Vibaka wataka kujiorodhesha mikopo elimu ya juu kimtandao

Makanyaga

JF-Expert Member
Sep 28, 2007
10,433
6,926
Source: Vibaka wataka kujiorodhesha mikopo elimu ya juu kimtandao

TAARIFA za kushangaza zimesikika hivi karibuni kuwa kulikuwa na majaribio 2700 ya kuingia kwa mabavu au mbinu tofauti katika dawati la mtandao la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), inadhaniwa kutaka kuongeza majina katika orodha ya waliofanikiwa kupata mikopo, au kubadili majina na kuweka mengine.

Juhudi hizo za kupenya katika viunganishi kimtandao vya kufanyia kazi na kutoa majibu ya maombi ya mikopo ni sehemu ya uhalifu mtandaoni, ambao mara nyingi hulenga taarifa za fedha, uhamishaji malipo, n.k. Kujiorodesha kwa hila ni sawa na wizi wa mamilioni ya shilingi.

Tatizo linaloonekana bayana la upenyezi huo mtandaoni, kwani siyo mtu anayejipenyeza bali anaajiriwa kusuka mbinu za kupenya katika viunganishi kimtandao vya vitengo tofauti vya taasisi hiyo, ili kuingia katika orodha ya wanaokopeshwa.

Siyo ajabu pia wangerekebisha taarifa za awali katika mtiririko wake ili ziendane na nyongeza hiyo au badiliko kama hilo lililofanywa kinyemela kuhusu nani waliopitishwa kupata mikopo.

Ujanja huo una gharama kwa maana kuwa inawezekana kufuatilia na kujua kompyuta au simu janja iliyotumika kufanya shughuli hiyo iliunganishiwa wapi, na endapo kituo cha awali kabisa cha kutoa ishara zinazohitajiwa kimtandao kinagunduliwa, aliyetumika kifaa hicho anapatikana bila matatizo.

Kupenyeza katika mtandao na kuongeza majina kinyemela au kubadili majina yaliyopo, bila kujulikana, ni kutazamia kuwa orodha zinatayarishwa kwa haraka haraka tu na hakuna njia ya kuhakikisha kama zinaendana na taarifa za ziada ambazo zimeshikwa na watu wengine.

Endapo yanatokea majina ambayo hayako katika taarifa rasmi zilizowasilishwa au kutayarishwa kwa pamoja katika hatua ya awali ni lazima kuwe na hisia ya tatizo kujitokeza mahali fulani, lakini vibaka mtandaoni wanatazamia kuwa wahusika wa kupelekwa taarifa rasmi wanaongoja mwishoni. Siyo rahisi wafahamu kuwa imerekebishwa kijanja.

Ina maana kuwa njia ya kuhakikisha kwamba hatokei mtu akatafuta tu wakala wa kompyuta akaingia katika viunganishi husika akapenyeza majina na kufuta mengine ni kina cha mawasiliano kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Kwa upande mwingine kuna suala la kina cha vizuizi vya kuingia katika viunganishi taarifa, kwa maana ya kupata ruhusa ya wahusika ngazi tofauti ambao ni washikadau katika orodha hiyo au wakati inatayarishwa.

Uhusiano huo wa kanzidata wakati wa kutayarisha orodha ya wanaokopeshwa na kuitoa rasmi kwa vyombo au taasisi tofauti ni kuwa kupeleka taarifa rasmi kuna kanuni zake, si taarifa ya kawaida ambayo inaingia tu katika sanduku la barua pepe la ofisi au mhusika fulani. Ni kizuizi kingine.

Wataalamu wa ofisi ya bodi ya mikopo wanasema kuwa wanafanya juhudi za kuunganisha kanzidata ya utayarishaji na urasimishaji wa maombi ya mikopo katika bodi na kanzidata zingine za taasisi zinazofanya kazi eneo hilo.

Mojawapo ni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kuweka mtawanyiko wa uhifadhi nyaraka, hivyo mtiririko huo usifanyike eneo moja tu na kazi hiyo iishie hapo, hivyo wakitokea wajanja wakafaulu kuingia katika kanzidata ya bodi ya mikopo inakuwa rahisi kwao kutenda uhalifu. Endapo kuna mtawanyiko taarifa kinzani zinaonekana kwa haraka.

