Uwazi katika Utendaji wa Serikali: Nyenzo Muhimu ya Ufuatiliaji wa Rasilimali za Umma na Mapambano dhidi ya Rushwa

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,799
Uwazi katika Utendaji wa Serikali.jpg


Katika miaka ya hivi karibuni nchi nyingi zimeendelea kutambua umuhimu wa uwazi wa serikali katika kuimarisha demokrasia, kukabiliana na rushwa na kukuza maendeleo.

Uwazi wa serikali kimsingi ni wajibu wa serikali kuwa wazi, kuwajibika, na kuwa ya kuaminika kwa raia wake. Uaminifu huu unahusisha uwazi kuhusu namna serikali inavyoendesha shughuli zake na namna inavyotumia kodi za wananchi kuboresha maisha yao.

Iwapo wananchi hawajui jinsi maamuzi yanavyofanywa, jinsi kodi inavyotumika au ni nani anayewajibika ndani ya serikali, wananchi hawawezi kuhakikisha kuwa serikali zinafanya kazi kwa manufaa yao.

Wananchi hulipa kodi zinazowezesha mipango na huduma za serikali. Lakini, ikiwa hawaoni pesa zao zinakwenda wapi, watajuaje kama wananufaika au wanadhulumiwa?

Uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji ni muhimu ili kuhakikisha kuwa rasilimali za umma zinatumika ipasavyo na sera zinaundwa kwa maslahi ya watu na serikali zinafanya kazi kwa uadilifu. Juhudi kubwa inahitajika ili kukuza uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji katika serikali.

Serikali zikiwa wazi wananchi wanahakikishiwa mazingira wezeshi ya ushiriki. Ushiriki wa wananchi katika sera na michakato mbalimbali ina maana kwamba wananchi wanaweza kuwajibisha mamlaka zao, kukemea matukio ya ubadhirifu na kuwaadhibu viongozi waliochaguliwa – yote hayo ni muhimu katika kupambana na ufisadi na rushwa. Ufisadi huharibu kabisa misingi ya ustawi wa binadamu.

Vyombo vya habari vina jukumu kubwa katika kufikisha taarifa kati ya serikali na umma. Kuingilia kati vyombo vya habari kunaweza kuzuia uhuru wa kujieleza unaotolewa na demokrasia. Hatua hizi zinaweza kuhesabiwa kuwa kukosekana kwa uwazi, jambo ambalo linaweza kuchochea rushwa na kukosekana kwa uwajibikaji. Ufisadi/rushwa ni njia mojawapo ya kuonesha kiwango cha uwazi na uwajibikaji wa serikali.

Kwa mujibu wa Corruption Perceptions Index (CPI) ya mwaka 2021, inayotolewa na taasisi ya Transparency International, ni kuwa licha ya ahadi kwenye karatasi nchi 131 hazijapiga hatua kubwa dhidi ya rushwa/ufisadi katika muongo uliopita. Theluthi mbili ya nchi ziko chini ya alama 50, jambo linaloashiria kuwa na matatizo makubwa ya rushwa, huku nchi 27 zikiwa katika alama za chini zaidi kuwahi kutokea.

Vyanzo vya data vilivyotumika kuunda CPI huzingatia masuala kama vile uwepo wa hongo, utoroshaji wa fedha za umma; viongozi kutumia ofisi zao za umma kujinufaisha binafsi bila kukabiliwa na madhara; uwezo wa serikali kudhibiti ufisadi katika sekta ya umma; ukandamizaji uliokithiri katika sekta ya umma ambao unaweza kuongeza mianya ya rushwa; uteuzi wa upendeleo katika utumishi wa umma; sheria zinazohakikisha kwamba maafisa wa umma lazima waweke wazi fedha zao na migongano ya kimaslahi inayoweza kutokea; ulinzi wa kisheria kwa watu wanaoripoti kesi za hongo na ufisadi; upatikanaji wa taarifa za mambo ya umma/shughuli za serikali n.k

Mambo yote haya yanaweza kutokea tu pale ambapo mamlaka hazitaonesha utayari wa kuweka bayana masuala yanayoihusu serikali na watu wake.

