SoC02 Uzalendo hauji kwa kufundishwa ama kulazimishwa, bali ni matokeo ya Wananchi kuridhishwa na namna nchi inavyoendeshwa

Stories of Change - 2022 Competition

Stephen Ngalya Chelu

JF-Expert Member
Oct 31, 2017
7,621
16,373
Utangulizi
Uzalendo ni hali ya mtu kulipenda na kulitumikia taifa lake kwa moyo wa dhati. Uzalendo ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote kwa kuwa ndicho kichocheo cha ndani kabisa kwa mwananchi mmoja mmoja kulijenga na kulipigania taifa lake katika nyakati ngumu na nzuri. Hivyo, ni vigumu kwa taifa lenye wananchi na viongozi wasio wazalendo kusonga mbele kimaendeleo.

Kumekuwa na mijadala katika maeneo tofauti tofauti ambapo watu wamekuwa wakionyesha kutokuridhishwa na kiwango cha uzalendo wa watanzania, hivyo kuhimiza juhudi za haraka zifanyike ili kuchochea uzalendo kwa watanzania.

Viashiria vya kukosekana kwa uzalendo katika taifa
Kabla ya kuchambua ni njia zipi zinaweza kusaidia kufanya watanzania na wananchi wa taifa lolote lile kuwa wazalendo, kwanza tuone ni mambo gani ambayo yanaashiria kukosekana kwa uzalendo ndani ya nchi.

Rushwa na ubadhilifu wa mali za umma; Wananchi na viongozi wasio na uzalendo ni watu wasio na moyo wa dhati wa kulitumikia na kulipigania taifa lao. Hii hupelekea wao kutumia nafasi zao, mali za umma na rasilimali za taifa kwa manufaa yao binafsi, hali ambayo huchangia kudumaza maendeleo ya nchi husika.

Kuzorota kwa uwajibikaji; Uzalendo unahusisha wananchi na viongozi, kila mmoja kwa nafasi yake, kujitoa kwa ajili ya maslahi ya taifa. Taifa yenye wananchi na viongozi wasio wazalendo huwa ni taifa la watu wasiotimiza majukumu yao ambapo kila mtu husubiri kubembelezwa au kusukumwa kufanya mambo ambayo kimsingi ni majukumu yake.

Kukithiri kwa vitendo ya kihalifu; Katika taifa lolote lile, matendo ya kihalifu ni ngumu kuyazuia yasitokee kabisa. Lakini viwango vya matukio ya kihalifu kukithiri ni moja ya kiashiria cha wananchi kutokuwa wazalendo. Wananchi wenye uzalendo hushiriki katika shughuli zinazolinufaisha taifa lao na si kufanya vitendo vya kihalifu ambavyo huchangia kurudisha nyuma maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Matukio haya ya uhalifu yanaweza kusababishwa na mifumo mibovu ya kiutawala ambayo hufanya wananchi wengi kukosa fursa nzuri ya kujiendeleza kiuchumi kwa njia halali hivyo baadhi yao kuamua kujiingiza katika vitendo vya kihalifu kama uporaji wa kutumia silaha nk.

Kuzaliwa kwa makundi ya uasi; Wananchi wasio na moyo wa uzalendo huiona nchi yao na viongozi wao kama maadui. Matokeo yake huamua kuungana wao wenyewe au kutumika na watu wa mataifa mengine ili kuendesha matendo ya uasi dhidi ya nchi yao wenyewe.

Lakini pia, viongozi wasio wazalendo wanaweza kuchochea kuundwa kwa makundi ya uasi yenye nia ya kulikomboa taifa kutoka kwenye makucha ya watawala hao wanaoweka mbele maslahi yao binasfi na kuyapuuza maslahi ya taifa.


Nini kifanyike ili kufanya wananchi wawe wazalendo?

