Uzi maalumu wa wachimbaji wadogo wadogo

Kasomeko

JF-Expert Member
Feb 10, 2018
441
743
Natumai mko poa.

Uzi huu itapendeza ukiwa maalumu kwa watu wote wanaojihusisha na uchimbaji mdogo mdogo wa madini ya aina mbali mbali. Lengo kuu likiwa ni kupeana taarifa mbali mbali zinazohusiana na uchimbaji. Mfano, sehemu zinazotoa madini kwa wingi/kiasi kwa muda (uliopo) huu. Kuelekezana, kukumbushana mambo yaliyotokea, yanayotokea na yatakayotokea huko migodini kwetu. Kupeana misemo na story zinazojiri migodini.

Nitaelezea misemo na majina ya vifaa vitumiavyo na wachimbaji wadogo wadogo hasa wa dhahabu huku kanda ya ziwa.

KUHIRA, ni neno au msema unaotumiwa na wachimbaji wadogo wadogo kumaanisha kwamba mgodi flani unatoa sana madini (dhahabu) kwa wakati huo. Kwahiyo ukisikia 'matabe pana hira' au lusahunga panahira wewe jua kua hilo eneo tajwa linatapika madini hivyo fanya kuwahi huko ukachimbe, ukafanye biashara kama za migahawa, baa/bup, saluni zote, gest za tents ama mahema au za mabati full juu hadi chini, mashine za kufua nguo, etc

DUARA. Ni shimo refu /refusana kwenda chini ambamo wachimbaji huingia kuchimba ili kutoa madini. Linaitwa duara hata kama ni la pembekumi sie tunaita duara hata sijui kwanini.

KUGOROGOSHA. Hua nalipenda hili neno japo ni la hatari. Lina maana ya kuteleza na kuangukia ndani ya shimo (duarani). Huenda ukawa unapita bahati mbaya ukatelezeamo au ulikua ndani ya duara na wakati unapanda ngazi ili utoke nje, ghafla unateleza na kurudi chini kwa spidi kubwa huku ukijibamiza kwenye kuta za duara. Sasa ule mlio wa goro goro papa kiki etc wakati unaporomoka kwenda chini ndio ukazaa msamiati wa KUGOROGOSHA.

KUJOGOMEJA. Huu ni msamiati wetu wachimbaji wenye maana kadhaa, kwanza kabisa unatumika kuashiria tendo la kuchimba bila kusawazisha, yaani mtu anachimba kaeneo kadogo, kafinyeee kwa kwenda mbele. Hii hua inatokea pale watu wanapokua wanafata sehemu iliyo na madini (mkanda). Kama umeona hapa kuna dhahabu ebana unapiga aaaa unajogomeja hapohapo kwenda mbele sio unaanza kupanulia unampanulia nani sasa? Jogomeja fasta usepe iingie shift mpya.

Maana ya pili ya kujogomeja, ni pale mtu / mchimbaji anapotumia moko (kifaa maarufu na namba1 cha kuchimba) kumchoma mwenzie. Ukisikia mtu anakwambia aseee NITAKUJOGOMEJAAA kaa mbali maana mda si mrefu atakutoboa uso kwa kutumia moko yake.

Maana ya tatu ya neno kujogomejaa, wewe mdada ukisikia njemba inakwambia nataka nikakujogomeje, jua limekuelewa sasa linataka mkapafomu hahahahaaa

SHIFUTI/SHIFT. Kama ulizani jamaa wachimbaji hawajui English unajidanganya. Neno shift lina maanisha zamu ya kuingia duarani kupiga kazi. Ukisikia tunaingia shift jua mnaingia kazini mda huo. Shift moja huenda ikawa ya masaa, siku, wiki au hata zaidi ya wiki. Ni kazi mfululizo, mfano shift moja mpo watu kumi, watatu wakilala basi wale saba mlobaki ni kupiga kazi hasa hadi mda mlopeana ukiisha mnawaamsha hao watatu, wanalala tena watatu.... Ukisikia mtu anasema tumetoka shift, muombe ya bia kabisaaa maana hua ni kutoka na hela tu.

