SoC01 Uwekezaji mpya kwa ukusanyaji wa kodi halali kwa ustawi wa uchumi wa taifa

Stories of Change - 2021 Competition

Mtelengu

New Member
Jul 14, 2021
4
6
Chapisho hili limegawanyika katika sehemu kuu nne;
1. Utangulizi
2. Mapendekezo
3. Hitimisho

UTANGULIZI
Serikali kupitia wizara ya fedha ina jukumu kubwa la kuhakikisha pato la Taifa linaongezeka kwa kuzingatia sheria katika ukusanyaji mapato na kudhibiti matumizi ya serikali. Serikali kupitia wizara ya fedha nchini hufanya majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi ili kutekeleza sera za umma za maendeleo, Dira ya Taifa ya maendeleo 2025, malengo ya milenia (MDGs), MKUKUTA na mikakati mingine ili kufikia malengo mkuu ya kiuchumi na utoaji wa huduma kwa raia.

Sera za maendeleo umma zimegawanyika katika makundi makuu matatu, ambayo ni kama zifuatazo;

Sera ya uwekezaji (Redistribute public policy). Hii ni sera ambayo Serikali inatumia fedha kutoka katika makusanyo ya Kodi na miradi mingine kisha kufanya uwekezaji kwa lengo kuu kuwa itakusanya na kurudisha mapato ya Taifa kutoka kwa watumiaji wa miradi iliyoanzishwa kwa kulipa Kodi halali na malipo ya huduma, mfano serikali inafanya uwekezaji katika sekta ya Afya, nishati, usafirishaji, Viwanda na sekta zingine ili raia wanapokua wakitumia huduma hizi watalipa Kodi na malipo ya huduma kama ilivyo kwenye sekta ya Afya, nishati, maji wananchi wanalipa ada ya huduma (service fee) na sio kuweka Tozo.

Sera ya utoaji huduma bure kwa makundi maalum (Distributive Policy). Hii Ni sera ambayo Serikali inatumia rasilimali zilizopo kutoa huduma bure kwa makundi maalum bila kutegemea kukusanya chochote kutoka kwenye makundi hayo ikiwemo wazee, watoto, wajawazito, watu wenye mtahitaji maalum (walemavu).

Sera ya udhibiti (Regulatory Policy). Katika sera hii serikali hutumia faini na adhabu ili kudhibiti tabia fulani, hizo faini pia huwa ni moja ya chanzo cha mapato. Mfano faini za adhabu wanazotozwa Makampuni na asasi mbalimbali zilizokuwa zikikwepa kulipa Kodi japo katika hili Serikali ilipatapa malalamiko mengi kuwa inabambikizia faini za adhabu kwa Makampuni, asasi na wafanyabiashara binafsi katika suala la ukwepaji Kodi.

Tathimini ya mwenendo, mafanikio ya mipango na Sera za maendeleo ya Taifa.
Kwa mujibu wa muhtasari wa mfumo wa sera za jumla za uchumi na maendeleo ya jamii katika kipindi cha mwaka 2011/12 - 2015/16, iliyotolewa na wizara ya fedha mei, 2011.
Muhtasari huo ulitoa taarifa ya mapato ya mapitio ya mwenendo wa uchumi katika kipindi cha mwaka 2010 kwenye nyanja zifuatazo:
• Ukuaji wa pato la Taifa
• Mwenendo wa bei
• Mapato na matumizi ya serikali
• Deni la Taifa
• Maboresho ya sekta ya fedha
• Ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda
• Uendelezaji wa sekta binafsi
• Tathimini ya Dira na mpango wa maendeleo wa muda wa kati na mrefu
• MKUKUTA na malengo ya maendeleo ya milenia (MDGs)
• Utafiti wa Afya na Demografia 2010 - TADHS.
Tathimini hii ilionyesha kuwa bado kuna changamoto nyingi na mapungufu katika maeneo haya muhimu ya uchumi wa Taifa. Wizara ikaamua kuweka nguzo kuu nne ili kutatua changamoto na mapungufu yaliyoonekana katika nyanja hizi. Nguzo hizo ni kama zifuatazo;

1.Kuendeleza utengamavu wa uchumi Jumla. Katika nguzo hii serikali iliimarisha viashiria vya uchumi Jumla kwa kuimarisha sera ya mapato na matumizi ya serikali, kudhibiti mfumuko wa bei, kuweka viwango sahihi vya ujazi wa fedha vinavyowiana na kasi ya ukuaji wa pato la Taifa na upandaji wa bei, kuimarisha usimamizi wa benki na mfumo wa malipo nchini. Vile vile utawala bora kuimarishwa katika sekta zote ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika ngazi zote. Sambamba na hili serikali iliendeleza mafanikio yaliyopatikana katika huduma za jamii na msukumo utakuwa katika kuongeza ubora wa elimu, huduma za afya, maji na ustawi wa jamii katika ngazi zote.

