwezi kuadhibu makosa yaliyotokea kabla ya kutungwa kwake.
"Sheria (ya kuanzisha Mahakama Maalumu ya Mafisadi) iliyotolewa Julai 8, mwaka huu, imeanza utekelezaji kuanzia kipindi hicho," alisema Mpanju.

Mpanju alisema watuhumiwa wa makosa ya ufisadi ya kuanzia Julai 8, mwaka huu ndiyo watafikishwa mahakamani humo baada ya upelelezi wa kesi zao kukamilika.

"(Mahakama ya Mafisadi) itatumika kuadhibu watakaohusika na makosa hayo (sasa na) baada ya Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), Ofisi ya DPP (Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali) kukamilisha upelelezi na kwenda kwa jaji ili ianze kusikilizwa," alisema Mpanju.

Alisema ili mahakama hiyo ianze kufanya kazi kunahitajika uwapo wa makosa, uchunguzi kutoka Takukuru na kibali cha DPP kesi kufikishwa mahakamani.

"Naweza nisisema kesi zinaanza lini ila inategemea uwapo wa kosa," alisema. "Vyombo vya serikali viwe vimefanya upelelezi wa mashauri hayo, ili tusifike mahakamani na kusema uchunguzi bado haujakamilika."

"Inatakiwa ikifika mahakamani ianze kusikilizwa moja kwa moja. Inatakiwa ofisi hizo zikamilishe kila kitu ndipo sisi tutaarifiwa na Jaji Mkuu apewe taarifa, ndipo tutajua zinaanza lini."

HARAKA IWEZEKANAVYO
Rais Magufuli alitoa ahadi ya kuanzisha mahakama hiyo kwenye mikoa kadhaa aliyopita kwa ajili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Aidha, katika siku ya kilele cha Wiki ya Mwaka Mpya wa Mahakama jijini Dar es Salaam mapema mwaka huu, Rais Magufuli alimtaka Jaji Mkuu, Othman Chande, kutosubiri Bunge kupitisha Sheria ya Uanzishwaji wa Mahakama Maalumu ya Mafasadi, badala yake mahakama hiyo ianze kufanya kazi haraka iwezekanavyo.

Jaji Mkuu Chande hivi karibuni alisema kanuni zitakazotumika kuendesha kesi zipo tayari.

Alisema kanuni hizo zinaeleza namna kesi zitakavyofunguliwa, jina zitakayopewa na jinsi ya kuwalinda mashahidi.

Alisema kesi zitasikilizwa kwa siku 30 na majaji na kwamba zitachukua muda usiozidi miezi tisa hadi kutolewa uamuzi.

Tangu mchakato wa kuanzisha kwa mahakama hiyo uanze kulikuwa na mtazamo kwamba huenda vigogo waliotuhumiwa kwa kashfa zenye thamani ya mabilioni ya shilingi kama vile sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, utoroshaji wanyama hai mfano twiga, ulipaji mishahara hewa kwa watumishi hewa wa umma na Richmond wangefikishwa katika mahakama hiyo.

VIGOGO WA ESCROW
Hii ni kashfa iliyotikisa nchi mwaka 2014 kwa kuhusisha uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow na kusababisha baadhi ya mawaziri na wenyeviti wa kamati za bunge kuwajibishwa.

Akaunti ya fedha hizo ilifunguliwa na Benki Kuu ya Tanzania (Bot) mwaka 2004 baada ya kuwapo kwa mgogoro kati ya IPTL na Tanesco kuhusu gharama ya uwekezaji ‘Capacity Charge’. Vigogo kadhaa walihusishwa na kashfa hiyo na baadhi walivuliwa nyadhifa zao, wakiwamo mawaziri.

MKATABA WA LUGUMI
Ni kashfa nyingine ambayo ilitarajiwa vigogo wake wangepelekwa katika Mahakama ya Mafisadi baada ya uchunguzi kukamilika.

Taarifa zinadai kuwa hadi sasa, uchunguzi bado unaendelea kuhusiana na sakata hilo linalohusisha matumizi yenye shaka ya zaidi ya Sh. bilioni 30 katika Jeshi la Polisi.