MTONYO. Watu wakipata madini wanauza wanapata pesa. Sasa mtonyo ni ile hela ambayo mchimbaji atakupa wewe kama ya soda vile bia etc. Huo ndio mtonyo. Kuna baadhi ya wachimbaji wamewekeana hadi asilimia kabisaaa kua ukipata laki moja basi elfu20 jua sio yako bali ni ya wenzako utawapa mtonyo wakazimue huko baaaar. Wachimbaji wengi nikiwemo Mimi sio wachoyo wa kutoa mtonyo hata kama alichopata ni kidogo. Mtonyo unatufanya tulindane, Leo nimepata Mimi nakupa mtonyo unapata ya tumizi nyumbani kwako. Kesho namimi nakua nimechacha wewe ukapata basi nawe utanipa mtonyo nipate ya mboga kwangu. Dhahabu ni kubahatisha.

FONKA. Ni kona na njia zilizopo chini ndani ya duara. Yaani wachimbaji wataanza kwa kuchimba kama kisima tu ila wakishafika kwenye mwamba wa dhahabu hua wanaanza kuchimba horizontally nakujikuta wametengeneza njia ndefu za chini kwa chini mnaweza kuweka hata mkokoteni huko ukawasaidia kubebea mawe yenu.

STENDI. Duara baadhi hua ni ndefu sana sana kiasi kwamba huwezi kushuka chini ama kupanda juu bila kupumzika. Sehemu tunapopumzika ndio tunaita stendi.

MAIMUNA. Ni upepo (kimbunga) ambacho hua kinapita mala moja moja migodini kutuonyesha mkanda au eneo ambamo dhahabu zinapitia. Kikivuma kimbuga tu utasikia miruzi na shangwe watu wakimshangilia jini wetu maimuna. Na anamopita ndo tunahamia humohumo.

MATIMBA. Ni magogo ambayo hua yanafungwa kiaina ndani ya duara ili kushikilia kuta za duara zisije kuanguka na kufunima watu humo ndani.

KUNYORONYOMBA. Ni kuiba. Na wezi wanaitwa wanyoronyombi au wanyori.

CHABO. Ni kitendo cha kuchukua sample ya mchanga wa madini na kwenda kuupima kama una madini kweli au laa.

KUGOBOJA. Ni pale mchimbaji anapoona dhahabu kwa macho yake mwenyewe awapo duarani. Akiiona anaificha na akishafanikiwa kutoka nayo duarani bila wenzake kujua, hiyo inakua yake kabisaaa hagawani na mtu. Iko hivi mnapokua mnachimba hua ni nadra sana kuiona dhahabu maana nyingi hua ni ndogo ndogo hivyo inahitaji process kadhaa ili kuziona. Sasa zipo za wastani na kubwa ambazo unaweza kuziona kwa macho bila process ya ziada, siku ukiiona ficha kabisaaa ukifanikiwa tu kutoka nayo ndani hiyo ishakua yako hata kama wenzio wataiona hawawezi kutaka mgao maana kugoboja ni utaratibu unajulikana.

Wengine mtaongezea asee, pia ningependa wachimbaji wa madini tofauti na dhahabu waje watupe maujuzi yao mfano tanzanite inachimbwaje hadi kuipata a-z, copper, aluminium etc

Picha namba moja ni moko (hizo zenye mipini)

Namba mbili ni ponchi inayopigiliwa kwenye mwamba ili kuulainisha kisha moko inakuja kumalizia. Ponchi inapigiliwa kwenye mwamba kwa kutumia nyundo kubwa ya kilo5
IMG_20190531_101837.jpeg
IMG_20190531_100042.jpeg
 
Mkuu hongera sana kwa kuleta hii threads naamini hapa tutajifunza mengi ya kutosha.

Yule jamaa aliyepiga billion 3 ama kweli kanishawishi kweli kweli. Nimejikuta nikipenda hii kazi. Japo najua si lelema wala mdobwedo ila wanaume tumezaliwa kupambana.
 
Back
Top Bottom