2. Kutumia fursa za kijiografia . Mwelekeo wa mpango ni kutumia kimkakati fursa ya kupakana na bahari ya Hindi na maziwa pamoja na nchi zilizoifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji katika nchi za ukanda wa maziwa makuu. Hivyo msukumo ulielekezwa katika kuboreshwa (kukarabati na kujenga) Miundombinu ya bandari, reli, nishati, barabara na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma hizo na zile za mamlaka ya mapato.

3. Kutumia fursa za rasilimali zilizopo katika kukuza uchumi. Eneo la msisitizo hapa liliwekwa kwenye kufanya mapinduzi ya kijani ili Tanzania ijitosheleze kwa chakula na kuuza ziada nje.

4. Kuboresha na kukuza matumizi ya TEKNOHAMA . Katika nguzo hii mpango na msukumo uliwekwa katika kuboresha teknolojia ili kusaidia katika kuongeza thamani na tija hususani katika viwanda, madini, usindikaji wa mazao ya kilimo na matumizi ya TEKNOHAMA katika kuboresha huduma kama vile “e-government”. Maeneo mengine yaliyopewa msisitizo ni katika kuongeza kiwango na ubora wa elimu hasa ya sayansi na ufundi stadi.

Serikali ya awamu iliyopita ilifanikiwa kwa kuwango fulani kuongeza na kuimarisha uchumi wa Taifa kwa sababu ilijitahidi kutumia nguzo hizi nne muhimu na sera za kiuchumi ( udhibiti, uwekezaji na huduma kwa jamii), hasa katika sera ya udhibiti (Regulatory Policy) serikali ilihakikisha mamlaka za mapato zinakusanya Kodi halali kwa usahihi na kuwabana waliothubutu kukwepa Kodi na kutorosha rasilimali za taifa kama madini na wanyamapoli, Vile vile kwenye sera ya uwekezaji (Redistribute Policy) Serikali ya awamu iliyopita iliweka msukumo na mikakati madhubuti katika kufanya uwekezaji.

Lakini Serikali ya awamu iliyopo madalakani imepungukiwa ubunifu katika kuongeza pato na uchumi wa Taifa, mwisho imekuja na mambo ambayo yanawaweka raia wake katika utata na kupandisha gharama za maisha kwa kuongeza mambo yafuatayo;
• kuweka Tozo katika huduma za miamala ya kifedha
• kuongeza Kodi
• kushindwa kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa na mengine mengi kwa kisingizio cha kukusanya fedha zitakazotumika kuboresha huduma za jamii.

MAPENDEKEZO
1. Kuboresha ushirikishwaji wa mamlaka ya serikali za mitaa. Serikali inatakiwa kuboresha mamlaka hii maana ndiyo mamlaka inayoweza kujua vipaumbele vya wananchi kuliko wambunge ambao wamekuwa bendera fuata upepo kwa sababu wakifika bungeni wanasahau kuwa wametumwa na wananchi badala yake wanafanya waliyotumwa na vyama vyao wamesahau kuwa ni wawakilishi wa wananchi.
Pia mamlaka za serikali za mitaa zilishirikishwe katika utungwaji wa sera za maendeleo maana hizi mamlaka zina mchango mkubwa sana katika utekelezaji wa sera za maendeleo, kuacha kushirikishwa kwa mamlaka hizi hufanya serikali kufanya maamuzi bila kuzingatia na kujua vipaumbele na mahitaji ya raia wake jambo ambalo huwafanya raia waingie kwenye utata na serikali yao mfano mkuu wa Wilaya wa sasa wa Temeke alivyogundua kuwa watumishi wa serikali za mitaa ngazi ya walikuwa hawashirikishwi katika maamuzi mengi ya maendeleo na kusababisha udumavu wa kiuchumi katika Wilaya.

2. Kuendeleza na kufanya matumizi sahihi ya rasilimali watu. Serikali ili kufikia malengo makuu ya kiuchumi inatakiwa pia kutengeneza mazingira rafiki kwa wataalam na watumishi katika sekta zote kwa kuzingatia mishahara yao, mazingira ya kazi, nyumba na makazi yao ili kupunguza tatizo la rushwa na itaongeza hamasa na ubunifu kazini, lakini serikali imeshindwa kutumia vizuri rasilimali watu kwa mfano serikali imeshindwa kutumia wataalam wabobevu katika fani zao wamejaa mtaani baada ya kuhitimu masomo yao imeamua kuwarudisha kazini watu wenye vyetu feki, kilichotakiwa kufanyika ni kuwapatia sitahiki zao(mafao) sio kuwarudisha kazini wakati tuna akiba kubwa ya rasilimali watu.

3. Maendeleo ya sayansi, teknolojia na matumizi ya TEKNOHAMA. Pia serikali kama inataka tuendelee katika kada ya teknolojia na matumizi ya TEKNOHAMA ambayo kwa karne ya sasa ndiyo chachu kubwa ya maendeleo duniani. Matumizi ya TEKNOHAMA yawekwe kwenye mifumo yetu ya elimu ya msingi ili watoto wafundishwe kuanzia elimu ya msingi.