Kwa hali ya Tanzania, kuanzia mwaka 2016 – 2021 ripoti hiyo imeonesha kuwepo na mabadiliko yanayoridhisha ambapo kwa mwaka 2016 ilipata alama 32/100; 36/100 (2017); 36/100 (2018); 37/100 (2019); 38/100 (2020) na kwa mwaka wa 2021 ikipata alama 39/100.

Hali ya Rushwa Tanzania 2016 2021.png

Alama za Mtazamo wa Rushwa nchini Tanzania kuanzia mwaka 2012 hadi 2021. CPI imerekodi mabadiliko chanya Tanzania tangu 2016, ingawa ni miongoni mwa nchi ambazo zipo chini ya alama 50, jambo linaloashiria kuwepo matatizo makubwa ya rushwa.

Katika miaka hiyo, nchi ambayo imefanya vizuri duniani ni Denmark ambayo katika suala la “usafi dhidi ya rushwa”, kwa mwaka 2012 ilishika nafasi ya kwanza kati ya nchi 176 ikiwa na alama 90/100, ambapo iliendelea kuongoza kwa miaka iliyofuata na mwaka 2021 pia ikishika nafasi ya kwanza kati ya nchi 180 ikiwa na alama 88/100.

Hata hivyo, pamoja na Tanzania kuonekana kufanya vizuri kuliko nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki katika eneo la rushwa kwa mwaka 2021, bado haipo katika nafasi ya kujivunia. Bado kuna juhudi zinazopaswa kuangaliwa vema kwani yapo maamuzi yanayofanywa na taasisi za serikali yanayoweza kuleta hali mbaya zaidi.

Kwa mfano, pamoja na Tanzania kuwa nchi ya pili barani Afrika kujiunga na Mpango wa Uwazi wa Serikali (Open Government Partnership - OGP) mwaka 2011 ikitanguliwa na Afrika Kusini, nchi hiyo mwaka 2017 ilitangaza kuamua kujitoa katika mpango huo. Hatua hiyo inazua wasiwasi kuhusu utekelezaji wa sera ya uwazi.

Mpango wa OGP ulianzishwa kama juhudi za dunia nzima kuhimiza wadau wa serikali na sekta binafsi kuendeleza uwazi na uwezeshaji wa raia. Mpango huo ambao ni jukwaa la kimataifa ambapo serikali wanachama hujitolea kutekeleza programu za kitaifa kama vile kukuza uwazi na uwajibikaji katika utawala; kukuza ushiriki wa wananchi katika kufanya maamuzi ya umma; na kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kwa ushiriki wa raia.

Pia, mnamo Januari 2016, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye, alitangaza TBC1 kusitisha kuonesha Mikutano ya bunge mubashara kutokana na gharama za kufanya hivyo kuwa kubwa. Waziri Nape alisema TBC1 wangerekodi na kuonesha katika kipindi maalum usiku kuanzia saa nne hadi saa tano.

Tangu mwaka 2013 kulikuwapo nia ya kuzima matangazo ya vikao vya bunge kwa kile kilichoelezwa na Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilila kuwa ni kuleta maadili kwa baadhi ya wabunge ambao walikuwa wakishindwa kufuata kanuni za bunge na kutumia nafasi hiyo kutafuta umaarufu. Lengo lilikuwa kuondoa matangazo ya moja kwa moja na kisha kuyarusha baada ya kurekodiwa na kuondolewa kwa “hoja zisizo za msingi”.

Wananchi waliona nia hiyo kama ni kuwekewa ukuta mbele ya wanachopaswa kuona kwani matangazo hayo huwawezesha kusikiliza na kuangalia wawakilishi wao wanavyotoa maamuzi ambayo moja kwa moja yanaathiri maisha yao, hivyo kupata na fursa ya kupima wao wenyewe mwenendo wa wawakilishi wao.

Aliyewahi kuwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Ludovick Utouh, amewahi kunukuliwa akisema: “Bila ya kuwepo kwa uwazi katika utendaji wa serikali, uwajibikaji hautakuwepo. Ili uwajibikaji uwepo, ni lazima kwanza utanguliwe na uwazi. Baada ya kuwepo kwa uwazi kwa kila mtu kujua kila kinachofanyika, watendaji watajikuta wanalazimika kuwajibika maana kila kitu kitakuwa kipo wazi”
 
Back
Top Bottom