VIDE0-Aina nne za saratani zinazowatesa Watanzania


Donatila

Donatila

JF-Expert Member
Joined
Oct 23, 2014
Messages
3,092
Likes
4,071
Points
280
Age
28
Donatila

Donatila

JF-Expert Member
Joined Oct 23, 2014
3,092 4,071 280

Ugonjwa wa saratani unazidi kuwatesa zaidi Watanzania baada ya idadi ya wagonjwa wapya kuongezeka kutoka 2,416 mwaka 2005 hadi 6,338 mwaka 2016, huku aina nne zikionyesha kuchukua theluthi mbili za wagonjwa wote wa maradhi hayo.

Takwimu zilizotolewa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kutoka mwaka 2005 hadi 2016 zinaonyesha kuwa asilimia 68 ya saratani zinazowasumbua Watanzania ni za matiti, ngozi (caposis sarcoma), shingo ya kizazi na mfumo wa njia ya chakula na kwa kila wagonjwa 10, saba wanasumbuliwa na saratani hizo.

Rekodi hiyo ni kwa wagonjwa wanaofika katika taasisi hiyo pekee mbali na hospitali zingine zinazotibu saratani nchini ikiwamo Bugando, KCMC na Mbeya.

Wakati aina hizo zikikithiri, saratani ya shingo ya kizazi ndiyo inayoongoza ambayo inachukua asilimia 34 (sawa na mgonjwa mmoja kwa kila watatu) wanaougua ugonjwa huo, ikipanda kutoka wagonjwa wapya 879 mwaka 2005 hadi 2,081 mwaka jana.

Akizungumza baada ya kutoa takwimu hizo, daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka taasisi hiyo, Crispin Kahesa alisema inayofuata ni saratani ya ngozi (caposis sarcoma) inayochukua asilimia 13 ya saratani zote, matiti asilimia 11 na ile ya mfumo wa njia ya chakula asilimia 10.

“Takwimu za Ocean Road peke yake zinatoa matokeo hayo, hapo bado kuna Bugando, KCMC na Mbeya huko kote zinashabihiana. Tangu mwaka 2005 wagonjwa wapya wa saratani ya matiti walikuwa 879, lakini kwa mwaka 2016 tumepokea 2,081 idadi inaongezeka,” alisema Dk Kahesa.

Alizitaja saratani zingine zinazoongezeka kwa kasi ni ya shingo na kichwa ambayo inachukua asilimia saba ya wagonjwa wote, saratani ya matezi kwa asilimia sita na ya damu asilimia nne.

Saratani ya mfumo wa mkojo inachukua asilimia tatu, ya ngozi asilimia tatu, jicho asilimia mbili na tezi dume ni asilimia mbili wakati aina zingine za saratani zikichukua asilimia tano.

Dk Kahesa alisema tangu mwaka 2005 mpaka sasa wagonjwa wapya wanaotibiwa katika taasisi ya Ocean Road wamefikia 129,075 na kwa wanaohudhuria kliniki ni 222,470.

“Waathirika wakuu wa magonjwa ya saratani ni akinamama kutokana na aina zinazowashambulia wao pekee kuchukua asilimia 44, carposis sarcoma inaathiri wote na hasa wale ambao mfumo wao wa kinga ya mwili umepungua lakini madhara yake tunaweza kuyaona kwenye ngozi, mfumo wa chakula, hewa na sehemu zingine,” alisema.

Dk Kahesa alisema, “hii imehusishwa kwa asilimia 80 ya wale wenye upungufu wa kinga ambao unachangiwa na ugonjwa wa Ukimwi na hasa wale ambao hawapo kwenye tiba. Hii ndiyo inatuumiza sana hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara ikilinganishwa na wenzetu kwa kuwa sisi ukanda wetu maambukizi yapo juu.”

Alizitaja saratani zingine zinazoongezeka kwa kasi kuwa ni inayohusisha njia ya chakula ikiwamo koromeo ambayo wagonjwa wengi ni akinababa kwa kuwa wengi wanatumia pombe kupita kiasi, vilevi, tumbaku, unene uliokithiri na baadhi yao matumizi ya vyakula vya viwandani.

Katika hatua nyingine, Dk Kahesa alisema Oktoba ni mwezi wa maadhimisho ya saratani ya matiti kwa ajili ya kujenga uelewa, kugundua na kuitibu.

Mratibu wa Programu ya Via vya Uzazi katika Wizara ya Afya, Dk Safina Yuma alisema saratani ya matiti ni ya pili katika kuchochea vifo vinavyohusisha ugonjwa huo kwa wanawake nchini, huku kuchelewa kupata ugunduzi na tiba haraka kukitajwa kuchangia kuleta ugumu wa matibabu.

“Asilimia 80 ya watu wakiugua wanapona, lakini kwetu ni asilimia 40. Ikabidi uwekwe mkakati maalumu wa kuhamasisha kuweza kuelewa kuhusu saratani ya matiti,” alisema Dk Yuma.

Akizungumzia kuhusu ugonjwa huo, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Sikika, Irinei Kiria alisema wakati ongezeko la wagonjwa wa saratani likikua nchini, bado kuna changamoto tatu ambazo zinawakabili wagonjwa.

“Changamoto kubwa ni dawa kuwa bei ya ghali, bado Serikali inatakiwa kufanya hima kuhakikisha inapungua. Watoa huduma bado ni wachache na maeneo ya kutolea huduma pia ni machache nchini, hili linasababisha wagonjwa wengi kuishia majumbani kutokana na umbali wa maeneo yanayotoa huduma hizo,” alisema.

Katika kukabiliana na saratani, wiki iliyopita Rais John Magufuli alitoa Sh1 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi ili kupambana na ongezeko la wagonjwa wapya wa maradhi hayo kwa asilimia 34 nchini ikilinganishwa na saratani zingine.

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinaonyesha wagonjwa wapya kila mwaka wanakadiriwa kuwa 50,000, huku asilimia 26 ndiyo hufika hospitalini.Chanzo: Mwananchi
 

Forum statistics

Threads 1,237,956
Members 475,774
Posts 29,307,815