4. Kwa kutumia Sera ya uwekezaji (Redistribute Policy) serikali inatakiwa kuongeza ubunifu wa kufanya uwekezaji na Maboresho katika sekta zifuatazo ili badaye wakusanye Kodi halali na kukuza pato la Taifa sio kuwa wabunifu wa kuongeza Kodi na Tozo zinazoumiza wananchi;
• Sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi. Msukumo na mikakati madhubuti iwekwe ili kukuza na kuboresha uzalishaji katika sekta hizi ambazo wakati mwingine zinaitwa sekta zisizo rasmi wakati zinachangia kwa asilimi kubwa katika pato la Taifa. Serikali iweke Miundombinu bora kuanzia kwenye uzalishaji, masoko, miundombinu ya usafirishaji na kuimarisha usimamizi.
Pia ipeleke wataalam wabobevu katika fani za kilimo, mifugo na uvuvi ili wakawasaidie wazalishaji kwa kuwapa elimu ya kuongeza uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao yao, sio kupeleka watumishi watakaoenda kuwa kero tena kwa wahusika na kushusha uzalishaji.

• Sekta ya viwanda. Serikali iwekeze katika sekta hii kwa kuanzisha na kuboresha viwanda, sio lazima kuanza na viwanda vikubwa vya uzalishaji inaweza kuanza na viwanda vidogo vya usindikaji wa mazao yanayopatikana katika kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuongeza thamani ya mazao yetu hata tunapouza nchi tuuze kwa thamani itayoinua uchumi wa raia mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

• Sekta ya Nishati na madini. Katika sekta hii serikali ina jukumu kubwa la kuimarisha usimamizi wa sekta hii maana ni sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa lakini inashindwa kuchangia maendeleo kwa kiwango sahihi hii inaonyesha usimamizi na sera zake zifanyiwe marekebisho na kuimarishwa zaidi.

• Sekta ya elimu. Hapa serikali inajitahidi kuboresha mfumo wa kuwasaidia Watanzania kugharamia elimu ya juu na kutoa elimu ya msingi bila ada.
Lakini ubunifu zaidi unahitajika katika kuwafanya uwekezaji katika sekta hii mfano kama wameweza kumkopesha mtu zaidi ya milioni 9 ili apate maarifa wanashindwa nini kumkopesha akiwa tayari amehitimu masomo yake na ana maarifa ya kutosha kufanya uzalishaji ili aweze kurudisha mkopo wa elimu na huo mkopo wa baada ya kuhitimu.

Iundwe bodi ambayo itahusika na mikopo kwa wanafunzi wanaohitimu vyuo vya kati na vikuu kama ilivyo bodi ya mikopo ya elimu ya juu(Heslb).
Bodi hiyo itamtaka mwanafunzi anaehitimu au waungane kwa idadi itakayoelekezwa (mfano 10) na kuandika pendekezo la biashara (business proposal or paper work) na kulituma kwenye kwenye hii bodi.
Bodi hii itafanya kazi ya kuyachambua na kufanya tathimini kuwa ni pendekezo lipi linafaa kupewa mkopo na kwa kiwango gani maana sio mapendekezo yote yatakuwa na vigezo vya kupata mkopo hivyo itasaidia mikopo ya elimu ya juu kuanza kurejeshwa kwa wakati na itapunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa wahitimu wa vyuo. Mfano kila mwaka wanahitimu wataalam wengi kwenye kada za biashara, kilimo na ufugaji, viwanda, madaktari ambao wakiwezeshwa ni rahisi kabisa kuendelea na kuwaajiri wengine.
Serikali ikifanya hivi hata inapokuwa ikisema vijana wajiajiri tutaielewa kidogo maana serikali inaendelea kukumbatia ardhi na mashamba yenye rutuba wakati kuna vijana wengi wamehitimu na wanaendelea kuhitimu vyuo katika kada ya kilimo, ufugaji kwanini wasipewe ili kuendeleza mashamba hayo.

• Pia serikali ifanye uwekezaji na ubunifu zaidi katika sekta zingine kama Afya, ardhi, maji, Uendelezaji wa miundombinu ya usafirishaji n.k.

HITIMISHO
Matunda mazuri ya Tozo na Kodi kubwa sio uhalali wa kuendelea kuumiza wananchi wajifunze kwa awamu za Mzee JK (aliweza kulipa hadi wafanyakazi hewa bila tozo za ajabu kwa raia) na hayati JPM aliwezaje kufanya hayo aliyoyafanya bila tozo za ajabu (history is a fairly Judge)

Viongozi wa serikali ya awamu hii wanatakiwa kuwa wabunifu katika kufanya uwekezaji ili badaye wakusanye Kodi halali na kukuza pato la Taifa sio kuwa wabunifu katika kuumiza wananchi kwa kupandisha Kodi na kuweka Tozo zisizo na maana.
(history is a fairly Judge).
 
Back
Top Bottom