Uzinduzi rasmi wa UDOM: Anachoongea Rais Kikwete (sasa hivi)


Invisible

Invisible

Admin
Joined
Feb 11, 2006
Messages
9,104
Likes
602
Points
280
Invisible

Invisible

Admin
Joined Feb 11, 2006
9,104 602 280
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE KWENYE SHEREHE ZA UZINDUZI WA CHUO KIKUU CHA DODOMA, TAREHE 25 NOVEMBA, 2010

Mhe. Benjamin William Mkapa, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma;
Mhe. Dkt. Amon Msekela, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;

Wahe. Wabunge;

Mheshimiwa, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo;

Mhe. Prof. Idris Kikula, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma;

Wahe. Mabalozi Mbali Mbali mliopo hapa;

Ndugu Viongozi;

Wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dodoma;

Wageni waalikwa;

Mabibi na Mabwana:

Asalaam Aleikum!


Ndugu Mkuu wa Chuo;

Napenda kuanza kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwako, na kwa jumuiya nzima ya Chuo Kikuu cha Dodoma kwa heshima kubwa mliyonipa ya kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizi za kihistoria za uzinduzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma na miundombinu mbalimbali ya Chuo hiki. Ni tendo la kihistoria kwa sababu baada ya miaka mingi, Serikali iliamua kujenga Chuo Kikuu kipya kuanzia mwanzo, yaani "from the scratch".

Uamuzi wa kujenga Chuo hiki ni utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuhusu kupanua fursa kwa vijana wetu na Watanznia wengine kupata elimu ya juu. Maelekezo yaliyojengeka juu ya sera ya msingi ya Chama chetu inayotambua na kusisitiza umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Nafurahi kwamba hata ujumbe wenu wa leo
unaosema "Elimu ya Juu ni Chachu ya Maendeleo ya Taifa" unabeba dhana hiyo.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Nachukua fursa hii kukushukuru wewe mzee wangu, kwa kunikubalia ombi langu la kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma. Kwa kweli nisingeshangaa wala kukukasirikia kama ungeniomba radhi na kunishauri nitafute mtu mwingine ili upate nafasi ya kufurahia kustaafu kwako baada ya miaka 10 ya kazi ngumu ya kuongoza taifa.

Nakushukuru na kukupongeza sana wewe, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Makamu wa Rais Mhe. Dr. Mohamed Ghalib Bilal, Wajumbe wa Baraza la Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Idris Kikula na Naibu wake wawili kwa kazi kubwa na nzuri mliyofanya katika ujenzi wa Chuo hiki.

Nasema mmefanya kazi nzuri na ya kustaajabisha kwani nilipowateua Februari, 2007 hapa kulikuwa na jengo moja tu la Ukumbi wa Mikutano wa Chimwaga na kwingineko kulikuwa pori na mbuga tu. Leo, miaka isiyozidi minne baadae, kuna mji mkubwa, tena wa kisasa kwa majengo na miundombinu na unaopendeza kwa jinsi ulivyopangwa na kupangika. Naamini hapo ujenzi utakapokamilika na miti na maua kupandwa UDOM patakuwa mji wa aina yake hapa Dodoma na nchini. UDOM itakuwa sehemu ya utalii wa maeneo yenye mandhari nzuri hapa Dodoma. Wakati nawapongeza na kuwatakiwa heri kwa mafanikio haya, sina wasiwasi kabisa kwamba kazi iliyo mbele yenu mtaifanikisha kwa kiwango tunachokitazamia sote.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Nawapongeza sana kwa uamuzi wenu wa kuandika kitabu nilichokizindua hivi punde, kinachoelezea kwa ufasaha historia ya kuzaliwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma. Nafurahi kwamba mmeandika historia hii wakati huu ambapo wenyewe mliohusika mpo na kumbukumbu zake bado zipo hai. Haya yaliyoandikwa ndiyo yenyewe hasa yaani "original". Si ya kusikia kutoka kwa aliyesikia au mwandishi anafikiria ndivyo ilivyokuwa. Mmefanya jambo jema ambalo linafaa kuigwa na wengi.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Kwangu mimi kuwepo kwa Chuo hiki ni ndoto iliyotimia kwa namna ambayo sikutegemea ingefanikiwa kiasi hiki katika muda mfupi huu. Ilani ya Uchaguzi ya CCM haikutaja moja kwa moja kujenga Chuo Kikuu kipya. Niliamua kuitafsiri dhamira ya kupanua fursa ya Watanzaia kupata elimu ya juu kwa kufanya mambo mawili. Kwanza, kuongeza majengo katika vyuo vikuu vilivyopo ili tuongeze idadi ya wanafunzi. Pili, kujenga Chuo Kikuu kipya.

