Uwaziri wanukia kwa Nahodha, Meghji


Bujibuji

Bujibuji

JF-Expert Member
Joined
Feb 4, 2009
Messages
42,412
Likes
38,591
Points
280
Bujibuji

Bujibuji

JF-Expert Member
Joined Feb 4, 2009
42,412 38,591 280
RAIS Jakaya Kikwete, amefanya uteuzi wa wabunge watatu akiwemo aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa zamani wa Fedha, Zakia Meghji, hali inayoashiria kuwa huenda akawateua kwenye nafasi za uwaziri.

Mbali na kuwa Waziri Kiongozi wa SMZ kwa miaka 10 ya uongozi wa Rais wa Sita wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Nahodha, alikuwa mmoja wa waliojitokeza kutaka kuteuliwa kuwania urais wa visiwa hivyo kupitia CCM.

Hata hivyo, Dk Ali Mohameid Shein aliteuliwa kuwania kiti hicho na kisha kuchaguliwa kuwa rais wa saba wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31.

Mbali na kuwahi kuwa Waziri wa kwanza wa Fedha mwanamke nchini, Meghji aliwahi pia kuwa Waziri wa Afya katika Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Benjamin Mkapa.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 66 (1)(e) kama ilivyorekebishwa, Rais amepewa mamlaka ya kuteua wabunge 10. Katika uteuzi wa jana wa tatu aliyeteuliwa ni Profesa Makame Mnyaa Mbarawa.

"Rais Jakaya Kikwete, amefanya uteuzi wa wabunge watatu kwa mujibu wa Ibara ya 66(1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyorekebishwa na kupewa mamlaka ya kuteua wabunge 10," ilieleza sehemu ya taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu mjini Dodoma jana ilisema kuwa tayari Rais Kikwete amewasilisha majina hayo matatu kwa spika wa Bunge, Anne Makinda, kwa hatua zinazozofuata ikiwa ni pamoja na kuapishwa.

Tayari wachambuzi wa mambo wamehusisha uteuzi huo wa Nahodha, Meghji na Profesa Mbarawa na uteuzi wa Baraza la Mawaziri wakieleza kuwa haitakuwa jambo la ajabu kwa wateule hao kuingia katika baraza hilo jipya la mawaziri litalatotangazwa hivi kribuni na Rais Kikwete.

Hata hivyo, Kikwete amefanya uteuzi huo huku kukiwa na kundi kubwa la mawaziri walioanguka katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM pamoja na walioanguka katika Uchaguzi Mkuu, wote wakisubiri huruma yake kuteuliwa katika nafasi hizo kumi.

Hali hiyo inaelezwa kuanza kupunguza matumaini kwa vigogo hao walioongoza wizara za serikali ya kwanza ya wamu ya nne ya Kikwete hadi ilipomaliza muda wake.

Wamo mawaziri kamili watano na manaibu wanne ambapo wawili kati yao walishindwa kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM huku wengine saba kimbunga cha Uchaguzi Mkuu kikiwakumba walipopambana na wagombea wa vyama vya upinzani.

Kimbunga hicho cha Uchaguzi Mkuu kilimkumba Dk Batilda Burian, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) ambaye alipigwa kumbo na kuachwa mbali na mgombea wa Chadema kwenye Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema.

Mwingine ni Lawrence Masha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani yeye alishindwa kutetea kiti chake mkoani Mwanza katika Jimbo la Nyamagana alipoangushwa na mgombea wa Chadema, Ezekiel Wenje.

Katika kundi hilo yumo mwanasiasa mkongwe Philip Marmo aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Mbulu mkoani Manyara na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), ambaye naye aliangushwa na mgombea wa Chadema.

Shamsa Mwangunga, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Diodorus Kamara aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na mbunge wa Jimbo la Nkenge pia ni miongoni mwa mawaziri walioanguka wakisubiri kukumbukwa na Rais Kikwete.

Kwa upande wa manaibu walioanguka katika uchaguzi huo ni Mwantunu Mahiza ambaye alikuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Aisha Kigoda, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Joel Bendera ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk James Wanyancha ambaye alikuwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Wakuu wa mikoa ni Mohamed Abdul Azizi (Tanga) ambaye alishindwa kutetea jimbo lake la Lindi Mjini pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Monica Mbega aliyeangushwa na mgombea wa Chadema kwenye Jimbo la Iringa Mjini.

Uchaguzi wa safari hii pia uliwatupilia mbali mawaziri wa zamani ambao Rais Kikwete angeweza kuwafikiria baada ya anguko hilo la mawaziri tisa. Miongoni mwa mawaziri hao wa zamani ni Getrude Mongela, ambaye aliwahi kuwa waziri kwenye wizara tatu na ambaye ameshika nafasi mbalimbali kwenye anga za kimataifa. Alishindwa kwenye Jimbo la Ukerewe na mgombea kutoka Chadema.

Wengine ni Anthony Diallo (Biashara na Viwanda), Kilontsi Mporogomyi (Naibu, Afya na Ustawi wa Jamii), Lucas Siame (Naibu, Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu), Zanir Karamagi (Waziri, Nishati na Madini), Ibrahim Msabaha (Waziri, Ushirikiano wa Afrika Mashariki), James Msekela (Mkuu wa Mkoa).

Kwa mujibu wa Katiba, rais ana madaraka ya kuteua wabunge kumi kutoka chama chake cha siasa au upinzani, kulingana na mikakati yake ya kufanikisha sera na mipango ya kuharakisha maendeleo ya nchi.
Wachambuzi wa mambo wanasema uzoefu wa marais waliopita unaonyesha kwamba hakuna aliyetumia kikamilifu madaraka yake kwa kujaza nafasi zote kumi.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Rais Kikwete aliteua wabunge saba na tena nafasi moja ya mwisho aliijaza katika miezi ya lala salama kabla ya kumaliza kipindi hicho.

Wakati huo huo, Dk Harrison Mwakyembe, Samuel Sitta, Profesa Anna Tibaijuka na January Makamba, ambao walioapishwa wiki iliyopita ni miongoni mwa wabunge wanaopewa nafasi kubwa ya kuwa kwenye baraza jipya la mawaziri ambalo litatangazwa wiki hii au ijayo.


SORCE:- MWANANCHI
 

Forum statistics

Threads 1,237,915
Members 475,774
Posts 29,306,068