Uzamiaji Afrika Kusini: Mikasa katika harakati za kuzamia Afrika Kusini kwa njia za panya

Sonship

Senior Member
Apr 13, 2021
147
215
SAFARI YA KUZAMIA AFRIKA YA KUSINI KWA NJIA ZA PANYA

Sehemu ya kwanza.


Utangulizi


Mimi ni mtanzania mzaliwa wa Mbeya. Kwa sasa umri wangu ni wa kutosha kidogo kwa sababu nipo duniani tangu miaka ya 1980.
Wakati nasoma shule ya msingi kwenye miaka ya 1990 hivi tulikuwa tunaimba nyimbo maarufu wakati huo za kupinga ubaguzi wa rangi uliokuwa unafanywa na serikali ya makabulu kule Afrika ya kusini. Tuliimba nyimbo hizo kwenye Mchakamchaka, mistarini (Assemble) na kwa kutumia kwaya ya shule.

Kwa kweli zile siku za madarasa ya mwanzo ya darasa la kwanza hadi la tatu sikuwa naelewa sababu za kuimba nyimbo zile ni nini na hata Afrika ya kusini yenyewe ni kitu gani. Nilipofika Darasa la nne nilikutana na rafiki yangu wa muda mrefu aliyeitwa Gilbert Simya na ambae kwa wakati ule alikuwa darasa la saba na alikuwa ndio mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa zaidi kitaaluma katika darasa lao.

Kwa kuwa nilikuwa namuamini sana kwa ujuvi wa mambo mbalimbali, niliamua kumuuliza ni kwanini tunaimba zile nyimbo za kupinga ubaguzi, ulioku- wa unaendelea nchini Afrika ya kusini na je Afrika kusini ni nchi gani? Ndugu Simya alinieleza sababu ya sisi kuimba zile nyimbo kwa kina sana na zaidi aliweza kunieleza kwa kina kwamba Afrika kusini ni nchi inayopatika eneo la kusini mwa bara la Afrika. Ili kunielewesha zaidi na vizuri alinionesha ramani ya Afrika kwenye eneo linaloonesha nchi ya Afrika ya kusini na kwa hakika nilimuelewa sana bwana Simya.

Jambo ambalo nalikumbuka sana katika yale mazungumzo yetu ni kwamba baada ya yale mazungumzo yetu nilianza kuipenda sana nchi ya Afrika kusini. Niliendelea kufuatilia habari za Afrika ya kusini kutoka kwa walimu na Redio ya Sauti ya Ujerumani (DW) na vyombo vya habari vya hapa nchini tangu wakati ule na hata baada ya uhuru wao mwaka 1994.

Nilipomaliza darasa la Saba tayari nilikuwa nimeshakata shauri kwamba lazima nitatafuta fedha ili niende Afrika ya kusini. Nilijiapiza kwamba siku nitakapo bahatika kwenda Afrika kusini nitakwenda kufanya kazi kabisa na ikiwezekana nitakaa moja kwa moja bila kurejea tena Tanzania. Hivyo, nikaanza kujiandaa kutimiza hiyo ndoto yangu ya Muda mrefu.

Katika kipindi chote ambacho nilikuwa nasoma sekondari, yaani miaka minne ya o-level, nilikuwa najiandaa kwa safari yangu kiujuvi, kirasilimali na kisaikolojia. Baada tu ya kumaliza kidato cha nne, mwaka 2003, kabla hata matokeo hayajatoka, niliamua kuanza safari yangu ya kwenda Afrika ya kusini na malengo yangu yalikuwa ni kufika katika jiji la Johannesburg.

Story hii inaeleza visa na mikasa ya safari za watu wanaojaribu kwenda Afrika ya kusini bila ya kufuata utaratibu, Kwa hiyo, utaweza kusoma safari zangu zote mbili ambazo nilizi- fanya kati ya mwaka 2004- 2006.

Naamini wasomaji wa stori hizi hasa watu ambao bado wana ndoto za kuzamia Afrika ya kusini watakuwa na jambo la kujifunza katika safari zao.