Lazima nikiri kuwa nililisema la kujenga Chuo Kikuu kipya kwa woga wakati wa kampeni. Lakini niliamua kulifuatilia kwa nguvu mara baada ya kuchaguliwa kwani ahadi ni deni. Sina budi kutoa shukrani maalum kwa Prof. Peter Msolla aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu wakati ule na Prof. Rwekaza Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa mawazo ya awali na ushauri wao kuhusu ujenzi wa Chuo hiki. Mawazo yao ndiyo msingi tulioutumia kuanza kazi iliyotufikisha hapa tulipo sasa.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Shukrani maalum nazitoa kwa Prof. Idris Kikula, Prof. Shabani Mlacha na Prof. Ludovick Kinabo kwa umahiri wao wa kutafsiri mawazo yale katika mpango kabambe, mpango mkakati na kuutekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu. Ubunifu wao na usimamizi wao makini chini ya uongozi wako na Mhe. Dr. Mohamed Ghalib Bilal ndiyo uliozaa matunda haya tunayojivunia leo. Ahsanteni sana hakika hamtasahaulika kamwe katika historia ya nchi yetu. Nawashukuru wajenzi kwa kazi nzuri waliyofanya. Bila ya wao tungekuwa hatuna cha kuonesha na kujivunia.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Napenda kutumia fursa hii pia, kutoa shukrani maalum kwa wenzetu wa mifuko yetu ya Pensheni ya NSSF, PPF, PSPF, LAPF na NHIF kwa kuunga mkono na kusaidia jitihada za Serikali katika ujenzi wa Chuo kikuu cha Dodoma. Uamuzi wao wa kukubali maombi ya Serikali kukopa fedha za ujenzi ndio umewezesha hatimae Chuo hiki kuwepo. Wakati nikiwashukuru napenda kutoa rai kwa mifuko hii iendelee kukisaidia chuo kikamilishe ujenzi katika maeneo yaliyobaki. Pia, tuendelee kushirikiana katika mambo mengine muhimu ya ujenzi wa taifa letu.

Ndugu Mkuu wa Chuo
;
Ningependa vilevile kutoa shukrani maalum kwa Kampuni ya Microsoft na IBM za Marekani kwa kukubali maombi yangu ya kushirikiana nasi katika ujenzi wa Shule ya Teknolojia ya Habari ya Chuo Kikuu hiki. Nilifarijika sana nilipokutana na Bwana Bill Gates, muasisi wa Kampuni ya Microsoft kule Cape Town, Afrika Kusini mwaka 2007 nilipomfikishia ombi letu hilo na kunikubalia bila ya kusita. Baada ya muda si mrefu tangu tukutane akamtuma Bwana Cheikh Diara, Makamu wa Rais wa Microsoft, Afrika kushughulika nasi jambo ambalo limeendelea mpaka sasa.

Nilipokutana na Dr. Mark Dean, Makamu wa Rais wa IBM mwaka 2008 kule Washington, Marekani naye hivyo hivyo alikubali kushirikiana nasi kama wenzao wa Microsoft. Jambo muhimu ni kwamba wote wamekubali kutusaidia kufanya Shule ya IT ya UDOM iwe taasisi bora ya mafunzo katika Afrika. Baada ya mazungumzo hayo Dr. Mark Dean alitembelea Dodoma na kufuatiwa na ziara kadhaa za wataalamu kutoka shirika hilo.

