Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Nilishiriki katika uzinduzi wa kampeni za Urais wa Zanzibar. Zilifana sana. Niliamini kuwa Maalim Seif atashinda Uchaguzi huo na kuwa Rais wa Zanzibar.
Nilihutubia mkutano huo na kuwaeleza Wazanzibari kuwa Mzigo mzito hupewa Mnyamwezi. Niliwaambia kuwa Urais ulikuwa ni mzigo mzito na mwenye kuweza kuumudu ni Mnyamwezi huyu aliyekuwa mbele yao. Mkutano wote ulianguka kicheko.

Kama alivyonieleza Maalim Seif, CUF ilikuwa kweli haijajiandaa kuweka Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hatukuwa na magari wala nyezo nyingine za kampeni.
Senti kidogo niliyokuwa nayo – kiasi cha dola za Marekani elfu sita - nilizitumia kwenye shughuli za kampeni za awali.
 
Pia niliagiza akiba yangu iliyokuwa inafikia dola elfu thelathini za Marekani iletwe kusaidia kampeni ya Mgombea Urais.
Katibu Mkuu, Marehemu Shaaban Khamis Mloo, ndiye alikuwa Meneja wa Kampeni ya Rais. Alishauri na nikakubali kuwa tuanzie kampeni zetu mikoa ya Kusini ya Mtwara na Lindi.
Hoja yake ilijikita kwenye ukweli kwamba mikoa hiyo ilikuwa imetelekezwa kwa muda mrefu na Serikali ya CCM. Tulitumia gari za kukodi kwenda kuzindua kampeni Mtwara.
 
Mikutano yetu ya kampeni katika hiyo mikoa ya Mtwara na Lindi ilifana sana. Watu wengi walihamasika na hoja zangu za kujenga uchumi shirikishi.
Nilifafanua kauli mbiu ya ‘Haki Sawa kwa Wote’ kuwa ni pamoja na haki za kiuchumi, haki za kisiasa na haki za kijamii.
Vijana wa Profesa Malima walihangaika kuhakikisha tunazunguka nchi nzima kufanya kampeni. Juma Kilaghai alikuwa Katibu wangu wakati wa Kampeni, japo kutokana na hali halisi tulikubaliana abakie Dar es Salaam kusukuma mambo pale ambapo kungekuwa na mkwamo wowote.
 
Nilipokosa gari ya Chama ya kusafiri toka Dar es Salaam kwenda Morogoro, Mzee Amin Mrisha alitoa gari yake ndogo aina ya Mercedes Benz. Hata hivyo tulipofika Dodoma tulikwama. Mercedes Benz haikuwa na uwezo wa kuhimili barabara za makorongo.
Katibu wangu, Juma Killaghai, alipigiwa simu kutoka Dodoma. Baada ya kupata simu aliwasiliana na wadau mbalimbali na harakati za kutafuta gari zikaanza mara moja zikiongozwa na yeye mwenyewe na mwanaharakati maarufu wa enzi zile, marehemu mzee Abdul Kileo.
Juhudi za kupata gari zilifanikiwa usiku wa manane. Mdau mmoja, ambaye hata hivyo sitamtaja jina kutokana na kutopata ridhaa yake, aliridhia kutoa gari lake jipya aina ya Toyota Hilux Double cabin, kuja kuungana na msafara wetu mjini Dodoma. Siku mbili baadaye mdau mwingine, ambaye pia sitamtaja jina, alituma gari lake jipya aina ya Musso kuja kujiunga na msafara wetu.
 
Katika Uchaguzi Mkuu wa 1995 uchaguzi wa Zanzibar ulipangwa kufanyika tarehe 22 Oktoba, ikiwa ni wiki moja kabla ya Uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano, uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 29 Oktoba. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilichelewa kutoa matokeo mpaka baada ya siku nne.
Baada ya kupata taarifa za matokeo ya uchaguzi kutoka kwa Mawakala, CUF tuliamini Mgombea wetu, Maalim Seif Sharif Hamad, alikuwa ameshinda. Aidha, kituo cha Televisheni cha Dar TV kilitangaza pia kuwa Maalim Seif alikuwa ameshinda.
Hata hivyo tarehe 26 Oktoba, Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilimtangaza Dr Salmin Amour kuwa mshindi. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar.
 