Ni wazi kuwa sote tutakubaliana kwamba baadhi ya viashiria vya kukosekana uzalendo vilivyoorodheshwa hapo juu vinaonekana pia kwenye nchi yetu. Hiyo ni ishara ya wazi kuwa hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kufanya watanzania wawe wazalendo ili kuchochea maendeleo ya taifa letu.

Watu wamekuwa watoa maoni mbalimnali juu ya kipi hasa kinapaswa kufanyika ili watanzania waongeze uzalendo wao kwa taifa. Moja kati ya mawazo hayo ni kuwa, kunapaswa kuanzishwa somo maalum la uzalendo kuanzia ngazi ya elimu ya msingi ili watoto wajifunze kuwa wazalendo tangu wakiwa wadogo.

Linawezekana likawa ni wazo linalofaa kwa kiasi fulani lakini lisiwe na nguvu katika mazingira halisia. Hii ni kwa sababu uzalendo siyo taaluma, bali ni hisia zinazotokana na kuridhishwa na namna nchi inavyoendeshwa.
Hivyo basi, mbali na kufikiria kuanzisha somo la uzalendo mashuleni kuna baadhi ya mambo ya msingi yanapaswa kufanyika ili kuhakikisha watanzania wanakuwa wazalendo wa kweli kwa taifa lao.

Kuimarisha misingi ya upatikanaji haki; Haki huleta usawa katika jamii na kuwafanya watu wote kujihisi ni wamoja hivyo kufanya wananchi wajisikie fahari ndani ya nchi yao. Hivyo basi, kunatakiwa kujengwa misingi imara kwenye vyombo vinavyosimamia upatikanaji wa haki ili kuimarisha moyo wa kizalendo kwa wananchi.

Uwepo wa fursa sawa za kiuchumi na kijamii kwa kila mwananchi; Viashiria vyovyote vya upendeleo katika utoaji wa fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii husababisha mpasuko katika taifa kwani wale ambao hunyimwa fursa hizo kuhisi kutengwa na taifa lao, hali inayopelekea wao kukosa moyo wa kulitumikia taifa kwa nguvu zote. Hivyo basi, serikali inapaswa kuhakikisha kuwa inatoa fursa sawa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote ili kufanya kila mwananchi kunufaika na fursa zilizopo. Hatua hiyo itaongeza ari kwa wananchi kulipenda na kulitumikia taifa kwa moyo wote.

Kupunguza tofauti kati ya wenye nacho na wasio nacho; Uzalendo ni pamoja wananchi wa madaraja yote kujihisi ni wamoja. Jambo hili litawezekana kwa kupunguza utofauti kati ya wenye nacho na wasio nacho kwa kuweka mifumo ambayo itafanya makundi haya mawili kushirikiana kwa maslahi mapana ya taifa. Hili linaweza kufanyika kwa kujenga mfumo utakaoimarisha sekta binafsi ili ziweze kukua na kutoa ajira na huduma bora kwa wananchi, jambo ambalo lichochea ustawi wa jamii yote kwa ujumla.

Ushirikishwaji wa wananchi katika mipango ya maendeleo; Wananchi kujisikia fahari juu ya taifa lao wakiona wao ni sehemu ya mabadiliko chanya yanayotokea katika jamii. Hivyo basi, ili kujenga uzalendo, wananchi wanapaswa kushirikishwa katika hatua zote muhumu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo. Hili linapaswa kufanyika kwa; kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili na pia kuwapa fursa ya kutoa maoni juu ya mambo mbalimbali yahusuyo maendeleo.

Matumizi mazuri ya rasilimali; Raslimali za taifa ni moja ya mtaji muhimu katika kuleta maendeleo kwa taifa lolote. Matumizi mazuri ya raslimali za nchi humnufaisha kila mwananchi pasipo kujali hali yake ya kiuchumi na kijamii. Hali hii huchochea ari ya wananchi kuipenda na kuitumikia nchi yao. Hivyo, serikali inapaswa kuhakikisha kuwa raslimali za taifa zinatumika vyema kwa ajili ya maendeleo ya taifa na si kwa manufaa ya watu wachache.