Mashirikiano yameendelea na Chuo kimeanza kunufaika kwa namna mbalimbali na ushirikiano huo na naamini tutanufaika zaidi siku za usoni. Naomba muendelee kushirikiana na marafiki zetu hawa kama vile ambavyo naomba muimarishe uhusiano na ushirikiano na vyuo vikuu vingine duniani ambavyo mna ushirikiano navyo.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Kuanzisha Chuo Kikuu ni kazi kubwa na ngumu. Kunahitajika rasilimali nyingi ambazo nchi changa na maskini kama yetu ni mtihani mkubwa kuzipata. Lakini ni mtihani ambao hatuna budi kuukabili na kushinda kwani kinyume chake ni hasara kubwa zaidi. Maendeleo tunayataka ili tutoke kwenye umaskini. Lakini hakuna maendeleo bila ya elimu. Kwa kutambua ukweli huo katika awamu zote tangu uhuru Serikali imetilia mkazo elimu na katika awamu hii tumeweka mkazo mkubwa katika upanuzi wa elimu ya sekondari. Matokeo yake ni ongezeko kubwa la wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita wanaohitaji na wanaostahili kupata elimu ya chuo kikuu. Bahati mbaya vyuo vimekuwa havitoshelezi mahitaji. Ukweli huo ndiyo uliotusukuma kuamua kujenga chuo hiki tena cha ukubwa huu wa kudahili wanafunzi 40,000. Lengo letu ni kusaidia kupunguza ukubwa wa tatizo. Ndiyo maana pia tumefanya kila tuwezalo kufanikisha ujenzi wake na leo tunakizindua rasmi. Kesho tunaanza kuvuna matunda mema ya uamuzi huo wa busara tunaposhuhudia kundi la kwanza la wanafunzi 1,020 wa UDOM wakipatiwa shahada zao. Katika miaka mitatu tu ya uhai wake, Chuo kimedahili wanafunzi takribani 21,000 pamoja na hao watakaopata shahada zao kesho. Hongereni sana.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Kuwepo kwa UDOM kumekuwa chachu ya maendeleo kwa eneo la Chimwaga na kwa mji wetu wa Dodoma. Chimwaga na Dodoma ya leo siyo ile ya miaka mitatu iliyopita. Sote ni mashahidi wa mabadiliko makubwa na yanayoendelea kutokea ambayo yasingekuwapo kama Chuo Kikuu cha Dodoma kisingekuwepo. Mwenye macho haambiwi tazama! Tutegemee mambo mazuri zaidi miaka ijayo.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Tunaingia gharama kubwa ya kuwekeza katika ujenzi wa shule na vyuo vye elimu ya juu nchini kwa sababu ya manufaa tunayoyapata kutokana na uwekezaji huo. Taifa ambalo watu wake wameelimika lina uhakika zaidi wa kujiletea maendeleo kuliko lile ambalo watu wake hawana elimu. Huu ndiyo ukweli kuhusu tofauti za maendeleo kati ya nchi maskini na nchi tajiri dunuani. Katika nchi zilizoendelea watu wake wameelimika zaidi kuliko katika nchi maskini. Nidyo maana Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa "ukitaka kumkomboa maskini, mpe elimu mtoto wake"

Hivyo basi, p
amoja na umaskini wetu na changamoto nyingi zinazotukabili tutahakikisha kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma na vyuo vyetu vikuu vingine vinakua, vinastawi na kufikia upeo wa juu kitaaluma. Tunataka viwe vitovu vya elimu bora utafiti na ubunifu utakaochochea kasi ya maendeleo nchini.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Kama nilivyosema katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge la Kumi, sisi serikalini tutaendelea kupanua na kuboresha elimu ya juu kupitia Mpango wetu wa Maendeleeo ya Elimu ya Juu (MMEJU). Nilisema kwamba katika miaka mitano ijayo, tutakamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma na kuanza mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere huko Butiama, Musoma.