*************************​

Kuanza kwa Safari
Mwezi Januari mwaka, 2004 nilipanda gari aina ya Fuso kutoka katika mji mdogo wa Namanyere ambao ni makao makuu ya wilaya na Nkasi mkoani Rukwa hadi Sumbawanga mjini makao makuu ya mkoa wa Rukwa, kwa kuwa sikuwa na uwenyeji wowote wa mji huo nilipofika nilimta futa rafiki yangu ambae alikuwa anaitwa Edward mizimu. Lengo la kumtafuta bwana Edward ilikuwa ni kwa kuwa malengo yangu kwanza ilikuwa ni kusafiri hadi kufika hapo Sumbawanga hadi jijini Lusaka, mji mkuu wa Zambia, na baada ya hapo ndipo nikajipange kuitafuta Harare mji mkuu wa Zimbabwe.

Ndugu Edward alikuwa na ABC za namna ya kufika Lusaka kutokana na kufanya ziara chache kwenda kwa ndugu zake waliokuwa wanaishi huko Lusaka Zambia. Baada ya kukutana na ndugu Edward Mizimu, tulifanya mjadala wa kina sana, ambapo aliweza kunipa changamoto zinazo weza kuipata safari yangu, pia alinishangaa sana kuona naanza safari bila kuwa na nyaraka yoyote ya kusafiria alinishauri nizitafute lakini nikamwambia mimi malengo yangu nataka nikifika kule nisirejee nchini hivi karibuni sasa nikienda kihalali naweza kugundulika mapema.

Baada ya majadiliano marefu alinipa njia mbili ambazo naweza kuzitumia kusafiria ambapo alisema njia ya kwanza naweza nikapita njia ya Kasanga ambapo nitalazimika kwenda kupanda Meli ya Mv Liemba kutoka Kasanga hadi Mpulungu ambao ni mji wa bandari kwa Upande wa Zambia, katika Ziwa Tanganyika, aliniambia kwamba kwa kupitia njia hiyo kuna vikwanzo vingi vya wanausalama wa Zambia na ni ndefu sana. Baada ya maelezo ya njia hiyo alinieleza njia ya pili ambayo ilikuwa ni kupitia Tunduma-Nakonde.

Alisema njia hii unakwenda moja kwa moja Lusaka kwa barabara lakini changamoto yake ni kwamba ina vizuizi vingi vya barabarani vya Polisi na Uhamiaji, alisema ni njia ambayo ni ngumu sana kutoboa kama huna nyaraka za kusafiria. Baada ya maelezo ya bwana Edward ambayo yalikuwa yameambatana na vitisho na tahadhari nyingi bado sikukata tamaa, zaidi nilichukulia kama changamoto za kawaida katika safari. Nilifanya uchambuzi wa njia zote mbili na kisha niliamua kuchagua njia ya kupitia Tunduma-Nakonde.

Baada ya siku kama nne za kukaa pale sumbawanga mjini nikiwa napanga na kuchora ramani zangu vizuri, hatimae nilianza safari ya kuelekea Tunduma kwa njia ya Lori moja hivi nakumbuka lilikuwa Limeandikwa Nyuma Kanjiranji Trans. Tuliondoka Sumbawanga jioni ya Saa moja tukiwa mimi, Dereva na Makondakta wawili, Gari ilikuwa imesheheni mifugo aina ya Ngombe, kwa hivyo safari
ilikuwa inakwenda taratibu sana, Ilikuwa ni msimu wa mvua maeneo yale na barabara wakati ule ilkuwa haina lami kwa hivyo ilikuwa imeharibika sana. Tulitembea usiku kucha huku tunapiga stori za hapa na pale, kwa bahati mbaya tulipofika maeneo ya kijiji cha chiwanda Gari iliharibika rejeta.

