Elections 2010 Vicent Nyerere mbunge mteule

YeshuaHaMelech

JF-Expert Member
Oct 12, 2010
2,597
37
Vicent Nyerere ni mbunge mteule kwa jimbo lake ambalo sijalinasa jina ila ni hukooo kwa akina mura...kwa asilimia 59. Source, taarifa ya habari Radio One.
 
JUMA hili nimeongea na mwanaharakati wa mabadiliko ajulikanaye kwa jina la Vincent Kiboko Nyerere. Vincent alizungumza nami kufuatia makala yangu ya juma lililopita iliyosema, "Watanzania tumsikilize Makamba".
Katika mazungumzo yake, Vincent alizungumza mengi ikiwa ni pamoja na mwelekeo wa taifa hili kisiasa na kimaendeleo. Anasema katika pita zake duniani amegundua kabisa Tanzania tuna hazina kubwa na bahati ya pekee ya mali ya asili iliyotunzwa vyema toka enzi ya uumbaji wa dunia ila bado haijatumika vyema kwa Tanzania na Watanzania wenyewe.
Mwalimu alilijua hili, na kwa upendo wa dhati aliopewa na Mungu kwa Watanzania aliamua yeye na CCM waache kabisa kugusa rasilimali hizi hadi hapo tutakapokuwa na uwezo (uwezo wa kuwa na vyama vingi na Watanzania wakaamua kwa dhati ni chama na watu gani walete maendeleo) ndio tuanze kuzitumia.
Mwalimu alijua kabisa kwamba wao walikuwa ni watu wa kuleta uhuru tu lakini maendeleo makubwa yangeletwa na chama kingine na watu wengine. Ila wana CCM baada ya Mwalimu kufariki wakaamua kufakamia kwa kasi kana kwamba dhahabu na raslimali nyingine za asili zinaoza.
"Bwana Mwigamba iko siku nilisikitika, eti sisi (Watanzania) hatuna uwezo wa kuchimba madini ndo maana tunaleta wawekezaji. Serikali inayoweza kununua ndege za kivita na vifaru vinavyokaa kambini vikiota majani, inashindwa kununua mitambo ya kuchimba na kuchambua dhahabu? Mie nadhani aliposema Rais aliyepita kuwa sisi hatuna uwezo alikuwa akiwaongelea wana wa CCM sio Watanzania!" anasema kwa masikitiko Vincent Nyerere.
Anaendelea kusema, na kushindwa kwetu (kushindwa kwa wana CCM hasa viongozi) ni jambo ambalo Mwalimu aliliona mapema kabisa na kwa kuwa pengine hakuwa na majority katika kulitamka wazi ndo akaamua tungoje kwanza hadi tutakapokuwa na uwezo. Kwa maana ya kukusanya nguvu kujenga nidhamu na kuwa na upeo. Hakika ni kweli huyu alikuwa baba wa taifa.
"CCM kazi yake kubwa ilikuwa kuleta uhuru. Kazi hiyo wameimaliza salama sasa wapumzike ili waletewe maendeleo na vyama vingine, waige mfano wa Zimbabwe wameleta uhuru maendeleo yanarudi nyuma kwa blaah blaah za ooh tulileta uhuru.
Tanzania ni ya Watanzania na sio ya CCM (japo CCM ina wenyewe). Tunapenda waendelee kuwepo maana salamu zao ni KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI (japo waliokianzisha hawakudumu). Hata ile salamu ya ‘Zidumu fikra sahihi za Mwenyekiti wa CCM' hawaisemi tena maana fikra wanazikiuka na mwenyekiti wa sasa labda hana fikra sahihi ndo maana hawasemi". Anasema Nyerere na kuendelea, "Kwa kweli anayempenda na kuujua msimamo wa Mwalimu hataichagua CCM maana CCM hii siyo ile ya Mwalimu. Hii ni CCM ya ‘chiporoporo'. Kama wenye mawazo ya mwalimu wanaitwa wehu, wana CCM hawa (chiporoporo) hivi wana maana gani kusema eti wanamuenzi?"
Vincent anapenda sana kurudia maneno ya Mwalimu "Ili tuendelee tunahitaji ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora". Anasema kama unakumbuka wakati wa uhuru tulikuwa na ardhi ndogo japo ilikuwa inatosha wakati ule ila tukaungana na Zanzibar, tulikuwa wachache kama milioni 10 na ushee sasa tupo milioni 40 mbona hatuendelei?