Tutajenga makazi mapya kwa ajili ya Chuo Kikuu cha Udaktari cha Muhimbili yatakayokuwa Mloganzila nje kidogo ya jiji la Dar-es-Salaam. Hapo tutapanua Chuo hicho na kuongeza udahili wa wanafunzi wa kusomea udaktari. Vile vile, nilisema kuwa tutaendeleza mchakato wa kuipandisha hadhi Taasisi ya Teknolojia ya Mbeya kuwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia. Aidha, nilielezea haja ya kutengeneza mpango wa muda wa kati na muda mrefu wa ujenzi wa vyuo vikuu nchini ambapo kila kanda itakuwa na Chuo Kikuu cha Serikali. Mimi naamini tukiamua hivyo na kujipanga vizuri tutaweza.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Napenda pia kutoa wito kwa wenzetu wa sekta binafsi nao kupanua vyuo vikuu walivyo navyo sasa na kujenga vipya. Wamefanya kazi nzuri ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika eneo hili lakini bado mahitaji ni makubwa kuliko uwezo uliopo sasa. Tuuongeze uwezo huo. Sisi katika Serikali tutaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji wa sekta binafsi katika elimu ya juu. Pia, tutaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu binafsi kama tufanyavyo sasa. Ombi langu kwao wasipandishe sana ada kwani watawakwaza wazazi na wanafunzi kwa kile kiasi ambacho itawabidi walipe wenyewe zaidi ya mkopo unaotolewa na Serikali.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Kuhusu mikopo ya elimu ya juu napenda kuwahakikishia wazazi na wanafunzi kuwa tutaendelea kuongeza fedha katika mfuko huo ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike. Tumefanya hivyo katika miaka mitano iliyopita na tutafanya hivyo siku za usoni. Serikali iliongeza fedha za mikopo kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka2005/06 hadi kuwa shilingi 237 bilioni mwaka 2010/11 na wanafunzi waliopatiwa mikopo hiyo wameongezeka kuotka 16,345 hadi 69,921. Haya ni mafanikio makubwa na naahidi kuwa tutafanya vizuri zaidi ili tuwafikie wanafunzi wengi zaidi. Pia tutautazama upya mfumo mzima wa utoaji wa mikopo ikiwepo na utendaji kazi wa Bodi ya Mikopo kwa nia ya kuuboresha na kuleta ufanisi zaidi. Mawazo ya wadau wakiwemo wamiliki wa vyuo, wahadhiri na wanafunzi yatasaidia sana. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itatoa maelekezo mahsusi wakati zoezi hilo litakapofanyika.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Nimezungumza mengi, naomba nimalize kwa kusema kuwa uzinduzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ni mwanzo wa safari ndefu ya kukijenga na kifikia kile kiwango cha juu tunachokitarajia sote. Safari yo yote haikosi changamoto zake lakini napenda kuwahkikishia kuwa Serikali itafanya kila liwezekanalo kuzikabili changamoto zilizopo na zitakazojitokeza siku za usoni. Maombi yangu kwa uongozi wa jumuiya ya Chuo hiki ni kwanza, muitunze na kuitumia vizuri miundombinu hii ili idumu. Wahenga walisema "kitunze kikutunze". Pili, muongeze bidii na maarifa katika kutambua na kutafuta majawabu kwa vikwazo vinavyojitokeza. Yaliyo juu ya uwezo tupo tutasaidiana.

Kwa mara nyingine tena nakupongeza wewe Mkuu wa Chuo, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo na Menejimenti ya Chuo bila kusahamu Rais wa Serikali ya Wanafunzi na wanafunzi wote na jumuiya ya Chuo Kikuu kwa kazi nzuri mliyoifanya. Serikali itakuwa nanyi bega kwa bega kuhakikisha kuwa dhamira yetu ya kuwa na Chuo kikuu kikubwa kuliko vyote nchini na kinachotoa elimu ya ubora wa hali ya juu inatimia.