Kutokana na mawasiliano ya wakati ule kuwa magumu pamoja na kwamba kuufikia mji wa Tunduma zilikuwa zimebaki kama Km 30 tu, tulijikuta tuna tumia siku nne pale kijijini. Ilibidi asubuhi kondakta mmoja aende Mbeya mjini kumchukua fundi wa Rejeta kisha wakaja kufungua rejeta wakaenda nayo kuchomelea Tunduma mjini ndipo siku ya tatu usiku wakarejea na hatimae siku ya nne ndipo tukaendelea na safari yetu. Siku zote hizo nne za mkasa wa gari kuharibika nilikuwa nimegeuka na kuwa mchunga ng’ombe.

Nakumbuka nilikuwa nachungia sehemu moja hivi ya pembeni ya kijiji cha Chiwanda ambayo iliitwa Ntachimba. Nilifanya kazi ile kwa moyo sana kutokana na utu wa wale jamaa wa gari ambao walinibeba bure na walikuwa wananinunulia chakula wakati wote wa safari, walikuwa ni watu wema sana, nakumbuka wakati tunaanza safari walikuwa wameniambia kwamba nitalipa nauli ya Tsh 5000 lakini baada ya changamoto za barabarani waliamua kunifanya sehemu ya safari yao hivyo sikulipia chochote.

Baada ya gari kupona tulipakia Ng’ombe na kuanza safari tena, ilikuwa kama saa 10 jioni hivi wakati tunaiacha Chiwanda. Haikuchukua muda mrefu Sana kwani baada ya Kama dk 50 hivi tulifika Tunduma katika eneo linaloitwa Mwaka. Wale jamaa walinijulisha kwamba natakiwa nishukie pale ili wao waendelee na safari ya kuelekea mbeya mjini.

Baada ya kushuka mwaka sikujua wapi nielekee kutokana na ugeni wangu, nilikuwa nimefanya kosa wale jamaa wa kwenye gari sikuwa nimewambia ukweli wa ugeni wangu kwenye ule mji wa kibiashara kwa hivyo kwa kiasi nilianza kupata wasiwasi kwamba sasa kama katika nchi yangu ambayo naelewa Lugha vizuri hali ipo hivyo, huko mbele ya safari mambo yatakuwaje, siyatanikuta makubwa, hata hivyo nilipiga moyo konde na kuendelea na kutokuruhusu roho wa uoga.

Nilikwenda kutafuta chumba cha kulala sehemu moja inaitwa mpakani, kisha nikapata chakula kwa mama ntilie ilikuwa kama saa moja hivi jioni, muda wote nilikuwa nafuatilia stori zinazohusu wazamiaji wa kuelekea Zambia kutoka kwa watu mbalimbali ili nijue namna ya kuvuka Boda ya Tanzania na Zambaia. Jioni hiyo sikufanikiwa kupata habari zozote za maana za hitaji langu. Kesho yake asubuhi niliamka muda wa kawaida kwa sababu sikupanga kuondoka siku hiyo.

Kitu nilicho kifanya siku hiyo ni pamoja na kutafuta habari za safari yangu kwa tahadhari ili nisije nikakamatwa mapema, bahati nzuri kwenye Nyumba ya wageni niliyofikia nilimuona kijana mmoja hivi mcheshi mwenye umri wa rika langu, nikajitahidi kujenga urafiki nae kwa muda mfupi kisha baada ya kumuamini na kupima uelewa wake niliamua kumshirikisha mpango wangu, akaniambia unaweza kufanikiwa lakini kuna vikwazo vingi japo huwa kuna watu wengi tu wanafanikiwa harakati zao za kuzamia Bondeni kwa mzee
Madiba. Kwa hiyo, alinishauri mambo mawili, la kwanza akasema kwamba nibadilishe fedha zangu kutoka shillingi kuwa Z-Kwacha na US-Dollar.