"Jibu ni rahisi kabisa siasa safi na uongozi bora ndiyo kikwazo cha kufika alipotaka Mwalimu. Akitoa mfano anasema, "Kwa mfano siasa inayoendeshwa jimboni kwangu ni chafu iko katika ushabiki zaidi kuliko uhalisia. Mtu anaweza kukuuliza ‘Una shilingi ngapi hadi ugombee?' Ni ujinga unaohitaji tuzo.
"Kwa mfano tunayo magari ya wagonjwa hapa manispaa ya Musoma lakini hata siku moja hutoyaona yakibeba wagonjwa mbali ya kutumika katika kutangaza mikutano ya hadhara inayoitishwa na mbunge na meya kwa ajili ya kujiandaa kushinda tena uchaguzi 2010 wakati kina mama wajawazito wanajifungulia nyumbani ndani ya manispaa inayotawaliwa na mbunge na madiwani 12 wa CCM.
Ikifika saa kumi na moja jioni magari yote ya wagonjwa yanafungiwa manispaa na madereva wanalala makwao. Inatia aibu na uchungu kuliko kuuma na nge. Sijui ni yapi wana CCM wanayotambia, hatutaendelea kabisa kama mambo ni haya. Sina hakika kama maeneo mengine yanafanyika haya yanayofanyika hapa, hii ni moja ya msukumo wa mimi kuingia katika harakati za siasa kiukweli.
"Yapo mengi sana yanayofanya tusiendelee, kama vile tuna gari jipya la zima moto (mercedes benz ACTROSS) la thamani ya milioni zaidi ya 400 lakini cha ajabu kazi kubwa ni kusomba maji katika shule ya mweka hazina wa CCM wilaya.
"Pia linatumika kusomba maji ya kujengea nyumba za watu binafsi wenye uwezo wa kununua kwa sh 30 elfu kwa tripu. Kwa mafuta na vipuri vya gharama za walipa kodi, hata mkuu wa mkoa analijua hili kama halijui basi yupo hapa si kwa kazi yake bali kwa kupumzika maana naye ni mstaafu jeshini.
"Kikubwa kinachofanya pia hatuendelei ni hawa wastaafu, ni serikali hiihii iliyoona sasa wamechoka na wanastahili kupumzika maana hata misuli na bongo zao hazifai kuhudumu tena, wakishapata kiinua mgongo wanafanya kazi upya kana kwamba hakuna vijana na wasomi wawezao kuifanya!"
"Ni udhalilishaji, nasikia huwa wanawashikia nafasi watoto na wajukuu zao wakue ili kina Kayumba wasiingie hapo maana wataaibika na utendaji wa vijana maana wana machungu na nchi. Sasa ni hiari yetu kama tunataka maendeleo au la, kila kitu tayari sasa kilichobaki ni siasa safi na uongozi bora. Uongozi bora hauko CCM (japo wao wanaita utawala bora) maana vichwa vyao ni kutawala sio kuongoza".
Lakini Vincent Nyerere ni nani? Jina lake anaitwa Nyerere, ndilo jina hasa la nyumbani ila baada ya ubatizo akapewa jina la Vincent. Baba yake ni Josephat Kiboko Nyerere, ambaye ni mzaliwa wa mwisho katika tumbo la Mgaya (Mama mzazi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere).
Hivyo Mwalimu ni baba yake mkubwa tumbo moja na baba yake. Makazi yake ni Musoma mjini ambako ‘anajasiriamali' katika kuusaka mkate wa kila siku.
Vincent anasema, "Mimi hapo kabla ya kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa hadi tarehe 10/8/2008 ndipo niliamua kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa kweli mbali na umakini wa viongozi wa chama na mwenendo mzima wa chama hiki, pia niliona ndicho chama pekee cha wakulima na wafanyakazi pamoja na wajasiliamali wadogo wadogo na walala hoi waliochoka na ahadi zisizo na mwisho.
Hapo nilikata shauri kujiunga moja kwa moja na kuwa wazi katika hisia na msimamo wangu kisiasa. Mchango wangu katika chama ni kuomba watanzania wajiunge na CHADEMA na wawe mstari wa mbele kupigania haki zao za msingi. Wengi sasa wamejiunga baada ya kuuona ukweli. Japo wengine wanabeza ila wataujua ukweli, TIME WILL TELL (muda utasema)".
Vincent anasema, "Nilikuwa shabiki wa CCM bila kuwa mwanachama wake, hilo nakiri kabisa maana msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Lakini kwa maneno, kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu nikaona nisijiunge nao maana naamini twaweza kuwashinda (if u can't beat them, join them)".