Kuheshimu misingi ya utawala bora; Mfumo mzuri wa kiulawala unaozingatia sheria ni chachu nyingine ya kuchochea uzalendo wa wananchi kwa taifa lao. Kuheshimu misingi ya kidemokrasia na utawala wa sheria utatengeneza utangamano wa kitaifa hivyo kufanya wananchi kuwa wazalendo.

Hitimisho
Uzalendo ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya taifa lolote lile. Hata hivyo, uzalendo siyo taaluma ya kujifunza darasani, bali ni matokeo ya wananchi kuridhishwa na namna nchi inavyoendeshwa. Hivyo natoa wito kwa serikali na wananchi wote, kila mmoja kwa nafasi yake, tuyafanyie kazi mapendekezo yaliyoorodheshwa hapo juu ili tupate kujenga taifa lenye wananchi wanye uzalendo wa kweli kwa ajili ya maendeleo endelevu ya taifa letu.​
 
Andiko lenye ukweli mwingi na inaonekana tumo kwenye mzunguko ambao hautupi matokeo chanya,ni kama CD 💿 always itaendelea kurudia nyimbo zile zile zilizorekodiwa,Taifa linahitaji tuanze upya ili tukate mzunguko huu,Maradhi, Umasikini, Ujinga pamoja na cousin wao Rushwa bado wametamalaki mno nchini, katiba mpya ni muhimu ili tupate taasisi imara za kutuendeleza mbele, wenzetu wanakimbia mno na Zambia 🇿🇲 (wamefanya mabadiliko less than 2yrs ago)leo wanazalisha umeme mwingi na wanategemea kuuza SA means ZESCO wataingiza usd kwenye kit yao!,Botswana pia wamezalisha umeme mwingi wa kusukuma maendeleo yao na sasa wataweza kuuza extra nje,sisi Tanesco yetu hadi leo imeshindwa kabisa kuitoshekeza nchi kwenye nishati hii(wazo langu ni kuifanya Tanesco iwe msambazaji tu sio manufacture wa nishati hii)
 
Andiko lenye ukweli mwingi na inaonekana tumo kwenye mzunguko ambao hautupi matokeo chanya,ni kama CD 💿 always itaendelea kurudia nyimbo zile zile zilizorekodiwa,Taifa linahitaji tuanze upya ili tukate mzunguko huu,Maradhi, Umasikini, Ujinga pamoja na cousin wao Rushwa bado wametamalaki mno nchini, katiba mpya ni muhimu ili tupate taasisi imara za kutuendeleza mbele, wenzetu wanakimbia mno na Zambia 🇿🇲 (wamefanya mabadiliko less than 2yrs ago)leo wanazalisha umeme mwingi na wanategemea kuuza SA means ZESCO wataingiza usd kwenye kit yao!,Botswana pia wamezalisha umeme mwingi wa kusukuma maendeleo yao na sasa wataweza kuuza extra nje,sisi Tanesco yetu hadi leo imeshindwa kabisa kuitoshekeza nchi kwenye nishati hii(wazo langu ni kuifanya Tanesco iwe msambazaji tu sio manufacture wa nishati hii)
Umenena vyema mkuu.
 
Umezungumzia mapendkezo mengi lakini ujaelezea mbinu zitakazo tumika kuwashawishi kufanisha hilo suala ?
 
Umezungumzia mapendkezo mengi lakini ujaelezea mbinu zitakazo tumika kuwashawishi kufanisha hilo suala ?
Sijui unajaribu kumaanisha nini hasa unaposema 'kuwashawishi', lakini sidhani kama tunahitaji kiwashawishi watu ili watekeleze majukumu yao kwa maslahi mapana ya taifa. Wanapaswa kuwajibika.
 
