SoC01 Uvuvi haramu, athari zake na wajibu wa wananchi katika kuzuia uvuvi haramu ziwa Victoria

Stories of Change - 2021 Competition

Chikwakala AA

Member
Sep 14, 2021
5
6
Nimeamua kuandika kuhusu swala la uvuvi haramu hapa nchini hasa nikiangazia ziwa Victoria Kwa sababu nina uzoefu mzuri kwenye shughuli za uvuvi. Nitaanza kwa kueleza maana uvuvi haramu na hali ya uvuvi haramu hapa nchini (hasa ziwa Victoria), athari zake na wajibu wa wananchi katika kuzuia uvuvi haramu.

Maana ya uvuvi haramu

Ni uvuvi ambao mbinu unatumia mbinu zisizofuata kanuni na sheria za uvuvi endelevu, unahusisha kuvua samaki wengi kwa wakati mfupi, kuvua samaki wadogo, au kusababisha vifo vya samaki wengi majini na kuharibu mazingira ambapo samaki huzaliana.

Mbinu zinazotumika kufanya uvuvi haramu, kwa upande wa ziwa Victoria mbinu maarufu ni matumizi ya nyavu zenye matundu madogo ambazo zinavua samaki walio chini ya kiwango (makokoro na nyavu zingine ni mifano mizuri), nyavu za nylon ambazo hazionekani majini(maarufu kama timba), matumizi ya kemikali ambazo zinaua asilimia kubwa ya vitu hai vinavyoiishi majini, matumizi ya fujo kwa njia za mabomu au katuli kufukuza samaki, Kutumia nyavu zenye kina kirefu zinazokinga sehemu kubwa ya kina zinapokuwa zimetegeshwa, na nyingine nyingi.

Athari za uvuvi haramu

Uvuvi haramu ndiyo chanzo kikubwa cha kuharibu mazingira na ekolojia ya ziwa au chanzo kingine cha maji, kupungua kwa idadi ya makundi ya samaki na hata kupotea kabisa kwa aina nyingine za samaki ni baadhi ya athari kubwa sana ambazo zimesababishwa na uvuvi haramu wa muda mrefu. Babu yangu alikuwa akinieleza takribani miongo 6 iliyopita walikuwa wakinasa samaki wengi sana, hadi gunia 8 za samaki, hali ikiwa mbaya walipata gunia 3, walikuwa samaki wengi sana, na wengi walikuwa wakubwa, walikuwa wakitumia nyavu chache sana, mtu mwenye mtaji mkubwa aliweza kumiliki nyavu si zaidi ya 10 ndani ya mtumbwi mmoja. Kwa sasa mtumbwi mmoja unaweza kuwa na nyavu 50 hadi 100 na wakarudi na samaki watatu tu.

Kila siku kuna mabadiliko ya hali ya upataji samaki kwa wavuvi hii ni kwa sababu wavuvi wengi hawajali kuhusu kesho yao, wengi wanatamani kupata samaki wengi sana leo bila kufikiri kuwa wanahitaji kupata samaki wengi hata kesho pia. Samaki wengi wanavuliwa wakiwa bado wadogo yaani hawajaanza kuzaa kabisa au wamezaa mara chache tu! Hii inapelekea kupungua kwa kiasi kikubwa cha idadi ya makundi ya samaki na wakati mwingine kusababisha baadhi ya makundi ya samaki kupotea kabisa (extinction). Mfano wa aina za samaki ambao wanaaminika kupotea kabisa licha ya kuwa walikuwepo miongo miwili iliyopita ni samaki aina ya njegere,sarakuyu, na aina nyingi za “cichlid” waliokuwepo ziwa Victoria,ni samaki ambao hadi mwishoni mwa miaka ya 1990 walikuwepo bado. Samaki wengine walio hatarini kutoweka ziwa Victoria ni kama Hongwe, mbete, nembe na wengine. Katika mazungumzo na mzee Asaph Lukiko mmoja ya wavuvi wa muda mrefu alisema kutoweka kwa makundi fulani ya samaki kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kupandikizwa kwa samaki aina ya sangara ziwa Victoria miaka ya 1950. Sangara ambao asili yao ni mto Nile, ziwa Chad, Turkana na mabonde mengine ya maji Afrika ni moja ya samaki wanaozaliana kwa kasi na ni samaki walao samaki wengine (predators). Licha ya kuja kwa kukawia lakini sangara kwa sasa wanaongoza kwa idadi kuliko makundi mengine ya samaki ndani ya ziwa Victoria tukiondoa dagaa na samaki wengine wadogo wadogo.

