Uzembe wawaponza walimu wakuu Mwanza

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
WALIMU wakuu wa shule tatu za msingi za jijini Mwanza wamevuliwa nyadhifa hizo kutokana na kukiuka taratibu za usajili wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka huu.

Hatua hiyo ni moja ya mapendekezo yaliyotolewa na kikao cha kamati ya mkoa ya uteuzi wa kupitisha wanafunzi waliopendekezwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani ambapo kiliridhia kuvuliwa madaraka kwa walimu wakuu waliokiuka taratibu za usajili wa wanafunzi.

Katika mahojiano na gazeti hili jana, Ofisa Elimu Taaluma wa Jiji la Mwanza, Elizabeth Mlekwa alisema kati ya walimu hao, wawili ni wa wilaya ya Nyamagana na mmoja ni kutoka wilaya ya Ilemela.

Katika mtihani wa darasa la saba uliofanyika Septemba mwaka huu, dosari mbalimbali zilijitokeza ikiwa ni pamoja na baadhi ya walimu wakuu kutofautisha namba za watahiniwa hali iliyosababisha Ofisa Elimu wa wilaya husika kuhakiki usaili wa kwenye karatasi na kompyuta.

Aidha dosari nyingine kuwa ni pamoja na baadhi ya wasimamizi kutokuwa makini katika kufunga bahasha za kurudisha majibu ambapo wasimamizi hao hawatapewa tena kazi ya usimamizi wa mitihani.

Nyingine ni baadhi ya wasimamizi kutoingiza karatasi za majibu za watahiniwa ndani ya bahasha ya majibu ambapo nao watachukuliwa hatua ya kutopewa tena nafasi ya kusimamia mitihani.

Mlekwa alisema hatua hiyo pia itasaidia katika kuhakikisha walimu wakuu wanakuwa makini katika kukuza kiwango cha elimu kwenye shule zao.

Hata hivyo hakuwa tayari kuzitaja shule ambazo walimu wakuu wamevuliwa nyazifa hizo na nafasi hizo kupewa walimu wengine Hivi karibuni ofisa elimu mkoa wa Mwanza, Ramadhan Chomola akitangaza matokeo ya darasa la saba alisema, kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba mkoani hapa kimepanda kutoka asilimia 52 mwaka jana hadi kufikia asilimia 58.64 ambapo wanafunzi 52,447 kati ya 89,434 wamechaguliwa kujiunga na sekondari mbalimbali zikiwemo za watoto wenye vipaji maalumu.
 
Back
Top Bottom