Baada ya kusema hayo; Ninayo heshima kubwa kutamka kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma Kimezinduliwa Rasmi.

Asanteni sana.
 
Elli

Elli

JF-Expert Member
Joined
Mar 17, 2008
Messages
29,407
Likes
14,655
Points
280
Elli

Elli

JF-Expert Member
Joined Mar 17, 2008
29,407 14,655 280
Ni sasa hivi au ilikua mchana??? mbona kama vile ilikua mchana flani ivi? haya asante
 
jyfranca

jyfranca

JF-Expert Member
Joined
Oct 3, 2010
Messages
299
Likes
2
Points
0
jyfranca

jyfranca

JF-Expert Member
Joined Oct 3, 2010
299 2 0
Naomba aeleze jinsi wanafunzi wa UDOM wamekosa kuelimika ni mbumbumbu wa siasa
 
M

Maamuma

JF-Expert Member
Joined
Dec 22, 2008
Messages
856
Likes
27
Points
45
M

Maamuma

JF-Expert Member
Joined Dec 22, 2008
856 27 45
Ni sasa hivi au ilikua mchana??? mbona kama vile ilikua mchana flani ivi? haya asante
Ndiyo, ilikuwa mchana. Hata hivyo tunashukuru kwa Invii kutubandikia hapa ili tuweze kuisoma kwa utulivu na kui-"punctuate".
 
Mzalendo80

Mzalendo80

JF-Expert Member
Joined
Oct 30, 2010
Messages
2,481
Likes
416
Points
180
Mzalendo80

Mzalendo80

JF-Expert Member
Joined Oct 30, 2010
2,481 416 180
Anazindua chuo wakati Shele za msingi wanamaliza bila ya kujua kusoma na kuandika, Kweli vichekesho:teeth:
 
Elli

Elli

JF-Expert Member
Joined
Mar 17, 2008
Messages
29,407
Likes
14,655
Points
280
Elli

Elli

JF-Expert Member
Joined Mar 17, 2008
29,407 14,655 280
Nilisikiliza weeee, nikaishia usingizini nakuota naangukiwa na gorofa, kuamka nikakumbuka jinsi haya magorofa yalivyojengwa fasta bila kuachwa muda wa kukauka na ku-stablize!! maskini wee!!!
 
Gosbertgoodluck

Gosbertgoodluck

JF-Expert Member
Joined
Mar 3, 2008
Messages
2,865
Likes
32
Points
0
Gosbertgoodluck

Gosbertgoodluck

JF-Expert Member
Joined Mar 3, 2008
2,865 32 0
Chuo kinachopokea wahitimu wa shule za sekondari za kata. Tunaongeza idadi ya wanafunzi bila kujali ubora wa elimu inayotolewa.
 
BIN BOR

BIN BOR

JF-Expert Member
Joined
Nov 23, 2010
Messages
853
Likes
74
Points
45
BIN BOR

BIN BOR

JF-Expert Member
Joined Nov 23, 2010
853 74 45
one more university to build in Musoma if am not mistaken.
 
suamakona

suamakona

Member
Joined
Oct 31, 2010
Messages
13
Likes
1
Points
0
suamakona

suamakona

Member
Joined Oct 31, 2010
13 1 0
Hizo ni fikra zako wewe ambaye unahisi umeelimika pasipokujua kuelimika ni nini.
 
Mwifwa

Mwifwa

JF-Expert Member
Joined
Apr 3, 2017
Messages
29,058
Likes
75,270
Points
280
Age
18
Mwifwa

Mwifwa

JF-Expert Member
Joined Apr 3, 2017
29,058 75,270 280
Nilisikiliza weeee, nikaishia usingizini nakuota naangukiwa na gorofa, kuamka nikakumbuka jinsi haya magorofa yalivyojengwa fasta bila kuachwa muda wa kukauka na ku-stablize!! maskini wee!!!
Aisee
 

Forum statistics

Threads 1,236,214
Members 475,029
Posts 29,250,026