Asante sana, nimeona hapo umezungumzia miongoni mwa kukosekana kwa uzalendo wa nchi ni kusababisha makundi ya uasi. Nika kuuliza je, serikali yetu siyo wazalendo umenijibu "ndiyo". kwakuwa umekubali kuwa serikali yetu siyo wazalendo. Sasa nikuulize Je, kwenye taifa letu kuna makundi ya uasi ?
Hapana.
 
Nimeona hapo kwenye makala yako kuna kipengele cha kukithili kwa uhalifu ukatwambia kuna sababishwa na kutokuwa wazalendo na nchi yetu. Kwani nikija kukukaba hapa sasa hivi nitakuwa siyo mazalendo wa nchi yangu ?
Ndiyo.

Uzalendo una maana ya kulipenda taifa lako na kulitumikia kwa manufaa. Taifa ni mjumuiko wa vitu vyote vinavyopatikana ndani ya mipaka ya kijografia ya taifa. Hapa tunazungumzia vitu kama; rasilimali, miundombinu, raia, sheria nk. Kwa hiyo ili mtu atambulike kama mzalendo anatakiwa kuchangamana na vitu tajwa hapo juu katika namna ambayo italeta manufaa chanja kwa taifa.

Kwa hiyo ukinikaba; kwanza utakuwa umevunja sheria. Mzalendo hapaswi kuvunja sheria za nchi yake mwenyewe.

Pili, mzalendo anatakiwa kutoa machanho chanya kwa raia wenzake, wewe kunikaba utakuwa umesababisha mchango hasi kwa kuniathiri kiuchumi na pengine kiafya pia.
 
Ndiyo.

Uzalendo una maana ya kulipenda taifa lako na kulitumikia kwa manufaa. Taifa ni mjumuiko wa vitu vyote vinavyopatikana ndani ya mipaka ya kijografia ya taifa. Hapa tunazungumzia vitu kama; rasilimali, miundombinu, raia, sheria nk. Kwa hiyo ili mtu atambulike kama mzalendo anatakiwa kuchangamana na vitu tajwa hapo juu katika namna ambayo italeta manufaa chanja kwa taifa.

Kwa hiyo ukinikaba; kwanza utakuwa umevunja sheria. Pili, mzalendo anatakiwa kutoa machanho chanya kwa raia wenzake, wewe kunikaba utakuwa umesababisha mchango hasi kwa kuniathiri kiuchumi na pengine kiafya pia.
Hapo umesema "uzalendo ni kulipenda taifa lako" nika kuuliza nikija kukukaba nitakuwa siyo mzalendo ukanijibu " ndiyo". Kwahiyo nikikukaba kwa sababu tu, umenikanyaga kidole nakuwa silipendi taifa langu ?
 
Hapo umesema "uzalendo ni kulipenda taifa lako" nika kuuliza nikija kukukaba nitakuwa siyo mzalendo ukanijibu " ndiyo". Kwahiyo nikikukaba kwa sababu tu, umenikanyaga kidole nakuwa silipendi taifa langu ?
Labda sikuelewa nini ulimaanisha uliposema 'kukaba', nilijua unamaanisha kama vibaka wafanyavyo.

Ili kufanya mambo yawe marahisi, kitendo chochote kinachohusisha uvunjivu wa sheria, kuwatendea vibaya raia, matumizi mabaya ya raslimali na miundombinu, ni matokeo ya kukosa uzalendo.
 
Labda sikuelewa nini ulimaanisha uliposema 'kukaba', nilijua unamaanisha kama vibaka wafanyavyo.

Ili kufanya mambo yawe marahisi, kitendo chochote kinachohusisha uvunjivu wa sheria, kuwatendea vibaya raia, matumizi mabaya ya raslimali na miundombinu, ni matokeo ya kukosa uzalendo.
Kwahiyo serikali na wananchi ni wazalendo au siyo wazalendo ?
 
Nimekubaliana an mtoa mada militia headline pekee, bila hata ya kupitia hoja yake.....!
 
Back
Top Bottom