Nusu muongo na kurudi nyuma sangara wengi walikuwa wakielea juu ya maji sababu ya mabadiliko ya hali ya joto majini, wavuvi walikuwa wakinufaika kwa kuokota sangara wengi na wakubwa lakini hali hiyo inapotokea siku hizi ni mara chache sana utaona sangara wakielea.

Matumizi ya kemikali ambazo ni sumu kufukuza na kuua samaki husababisha madhara makubwa ambayo ni kuua samaki na vitu vingine hai vinavyokuwepo kwenye eneo lililoathiriwa. Kamongo kwa sababu ya uwezo wao wa kujificha chini ya tope mara nyingi hunusurika. Sumu zinazotumika huingia moja kwa moja kwenye mnyororo wa chakula au mlishano wa wanyama(food chain) kutokana na binadamu, wanyama na ndege kula samaki waliothiriwa na kemikali au kunywa maji yenye kemikali hiyo, wakati mwingine zinatumika kemikali ambazo ni ngumu sana kwenye mazingira (non-biodegradable) ambazo husababisha madhara kwa wanyama wengine walio madaraja ya juu kwenye mnyororo wa chakula. Mfano wa kemikali zilizowahi kutumika sana ziwa Victoria ni Thiodan (Endosulfan) ambayo ipo kwenye makundi ya kemikali zinazoitwa Organochlorides zilizokuwa zikitumika kuua wadudu haribifu mashambani, Thiodan na Organochloride zingine kama DDT hazitumiki tena duniani kote kwa sababu ya athari zake zilizogundulika kwenye mazingira na vitu hai!

Athari hizi zote kwa pamoja zinachangia kushuka kwa uchumi wa nyanja ya uvuvi. Uchumi wa familia nyingi zinazozunguka ziwa Victoria zinategemea uvuvi. Samaki ni chakula muhimu kwenye jamii za watanzania, kupungua kwa samaki kuna athari za moja kwa moja za kiuchumi na kiafya pia. Viwanda vya samaki hasa sangara vinadolola kwa sababu ya upungufu mkubwa wa malighafi. Viwanda hivi vingi viliiibuka miaka ya 1980 baada ya sangara kuanza kuvuliwa kwa kasi ziwa Victoria. Kupungua kwa mabondo (swim bladder ya sangara) ambayo ni malighafi ya muhimu kwa ajili ya kutengenezeza nyuzi (absorbable stiches) zinazotumika hospitali kushonea wagonjwa wa upasuaji ni athari nyingine pia.

Changamoto zilizopo katika kupambana na uvuvi haramu

Watu wengi hudhani jukumu la kupambana na uvuvi haramu ni la serikali peke yake, na kwamba uvuvi haramu unaiharibia serikali tu, hii si kweli kabisa. Serikali ina sehemu yake ya utekelezaji na wananchi wana nafasi yao pia. Serikali inahitaji kusimamia sheria zilizowekwa kuhusu uvuvi haramu kwa kuweka bajeti itakayowezesha ufuatiliaji mzuri wa watu wanaojihusisha na vitendo vya uvuvi haramu, kwa kupiga patrol mara kwa mara na kuwakamata.

Watendaji wa muhimu ni maafisa uvuvi, waliopo hadi ngazi ya kata ambao wana jukumu la kudhibiti uvuvi haramu unaofanyika kwenye maeneo yao. Maafisa uvuvi hushindwa kutekeleza majukumu yao sababu ya rushwa wanayopewa na wavuvi, wakati mwingine wavuvi huchanga pesa kila mwezi ambayo hutumika kama rushwa kumshawishi afisa uvuvi wa eneo husika asipite kufanya patrol. Muda wote maafisa uvuvi wanakuwa tayari kuwarudishia wavuvi dhana haramu baada ya kupewa pesa ya kula.

Matumizi mabaya ya siasa ni changamoto nyingine kubwa katika kupambana na uvuvi haramu, wananchi wa kawaida siku zote hudhani kuwa serikali inawaonea inapoamua kusimamia sheria za uvuvi haramu kwa kukamata nyavu na dhana zingine haramu na kuziteketeza sababu wamiliki hupata hasara. Wanapopata hasara hasira zao wanazielekeza kwa serikali iliyopo madarakani wakiishutumu kuwa haina huruma na wananchi wake, ilihali serikali husika inatimiza wajibu wake ambao ni kwa manufaa ya wananchi wenyewe! Wanasiasa huamua kutumia fursa hiyo kwa kupunguza juhudi za kuzuia uvuvi haramu ili uongozi husika uonekane unafaa kwa wananchi husika, maana yake uongozi huo utajipatia kura kiurahisi wakati wa uchaguzi wa viongozi. wakati mwingine baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali za serikali huahidi kutosimamia sheria zinazowakandamiza wavuvi haramu endapo watapewa madaraka.