Kufuatia kupinduliwa huku kwa matokeo nilikwenda Zanzibar kubadilishana mawazo na Maalim Seif. Hoja yake ya msingi ilikuwa kwamba kama haki haikutendeka katika uchaguzi wa Zanzibar, tusitegemee Uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano kuwa huru na wa haki.
Kuonyesha kuchukizwa kwetu ni bora tutangaze kujitoa kwenye uchaguzi huo. Mimi nilikubaliana naye. Hata hivyo Mzee Shabani Khamis Mloo aliona ni muhimu tushiriki Uchaguzi huo kwa sababu itatusaidia kukijenga Chama, hasa baada ya kuona kampeni yetu imefanikiwa sana Tanzania Bara.
Baadhi ya Vyombo vya habari vilivyopata tetesi ya mjadala wetu vilitangaza kuwa CUF imejitoa kwenye uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano. Ninaamini kuwa taarifa hizo zilipunguza kwa kiasi fulani kura za Chama chetu.
 
Hata hivyo Uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano pia haukwenda vizuri. Uchaguzi wa majimbo ya Dar es Salaam ulifutwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikasema utarudiwa.
Msimamo wa Vyama vya siasa isipokuwa CCM ulikuwa kwamba uchaguzi nchi nzima umevurugika na ni muhimu urudiwe kote. Baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutokubaliana na madai ya Vyama, vyama viliamua kutoshiriki uchaguzi wa marudio wa Dar es salaam, na kutoa Tamko la kutotambua matokeo ya uchaguzi wa Rais.
Hata hivyo baadhi ya Wagombea Ubunge wa Vyama vya Upinzani walipewa fedha za kuwalipa Mawakala na Tume ya Uchaguzi, hivyo wakaamua kushiriki.
 
Baada ya Uchaguzi, Maalim Seif alisafiri nje ya nchi kwenda kuelezea namna demokrasia ilivyofinyangwa Zanzibar. Wanachama wa CUF na wananchi wa Pemba waliandaa Maandamano na Mkutano wa hadhara. Nilikaribishwa kuwa mgeni rasmi kwenye maandamano hayo.
Hotuba yangu iliilaumu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutotenda haki na kupora ushindi wa CUF.
Nilieleza kuwa wizi wa kura ni rushwa mbaya kuliko rushwa zote. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Zubeir Juma Mzee, alifungua kesi ya madai dhidi yangu kuwa nimemkashifu kuwa amepokea rushwa.
 
Mwaka 1996 baada ya kumaliza muhula wa mwisho wa Chuo Kikuu, nilienda New York kwenye Mkutano wa CDP. Baada ya hapo nilikaribishwa na Benki ya Dunia kwenda Makao Makuu ya Benki hiyo, Washington DC kutoa ushauri kuhusu maendeleo ya kiuchumi ya nchi za Kiafrika na hususan Tanzania. Nilikutana na Makamo wa Rais wa Benki ya Dunia wa Bara la Afrika, Bwana Callisto Madavo nikamueleza matatizo ya uchumi wa Tanzania na namna ya kuyashughulikia.
 
Baada ya kikao changu na Bwana Madavo, Washington DC, alikwenda kwenye Mkutano wa nchi huru za Kiafrika, Libreville, Gabon. Kwenye Mkutano huo Bwana Madavo alikutana na Rais Mkapa. Kwa nia njema alimueleza ‘rafiki’ yako Prof. Lipumba tunaye Washington DC anatushauri kuhusu maendeleo ya uchumi Afrika na hasa Tanzania.
 
Rais Mkapa alistuka kidogo. Watu wa usalama walitumwa kuuliza Chuo Kikuu Lipumba yuko wapi? Barua yangu niliyoombea ruhusa kusafiri nilieleza nilkuwa naenda New York kwenye Mkutano wa CDP.
Ilikuwaje sasa nilikwa Washington DC na sijarudi Dar es Salaam?
Kwa kawaida wakati wa likizo ndefu walimu wa Chuo Kikuu hatuna majukumu ya kufundisha.
 
Tunaposafiri tunaandika barua kukamilisha utaratibu. Kuwa kwangu Washington DC hakukuwa kunaathiri majukumu yangu ya Chuo Kikuu. Katika hali ya kushangaza niliandikiwa barua kuulizwa ni kwa nini siko Chuo Kikuu wakati wa likizo ndefu, na ni kwa nini nisichukuliwe hatua za nidhamu.
Niliporudi Dar es Salaam, mazingira ya chuoni hayakuwa mazuri. Muda mfupi baadaye nilifukuzwa kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa bahati Taasisi ya Utafiti wa Maendeleo ya Uchumi Duniani, Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa (UN-WIDER) kilichopo Helsinki, Finland kilinipa fursa ya kuwa Mtafiti Muandamizi.
 
Nikaenda kufanya kazi huko kwa miaka miwili. Nikiwa UN-WIDER nilifanya utafiti na wachumi wa nchi nyingi za kiafrika ikiwemo Uganda kuhusu sera za thamani ya sarafu na fedha. Nilikwenda Uganda kushaurina na wataalam wa uchumi kuhusu namna ya kurekebisha sera za fedha ili kukuza uchumi wa nchi za Kiafrika.

Mwaka 1997, wakati nikiwa Uganda ilinibidi niende Zanzibar kwenye kesi ya madai ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar dhidi yangu. Jaji alitoa hukumu kuwa nimlipe Zubeir Juma Mzee shilingi milioni 30. Mawakili wangu walikata rufaa na hatimaye Chama kilimlipa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar shilingi milioni 10.
 
Katika safari hiyo nilikutana na Maalim Seif akanipa taarifa ya juhudi zilizokuwa zinafanywa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Chief Anyauko kusuluhisha mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar
Nilirejea Dar es Salaam mwaka 1998. Nikiwa Tanzania niliendelea na shughuli za utafiti na ushauri wa mambo ya uchumi nje ya Tanzania. Hata hivyo sikupata fursa ya kufanya kazi za ushauri nchini Tanzania.
Viongozi Wakuu wa Chama - Mzee Musobi Mageni, Mwenyekiti wa Chama; Maalim Seif, Makamu Mwenyekiti; na Shaaban Khamis Mloo, Katibu Mkuu wa Chama waliniomba niwe Mshauri wa Chama. Hata hivyo hii haikuwa nafasi rasmi kwa sababu haikuwemo ndani ya Katiba ya Chama.
 
Wakati wa msiba wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Maalim aliniomba na nikakubali, nijumuike na viongozi wa CUF; mimi nikiwa mwanachama wa kawaida,kwenda kuupokea mwili wa Mwalimu.
Rais Mkapa alituona na kuonyesha ishara ya kushukuru kuwepo kwetu.
Makala inayofuata nitajadili kuchaguliwa kwangu kuwa Mwenyekiti wa Taifa na Maalim Seif kuwa Katibu Mkuu wa CUF na matokeo ya Uhaguzi wa mwaka 2000.
=======================
siasa ziliwafarakanisha malegendary wawili
1614266209426.png
 
Walimu wake wa Chuo Kikuu na hasa Prof. Goran Hyden (raia wa Sweden) na Marehemu Nathan Shamuyarila (Mzimbabwe aliyekuja kuwa Waziri wa Mambo ya Nje baada ya Uhuru wa Zimbabwe 1980) walijaribu sana kumshawishi Maalim abakie Chuo Kikuu kama Mkufunzi Msaidizi na hatimaye kuendelea na masomo ya juu, lakini alichagua kuitikia wito wa kurudi Zanzibar na kwenda kuwa Msaidizi wa Rais wa Zanzibar, Marehemu Aboud Jumbe.
Aisee
 
Back
Top Bottom