Na la pili nisipandie gari stendi ya hapo boda, bali nivuke boda kwa miguu kisha nikapandie gari mbele ya safari ili niweze kukwepa kizuizi cha mapema cha polisi ambacho kipo nje kidogo mji wa Nakonde upande wa Zambia. Alisema ukikwepa hiyo ‘road block’ utakuwa umefanikiwa kuingia Kilomita nyingi sana ndani ya Zambia. Alinisaidia kubadilisha hela zangu kiasi cha Tsh 370,000 kuwa Z-kwacha na US-dollar na kisha baada ya zoezi hilo aliniambia kwamba ataniunganisha na mjomba yake ambae hufanya biashara za kuvusha sukari ya magendo na mafuta ya petrol upande wa Zambia ili aniombee lifty kwenye gari yake atakapo kuwa anakwenda kwenye madili yake.

Siku hiyo hiyo majira ya mchana yule bwana alinipeleka kwa mjomba yake huyo ambae alikuwa anaishi upande wa Zambia kwenye mji wa Nakonde, baada ya kufika nilimueleza shida yangu na bahati nzuri yule uncle alikuwa hana shida yoyote, akanikubalia akaniambia nitatakiwa niondoke nae siku hiyo hiyo saa 4 usiku na atakwenda kuniacha sehemu moja hivi inaitwa Isoka umbali wa Km 84 kutoka Nakonde, kisha akanishauri kwamba kwa kuwa wewe ni baharia yaani mzamiaji, itabidi usiku huo huo utafute usafiri wa Lori uondoke ili uweze kusogea mbele zaidi ndani ya Zambia ili angalau ufike hata Isoka umbali wa Kama Km 146.8.

Muda wa kuondoka ulipofika tulipakia mafuta ya petroli kwenye gari ndogo aina ya Toyota peak up ambayo yalikuwa yanavushwa upande wa zambia ili wakati wa kurudi warejee na sukari. Baada ya kumaliza kupakia mida ya Saa nne na nusu usiku tuliondoka kwa babarabara kuu iendayo Lusaka na tulipo tembea umbali wa kama Km 5 tu hivi, tulikuta Road Block ya askari polisi wa Zambia. Kutokana na umaarufu wa uncle Chilo tulivuka bila shida, kisha tukatembea Km 10 nyingine tukakutana na Gari aina ya Toyota Land Cruiser, ikatupita kimashamasha sana lakini kwa kasi sana.

Uncle Chilo akasema itakuwa ni watu wa ZRA (Mamlaka ya mapato ya zambia) au Migration wapo kwenye patro, akasema kwa anavyowafahamu kutokana na uzoefu wake kwenye hiyo barabara, lazima watarudi kwa hivyo akazima taa za gari na kisha akaliingiza kwenye kinjia cha porini umbali wa kama Km 1 hivi.

Baada ya muda wa kama dakika 10 hivi ile gari tuliyopishana nayo ilirudi ikiwa kwenye mwendo wa kawaida uncle Chilo akatukumbusha yale maneno yakeya kwamba alisema watarudi, basi tukakaa pale porini kama dk 30 tukaondoka. Wenyeji wangu walisema kwa huo muda hawawezi kurudi tena.

Tulirudi barabarani kisha muda mfupi tu, baada ya kurejea barabarani tukaona gari inakuja mbele yetu, wote kwenye gari tulitulia kimya kila mtu akiwa na wasiwasi sana huku akisubiri kitakachotokea!

Itaendelea...
 
Hongera sana Mkuu! Jitahidi sana story Imalizike, kumekua na utoto mwingi sana humu Wa kukatiza story, yaani waleta story wanalewa sifa na wingi wa wafuatiliaji hivyo pozi zinaanza sasa wewe epuka hilo, najua wewe unakaribia kua mtu wa makamo hivyo hutokua kama hawa watoto waliozaliwa kipindi cha Jakaya! Kila la kheri!
 
Nyie watu mnaotoa story kuhusu maisha yenu huko south Africa ni wa ajabu sn,mwanzo mnaanza vizuri sn unakuta episode ya Kwanza Hadi ya 10 unatiririka safi sn, sasa Uzi ukishaanza kuwa na traffic jam mnaanza kuringa. Sijui mnatuchukuliaje asee.

Ni heri tu mkae na Stori zeni msizilete huku.
 
Back
Top Bottom