Licha ya kusema kuwa kulikuwa na tatizo la kutaka kuvunja na kuingia katika mtandao na inaelekea kuna watu wengi au wasomi wa kompyuta walikuwa wanaletewa kazi za kuingia katika orodha hiyo, labda kuna kilichojificha.

Mara nyingi hujuma za namna hiyo zinatoka ndani, mkopo uelekezwe jina hewa, fedha ziingie mifukoni mwa watu wajanja, si ajabu wanaofanya kazi mle mle. Ni upigaji 'dili' wa kawaida.

Haikutolewa taarifa kuwa majina feki yaliongezwa au kanzidata ilihujumiwa kumbukumbu zikaonyesha hitilafu mahali popote, ila tu kwamba kulikuwa na majaribio maelfu ya kuingia katika kanzidata husika ili kuongeza data za kughushi kuhusu wanaotakiwa au kukubaliwa kupelekewa mikopo.

Ina maana kimsingi kanzidata hiyo ilibaki salama lakini kulikuwa na wasiwasi kuhusu majaribio mengi tu ya kutaka kuingia katika hifadhi zake za nyaraka au taarifa na ‘kurekebisha’ kile walichokitaka.

Ila kwa msemo ule wa ‘panapofuka moshi panaficha moto,’ kwani haiwezekani kuwa hujuma kama hizo ziliwahi kufaulu awali?

Suala jingine ni tofauti kati ya hujuma inayofanyika kwa ndani halafu maofisa wakaongeza majina feki wanayotaka ili fedha ziingie katika akaunti wanazozijua wenyewe, na kujaribu kuingiza majina kutoka nje.

Ili hujuma ifaulu inabidi iingie kwa njia ambayo haitofautiani na shughuli hiyo kufanyika kikawaida, lakini watu 2700 wakiajiri wataalamu kuingia katika kanzidata ya bodi na kuweka majina yao katika orodha inayotayarishwa au iliyokamilika, ni wazi hapo kuna ishara ya vurugu na upachikaji wa taarifa za kuchekesha katika kanzidata.

Ikitokea asubuhi ofisa anaingia anakuta orodha mpya katika hifadhi ya orodha ya wanaokopeshwa, au mtiririko tofauti kabisa, lazima atajua kuna hitilafu ilitokea ni mamluki.

Kuna taarifa za ziada ambazo zinaweza kubadili mtiririko wa maombi ya mikopo na hatua za utayarishaji wa orodha, kuwa dirisha la maombi lifunguliwe mwaka mzima, na siyo kipindi ambacho majina ya waliokubaliwa kujiunga na vyuo vikuu na wanaoendelea mwaka mwingine yameshatoka.

Ina maana kuwa wanafunzi au wanafunzi tarajiwa waweze kupeleka maombi yao wakati wowote, hali ambayo inaleta mkanganyiko fulani, kwani itakuwa haihusiani na matokeo ya mitihani ila vigezo vya kuomba vihusiane na masuala mengine.

Mitihani na matokeo ya kuomba kujiunga na vyuo itakuwa bado sana, au kwa wanaoendelea matokeo ya mitihani mwaka uliotangulia, labda ifahamike kuwa ni maombi ya awali.

Kuwapo kwa hatua mbili tofauti katika maombi ni kuwezesha majina kuwahi na kufanyiwa upembuzi wa awali, lakini kuna udhaifu kuwa suala la msingi zaidi ni mitihani na kuruhusiwa kujiunga vyuoni, hivyo inakuwa shida kuona tija ya maombi hayo ya awali.

Kwa upande mwingine, endapo kuna ofisa mwenye uwezo wa kutayarisha majina ya ziada akishirikiana na watu wengine wachache, anapata muda wa ziada wa kushughulikia mchakato huo ambao kimsingi ni hujuma, kwani mhusika akingoja hadi majibu ya mitihani yapokelewe au maombi ya kujiunga chuoni atakuwa amechelewa.

Kunakuwa na msongamano wakati huo na kazi hiyo inahitajiwa imalizike kwa haraka kwa vigezo mahsusi, bila kuwapo mwanya wa wakopeshwaji tarajiwa kufika ofisini kwa bosi huyo kwa maongezi marefu, au pia wakutane kwingineko.
Source: Vibaka wataka kujiorodhesha mikopo elimu ya juu kimtandao
 
Back
Top Bottom