Mimi nimeamua kuwa ifikapo 2010 nitagombea ubunge na udiwani hapa Musoma mjini. Ila kutangaza azma yangu hakumfungii mtu mwingine kuja na kutangaza azma hiyo hiyo kupitia CHADEMA.
Akija na akaonekana ni bora zaidi na wananchi wakaamua, nitaungana naye bega kwa bega hadi mwisho na kuhakikisha mgombea wa CCM anabaki kuwa msikilizaji na shabiki wa maendeleo yatayoletwa na CHADEMA.
Anasema anapenda sana kusoma na kusikia habari za maendeleo kuliko kelele za Makamba na Simba. Hawa na chama chao hawataleta maendeleo tena, anapenda vijana waamke wapiganie maendeleo wasingoje kubebwa na kupewa madaraka.
"Madaraka tunayo sisi ila maamuzi wanayo hao watawala wenye wizara ya kututawala (bora) maana kwao kilicho bora ni kututawala. Anasema na kurudia tena kwamba CCM ni mwalimu wa chekechea, hawezi kutufunza masomo ya sekondari. Walipotufikisha tumehitimu panatosha. Anasema, "Mwisho wa yote ndugu yangu Mwigamba najiskia faraja kuona na wewe umeyaona na umeamua tuwaamshe na wengine ili ndoto ya mwalimu itimie kabla ya mwisho wa Dunia."
Hayo ndiyo ya Vicent Kiboko Nyerere, mwana familia mmoja kati ya wawili wa familia ya Mwalimu Nyerere ambao tayari wamejiunga na CHADEMA na kutangaza hadharani ikiwa ni pamoja na kufanya harakati hadharani za kuitangaza CHADEMA.
Ni kweli kwamba kila kitu kina majukumu na uwezo wake kwa wakati wake. Ametoa mfano mzuri wa mwalimu wa chekechea. Kama nilivyowahi kueleza huko nyuma, mimi pia nimewahi kufundisha.
Lakini kila mwalimu ana uwezo wake na ngazi yake anayoweza kufundisha. Mwalimu mwenye cheti cha ualimu wa watoto wadogo ana uwezo mzuri sana wa kufundisha chekechea.
Anapowafundisha chekechea huwaandaa vizuri kwa ajili ya kuingia madarasa ya juu yaani elimu ya msingi. Na yule mwenye cheti cha ualimu wa msingi pia kazi yake na kuwaandaa watoto kwa ajili ya kuingia sekondari ambapo watakutana na walimu wenye stashahada ya ualimu. Vivyo hivyo kwa watakaoingia kidato cha tano na sita watakuta wenye elimu ya shahada.
Sikuwahi kuona mwalimu wa chekechea akaanza kumfundisha mtoto akiwa chekechea halafu akaendelea kumfundisha akiwa shule ya msingi na kwenda naye hadi akiwa sekondari hadi chuo kikuu.
Ikitokea hivyo huyo mwanafunzi atafeli vibaya. Vivyo hivyo vyama vikongwe vilivyoleta uhuru kazi yao ilikuwa ni kuleta uhuru. Vifike mahali vitambue kwamba kwenye ulimwengu wa leo vyama vikongwe kama CCM vinajitwisha jukumu la kufundisha hesabu za kidato cha sita wakati vimesomea kufundisha watoto wa chekechea kuhesabu.
Hatukatai kwamba mwalimu anaweza kupanda daraja kutoka kufundisha shule ya msingi na kwenda kufundisha sekondari. Lakini hiyo humlazimu mwalimu kuacha kufundisha, akarudi shule kusomea ualimu wa juu zaidi ndipo aje kufundisha elimu ya juu zaidi.
Ndicho kinachotokea kwa vyama vya miaka mingi tunavyovisikia huko katika nchi za wenzetu kama Demokrats na Republican (Marekani) ama Conservative na Labour (Uingereza).
Chama huondolewa madarakani, hurudi kujipanga na kuangalia wapi hawakufanya vizuri na kujifunza mazingira mapya ya kuongoza nchi kisha hurudi na maarifa mapya na kuweza kuleta changamoto kwa chama kilicho madarakani na baadaye hushinda tena. Tukiendelea kuwaacha hawa akina CCM, ZANU-PF madarakani tutapiga hatua kurudi nyuma kimaendeleo kwa kuwa walioshika madaraka humo ndani ni akina Kingunge na akina Mugabe waliozaliwa na kusoma enzi za zana za mawe ambao kuwaambia wabadili kilimo kiwe cha matrekta ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa na kumtegemea acheze. Kazi kwenu vijana wa leo!
 
Back
Top Bottom