Ex Spy
JF-Expert Member
- Jan 15, 2007
- 213
- 1,726
- Kikwete aongoza kikao cha maadili kwa usiri
Gazeti la Mwananchi
KAMATI ya Maadili ya CCM jana ilifanya kikao chake mjini hapa na kujadili mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kitendo cha baadhi ya vigogo wa chama hicho kuonekana kuwa mwiba mkali kwa serikali.
Kikao hicho kilifanyika mjini hapa jana chini ya mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete huku kukiwa na usiri mkubwa wa mambo ambayo yanajadiliwa.
Kikao hicho kimefanyika siku moja kabla ya vikao viwili vikubwa kichama, yaani Kamati Kuu ambayo kikao chake kitafanyika leo na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) kesho.
Habari ambazo zililifikia gazeti hili juu ya kile kilichojadiliwa na kamati ya maadili, zilisema kwamba, walijadili kwa undani hali ya mvutano na upinzani ambayo inaonekana kushika kasi ndani ya CCM katika siku za karibuni na hata kuiweka serikali katika wakati mgumu.
Kikao hicho cha maadili kwa kawaida kinakuwa na wajumbe wachache ambao idadi yao ni kati ya 12 na 13 na ndicho kikao pekee kinachotunza siri za chama ndani na nje na maamuzi yake huwa hayawezi kupingwa.
Wajumbe wanaounda kamati hiyo ni pamoja na mwenyekiti wa CCM, katibu mkuu, manaibu katibu wa Bara na Zanzibar, makamu wenyeviti pande zote pamoja na marais wastaafu.
Wengine ni pamoja na wajumbe wa kuteuliwa ambao kwa upande wa Bara ni Andrew Chenge na Pindi Chana, ambao waliwasili jana katika ukumbi huo majira ya mchana.
Chanzo chetu ndani ya CCM kilieleza kwamba, moja ya mambo makubwa yaliyojadiliwa ni wabunge wa CCM kuishika pabaya serikali kuhusiana na utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya kashfa ya utoaji wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura kwa kampuni tata ya Richmond Development LLC.
Mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni uliikataa ripoti ya serikali ambayo ilionekana wazi kumsafisha mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Johnson Mwanyika.
Wabunge wengi wa CCM, wakishirikiana na wale wa upinzani waliweka wazi misimamo yao kwamba, serikali itoe upya ripoti ya utekelezaji wa maazimio hayo katika kikao kijacho cha bunge kitakachokuwa Novemba mwaka huu na iwapo hawataridhika nayo watatoa msimamo wao.
Wabunge kadhaa walionyesha msimamo wa kutokuwa na imani na serikali kwa namna ilivyoshughulikia suala hilo, jambo ambalo linaweza kusababisha kuilazimisha serikali kujiuzulu na kuitishwa uchaguzi mwingine.
Jambo jingine ambalo chanzo chetu kimetutaarifu kuwa lilijadiliwa kwenye kamati hiyo ya maadili ni mzozo ulioshika kasi hivi karibuni kuhusu vita ya ufisadi ambayo imewaparaganyisha viongozi wengi wa chama kimsimamo, wakiwemo makada wanaoheshimika.
Suala hilo la ufisadi limeigawa CCM katika makundi mawili yanayohasimiana, moja likiwa ni la wale ambao wanapambana na ufisadi na ambao wamekuwa wakijionyesha hadharani na pili ni lile linalotuhumiwa kwa ufisadi, ambalo vita yake imekuwa ni ya chini kwa chini.
Tayari baadhi ya wabunge walio mstari wa mbele kupambana na ufisadi wamelalamika kuwa, wanafanyiwa visa na kundi hilo la mafisadi, vikiwepo vitisho pamoja na mikakati ya kuhakikisha hawapitishwi au kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Hatua ya mwanasiasa mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru kufanya kikao na waandishi wa habari nyumbani kwake na kukemea viongozi wanaokikosoa chama hadharani, ni dalili mojawapo ya kwamba kikao hicho kingejadili ajenda hiyo.
Ingawa Kingunge alifanya mkutano wake nyumbani kwake, lakini maandalizi yote yalifanywa na ofisi ndogo ya CCM na hata viongozi wa Umoja wa Vijana wa chama hicho waliohudhuria.
Pia katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alinukuliwa juzi akidai kwamba, wale wote ambao wamekuwa wakikituhumu chama hicho kwa ufisadi lazima waondoke.
Tofauti na siku nyingine, kwenye kikao cha jana kulikuwa na ulinzi mkali wa chama na waandishi walizuiwa hata kulikaribia jengo.
Akizungumza na Mwananchi juzi, Makamba alisema kuwa, hawezi kuzungumza kitu chochote nje ya kikao, hivyo akasema hawezi kuanika hadharani agenda za kikao hicho.
Kauli ya Makamba iliungwa mkono na ofisa habari wa CCM, Gabriel Athuman ambaye jana alizungumza na mwandishi wa gazeti dada la Citizen akisema kikao cha jana kingekuwa cha siri kubwa na akawatahadharisha waandishi kutofika wala kupiga picha.
Majina ambayo yalitajwa kuwa yangeweza kujadiliwa ni pamoja na mbunge wa Nzega Lukas Selelii, Spika wa Bunge Samuel Sitta na Mbunge wa Ilemela; Anthony Diallo. Hata hivyo, Mwananchi haikuweza kuthibitisha habari hiyo.
Kikao hicho kilipangwa kuanza asubuhi, lakini kikachelewa hadi saa 9:40 baada ya Rais Kikwete kuwasili.