Inadaiwa kuwa Jeshi la Polisi liliangia mkataba wa thamani wa Sh. bilioni 37 na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd wa kusambaza na kufunga mitambo ya kuchukulia alama za vidole katika vituo vya polisi 108 lakini ni vituo 14 tu ndivyo vilivyofungwa huku malipo ya zaidi ya asilimia 90 yakiwa tayari yamelipwa kwa kampuni hiyo.

Kashfa kuhusu mkataba iliibuliwa Aprili 5, mwaka huu na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Aeshi Hilary, wakati wakipitia mahesabu ya jeshi hilo na kukuta upungufu huo na kuitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuwakabidhi makubaliano ya mkataba huo Aprili 11, mwaka huu.

MABILIONI USWISI
Ni mojawapo ya kashfa iliyowahi kutikisa nchi baada ya kuwapo kwa madai kuwa kuna baadhi ya viongozi maarufu pamoja na wafanyabiashara wa Tanzania ambao wameficha takribani Sh. trilioni 1.3 katika benki za Uswisi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Uswisi iliyotolewa Juni 2012, kuna Watanzania wamehifadhi kiasi cha dola za Marekani milioni 178 katika benki mbalimbali nchini humo.


Chanzo:
Nipashe

*Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe na Sanula Athanas
 
Nadhani Mwakyembe anachanganya mambo. Sheria ya kukata 15% wadaiwa wa heslb imetungwa sasa, kwa nini inatumika mpaka kwetu ambao tulikopeshwa miaka hiyo?

Ni dhahiri shahiri hii ni double standards ambapo wanyonge ndiyo wanaoonewa. Hovyo kabisa
 
Then hiyo mahakama haina faida yoyote ivunjiliwe mbali watubwaendelee na kupiga madili makubwa makubwa
 
  • Thanks
Reactions: BAK
Katika mambo ambayo yataharibu msingi wa umoja wa kitaifa ni ubaguzi mbele ya sheria, ukabila na ukanda na mengine yanayofanana na hayo.
Hata hivyo, kashfa ya escrow ilivyoshughulikiwa inatia doa kubwa sana taifa.
 
Ndiyo katika mwendo ule ule wa kupindisha sheria ili mafisadi, wezi, watoa na wapokea rushwa waendelee kutuzuga Watanzania huku wakingiana vifua kwenye maovu yao chungu nzima dhidi ya Tanzania na Watanzania.

Nadhani Mwakyembe anachanganya mambo. Sheria ya kukata 15% wadaiwa wa heslb imetungwa sasa, kwa nini inatumika mpaka kwetu ambao tulikopeshwa miaka hiyo?

Ni dhahiri shahiri hii ni double standards ambapo wanyonge ndiyo wanaoonewa. Hovyo kabisa
 
Hakuna kitu hapo ni Comedy tu .....labda kesi za wezi wa simu kuku na walala hoi....ila wakula thubutu....yako
 
Watu wa ajabu kweli, hivi habari kutoka nipashe ndio inawaweka kiwewe namna hii. Someni sheria zote ambazo zimeongezwa kwenye kesi za uhujumu uchumi ili muweze kujiridhisha na nini kinafanyika kabla ya kubwabwaja. Huwezi kuweka informed decision kwa kusoma paragraph moja bila kuwa na other caveats. Kama kawaida baadhi ya JF members copy n paste na kuangalia matumbo yao zaidi na sio taifa.
 
Watu wa ajabu kweli, hivi habari kutoka nipashe ndio inawaweka kiwewe namna hii. Someni sheria zote ambazo zimeongezwa kwenye kesi za uhujumu uchumi ili muweze kujiridhisha na nini kinafanyika kabla ya kubwabwaja. Huwezi kuweka informed decision kwa kusoma paragraph moja bila kuwa na other caveats. Kama kawaida baadhi ya JF members copy n paste na kuangalia matumbo yao zaidi na sio taifa.
Kesi za mafisadi zipo ?
 
Back
Top Bottom