Uwekezaji wa moja kwa moja kutoka China barani Afrika, umekuwa ni sehemu ya mtindo mpya ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na nchi za Afrika, ambao tangu mwaka 2000 umekuwa ukiongezeka kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 25 kwa mwaka, na kupungua kiasi kutokana na changamoto za janga la UVIKO na msukosuko wa uchumi duniani. Hata hivyo makampuni mengi ya Kichina, hasa makampuni madogo na yenye ukubwa wa kati (SMEs) yamekuwa sehemu muhimu ya uchumi wa baadhi ya nchi za Afrika.
Wizara ya Biashara ya China (MOFCOM) ilitoa takwimu zinazoonesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2020, thamani ya uwekezaji wa moja kwa moja wa China barani Afrika ulikuwa dola bilioni 47.35. Kwenye uwekezaji huo, mchango wa makampuni binafsi ya China ulikuwa ni asilimia 70, na theluthi moja ya makampuni binafsi, yanajihusisha na viwanda na mengine ni biashara ndogo ndogo. Licha ya kuboreka kwa mazingira ya uwekezaji katika nchi mbalimbali za Afrika, sababu nyingine iliyovutia makampuni hayo ni matumaini ya kuokoa gharama za forodha na usafirishaji. Matokeo ya hatua hiyo, sio tu yamekuwa chanya kwa wawekezaji, bali pia kwa serikali na wenyeji.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa Kampuni ya McKinsey, makampuni ya China barani Afrika huajiri wenyeji kwa kiwango cha asilimia 89. Makampuni hayo pia yameongeza kwa kiasi kikubwa nafasi za ajira na viwango vya mapato ya wenyeji. Mfano mzuri ni wa wafanyakazi wa viwanda vya nguo wa Ethiopia, ambao mishahara yao ni takriban asilimia 50 zaidi kuliko wenzao wa Ethiopia.
Mbali na kuongeza nafasi za ajira na mapato kwa wenyeji, makampuni ya China yamekuwa ni kichocheo chanya kwa maendeleo ya sekta mbalimbali katika maeneo waliyowekeza barani Afrika. Watu wanaofanya kazi kwenye makampuni hayo wananufaika na teknolojia, ujuzi, na mambo mengine wanayojifunza au kulazimika kuwa nayo wanapokuwa wafanyakazi kwenye viwanda vilivyowekezwa na China.
Makampuni binafsi ya China yanazidi kuwekeza katika nchi mbalimbali za Afrika, hasa nchi ambazo zina matarajio mazuri ya ukuaji. Kenya ambayo ina mwelekeo mzuri wa ukuaji ni nyumbani kwa kampuni 396 za China, huku asilimia 80 zikiwa za kampuni binafsi, na asilimia 44 kati ya hizo ziko kwenye sekta ya viwanda. Mkurugenzwa benki ya maendeleo ya Afrika Bw. Akinwumi Adesina, amesema makampuni binafsi ya China yamekuwa na mchango mkubwa katika kuhamisha baadhi ya mistari ya uzalishaji barani Afrika, na kuchochea ukuaji wa minyororo ya viwanda na kusaidia kuongezeka kwa idadi ya makampuni kutoka nje.
Jambo lingine muhimu lililoletwa na makampuni ya China barani Afrika ni ushindani, ambao umekuwa na athari chanya kwa bara la Afrika. Kama ilivyo katika sehemu mbalimbali duniani, ushindani huyalazimisha makampuni kushusha gharama za bidhaa au huduma zake na kuhakikisha ubora wa bidhaa. Wafanyabiashara kutoka maeneo mengine nje ya Afrika ambao hapo awali walichukulia Afrika kama himaya yao, sasa wanakumbana na ushindani mkali ambao unawalazimisha kuendana na mahitaji ya soko.
Eneo moja ambalo sasa limekuwa ni gumzo kwenye sekta ya teknolojia ni simu za mkononi. Zamani simu za mkononi zilikuwa ghali na za kiwango cha chini, lakini kutokana na uwekezaji wa makampuni ya China barani Afrika, simu hizo sasa zinatengenezwa barani Afrika zikiwa na ubora wa juu na gharama nafuu. Maendeleo kama hayo pia yanaonekana katika sekta nyingine.