Wavuvi wengi au wananchi kwa ujumla hawana elimu juu ya madhara ya uvuvi haramu ya muda mrefu hasa kwa maendeleo yao wao wenyewe, wengi wao hawajali kuhusu kizazi kijacho. Hawana elimu kuhusu wajibu wao katika kuhakikisha uvuvi endelevu.

Wajibu wa kila wananchi katika kupambana na uvuvi haramu

Wananchi wanahitaji kuambiwa ukweli kwamba sheria za kupambana na uvuvi haramu zimewekwa kuwasaidia wao wenyewe, watambue kuwa sheria zimewekwa na wao wenyewe japo kwa kupitia wawakilishi wao bungeni. Sheria hizo zinalenga kusaidia samaki waendelee kuzaliana kwa wingi huku binadamu wakiendelea kufaidi samaki hao milele, sheria inalenga kuwepo kwa uvuvi endelevu, samaki wapatikane kwa urahisi, samaki wengi na wakubwa. Bahati nzuri wavuvi wanazijua vizuri kanuni za uvuvi endelevu, wanafahamu ukomo wa kipimo cha macho matundu ya nyavu unaoruhusiwa, wanafahamu aina za nyavu zisizoruhusiwa n.k

Wananchi watambue kuwa wanapozuia utendaji kazi wa kawaida wa maafisa uvuvi kwa kuwapa rushwa maana yake wanaibiwa mara mbili, kwa sababu ni pesa zao zinazomlipa mshahara kila mwezi afisa huyo ili atimize majukumu yake halafu wanatumia pesa tena kumshawishi asitimize majukumu yake! Wanachokifanya wavuvi wanamlipa afisa uvuvi azuie uvuvi haramu halafu tena wanamlipa ili asitimize majukumu yake, inashangaza sana.

Wananchi washiriki moja kwa moja katika kuzuia uvuvi haramu, kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake, mara nyingi wavuvi wanakuwa na uongozi wa beach (beach management unit, BMU) ambao pamoja na kuhakikisha mazingira mazuri ya mwalo(beach) uongozi unasaidia kuunganisha shughuli za wavuvi ikiwemo ulinzi wa mali zao n.k, katika baadhi ya maeneo ambayo yameshuhudia kupungua kwa samaki kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya uvuvi haramu yamejitambua na wanatumia BMU kuhakikisha hakuna tena uvuvi haramu, ukionekana unatumia dhana haramu tu wananchi watakupigia yowe kama mwizi, utakamatwa na utawajibishwa kwa kulipa faini kubwa na dhana zako zitateketezwa kwa moto.

Wananchi wajifunze kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira ya vyanzo vya maji ili kulinda uhai wa vitu vinavyoishi majini, kuepuka kutupa taka hatari majini kama vipande vya nyavu vilivyochakaa, madhara yake ni makubwa,mimi mwenyewe nimewahi kunasa samaki ambao wanatembea na kipande cha wavu kilichojivika kwenye mwili wake kinamkata na kumuumiza siku zote kila anavyoongezeka ukubwa, hii inatokea mara nyingi sana, fikiria kuhusu maisha ya samaki ambae anajikuta ndani ya mfuko wa plastiki ambao una rangi sawa na maji, haoni njia ya kutoka mwisho anakufa bila msaada, kuepuka kumwaga kemikali za hatari kwenye vyanzo vya maji, kuepuka kuharibu mazingira ambayo samaki wanazaliana hasa kwa kuepuka kuanzisha shughuli za binadamu kama kilimo pembezoni mwa ziwa ambapo mara nyingi samaki huzaliana.

Kila mvuvi akijihusisha na nyia halali za uvuvi ndani ya miezi michache tu samaki watakuwa wengi sana ziwa Victoria, na tutaweza kuvuna samaki wengi na wakubwa pia.

Wananchi wajifunze kutafakari athari za kukubaliana na uhuru wa muda wanaopewa kama zawadi na wanasiasa, wajifunze kuwa madhara yake watayaishi wao, huku mwanasiasa akiwa hana shida maana hatokuja kuvua samaki.

Wavuvi pia hawapati nafasi ya kula samaki wazuri na wakubwa wanaowavua sababu samaki hao ni wachache kwa hiyo mvuvi anauza samaki wazuri ajipatie kipato wakati huo yeye anaenda kununua dagaa wakavu watoto wakale. Tukiwa na samaki wengi ziwani watu wengi wataweza kumudu kula samaki wazuri.

Mabadiliko yanaanza na wewe, mtu mmoja awe chachu ya mabadiliko kwenye jamii!
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom