Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Hivi karibuni umetokea msiba wa mtoto wa miezi miwili maeneo ninapoishi. Mtoto huyo alifariki ghafla akiwa usingizini. Mama wa mtoto huyo aliamka asubuhi na kukuta mwanaye amefariki. Wakati tunandaa mazishi, nilisikia minong'ono juu ya kifo cha yule mtoto kuhusishwa na imani za kishirikina na mlengwa alikuwa ni bibi mmoja anayeishi hapo mtaani. Ile minong'ono iliendelea hadi tukazika, na kila mtu kuendelea na shughuli zake. Vifo vya ghafla vya watoto chini ya mwaka mmoja huwa vinatokea sana, ingawa hakuna takwimu sahihi kwa sababu watu huwa wanazika kimyakimya, bila watoto hao kufanyiwa uchunguzi kitaalamu ili kujua sababu ya kifo cha mtoto huyo.
Huenda hata wewe unayesoma hapa utakuwa shahidi yangu kuwa pia umewahi kusikia au kushuhudia kifo cha ghafla cha mtoto wa chini ya mwaka mmoja. Na bahati mbaya zaidi vifo hivyo vimekuwa vikihusishwa na imani za kishirikina. Familia nyingi zimesambaratika na wengine wameuawa kwa kuhusishwa na vifo vya namna hii. Lipo tatizo ambalo linafahamika kama Sudden Infant Death Syndrome (SIDS), ambalo kwa Marekani hujulikana kama Crib Death. Hiki ni kifo cha ghafla cha mtoto wa chini ya mwaka mmoja ambapo sababu ya kifo inakuwa haifahamiki, pengine hata baada ya uchunguzi wa mwili wa mtoto kufanyika.
Tatizo hili ndilo linalosababisha vifo vya watoto wengi wa umri chini ya mwaka mmoja, na siyo kwa Tanzania pekee bali duniani kote. Kwa mfano Marekani kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2009, ilionyesha kwamba watoto wapatao 2,226 walifariki kutokana na tatizo hilo. Hata hivyo kwa mujibu wa takwimu za nyuma inaonyesha kwamba idadi hiyo imepungua kwa asilimia 50, na hiyo ilitokana na kampeni iliyoanzishwa nchini humo iliyopewa jina la Back-to-Sleep Campaign ambayo ilizinduliwa mwaka 1994. Hiyo ni Marekani ambapo wenzetu wametutangulia kwa teknolojia ya utabibu. Naamini kwa nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi.
Kwenye kitabu cha Molecular Link Between the Sudden Infant Death Syndrome and the long- QT Syndrome, pamoja na jarida la Medical Association la Oktoba 2006 inaonekana kwamba, watoto wengi wanaofariki kwa vifo vya namna hii, wale wa kiume wanaongoza kwa asilimia 61, ukilinganisha na watoto wa kike. Imebainika kwamba, watoto hao wamekuwa wakikabiliwa na matatizo ya ubongo kwa upande unaohusika na upumuaji ambapo pia vifo hivi vinahusishwa na sababu za kizalia (genetic), ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja.
Zipo sababu nyingi mbazo zinahusishwa na kuzaliwa kwa watoto wanaokumbwa na vifo vya ghafla usingizini ambazo baadhi yake ni hizi zifuazo:
-Mama mzazi kutohudhuria kliniki wakati wa ujauzito
-Mama mjamzito kutopata vyakula vyenye virutubisho.
-Mimba za utotoni
-Mama kuzaa haraka haraka bila kupata muda wa kupumzika baada ya kujifungua
-Mama mjamzito kuvuta sigara
-Mama mjamzito kutumia madawa ya kulevya au pombe kupita kiasi
-Mtoto kuzaliwa na uzito mdogo.
Sababu nyingine inayotajwa mbali na hizo hapo juu ni ile inayotokana na ulalaji wa mtoto. Inawezekana mtoto akazaliwa akiwa na afya yake njema, lakini anaweza kupatwa na kifo cha ghafla usingizini kutokana na namna alivyolazwa. Kwa mfano kumlaza kifudifudi mtoto wa umri wa chini ya mwaka mmoja kunahusishwa na vifo vya namna hii, lakini pia hata kumlaza kiubavu nayo si salama, kwani ni rahisi sana mtoto kugeuka mwenyewe na kama ikitokea amejiziba pumzi ni rahisi kupoteza maisha. Inashauriwa kama mtoto analazwa kifudifudi asilazwe kwenye godoro laini mto laini au blangeti laini kama sufi, kwani ni rahisi kusababisha joto na kumfanya mtoto kuvuta hewa yenye joto na hivyo kumsababishia kifo. Inashauriwa mtoto wa umri huo kulazwa chali, kwani ulalaji wa namna hiyo ni salama na ndio sababu Marekani walianzisha kampeni ya kuwahimiza kina mama kuwalaza watoto wa chini ya mwaka mmoja chali na wakafanikiwa kupunguza vifo vya ghafla kwa watoto wa umri huo kwa asilimia 50.
Pia mama kumnyonyesha mtoto huku akiwa amelala husababisha vifo vya ghafla. Inashauriwa mama anapomnyonyesha mtoto awe amekaa kwani akimnyonyesha huku akiwa amelala anaweza kupitiwa na usingizi na kusababisha mtoto kuzibwa pumzi na ziwa la mama na hivyo kupoteza maisha. Uvutaji wa sigara karibu na mtoto na kumlaza mtoto katika chumba kisicho na hewa ya kutosha huweza kusababisha kifo cha ghafla kwa mtoto huyo.
Kwa hiyo basi, vifo vingi vya ghafla vya watoto wa umri huu, ambavyo vinahusishwa na imani za kishirikina, vikichunguzwa sana, itagundulika kwamba, sababu nilizozitaja, zinahusika moja kwa moja. Lakini kwa sababu ya kutojua, watu wanakimbilia kushikana uchawi. Ni vyema kama mama wajawazito wataelimishwa kuhusu tatizo hili na sababu zinazosababisha pale wanapohudhuria kliniki ili wachukue tahadhari.